Mwanamke atakubomoa, mwanamke atakujenga!

James Hadley Chase

JF-Expert Member
Mar 25, 2020
1,496
2,691
HAIPUNGUI miaka mitatu sijakutana na Kajole. Hapo kabla tulikutana mara ya nyingi. Alikuwa anapitia nyakati ngumu. Nami nilihakikisha nampa kila kilichokuwa ndani ya uwezo wangu ili kumwezesha kuvuka magumu aliyopitia. Kajole akawa rafiki.

Hapo katikati alikuwa akinipigia simu. Aliniambia aliendelea vizuri. Basi, baada ya zaidi ya ‘masiku' 1,095, Kajole akanipigia simu, akaniuliza nilipo. Nikamjibu “kibaruani kwangu”, uzuri anapajua. Akaja.

Nilimzoea Kajole usafiri wake bodaboda au akijitutumua bajaji. Kajole alipaki gari. Sio baby walker, ni SUV ya bei iliyochangamka. Kajole alivaa suti kali. Akaniambia: “Nataka upande gari langu, nikuendeshe, nipate muda wa pamoja na wewe.”

Nikaingia kwenye gari la Kajole. Redio ilikuwa inarudia wimbo mmoja, “You Raise Me Up”, lakini wanamuziki tofauti. Wimbo original uliimbwa na bendi ya Secret Garden, kisha ukarudiwa na wanamuziki wengi.

Kwenye redio ya gari la Kajole, niliwasikia Secret Garden, kisha Westlife, halafu mbabe wa sauti, Martin Hurkens. Alipomaliza Hurkens na lisauti lake, zilifuata versions za Josh Groban na Selah. Mbona wimbo huohuo tu muda wote? Matoleo tofauti lakini ujumbe uleule.

Nikazama kusikiliza muziki mzuri na ujumbe uliomo: When I am down and, oh, my soul so weary; When troubles come and my heart burdened be; Then I am still and wait here in the silence; Until you come and sit awhile with me.

You raise me up, so I can stand on mountains; You raise me up to walk on stormy seas; I am strong when I am on your shoulders; You raise me up to more than I can be.

Kiswahili: Ninapokuwa mnyonge na, oh, nafsi yangu inapojaa uchovu; Matatizo yanapokuja na moyo wangu unapozidiwa mizigo; Kisha nabaki mtulivu na nasubiri hapa nikiwa kimya; Mpaka uje na uketi kidogo na mimi.

Unaninyanyua, hivyo naweza kusimama kwenye milima. Unaninyanyua, kuweza kutembea kwenye bahari yenye dhoruba. Mimi ni imara ninapokuwa kwenye mabega yako. Unaninyanyua kushinda ninavyoweza kuwa.

Inanifanya nikumbuke nukuu moja ya Kiingereza ambayo simjui aliyeisema kwa mara ya kwanza: “If someone ever tells you a certain song is important to them, you should turn it up and lay in your bed and close your eyes, and really listen to it, even if it's 10 minutes long. Because at the end, you will know that person better.”

Kiswahili: Kama mtu anakwambia wimbo fulani ni muhimu kwake. Unatakiwa uucheze na ulale kitandani kwako na ufumbe macho, usikilize hasa, hata kama wimbo ni wa dakika 10. Kwa sababu mwishoni, utamjua huyo mtu vizuri.

Ipo nukuu nyingine inasema: “Playlist ya nyimbo ninazozipenda ni kitu cha siri mno ambacho naweza kuchangia na mtu ninayemwamini.” Hakika, aina ya nyimbo humpambanua mwanamuziki. Humpambanua anayezipenda.

Utamjua Manfongo kwa “Haina Ushemeji”, na anayeupenda huo wimbo sana, ni rahisi kuijua tabia yake. Ni kama “Asiwaze” jinsi ambavyo umempambanua Stamina na mikasa ya ndoa yake. Msagasumu na nyimbo zake, mara Mwanaume Mashine na nyingine, muziki hauongopi. Nyimbo huwasilisha fikra na huteka fikra.

Kitendo cha Kajole kusikiliza sana “You Raise Me Up” kikanipa picha kwamba lipo jambo kuhusu huo wimbo. Tulikuwa kimya, nikavunja ukimya: “Unaupenda sana huu wimbo?” Kajole akanitazama akitabasamu, akaniambia: “Ndio maana nimekufuata tuzungumze. Mambo makuu mno yamenitokea.”

Nikamwambia: “Naona, leo umekuja unaendesha SUV. Halafu umetinga suti kali na kiatu cha Monk Strap.”

Akasema: “Nataka kuoa!” Nikampa hongera, badala ya kuitika akanitazama akitabasamu. Tukasikiliza tena wimbo. Josh Groban ndiye alikuwa anaimba wakati huo. You Raise Me Up. Umeninyanyua!

Kajole amependeza, ana afya nzuri, sura ina matumaini, ngozi inaakisi siha njema. Nikamuuliza: “Unamuoa nani?”

Akanijibu: “Mwanamke atakubomoa, mwanamke atakujenga. Mwanamke atakutesa, mwanamke atakusahaulisha mateso. Akikutenda mmoja, usichukie wote. Akiondoka wa kukuumiza, atakuja wa kukufariji. Usifunge mlango baada ya kutendwa. Ruhusu mwingine aingie. Unakumbuka hayo maneno uliniambia wewe?” Kajole aliniuliza, akanitazama, akatabasamu tena! Nikatikisa kichwa.

Uzuri naifahamu stori ya Kajole. Ni mtoto wa baba bila mama. Kajole angekuwa na pacha wake, lakini hakutoka, alifia tumboni, akaondoka na mama yao. Baba yake Kajole akaamua kuwekeza nguvu zote kumlea Kajole. Hakuoa. Maisha yalikuwa magumu sana.

Baba yake Kajole angerudi nyumbani usiku na andazi, kisha angempa Kajole ale asindikize na maji. Kibatali ndicho kiliingiza nuru nyumbani usiku. Na ile hulka ya walimwengu kuwa asiye na kitu si mtu, Kajole na baba yake wakawa wapweke.

Kajole alifika darasa la sita. Muhula wa kwanza ndoto za elimu ziliyeyuka. Baba Kajole alipatwa ugonjwa wa akili. Nani angemhudumia Kajole? Na baba yake je? Kajole akaacha shule afanye kazi ndogondogo, ajihudumie yeye na baba yake aliyegeuka tegemezi.

Mgaagaa na upwa hali wali mkavu. Katika vibarua, Kajole alikusanya senti, thumni hadi shilingi. Mara Kajole akaanzisha genge la kuuza matunda. Tataribu mtaji ukakua, akaanza kuuza na mkaa. Si nilikwambia? Walimwengu ni walemavu wa fikra, huwaona wasio nacho sio watu.

Kajole baada ya mafanikio kidogo ya genge lake la kuuza matunda, nyanya, vitu vya upishi na mkaa, walimwengu walianza kumwona Kajole mtu. Walikwenda kukopa. Kajole mwenye umri wa miaka 15 alianza kuiona mitego ya wanawake watu wazima. Tena wake za watu!

Nimekwambia baba Kajole alipatwa ugonjwa wa akili. Hata hivyo, hakuwa mbali kumlinda mtoto wake. Baba Kajole aliwafurusha wanawake waliomzengea mtoto wake kwa fimbo na mawe. Unajua nini? Damu ni kimiminika kizito kuliko kitu chochote. Kwa mzazi na mwanaye, hata ndugu. Labda damu ichakachuliwe na seli za utumwa.

Akatokea Sikuzani. Binti mwenye mama tu. Nao maisha yakawa magumu. Kajole alimhurumia Sikuzani, maana naye alipitia mazingira magumu kama yake. Basi ikawa, Sikuzani angekwenda gengeni kwa Kajole, kisha angesaidiwa mlo wa siku na mama yake. Sikuzani alikuwa mrembo, nani angeuona urembo wake na ule uchafu kwa jinsi alivyokosa matunzo?

Sikuzani na mama yake walipofukuzwa na ndugu kwenye nyumba waliyoishi, Kajole aliwakaribisha nyumbani kwao. Walichangia kila kitu. Ikawa familia moja. Kajole aliwapenda Sikuzani na mama yake walivyomjali baba yake. Baba Kajole akawa mtulivu. Hakusumbua. Maisha yalikuwa murua.

Kadiri biashara zilivyokwenda vizuri ndivyo na Kajole alivyoelekeza nguvu kwenye ujenzi. Alijenga vijumba vitatu na kupangisha. Alikarabati nyumba ya baba yake, ikawa na mwonekano mzuri kiasi.

Sikuzani alitaka shule, Kajole alimsomesha. Mama Sikuzani aliumwa homa ya ini (hepatitis B). Ini lake liliharibika (cirrhosis of the liver). Walikata tamaa. Siku Kajole alipoambiwa gharama za kumpandikiza ini mama Sikuzani ni Sh25 milioni India. Sikuzani hakuamini Kajole alipozitoa pesa. Sikuzani alikwenda India na mama yake. Sikuzani alikatwa ini nusu na kupandikizwa mama yake. Wakarejea wazima, afya timamu. Mama Sikuzani alishukuru kwa shukurani za moyoni.

Kila baada ya masomo ungemkuta Sikuzani gengeni na Kajole wakisaidiana biashara. Huku mkaa, kule matunda, nyanya, vitunguu, bamia, viazi mbatata, ndizi na bidhaa nyingine. Na usiku walirudi pamoja nyumbani. Wangemkuta mama Sikuzani alishapika. Waliketi na kula pamoja. Familia ilijaa upendo.

Kajole alimchukulia Sikuzani kama mdogo wake na waliishi kama kaka na dada. Mama Sikuzani akayachokoza mapenzi. Na mapenzi ni kama kidonge kichungu kilichopakwa sukari. Mwanzoni utakiona kitamu, utamu wa juu ukiisha, uchungu wake hauvumiliki.

Mama Sikuzani akamketisha Sikuzani, akamwambia akimaliza shule aolewe na Kajole. Kisha mama Sikuzani akamshawishi Kajole, kwamba kwa walivyoelewana na Sikuzani, wangejenga familia bora kama wangeoana.

Ushawishi wa mama Sikuzani ulipasha moto vilivyokuwa vimelala. Mapenzi yakachipua kati ya Kajole na Sikuzani. Waliambiwa wasubiri Sikuzani amalize shule, kwani walisubiri? Wamsubiri nani? Zikafika nyakati Sikuzani na Kajole walilala pamoja.

Maisha ya kusoma ukiwa mke wa mtu kivitendo. Unaingia darasani asubuhi na mawazo ya namna ulivyomhudumia mumeo usiku. Jamani! Sikuzani akafeli kidato cha nne.

Kajole akamrudisha shule aweze kurejea mitihani. Wakajitahidi kudhibiti mapenzi ili Sikuzani asome. Mambo yaliwezekana. Sikuzani alifika mpaka chuo kikuu kwa fedha za Kajole. Kule chuo Sikuzani akakutana na vijana wengine wazuri, wasomi, wenye kuijua dunia, sio Kajole aliyeishia kujua biashara zake za hoho na mkaa.

Sikuzani chuoni alikutana na vijana ambao wameshasafiri kuizunguka dunia. Wapo walioijua Marekani, walishafika Canada. Wameizoea mitaa ya London, Paris, Geneva hadi Luxembourg. Ni hapo Sikuzani aligundua mzunguko wa dunia ulimwacha mbali Kajole na maisha yake ya kuuza genge.

Likizo ya mwaka wake wa kwanza alianza kuonesha tofauti kwa Kajole. Hakutaka tena mambo ya kukaa gengeni. Siku Kajole alipomwambia waende wote gengeni, Sikuzani alimjibu: “Msomi wa chuo kikuu nikae gengeni nauza bilinganya na mkaa, nimerogwa?”

Likizo ilipokwisha alirudi chuo. Kajole aliendelea kumgharamia kila kitu. Likizo ya mwaka wa pili akamdanganya Kajole kuwa alitakiwa kufanya ziara ya lazima ya kimasomo Dubai. Kajole alipoambiwa pesa iliyotakiwa kugharamia safari, alijipinda, akamlipia tiketi ya ndege kwenda na kurudi, pia gharama zote za malazi, chakula, mizunguko yote ndani ya Dubai na dharura.

Kumbe Sikuzani alikuwa ameshampata Raven. Kijana msomi, mwanachuo mwenzake wa darasa moja. Walipotoka Dubai, walirejea chuo. Mwaka wa tatu ukaisha. Sikuzani alihitimu Shahada ya Fedha (Bachelor in Finance).

Sikuzani akarejea na taarifa ya kutaka kufunga ndoa na Raven. Kajole mshamba, hajasoma, yeye wa nini tena? Mama Sikuzani alipomwona Raven anaendesha gari, halafu msomi, akasahau mema yote ya Kajole. Walimgeuka. Walihama nyumba ya Kajole. Walipanga nyumba nyingine.

Ilikuwa jeuri kwamba Sikuzani ni msomi, angekosaje ajira? Raven pia msomi, halafu alitokea familia bora. Sikuzani na Raven walifunga ndoa. Fungate walikwenda kisiwani Bahari ya Pacific, Laucala, Fiji. Mama Sikuzani naye alipanda ndege kwenda Fiji.

Sikuzani alikuwa na rafiki yake aliyeitwa Shani. Walikuwa wote tangu high school, walifika chuo pamoja. Walisoma wote Finance. Walihitimu pamoja. Shani alijua umuhimu wa Kajole kwa Sikuzani. Alifahamu alipomtoa. Chuoni wakati Sikuzani anaanza kudeti na Raven, alimuonya. Alimwambia: “Kajole hastahili kuumizwa.”

Kwani Sikuzani alijali? Shani alimkumbusha Sikuzani alipotolewa na Kajole. Yalikuwa maneno tu! Yaliyeyuka kwenye sikio lilelile yaliyoingilia. Kwa hasira na uchungu, Shani hakuhudhuria ndoa ya Sikuzani na Raven, badala yake alitenga muda wake kumjali na kumfariji Kajole.

Ni kipindi hicho Kajole alikuwa karibu yangu, akinielezea aliyopitia. Nilimshauri namna ya kuishi baada ya yaliyomfika. Mara kadhaa alinigusia kuhusu Shani, jinsi alivyokuwa faraja yake. Kajole aliniambia kuwa Shani ndiye alimuibia siri ya Sikuzani kwenda Dubai na Raven.

Sasa, baada ya tabasamu, Kajole akaniambia: “Namuoa Shani.” Hapo nilizima kabisa sauti ya redio ili tusikilizane vizuri. Nikamuuliza: “Yule Shani rafiki yake Sikuzani uliyenisimulia?”

Akanijibu: “Huyohuyo. Si mwingine. Shani ndiye sababu navaa suti, naendesha gari. Ndiye yeye anafanya nisichoshwe kusikiliza You Raise Me Up. Ameninyanyua. Mungu amemtumia Shani kuninyanyua.”

Kajole alipaki gari kwenye nyumba ya ghorofa mbili. Waingereza wanaita “three-story building”. Akaseti gia ya gari kwenye parking. Akaniambia: “Hii ni nyumba yangu sasa. Shani alinifumbua macho. Si unajua mimi sikusoma na sikuwa na najichanganya? Nilikuwa siijui nguvu yangu. Shani ameniwezesha kujitambua. Nipo mbali sana sasa.”

Kajole alinisimulia: “Mimi sikuwa na elimu, sikuwa na maarifa makubwa ya kifedha na kufungua kampuni. Nilimsomesha Sikuzani nikitegemea angekuja na elimu yake tutanue biashara zetu, ila yeye alipoelimika alichagua kunidharau. Lakini sikupata hasara, Shani yupo. Milango imefunguka.”

Tuliingia ndani ya nyumba, akanionesha uzuri wake. Ina bwawa la kuogelea, vyumba sita vya kulala, theatre, veranda mbili. Akasema: “Sasa hivi naishi hapa.” Akanitambulisha kwa baba yake. Nikamuuliza: “Ulisema baba ni mgonjwa wa akili. Mbona ni mzima?”

Akanijibu: “Shani amefanikisha yote.”

Tukaingia kwenye SUV la Kajole, njiani wimbo You Raise Me Up unaendelea. Alinionesha majumba yake manne ambayo ni six-story kila moja. Amefanya apartments. Kajole akaniambia: “Mimi siku hizi siitwi baba mwenye nyumba. Ni mmiliki wa kampuni ya Kajole Real Estate.”

Tulifika kwenye kituo kikubwa cha mafuta, nikadhani tunaingia kuweka mafuta. Kumbe hicho kituo ni cha Kajole. Tukaingia ndani ya jengo la ghorofa nne mbele ya ile petrol station. Tukeketi kwenye ofisi nadhifu ambayo mlangoni iliandikwa Managing Director. Kajole akaniambia: “Karibu ofisini kwangu.”

Ikabidi Kajole anisimulie siri nyuma ya maajabu yake ya miaka mitatu. Alianza: “Nyakati ngumu za kuachwa na Sikuzani, ikatokea Shani akawa rafiki aliyenifariji. Tulisimuliana mambo mengi. Aliniambia ugumu alioupitia ili kupata kazi. Sehemu nyingi aliombwa rushwa ya ngono au fedha. Nami nilimfariji kwa magumu yake.

“Ungemkuta Shani anashinda gengeni kwangu, ananisaidia kuuza bidhaa mpaka mkaa. Nikashangaa, mrembo msomi kama Shani kujitoa vile kwa kazi ndogondogo. Nikaanza kumuona wa tofauti. Siku moja nilimwambia changamoto niliyopitia kwa wapangaji wangu kutolipia pango kwa wakati.”

Kajole alisema kuwa Shani alishangaa kusikia Kajole alikuwa na nyumba zenye wapangaji. Alipomwambia alikuwanazo saba, alishituka. Shani akataka azione hizo nyumba. Wakazitembelea. Baada ya siku mbili, Shani alimfuata Kajole akiwa na wazo la kuanzisha kampuni ya real estate.

Shani akaanza mchakato wa kusajili kampuni ya Kajole Real Estate. Baada ya usajili, alitengeneza andiko la kuomba mkopo benki kwa dhamana ya zilezile nyumba. Ni fedha hizo za mkopo zilijenga apartments nne, nyingine tatu ujenzi wake unaendelea.

Kituo cha mafuta je? Kajole alisema: “Zamani nikiuza mkaa na genge langu, nilikuwa natunza pesa ndani. Siku moja nilisikia kuwa matajiri hutunza dola, kwani ndio sarafu imara. Nilijiwekea utaratibu wa kununua dola 300 kila wiki na kufungia kwenye trunk la chuma chini ya kitanda changu.

“Sikuwa naweka pesa benki. Baada ya Shani kunifanyia maajabu ya kupata mkopo na kufungua kampuni, nilimwamini. Nikamwonesha akiba yangu ya mauzo ya mkaa kwa miaka 23. Shani alishangaa dola zote zile kuziweka ndani bila kuziingiza kwenye mzunguko zizaliane.

“Ndio tukajenga ile nyumba ya ghorofa mbili. Tukafungua kampuni ya Kajole Energy, tukachukua mkopo ambao umewezesha kujenga hii petrol station na majengo yake. Zamani hapa palikuwa panajaa magunia ya mkaa. Leo tunauza mafuta, gesi, mitungi na majiko. Supermarket na gym vyote ni vyetu.”

Kufikia hapo nikampongeza Kajole kumpata Shani, akaniwahi: “Natamani umpongeze Sikuzani kwa kuniacha.” Nikamjibu aache vijembe. Akanijibu: “Sitanii, Sikuzani aliponiacha ndipo Shani akaja. Sikuzani alinibomoa kihisia. Moyo ulipondeka, nikachukia wanawake, lakini Shani ameujenga moyo wangu, ameuimarisha na amenifanya niwapende zaidi wanawake.”

Baba yake naye aliponaje? Kajole alinijibu: “Shani alipendekeza tumtafutie matibabu. Miezi mitatu Ukraine baba alipona. Alirudi akiwa mzima kama ulivyomuona.”

Nini kingine Kajole hakunisimulia? Alisema: “Siku hizi naongea Kiingereza na Kifaransa. Shani alinipa mkazo kuwa lazima nisome hizo lugha ili niweze kuendesha kampuni zangu. Wakati nikisoma Kiingereza na Kifaransa, yeye akawa mwalimu wangu wa jinsi ya kutunza hesabu za biashara na ukaguzi ili nisiibiwe. Nipo vizuri kwa sasa. Ni mkurugenzi mtendaji hasa.”

Enheee, ndoa sasa! Kajole alisema kuwa siku zote alitamani Shani awe mke wake tangu alipomuona tabia zake na hasa alivyomsaidia kubadili maisha yake, ila akawa anamuogopa. Maana Shani aligeuka mwalimu wake. Hata hivyo, miezi sita iliyopita alimuomba wafunge ndoa.

Unajua Shani alijibu nini? Alimwambia Kajole: “Nilikuwa nakutazama tu, nifanye yoote haya halafu uende kuoa mwanamke mwingine, ningekupiga kipapai.” Walifurahi wenyewe. Pete ya uchumba ikapenya kwenye kidole cha Shani.

Kajole akaniambia: “Twende nikakuoneshe kitu muhimu kuliko vyote nilivyokuonesha.” Tukaingia kwenye mlango wenye maandishi “Director of Finance”, Nikamuona Shani. Kumbe Shani ni Shani kweli. Yaani ni Shani mno! Mrembo sana. Shani ndiye Mkurugenzi wa Fedha.

Nikampongeza, nikamwambia: “Shani is a real thing.” Akanijibu: “She’s mine.” Nikamjibu: “Ni wako ndio, huna sababu ya kunikumbusha.” Akanishushua: “Nimekwambia hivyo ili upunguze kumtolea macho.”

Tulifurahi pamoja. Nikamsifu Shani, shem wangu, kwa kuyabadili maisha ya Kajole. Shani alipokea pongezi, akasema: “Namshukuru zaidi Mungu, niliiona almasi ikiwa imefunikwa na vumbi la mkaa, nikaisafisha. Namsikitikia shosti wangu Sikuzani aliyekimbilia chupa yenye kung'aa na kuacha almasi.”

Kajole akaniambia lilikuwepo jambo hasa lililofanya anitafute. Nikamtazama kwa umakini. Akasema: “Raven, yule jamaa aliyemuoa Sikuzani ni mtoto wa aliyekuwa kigogo wa Wizara ya Fedha. Na aliwaahidi Sikuzani na Raven kuwapa kazi wizarani baada ya honeymoon. Sikuzani na Raven waliporejea kutoka honeymoon Fiji, walikuta mambo yamegeuka.

“Baba yake Raven alisimamishwa kazi kwa makosa ya matumizi mabaya ya ofisi, kisha akashitakiwa kwa uhujumu uchumi. Sikuzani na Raven wapo hawana kazi mpaka leo. Matumaini yote yalikuwa kwa baba yake Raven ambaye yupo mahabusu. Sasa juzi Sikuzani alinifuata kuomba nimuajiri yeye na mume wake. Ndio maana nimekutafuta ili unishauri.”

Nikamuuliza “Unasema?”, akajibu: “Eeh, nataka unishauri, niwaajiri Sikuzani na mume wake? Maana nafasi zipo, na naona wanahangaika mjini ajira ngumu.”

Mimi nikamgeukia Shani, shem wangu, nikamuuliza: “Kwenye simu una You Raise Me Up?” Akajibu labda aucheze kutokea YouTube. Akaniuliza version ninayotaka. Nikamwambia aweke ya Martin Hurkens, maana nilikuwa na shida ya ule ‘msauti' wake. Akaweka. Wote tukaimba.

When I am down and, oh, my soul so weary; When troubles come and my heart burdened be; Then I am still and wait here in the silence, Until you come and sit awhile with me.

You raise me up, so I can stand on mountains; You raise me up to walk on stormy seas; I am strong when I am on your shoulders; You raise me up to more than I can be.

Ndio, mwanamke atakubomoa, mwanamke atakujenga. Mwanamke atakudharau, mwanamke atakuheshimu. Mwanamke atakunyanyapaa, mwanamke atakuthamini. Acha anayekushusha hadhi aondoke, kisha aje atakayekupandisha thamani. Hawafanani, japo ni ukweli kuwa hakuna mwanamke asiye mwanamke.



Ndimi Luqman MALOTO
 
Aahh hii nakala sijui makala labda ingekuja kwa jina la Eric Shigongo la siwezi kusoma

Uzi mrefu mno
 
Sawa Bro Maloto...naelewa makala zako...ila hapo kutunza usd miaka 23!! Naomba ucjarib
 
6 Reactions
Reply
Back
Top Bottom