Kwa muda mrefu nimekuwa nikimchukulia Dr Mwakyembe kama mwanasiasa aliye tofauti na wanasiasa wengine wengi ndani ya Chama cha mapinduzi japo utendaji wake kwenye nafasi yake ya uwaziri si ya kuvutia sana.
Kitu kimoja ambacho sikuwahi kukijua kuhusu huyu mheshimiwa ni juu ya tabia yake ya majivuno kutokana na usomi wake.Nilimshangaa sana jana kwa jinsi alivyokuwa anawasilisha hoja yake ya kutetea serikali mbili,Mheshimiwa Mwakyembe alitumia muda mwingi kuwakejeli akina Lissu na Jussa kutokana udogo wa umri wao na viwango vya elimu yao kuliko kujadili hoja zao.Ni dhahiri Dr Mwakyembe alikuwa amefadhaika sana kwa kuumbuliwa juu ya unafiki wake sasa akawa anatafuta namna jinsi ya kujinasua kutoka kwenye aibu ile,Kwa bahati mbaya sana alishindwa kuwahakikishia wenzie ndani ya Bunge kama kilichosemwa na wapinzani juu ya msimamo wake wa kuunga mkono muungano wa serikali tatu kwenye ile THESIS yake wakati ana-persue Ph.D yake nchini Ujerumani kama ni kweli ama la.Kusema kweli hakuna hoja ya maana Dr Mwakyembe aliyoiongea kupangua hoja za akina Lissu zaidi ya mashambulizi binafsi na majivuno.
Tukiachana na hayo ya utetezi wake wa kukana kwamba hakuwahi kuunga mkono muungano wa serikali tatu.Ebu tugeukie kwenye utetezi wa Dr Mwakyembe juu ya muungano wa serikali mbili.Hapa pia aliutumia muda mwingi kujisifia kuhusu usomi wake na kushiriki kuandika vitabu mbalimbali akishirikiana na wasomi wengine kama akina Prof Issa Shivji,Kweli rangi nyeusi inayoishi Afrika haiwezi kuacha asili yake ya ulimbukeni hata siku moja.Kwa namna ninavyofahamu wasomi wengi duniani ambao wamepata fursa wamefanya mambo makubwa sana kwenye jamii zao na ulimwnguni kwa jumla.Mfano Dr Carson,The NEURO SURGEON amefanya mambo makubwa kwenye kuboresha matibabu ya ubongo,Hawa ndiyo watu ambao hata wakijisifia kuwa wamesoma utakubaliana nao kwasababu wanastahili lakini kamwe hutawasikia akina Dr Ben Carson wakijisifia kuwa wao ni wasomi kuliko wengine isipokuwa matendo yao yanaongea mengi na hata kujizolea sifa lukuki ulimwenguni.
Nikirudi kwa wasomi wetu wa Afrika kusema kweli wanakera sana.Wao wanadhani kukusanya vyeti kutoka vyuo mbalimbali na kujifungia library kuandika vitabu wakitumia kazi za watu wengine ndiyo wamemaliza wajibu wao wa kulijenga Bara la Afrika.Leo Mwakyembe anaposimama pale Bungeni na kuanza kukejeli elimu za wenzake na kujisifia kwamba yeye amesoma sana kwakweli inasikitisha sana.Sisi hatukutaka kujua kuhusu elimu yake au kama aliandika vitabu,Tulichotaka kujua ni kama ni kweli aliunga mkono muungano wa serikali tatu kwenye THESIS yake wakati anasomea Ph.D yake nchini Ujerumani?Na jambo jingine tulilotaka kujua ni kwanini anatete muungano wa serikali mbili basi.
Tulichokishuhudia pale Bungeni ni Dr Mwakyembe kujaribu kutaka kupimana msuli na Lissu kwenye tasnia ya sheria,Kiuhalisia Dr Mwakyembe anatishwa na uwezo wa Lissu katika kuzichambua sheria na kwakuwa asili ya huyu mheshimiwa ni kutaka kujiona yuko ya wengine kwahiyo sehemu salama kwake ilikuwa ni kukimbilia kwenye Ph.D yake.Hakuna asiyejua kuwa Tundu Lissu amefanya mambo mengi ya kutukuka kwenye medani ya sheria hata kabla hajawa Mbunge.Lissu anazifahamu sheria za nchi hii practically.Nikija kwa mheshimiwa Mwakyembe sikumbuki aliwahi kufanya nini cha kukumbukwa katika nchi hii zaidi ya kushika chaki darasani.Nje ya taaluma yake ya ualimu hakuwahi kufanya jambo lolote la kujivunia.Kimafanikio kwenye medani ya sheria Lissu amefanya mambo mengi makubwa kuliko huyu mheshimiwa kwasababu Lissu amefanya kazi za uanasheria kwenye mahakama mbalimbali kwahiyo anafahamu vyema anachokipigania,Tofauti na Dr Mwakyembe ambaye anazifahamu sheria za nchi hii kinadharia zaidi.Natamani kumwona Dr Mwakyembe akisimama mahakamani akimtetea mtu au akitetea upandea wa pili halafu akashinda kesi,Mpaka atakapoanza kuyapata mafanikio ya kweli ya kutoa msaada wa kisheria kwa wengine kama afanyavyo Lissu ndipo tutakapoanza kumpa heshima anayotamani apewe.
Amepewa uwaziri wa mawasiliano na uchukuzi na sijaona kipya alichokileta kwenye sekta hiyo pamoja na kusoma kwake sana.Ifike wakati wasomi wa Afrika wabadilike sasa,Badala ya kukaa na kujisifia juu ya usomi wao ingekuwa busara kama wangeutumia usomi wao kuifanya Afrika sehemu bora ya kuishi duniani.Namsifu Tundu Lissu kwa kujaribu kufanya kile wasomi wengi wanashindwa kukifanya katika nchi hii,Nacho ni kusimama na wanyonge na kupambana na mfumo kandamizi unaowanyima fursa Watanzania kutimiza ndoto zao.Kwetu sisi Tundu Lissu ndiye msomi mwenye manufaa kwa nchi hii anayeitendea haki elimu yake na ndiye tunayemuamini na kumsikiliza zaidi kuliko hao wasomi wengine uchwara.