Mwanamke Katika Jamii yenye "Nafasi Sawa" - Katika Dunia ya Ubepari

Mwanamke Katika Jamii yenye "Nafasi Sawa" - Katika Dunia ya Ubepari

Pile F

Senior Member
Joined
Aug 15, 2020
Posts
124
Reaction score
173
Katika nusu ya pili ya karne ya ishirini huko Marekani na nchi nyingine za magharibi kulichomoza mwendo wa neofeminism, yaani "nafasi sawa".

Kwa leo hali sawa za wanawake na wanaume zimetangazwa rasmi katika nchi nyingi duniani.

Mwishoni mwa karne iliyopita ilisisitizwa na wanaelimujamii kwamba mwanamke anayetupendeza zaidi kwa sasa ni yule mwenye akili sana na elimu, anayeshiriki kwa dhati katika shughuli za kijamii, anayeweza kuzungumza kuhusu mada yoyote, mwenye sura ya kuvutia na mchangamfu.

Mtaalam maarufu wa Kimarekani Bi. K. Amundsen ameandika juu ya mwanamke wa Marekani: "Hapati malipo ya kutosha kwa ajili ya kazi yake, daima anaonekana amechoka na mara nyingi anapaswa kubeba peke yake mzigo mzito wa shughuli za kutunza nyumba na kuwalea watoto, anaweza kuwa yeyote isipokuwa mtu asiye na shida, asiyejua maudhi wala matatizo, anayeridhika na hali yake na kufanyiwa kila la faraja. ...Kuwa mwanamke katika jamii yetu kwa wakati wa sasa kunamaanisha kukumbwa na uhalisia wa kuchukiza, tena kukabiliwa na mambo ya hatari."

Katika nchi nyingi za kibepari kumepitishwa sheria kwa wanaume na wanawake kupewa malipo sawa kwa kazi sawa, tena kuna sheria ya uhifadhi wa afya kwa mwanamke kwenye sehemu yake ya kazi na mahali pengine akina mama wameongezewa viinua mgongo wakati wa likizo ya uzazi. Hayo ni ushahidi wa akina mama kutambuliwa kuwa na jukumu muhimu katika jamii.

Lakini katika upande wa kuongezeka kwa tatizo la ukosefu wa ajira, wanawake wako mbele ya wanaume kwenye nchi za kibepari na ili kuhalalisha hili hutolewa matamshi ya kichochezi ya kwamba mwanamke akipewa kazi anamnyima mwanamume nafasi hiyo ya kazi. Lakini ukweli usiopingika ni kwamba wanawake wengi zaidi wafanyao kazi wanaihitaji kazi kama asili ya riziki.

Kwa wakati wa sasa wa mapinduzi ya kisayansi na ya kiufundi duniani kunaongezeka umuhimu wa kazi za akili na kupelekea tatizo la ukosefu wa ajira na anayeweza kukwepa tatizo hilo ni aliye na elimu kubwa ya jumla na elimu maalum, kwani ni yeye ndiye atakayefaa kwa kazi za aina mbalimbali.
Lakini utaratibu wa kuwaandaa wataalamu unakusudiwa hasa kumfundisha mtu taaluma mojawapo maalum jambo ambalo humfaidisha zaidi mwajiri binafsi kwani anaweza kuwa na uhakika kwamba mtaalamu ajuaye kazi moja tu atakuwa mtiifu zaidi jambo linaloleta athari mbaya kwa hali ya mwanamke katika jamii.

Usawa wa nafasi unaosifiwa sana katika jamii ya kibepari unaonekana kuwa upuuzi mtupu vilevile wakati wa kuajiriwa kwa vijana. Katika hali ya kutothaminiwa kabisa shahada ya elimu ya juu, shahada wanazopewa wanawake zinageuka kuwa karatasi isiyokuwa na thamani yoyote.

Matokeo ya aina zote za utaratibu wa kutopatikana usawa kwa akina mama katika jamii ya kibepari ni kwamba wanafanyiwa ubaguzi katika malipo ya kazi zao.
Mahali pengi mishahara wanayolipwa wanawake iko chini ya mishahara ya wanaume.
Hata katika nchi zenye sheria ya kukataza ubaguzi huo, waajiri binafsi hutumia mitindo mbalimbali ya kuwapunguzia akina mama malipo ya kazi. Kwa mfano, akina mama hupewa kazi zilizo rahisi zaidi, yaani kazi za mishahara ya chini.

Ijapokuwa mshahara wa mwanamke ni mdogo, umuhimu wake kwa bajeti ya familia au ukoo wake umeongezeka.

Mwanamke afanyaye kazi anaongezewa wajibu wa kuubeba ukoo wake na jambo lililo muhimu zaidi ni kwamba anaongezewa pia wajibu wa kuwalea watoto. Lakini wakati huohuo bajeti ya serikali inazidi kupunguza matumizi ya fedha kwa ajili ya bima ya kijamii, uhifadhi wa afya, ujenzi wa nyumba, vyombo vya usafiri, elimu na kadhalika.

Utaratibu wa matumizi ya bidhaa uliopo nchi za magharibi husifiwa sana huko, lakini hauwezi kuitwa vingine isipokuwa kuwa ni KEJELI. maana mwanamke kila wakati huambiwa: "Nunua bidhaa hii! Tumia bidhaa ile! Ukipata bidhaa hizi utakuwa na heri, utafanikiwa katika maisha yako!"
Naam, kila mwanamke anataka kuwa mzuri kama wale wasichana kwenye picha za majarida yanayochapishwa kwa ajili ya akina mama.

Mwanamke gani hataki kumiliki vitu vya nyumbani ambayo hurahisisha kweli kazi za utunzaji wa nyumba? Nani asiyetaka kuishi katika nyumba yenye raha zote? Mama gani asiyetaka watoto wake wafurahie maisha, wasome vitabu vizuri, wasikilize muziki wa kuvutia na wajionee dunia kwa kufanya safari za utalii?

Lakini yote hayo yanataka kulipiwa. Tena, bei zote kabisa zinazidi kupanda. Kumepanda kodi za nyumba, ada za masomo na nauli za kusafiri.

Mwanaitikadi wa neofeminism B. Friedan ameandika wazi kabisa kwamba katika jamii ya kibepari mwanamke anadanganywa na kufanyiwa vitimbi vya "kuchafua akili". Kutokana na mambo hayo akina mama huvunjika moyo na hufikia katika hali ya kutojali chochote. Kwa hiyo ili kujitoa katika hali hii ya kuvunjika moyo hutumia ndoto binafsi, mvinyo na shughuli mbalimbali za kujisahaulisha na maudhi waliyonayo.

Hayo ni machache juu ya hali ambayo mwanamke amejaaliwa kuwa nayo katika nchi za kibepari. Ndiyo sababu watu zaidi na zaidi wanajitahidi kutafuta malengo mengine ya maisha na mitindo mingine ya mahusiano baina ya wanadamu.
 
Back
Top Bottom