Muungano sasa uwe wa Mkataba, si wa Katiba

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
DSC02654-564x272.jpg


Wazanzibari wakiwa katika mjadala wa wazi kuhusu mchakato wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwa katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA)

Na Ahmed Rajab

KUNA sababu moja kuu inayowafanya Watanzania waukaribishe kwa msisimko mwaka mpya wa 2012. Nayo ni kwamba, mwakani ndipo suala la Katiba mpya ya nchi hiyo litapoanza hasa kutokota. Hatuhitaji wapiga ramli kutwambia kwamba mwaka ujao hilo ndilo litalokuwa suala kubwa la kisiasa nchini Tanzania.

Kwanza kuna wenye kuupinga Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011 kama ulivyo hivi sasa. Wanahoji kwamba muswada huo una taksiri kadha wa kadha ambazo zitazuia isipatikane Katiba iliyo halali na itayotungwa kwa kuwashirikisha vilivyo wadau wote wanaostahiki kushirikishwa.

Miongoni mwa wapinzani hao ni asasi za kiraia ambazo zitaendelea kuupinga muswada huo kwa hamasa kuu na wataishtaki Serikali mahakamani katika jaribio la kuuzuia. Wakishinda mahakamani watakuwa wamepata mradi wao.

Wakishindwa wataendelea kuwa nguvu ya kutosha itayoweza kuwashawishi wananchi waikatae Katiba itayoibuka baada ya kumalizika kwa mchakato wake.

Hata hivyo, wakati wa mchakato wa kuipitia upya Katiba wanasiasa wa Tanganyika na viongozi wao watakabiliwa na hali wasiowahi kukutana nayo kabla. Kwa mara ya kwanza huko Zanzibar, kuna mjadala mkubwa unaoendelea ndani na nje ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuhusu mustakabali wa visiwa hivyo.

Hilo ni jipya kwani hapajawahi kutokea hali kama hiyo kabla. Tena majadiliano hayo si ya kulazimishwa bali ni ya hiari na Wazanzibari wanatoa maoni yao kwa uhuru kamili. Wanafanya hivyo wakitambua kwamba fursa waliyonayo sasa huenda wasiipate tena.

Wanaelewa vyema umuhimu wa kuwa na msimamo mmoja ili waweze kuigomboa nchi yao. La sivyo, wakichezacheza na wasipoungana kifikra basi fursa hiyo inaweza ikawaponyoka, wakajikuta wamekwenda kape. Katika hayo majadiliano kuhusu mustakabali wa Zanzibar suala la Muungano ndo jambo kubwa linalozungumzwa Visiwani. Muungano unajadiliwa mijini, vijijini na kwenye vitongoji Unguja na Pemba.

Ukiwasikiliza wananchi wa huko utawasikia wanataka irejee Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, ikiwa ni dola kamili iliyo huru ikiwa na funganisho na Tanganyika pamoja na nchi nyingine za eneo hili. Tofauti ya mahusiano yaliyopo sasa na hayo wayatakayo ni kwamba wangependelea huo mfumo mpya wa mahusiano ya kufungamana uwe wa mikataba na si wa Katiba.

Msimamo huo ni sehemu ya ile iitwayo Ajenda ya Zanzibar niliyowahi kuizungumzia miezi kadhaa iliyopita. Ni ajenda inayopigiwa debe na wengi wa Wazanzibari wakiwa pamoja na viongozi wao kutoka vyama tofauti vya kisiasa.

Wengi wao wanaamini kwamba kutokana na Hati za Muungano na mambo mengine yaliyoingizwa kuwa ni ya Muungano rais wao amepungukiwa na madaraka. Na si yeye tu bali pia na baraza lao la kutunga sheria (Baraza la Wawakilishi) na Mahakama yao. Mamlaka ya taasisi zote hizo tatu za Zanzibar, ambazo ni mihimili mikuu ya dola, yamepunguzwa katika kipindi cha miaka 47 ya Muungano.

Kilichotokea ni kwamba kwa muda wote huo unaokaribia nusu karne mamlaka au madaraka yote ya Zanzibar yaliyo muhimu yamehaulishwa Tanganyika. Ujanja ulitumika kulifanya Bunge la Tanganyika liwe Bunge la Muungano na kuigeuza Katiba ya Tanganyika iwe Katiba ya Muungano. Ujanja vilevile ulitumika kuifanya Serikali ya Muungano iwe ndiyo Serikali ya Tanganyika na ya Tanganyika iwe ya Muungano. Shughuli za Jamhuri ya Muungano ya Tanzania na za Jamhuri ya Tanganyika zimekuwa zikiendeshwa na Serikali moja.

Kwa upande mwingine, Zanzibar na Serikali yake hazina jukumu kubwa au la maana katika utawala na uongozi wa Muungano. Ingawa kwa mujibu wa Sheria za Kimataifa na kwa mujibu wa Hati za Muungano, Zanzibar na Tanganyika ni washirika wenye hadhi sawa ndani ya Muungano, mambo yanavyokwenda ni kwamba Zanzibar imewekwa kando.

Zanzibar imetoweka hata kutoka kwenye ramani ya dunia na haina jukumu lolote la maana katika shughuli za eneo letu la Afrika Mashariki au la Afrika au ulimwenguni kwa jumla. Wala Zanzibar haipati manufaa yoyote inayopata nchi yenye kushiriki katika uchumi wa dunia; isitoshe, hairuhusiwi kujihusisha na taasisi za kimataifa.

Hii leo wanasiasa wa Tanzania Bara hawawezi tena kuyapuuza manung'uniko na matakwa ya Wazanzibari kwa sababu wamekwishatanabahi kwamba Muungano kwa namna ulivyo sasa, uko kwenye njia panda na wakati umefika wa kufanya uamuzi muhimu kuhusu mustakabali wake.

Kwa sasa hakuna anayeweza kutabiri nini yatakuwa matokeo ya mchakato wa kuiandika upya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania. Ingawa hakuna jedwali rasmi lililowekwa, inavyoonyesha ni kwamba kabla ya Juni 2012 Wazanzibari watapata fursa ya kutoa maoni yao pale Tume ya Kuichunguza Katiba au wawakilishi wake watapozitembela shehia za Unguja na Pemba.

Hii si mara ya awali kutungwa Katiba ya Muungano wa Tanzania. Tofauti kubwa iliyopo ni kwamba safari zilizopita Wazanzibari na wawakilishi wao ama hawakushauriwa ipasavyo au walijikuta wanayakubali bila ya upinzani wowote, matakwa ya Tanzania Bara.

Mnamo miaka ya 1990 palitolewa pendekezo la kutaka pawepo na mfumo wa serikali tatu, yaani Serikali ya Tanganyika, ya Zanzibar na ya Muungano. Waliopendekeza hivyo waliamini kwamba mfumo huo wa serikali tatu ndio ulio bora na utaokubaliwa na washirika wote wawili, yaani Tanganyika na Zanzibar.

Kwa hakika, baadhi ya wanasiasa mashuhuri wa Tanganyika nao walifanya jaribio la kuifanya nchi yao iwe na serikali yake ndani ya Muungano. Jaribio hilo halikufika mbali kwani Mwalimu Julius Nyerere alitumia nguvu zake za turufu na kulizima suala hilo.

Pendekezo hilo liliibuka tena lilipotolewa kwa mara nyingine na Tume ya Muungano iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Robert Kisanga. Rais wa Muungano wa wakati huo, Benjamin Mkapa naye alilipinga. Hatujui ikiwa huo ndio mwisho wa pendekezo hilo au iwapo Serikali ya Muungano italikubali kuwa njia murua ya kuunusuru Muungano usiporomoke.

Iwapo Serikali ya Muungano hatimaye italikubali pendekezo hilo hatujui kama Wazanzibari nao wataliridhia kwa vile pendekezo hilo ukiliangalia kwa undani haliipi nchi yao uhuru wake kamili bali linauwekea mipaka. Muungano huo wa serikali tatu utakuwa Muungano utaojengwa juu ya misingi ya Katiba na si mkataba.

Ndio maana siku hizi huko Zanzibar mazungumzo kuhusu Muungano ni ya kutaka serikali mbili. Wazanzibari wengi wanahisi kwamba ule mfumo wa serikali tatu za Muungano umekwishapitwa na wakati. Wanapotoa hoja zao wanasema kwamba mfumo huo labda ungekubalika katika miongo iliyopita lakini si mnamo mwaka 2015.

Hata wale wenye kuunga mkono mfumo wa serikali tatu sasa wanasema kwamba ile serikali ya tatu, yaani ya Muungano, isiwe na mamlaka mengi kwani wanachotaka ni Zanzibar kuwa na uhuru zaidi ndani ya mfumo mpya wa Muungano.

Hao Wazanzibari wenye kutaka Muungano utaoundwa juu ya misingi ya Mkataba na sio Katiba wanahoji kwamba mfumo wa Muungano wa Mkataba ndio ufaao kwa mataifa yaliyo huru. Wanaendelea kuhoji kwamba hakuna haja ya kuwepo Serikali ya Tanzania. Badala yake, wanasema, pawepo Tume Maalumu ya Muungano itayokuwa na nguvu hafifu au mamlaka machache na itayosimamia vifungu vya Mkataba wa Muungano.

Mfano wanaoutaja mara kwa mara ni ule wa Tume ya Muungano wa Ulaya. Wanataka Muungano wao uwe mithili ya ule wa Ulaya ambao umeundwa kwa mikataba ya kimataifa kati ya nchi 27 zilizo huru. Majaribio ya kutaka pawepo Katiba moja ya Muungano huo yalikataliwa pale palipofanywa kura za maoni katika baadhi ya nchi wanachama. Hii ni kwa sababu kwa mujibu wa Muungano huo kila nchi ina kura ya turufu, na inaweza kujivuta na kujitoa kutoka kwenye Muungano kwa vile maamuzi yote makuu hukatwa kwa nchi kukubaliana.

Wazanzibari wenye kuupigania mfumo huo wanasema kwamba mfumo huo si kwamba unazifaa nchi za Zanzibar na Tanganyika tu bali pia ni mujarab kwa bara zima la Afrika. Bara hilo nalo linahitaji kuwa na chombo kitachoziunganisha nchi zake zote kwa maslahi ya nchi wanachama.

Kuna jambo moja tu lenye uhakika katika mchakato wa kuiangalia upya Katiba ya Muungano. Nalo ni kwamba hatima ya Muungano itategemea sana juu ya kura ya maoni. Watanganyika na Wazanzibari wataulizwa iwapo wanaidhinisha na kuiunga mkono au wanaipinga Katiba mpya ya Muungano. Jibu litalopatikana ndilo litaloamua kama Muungano utadumu ama la na ikiwa utadumu utakuwa na umbo au sura gani.

CHANZO: RAIA MWEMA
 
..that sounds like a plan.

..bora tushirikiane kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki.

..actually kutokana na tabia ya Wazanzibari kulalamika kila wakati, napendekeza Tanganyika isiwe na any bilateral agreement na Zanzibar.

..njia ya ku-deal na Zanzibar ni kuhakikisha uhusiano au mkataba wowote ule baina yetu na wao unahusisha nchi 3,4, na kuendelea.
 
Back
Top Bottom