Muziki na siasa

John Kitime

Member
May 25, 2020
7
30
Joto la uchaguzi limeanza, wanasiasa wanapishana huku na kule wakitafuta njia za kuweza kuendelea kushiriki kwa namna moja au nyingine katika ngazi mbalimbali za uongozi wa kisiasa. Wanamuziki nao, wengine kwa upenzi wa kambi moja au nyingine ya kisiasa, au kwa kuona fursa ya kutengeneza fedha, nao wanapishana studio wakitunga nyimbo mbalimbali za kusifia vyama na wagombea wa nafasi za uongozi. Utamaduni wa kutunga nyimbo za kampeni za uchaguzi wa viongozi wa siasa, una historia ndefu kama historiaya uchaguzi wenyewe.

Kwa mfano katika nchi ya Marekani, nyimbo za kampeni zimekuweko katika kila chaguzi kuanzia mwaka 1840. Nyimbo za wakati huo zilikuwa na sifa za mgombea, zikitaja sifa zake kama alikuwa mkulima au alipigana vita fulani akashinda, na zilitaja hata jimbo alikozaliwa na sifa nyingine ambazo zilionekana zingemfanyamgombea apendeke kwa wapiga kura.

Katika miaka ya karibuni wagombea wamekuwa wakitumia nyimbo za wasaniimaarufu kuhamasisha uhudhuriaji wa mikutano ya kampeni na hata kupitisha ujumbe wa sera zao. Jambo hili limekuwa likileta mgogoro kati yawasanii na wagombea, baada ya baadhi ya wasanii kukuta wagombea ambao hawawaungi mkono wakitumia nyimbo zao.

Kadhia hii imemkuta sana Rais wa sasa wa Marekani Donald Trump. Trump amejikuta akikatazwa na wasanii mbalimbaliasitumie nyimbo zao kwenye kampeni zake. Wasanii kama Rihanna, Adele, R.E.M, Elton John, Guns N' Roses, O Jays,na wengine wengi walimpelekea katazo la kisheria Trump asitumie nyimbo zao kwenye kampeni zake.

Familia yamarehemu Luciano Pavarotti, aliyekuwa muimbaji mahiri sana wa muziki wa Opera, ilikataza nyimbo za marehemu kutumika kwenye mikutano ya Trump kwa maelezo ya kuwa sera za Trumpzilitofautiana na imani ya Luciano alipokuwa hai.

Trump pia amekuwa akitumia wimbo uitwao You can't get what you want wa kundi la Rolling Stones, bendi ya kutoka Uingereza, pamoja na kundi hilo kumkataza kutumia wimbo wao, Trump amekuwa akiendelea kutumia wimbo huo.

Katika nchi za Kiafrika, muziki wa kusifia au kukosoa viongozi upo katika historia ya nyakati mbalimbali. Zamaza enzi za utawala wa Machifu, ambapo uongozi ulikuwa ni koo fulani tu, nyimbo za kusifu na kumkosoa kiongozi
zilikuwepo katika jamii mbalimbali, japo kukosoa ilikuwa ni jambo la hatari, lakini watu walitunga nyimbo za aina hizo, ilikuwa ni aina fulani ya demokrasia katika jamii hizo.

Ujio wa wakoloni ukaleta aina mpya ya utawala na kuingiza dhana ya siasa ambayo ndiyo tunayoifuata sasa, baada yakuwaondoa wakoloni hao!!
Wakati wa kutafuta Uhuru toka kwa wakoloni, muziki ulitumika sana kutoa elimu, na kuhamasisha ari ya kumng'oa mkoloni.

Utawala wa kikoloni ulijua nguvu ya muziki, na kuna juhudi nyingi zilifanywa kuratibu sanaa hii ikiwemo kuanzisha sheria ya kutoa vibali kwa ajili ya shughuli za ngoma, ni jambo la kichekesho na kusikitisha kuwa miaka zaidi ya 50
baada ya Uhuru sheria hiyo ipo bado kwa namna moja au nyingine. Hakuna ubishi kuwa muziki ulikuwa nyenzo muhimu sana katika kuelimisha na kuunganisha watu kudai Uhuru hapa nchini.

Baada ya Uhuru muziki ulitumika katika kampeni mbali mbali, kama vile siasa, kilimo, elimu, afya na kadhalika, maelfu ya vikundi vya kwaya vilianzishwa kila kona nchini, hakika nyimbo zote za vikundi hivi zingeweza kurekodiwa, makataba yake ingekuwa kubwa sana.

Huko Kongo utamaduni wa wanamuziki kusifia viongozi ulishamiri zaidi wakati wa utawala wa Mobutu, mwaka 1971 Franco Luambo alitoa wimbo ulioitwa Tolanda Nzela Moko, wimbo huo ulitungwa na Franco na kupigwa na bendi
yake ya OK Jazz, ulikuwa maalumu kwa ajili ya kumsifia Mobutu Sese Seko ambaye mwezi Novemba 1970 alichaguliwa kuwa Rais wa Kongo kwa kipindi cha miaka saba. Wimbo huu ulikuja kuwa wimbo maarufu sana katika nchi za Afrika
Mashariki na Kati, na mpaka leo unapendwa na wapenzi wengi wa nyimbo za zamani.

Franco alifaidika sana na taratibu hizi za kumsifu Rais wake, japo kuwa pia alijikuta kwenye mgogoro mkubwa pale alipotunga nyimbo zilizoonekana kuwa zinampinga Mobutu, wimbo wa Lovumbu Ndoki ulisababisha atoroke nchi na kuhamia Kongo Brazaville kwa miezi kadhaa.

NYimbo nyingi za kampeni za uchaguzi zimekuja kufikia kupendwa hata baada ya chaguzi, kwa mfano nyimbo ya Vijana Jazz Band ya Ally Hassani Mwinyi apewe kura za ndio, ulikuwa maarufu kwenye majumba ya starehe, nyimbo kadhaa za Tanzania One Theatre kaa vile Nambari one, Hatunywi sumu na kadhalika ni mifano ya nyimbo za kampeni za siasa zilizokuja kupata umaarufu mkubwa na kuendelea kupendwa hata baada ya kampeni hizo za siasa. Kuna kitu kipya nakiona kwenye anga za muziki waleo ni kuwa wimbo ambaoumeshakuwa maarufu, unabadilishwa na kupewa mashairi ya kisiasa.

Zama hizi ni za vyama vingi, hivyo katika kipindi hiki cha uchaguzi, kutakuwa na nyimbo za kusifia vyama na wagombea tofauti, ushauri kwa wanamuziki ni kuwa baada ya uchaguzi hakikisheni kuwa viongozi mtakaowaimbia wakishinda
wawarudishie fadhila kwa kuhakikisha mazingira stahiki ya kazi zenu yanalindwa kisheria. Inasikitisha pale mwanamuziki unapotumia muda mwingi kumpigia debe kiongozi na akishachaguliwa, kazi yako ananza kuiita ni kelele kwa wananchi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom