Zinduna
JF-Expert Member
- Nov 6, 2011
- 2,378
- 3,392
Tafsiri ya awali ambayo ni potofu inamhusu Adam na Hawa au Eva zimewaaminisha waumini wa hizi dini mbili maarufu hapa nchini kwamba Hawa au Eva ndiye aliyemhadaa Adam kula tunda lililokatazwa la ule mti wa katikati.
Kwa tafsiri hiyo potofu inaonekana kama vile Hawa ndiye aliyemtongoza Adam hadi kumfikisha mahali ambapo alikubali kumuasi Mungu. Naamini miongoni mwetu tumewahi kusikia baadhi ya wanaume wakisema kwamba, mwanamke ni kiumbe aliyelaaniwa kwa sababu ya kumdanganya Adam.
Nadharia hii ambayo ilipotoshwa imekuwa ikifundishwa hivyo kwenye mafunzo ya dini yenye kuhusu chanzo cha binadamu na dhambi. Kwa jinsi mafunzo hayo yanavyotafsiriwa na wengi yamemfanya mwanamke kuonekana kama mdanganyifu kama nyoka na laghai jambo ambalo si kweli hata kidogo.
Kwa mfano unaposoma Quran, kuna maelezo yanayobainisha ukweli kwamba Adam anahusika mwenyewe kwenye kosa hilo. Ukisoma kwenye Suratu Taha, yaani Sura ya 20: 115 Mungu anasema, Na tulimpa ahadi (nabii) Adam zamani, lakini alisahau. Hatukuona kwake azma kubwa (kama za wale mitume wengine). Aya ya 21 Inasema, Basi wakaula wote wawili, na uchi waoukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani peponi (humo). Na Adam akamkosea Mola wake, na akapotea kidogo njia.
Je ni wangapi kati yetu ambao wanaujua ukweli kuhusu huu ushawishi ambao baadhi ya wanaume huutumia kuwakandamiza wanawake?
Ukweli ni kwamba hakuna kwenye vitabu vyote viwili vya hizi dini zetu maarufu hapa nchini ambapo kuna mahali panaonyesha kuwa mwanamke ndiye chanzo au aliyelaanika kwa kumlaghai Adam kula tunda la mti wa katikati. Ni tafsiri tu iliyotengenezwa ili kuupa nguvu mfumo dume na kumkandamiza mwanamke.