Tukiwachambua akina Lema, Lisu, Mnyika na Zito, Filikunjombe na wengine, isiwe kutaja majina tu bila kuwachambua itaonekana JF si wa kiwango tunachotarajia. Kuna mambo kadhaa ambayo yanaweza kumpa mtu nafasi ya kupaa na papo akawa na yanayomteremsha, bora kuwa na mizani ambayo inampa mtu haki yake bila upendeleo. Hii ni kwa wenye upeo wa kuelewa wanaweza nielewa wengine wataishia mipasho lakini wote mmetumia uhuru wenu kuchangia na halijaharibika neno, ila nifanyayo ndiyo njia bora ambayo wasomi, wataalamu na watu makini hutumia kupima uwezo wa mtu.
Lema namtolea nje kwa jambo moja ambalo ni papara, bila kutuliza akili na kuangalia madhara yake. Anafaa kwa uhamasishaji lakini si kuongoza. Lema hatumii zaidi akili na busara. Kuna nafasi ambazo anatakiwa kutumia zaidi akili, na busara lakini yeye anaendekeza zaidi utashi hiyo ndiyo kasoro ambayo anayo. Jambo kama hilo alikuwa nalo pia Mrema enzi zake, kuna mambo na nafasi mtu unatakiwa kupunguza jazba, kufikiri kabla ya kutoa tamko na kuangalia athari zake zinazoweza kutokea na namna gani uongee kwa lugha ambayo haitaleta mtafaruku zaidi kwa walio kinyume cha itikadi yako.
Zitto ni mlipuaji zaidi na anafaa kuwa katika nafasi ya wizara nyeti kwa ajili ya umakini wake. Anaweza kuwa kiongozi mzuri hapo baadaye baada ya mchemko wa ujana kupungua na utu uzima kushika nafasi na hivyo kujenga dhana ya ustahimilivu. Kuna mambo ya kunyooshea vidole kwa nafasi aliyo nayo, lakini kwa mwendo huu kama kiongozi wa nchi afanye hivyo mambo yataharibika, yatakiwa kuwa na hali ya ustahimilivu, busara, hekima na moyo wa subira.
Mnyika anaonekana kukomaa kiakili angali kijana mbichi, anaongea kwa busara, hoja yenye mvuto na ustahimilivu katika ukokotoaji wake. Ustahimilivu alio nao ni hazina nzuri sana kwa siku za usoni kwani akishakomaa zaidi ni chombo cha thamani kubwa.
Lisu ni hazina kubwa sana ya ufumbuzi wa mengi yahusuyo masuala ya kisheria. Hana woga, mwazi na mwelimishaji mzuri. Anahitaji muda zaidi katika kuimarika zaidi katika utumishi wa umma, na ni mmoja ambaye kama Chadema wanaweza kushika dola anafaa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Deo Filikunjombe ni kijana ambaye anajiamini, anaaminika, ana utashi mkubwa, anajituma na anajitolea. Anamwamko wa kimageuzi, mpole, mvumilivu, mkweli, hana woga na ni mtetezi wa wananchi bila kujali itikadi za chama chake. Ana ushupavu wa pekee kiasi cha kupinga wazi wazi dhuluma na udhalilishaji unaofanywa na viongozi wa Chama chake au serikali yake. Ni jambo la pelee na lisilo la kawaida kwenda kinyume cha chama kilichomdhamini kuingia bungeni. Wengine wayafanyayo nafasi na mazingira yao ndiyo hayo, lakini huyu Deo naweza kumfananisha na Kambona, Edwin Mtei, Kaserabantu, Horace Kolimba, Abdu Jumbe na wengineo kwa kuwataja wachache.