Mwalimu wa Upe; 'Tuikomboe Elimu Yetu'

motonkafu

JF-Expert Member
Dec 2, 2015
1,019
703
Mwalimu wangu ameniita leo, ameniambia anataka tuzungumze mawili matatu kuhusu mustakabali wa elimu yetu. Hivi najiuliza sijui niende ama nisiende manaake sijui huyu mzee na elimu yake ya UPE ataniambia nini, 'anyway ngoja nikamsikilize wakati mwingine hawa wazee wetu hata wasipoongea 'logic' lakini maneno yao yanakuwa na busara.

Mwalimu huyu mzee wangu alinifundisha historia zamani kwamba watanzania walipata uhuru mwaka wa 'alufu mia kenda sitini na moja'. Wakajikomboa japo kwa maneno ya mdomo lakini mkoloni akawaachia ardhi yao, akawaachia malighafi zao, akaawachia nguvu kazi zao, akawaachia mifugo yao, akawachia serikali yao, akawachia na wake zao, nikacheka nikamuuliza mwalimu kumbe mzungu alitawala na wake zao, mwalimu akaniambia mzungu hakuchagua cha kutawala, alitawala hadi mizimu yao akawadanganya watanzania kwamba dini zao za mizimu zimepitwa na wakati nao wakaiacha wakaanza kusali misalaba ndo maana mpaka leo hawana mwelekeo.

Mwalimu huyu enzi izo alikuwa na makamo ya kawaida lakini sasa amezeeka mpaka namwita babu. Siku moja aliwahi kunifundisha kuwa alikuwepo mwalimu mwingine ambaye hata yeye alimfundisha mambo mengi. Mwalimu huyo alikuwa na weredi mkubwa wa kufundisha hata wazungu wakati wanaondoka wakamwachia nchi nae hakuongoza bali aliwafundisha watu maisha hata wananchi wake kwa kumpenda wakaanza kumuita baba wa taifa.

Mwalimu huyu ndie aliyeikomboa elimu ya Tanzania kutoka kwenye mifumo ya kikoloni. Elimu ya kikoloni ilijaa mafunzo ya ulaya, ilisifia viongozi wa ulaya, ilisifia milima ya ulaya, ilisifia viwanda vya ulaya, ilisifia tamaduni za ulaya, ilisifia hata wanawake wa ulaya ndio maana hadi leo watu weusi wakioa, kuolewa na wazungu wanaona wamefika mbinguni. Hata waliosoma elimu hiyo walijiona wamekuwa wazungu, wakawa vibaraka wa wazungu. Lakini akaja mwalimu huyu mwenye asili ya 'mwafrika', mwenye akili za kiafrika akasema elimu ile haitufai watanzania, akaanzisha elimu ya kujitegemea. Lengo la mwalimu huyu lilikuwa ni kuwafundisha watanzania maisha halisi ya kiafrika, akaanzisha somo la kilimo akasema kila shule lazima iwe na shamba, wanafunzi wakajifunza kulima shuleni na walipomaliza shule hawakusubiri kamwe ajira za serikali. Mwalimu huyu akaanzisha somo la ufundi, wanafunzi wakajifunza ufundi shuleni, walipomaliza shule hawakusubiri wachina waje wawajengee barabara wakajenga wenyewe. Akaanzisha somo la sayansi ya kujikimu, wanafunzi wakasoma kufua, wakasoma upishi njaa ilipowashika hawakwenda kula hotelini, wakajipikia majumbani kwao wakala wakashiba, nguo zilipochafuka hawakuita madobi wala hawakupeleka makufuri yao kwenye 'draya', walifua wenyewe wakavaa wakapendeza. Huyu ndiye mwalimu pekee mwenye akili nyingi aliyewahi kuishi Tanzania.

Sasa ndio nafika kwa mwalimu wangu niwewaambia naenda kumsikiliza japo amezeeka, nimemkuta analia 'hi hii hiii' na mimi machozi yananitoka si unajua wazee wakilia wanatia huruma na waswahili wanasema 'ukiona mtu mzima analia ujue kuna jambo'. Mzee ananyamaza Namuuliza 'mwalimu unalilia nini? Ananiambia; 'kijana, mwanafunzi wangu...' Naitika naaam, anauliza 'yako wapi?? Yako wapi mwanangu??? Yako wapi masomo aliyoanzisha mwalimu??? Mbona mnalia hakuna ajira wakati hamjifunzi kilimo na ufundi??? Mbona wote mnataka kukaa ifisini??? Mbona mnasema kilimo kwanza wakati mnakaa mjini??? Mbona hakuna wataalamu wa kilimo, mnamwita 'agrikachuro ofisa' wakati anakaa 'darisalamu' analima nini huko??? Iko wapi sayansi kimu watoto hawajui kufua, kina mama wanapeleka makufuri yao kwenye 'draya' aibu hii tunaificha wapi??? Wanawake wanaolewa hawajui kupika, elimu hii inawafundisha nini??? Mbona hakuna mainjinia, wachina watawajengea barabara mpaka lini???? Yako wapi maarifa aliyowafundisha mwalimu....??????

Nimeshindwa cha kumjibu mzee, mwalimu wangu huyu nimeamua kurudi nyumbani huku nimeangua kilio; 'hiiiiiii hiiiii hiiii hii hihihihihihihihiii ghwejooooooo...'

Shared with https://goo.gl/9IgP7
 
Back
Top Bottom