pageup
Senior Member
- Oct 12, 2012
- 156
- 59
28/11/012
WATOTO saba wamenusurika kuuawa kwenye hospitali ya wilaya ya Chato mkoani Geita baada ya mhudumu wa afya Maliagoreth Kyaruzi kuwanyofolea maji yenye dawa (drip) wagonjwa waliolazwa kwenye wodi ya watoto kwa madai kuwa ndugu zao walikataa kufanya usafi wa vyoo vya hospitali hiyo.
Watoto walionusurika na vifo hivyo ni Edward Robert (4), mkazi wa kijiji cha Nyamirembe; Kashinje Lukanya (12), mkazi wa Busaka; Irene Nasib (3), mkazi wa Bwanga; Naomi Tumain (5), mkazi wa Kachwamba; Eunice William (3), mkazi wa Kasala; Astelia Siajali (2), mkazi wa Kahumo; na Alphonce Makolobelo.
Tukio hilo la kusikitisha limetokea jana majira ya saa 2:30 asubuhi baada ya mhudumu huyo wa afya kuwataka ndugu wa wagonjwa wote walilazwa kwenye wodi ya wanawake na watoto, kwenda kufanya usafi wa vyoo kutokana na kuwepo kwa uchafu unaodaiwa kusababishwa na wagonjwa wenyewe.
Wakizungumza na Tanzania Daima Jumatano, baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo William Masai na Ester Misungwi kwa nyakati tofauti, walisema kuwa hatua hiyo ilikuja baada ya ndugu wa wagonjwa kukaidi amri kwenda kufanya usafi kwenye vyoo vya hospitali hiyo.
Baada ya wananchi hao kukaidi amri hiyo, mhudumu huyo kwa hasira aliamua kunyofoa maji yenye dawa waliyokuwa wameninginiziwa wagonjwa kwa ajili ya matibabu kisha kuondoka kwa majigambo, huku akiwataka watu walioumizwa na kitendo hicho, wakashtaki mahala popote ambapo wangeliona panafaa.
Hatua hiyo iliwalazimu baadhi ya ndugu wa wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo, kuutafuta uongozi wa hospitali kabla ya kuwasiliana na Katibu wa Mbunge wa jimbo la Chato, Gelvas Stephano, ambaye naye alizungumza na Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ambaye alifika eneo la tukio akiwa ameongozana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Waziri Magufuli alilazimika kuzungumza na wagonjwa na watumishi wa afya kwa lengo la kusikiliza kero zao muda mfupi baada ya kumaliza kujionea hali halisi ya watoto walionyofolewa drip za dawa kisha kurejeshewa.
Kutokana na malalamiko mengi yaliyotolewa na wagonjwa kuhusu vitendo vinavyofanywa na mhudumu huyo, Waziri Magufuli amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuhakikisha wanamtafuta na kumkamata na kumfikisha mahakamani.
Bahati nzuri mkuu wa wilaya yupo hapa na OCD na wewe upo hapa, ninaagiza huyo Maliagoreth akamatwe mara moja na kesho afikishwe mahakamani kujibu tuhuma za kutaka kuua wagonjwa saba kwa makusudi, alisema Waziri Magufuli.
Nasema huyo siyo mhudumu anayetakiwa kufanya kazi ya afya maana kuwanyofolea drip wagonjwa kwa kosa la ndugu zao kukataa kufanya usafi wa vyoo haliwezi kufumbiwa macho, huyo Maliagoreth hafai na ninaomba kuanzia leo asikanyage hapa kwenye hospitali kuja kuhudumia wagonjwa maana ipo siku hata mimi ataninyofolea drip, alisema Magufuli na kushangiliwa na wagonjwa.
Kadhalika Magufuli aliwataka waganga na wauguzi wengine kutoa huduma nzuri kadri inavyopaswa na kuwatahadharisha iwapo watawahudumia wagonjwa vibaya kwa lengo la kulipiza kisasi kwa madai wagonjwa wamewashtaki itakuwa ni kutowatendea haki wagonjwa.
Vilevile alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Shaban Ntarambe, kuhakikisha anamsimamisha kazi mara moja nesi huyo kwa madai kuwa hana sifa za kuendelea kuwa mtumishi kwenye wilaya ya Chato.
Mkuu wa wilaya ya Chato, Rodrick Mpogolo, mbali na kudai kusikitishwa na tukio hilo ameahidi kuunda tume kuchunguza utolewaji wa huduma za afya kwa wananchi kutokana na kuwapo kwa malalamiko mengi.
Aidha alisema nia ya serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora na kwamba dosari zinazojitokeza atahakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kusijitokeza vitendo kama vilivyojitokeza.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa hospitali ya wilaya hiyo, Dk. Pius Buchukundi, amekiri kutokea tukio hilo na kudai kuwa kitendo kilichofanywa na mhudumu wake siyo msimamo wa hospitali bali ni matakwa yake mwenyewe na kwamba atahukumiwa kwa matendo aliyoyatenda.
Dk. Buchukundi amewataka wagonjwa kutoa ushirikiano kwa uongozi wa hospitali hiyo kwenye matukio ya aina hiyo na mengine yanayoweza kuathiri sifa za hospitali na serikali.
Source: Tanzania Daima