Muuaji mwenye tai nyekundu

Kanungila Karim

JF-Expert Member
Apr 29, 2016
20,744
25,446
Image may contain: 1 person

Mlipuko wa bomu unatokea katika sherehe ya kumpongeza Kamishina wa Jeshi la Polisi, Ibrahim Miraji baada ya kuteuliwa na rais kuchukua nafasi hiyo.

Hapo nyumbani kwake kwenye sherehe hiyo kuna viongozi wengi wa polisi akiwemo IGP Godlove. Mlipuko huo unammaliza Miraji na mkewe tu.

Ukiachana na vifo vya wawili hao, kuna watu wengi wakijeruhiwa na hivyo kukimbizwa hospitalini. Miongoni mwa majuruhi hao alikuwepo mke wa Dilunga, Aisha.

Dilunga alikuwa Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi, yaani akitoka Miraji kwa cheo anafuata yeye. Mwanaume huyo anachanganyikiwa, anamchukua mke wake na kumpeleka hospitali huku akiwa na majeraha makubwa mwilini mwake.

Baada ya kukaa kwa siku mbili, anaambiwa kwamba mkewe alimeuawa hospitalini kwa kuchomwa sindano iliyokuwa na sumu.
Hilo linamuuma na kwa maelezo ya mlinzi aliyewekwa hapo, anasema muuaji alivalia shati jeupe, tai nyekundu na koti la kidaktari.

Dilunga hakubali, anaamua kumtafuta muuaji kwa nguvu zote. Huku akiendelea kusisitiza lazima muuaji apatikane, anapokea taarifa na kuambiwa mkubwa wa polisi mwingine, Dikwe ameuawa nyumbani kwake huko Kibaha, na muuaji alivalia shati jeupe na tai nyekundu, yaani ni muuaji yuleyule ambaye alimuua mkewe kitandani.

Hapo ndipo msako rasmi unaanza, Muuaji Mwenye Tai Nyekundu anaanza kusakwa kila kona pasipo kugundua kwamba angeendelea kuwamaliza viongozi wa jeshi la polisi kila alipojisikia kufanya hivyo.

Kitabu kinapatikana kwa sh. 10000 kwa wakazi wa Dar na 15,000 kwa watu wa mikoani. Kumbuka kwamba hiyo 5000 ni gharama ya kusafirisha kitabu kikufikie.

Mawasiliano: 0718069269.


@chilojr
 
SURA YA KWANZA.

“PUUUU....!!!!” Ulisikika mlio mkubwa wa bomu, watu waliokuwa nyumbani kwa Kamishina wa Polisi, Ibrahim Miraji iliyokuwa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam wakaanza kukimbia huku na kule.

Kelele za majeruhi zikaanza kusikika kutoka mahali hapo huku moto mkubwa ukiwaka katika kila eneo la uwanja wa nyumba hiyo.

Watu waliokuwa mbali wakaanza kusogea kujua ni kitu gani kilitokea, kila mmoja alishtushwa na hali hiyo kwani mlipuko huo wa bomu ulikuwa mkubwa kiasi kwamba hata wale watu waliokuwa umbali wa mita elfu mbili waliusikia vizuri kabisa.
Kila kitu kilikuwa kimeharibiwa, majeruhi walikuwa chini, kila mmoja alikuwa akiomba msaada kwa watu ambao walianza kujitokeza mahali hapo.

Nyumba hiyo ilikuwa kwenye hali mbaya, kwa kiasi kikubwa ilishambuliwa kwa bomu hilo ambalo hakukuwa na mtu aliyejua ni nani ambaye alilitega ndani ya uwanja wa nyumba hiyo ambapo kulikuwa kukifanyika sherehe ya kumpongeza Miraji kwa kuteuliwa na kuwa Kamishina wa Polisi (CP)

Polisi walikusanyika kwa wingi, kila mmoja alikuwa na furaha na kumpongeza Miraji kwa uteuzi huo ambao kwake ulionekana kama ndoto kwani kipindi cha nyuma alitamani sana kuwa na cheo hicho na mwisho wa siku, alifanikiwa kuchaguliwa na hatimaye kutakiwa kuanza kukitumikia.

Furaha hiyo iligeuka na kuwa majonzi makubwa. Miraji alikuwa pembeni kabisa, alitulia pale alipokuwa amelala, mwili wake uliunguzwa vibaya na moto uliokuwa umesababishwa na bomu hilo ambalo liliwafanya watu wengi kushangaa kwamba ni kwa namna gani kungekuwa na mtu ambaye alikuwa na uwezo wa kufika nyumbani kwake hapo na kutega bomu hilo.

Kwa jinsi ilivyoonekana, mtegaji wa bomu hilo alionekana kufahamu kila kitu kuhusu mazingira ya hapo kwani pale ambapo kulitegwa bomu ni karibu sana na mahali Miraji alikaa na mkewe.

Watu wakaanza kujazana, kila mmoja alihitaji kufahamu ni kitu gani kilikuwa kimetokea. Wale ambao walikuwa na majeraha madogo wakaanza kuwasaidia wengine kwa kuwachukua na kuwapandisha kwenye magari yao na kuondoka mahali hapo kuwawahisha hospitalini kupata matibabu.

“Mke wangu...mke wanguuu...” alisikika mwanaume mmoja aliyekuwa amesimama pembeni kabisa.

Alionekana kushtushwa na kile kilichokuwa kimetokea, pale aliposimama alishika kichwa chake, ni kama alipigwa na butwaa juu ya hali ilivyobadilika kwa sekunde chache tu.

Huku akionekana kuchanganyikiwa, akaanza kupiga hatua na kuelekea mahali ambapo aliamini kwamba huyo mke wake alikaa, alianza kuangalia hapa na pale, aliipita miili yote mpaka alipoufikia mwili wa mwanamke mmoja uliokuwa umejeruhiwa vibaya na kuuinamia.

Alilia kama mtoto, kile alichokiona kilimuumiza moyo wake, machozi yalikuwa yakimbubujika mashavuni mwake, alionekana kuwa na maumivu makali kuliko mtu yeyote aliyekuwa hapo.

Mke wake huyo alikuwa akihema kwa mbali, mwili wake ulitapakaa damu na kwa jinsi alivyoonekana, hakuonyesha matumaini ya kuendelea kuishi,

Mbali na mwanamke huyo, pia kulikuwa na watu wengine waliokuwa wameumizwa vibaya, watu waliwasogelea na kuwachukua, wakawaingiza ndani ya gari na kuanza kuondoka nao pia.

Kila mmoja alishangaa, kwao, hapakuwa na aliyeamini kama sherehe ile ingebadilika na kuwa kilio kama ilivyokuwa. Lilikuwa ni tukio lililoshtua sana, katikati ya sherehe ya kumpongeza Miraji kwa kuteuliwa na rais kuwa Kamishina wa Polisi (CP), mlipuko wa bomu ulitokea.

Ndani ya gari mwanaume yule ambaye alikuwa akimlilia mke wake alikuwa naye kwenye kiti kimoja huku akiendelea kumwamsha mke wake, aamke na kumwangalia tena kwani kila kitu kingekuwa salama, asingeweza kufa, angeishi naye kwa miaka mingine mingi.

Mwanamke huyo alikuwa kimya, hakutingisha kiungo chake chochote cha mwili wake kile mpaka gari lilipoingia hapo hospitalini.

Haraka sana machela kadhaa zikasogezwa na kupakizwa majeruhi wale. Mwanaume yule hakukoma, bado alikuwa akiendelea kumuita mke wake kwa kuamini angeyafumbua macho yake na kumwangalia tena.

“Mke wangu! Naomba usiniache...naomba usiniache...” aliendelea kusema huku kilio kikiongezeka mdomoni mwake.
Machela iliyombeba mke wake ikasukumwa mpaka ndani ya chumba kimoja kilichoandikwa Theatre na kuambiwa abaki nje kwenye benchi lililokuwa nje.

Hakukaa, alisimama huku akitembea huku na kule kiasi kwamba kila mtu aliyemuona, alimuonea huruma mno.

Mwanaume huyo aliitwa Samuel Dilunga, alikuwa mmoja wa polisi waliokuwa wakiaminiwa sana kutokana na utendaji wake wa kazi.

Katika maisha yake ya kazi hiyo, alikuwa mchapakazi, alipambana usiku na mchana kuhakikisha analisafisha jeshi la polisi kwa kufanya kazi kwa uweledi mkubwa.

Dilunga alikubalika kila kona, watu walimwamini kiasi kwamba alipendekezwa kuchukua nafasi ya Ukamishina wa Polisi(CP) katika jeshi la polisi lakini kwa kuwa Miraji alionekana kuwa bora zaidi, akateuliwa kuchukua nafasi hiyo kutoka katika nafasi ya Ukamishina Msaidizi wa Polisi(ACP).

Wakati bomu likilipuka mahali hapo, yeye alikuwa chooni akijisaidia, alimuacha mke wake kwenye kiti. Alipokuwa huko, akasikia mlio mkubwa wa bomu nje kitu kilichomfanya kuogopa, akatoka harakaharaka kwani kwa jinsi mlipuko ulivyosikika, hakuwa na uhakika kama kungekuwa na mtu amepona.

“Mke wangu!” alijisemea chooni baada ya kusikia mlio wa bomu hilo.

Hakuamini kama kitendo cha kwenda kwenye sherehe ile kingemfanya kuwa katika hali ya majonzi kama aliyokuwanayo. Aliumia mno na wakati mwingi alijisemea kufanya kosa kubwa kwenda na mkewe katika sherehe hiyo.

“Kwa nini nilikwenda na mke wangu? Aliniambia anaumwa, ila nikamkazania kwenda naye, kwa nini?” alijiuliza huku akiendelea kububujikwa na machozi ambayo yalitiririka mpaka mashavuni mwake.

Machozi yake mengi, kulia kwake, huzuni yake, kuumia kwake, vyote hivyo havikuweza kubadilisha hali halisi juu ya kile kilichotokea, bado mke wake aliendelea kuwa kitandani akiutetea uhai wake kwa nguvu zote.

Pale alipokaa, alisubiri kwa saa tano, mlango wa chumba kile haukufunguliwa, madaktari walikuwa wakiendelea kupambania uhai wa mke wake aliyekuwa amejeruhiwa vibaya.

Madaktari hao walitoka majira ya saa nane usiku na kumwambia alitakiwa kuondoka kwani kwa siku hiyo asingeweza kumuona mke wake mpaka mchana wa siku inayofuata kwa sababu hakuwa kwenye hali nzuri kabisa.

“Unatakiwa kuondoka, kwa leo hutoweza kumuona mke wako,” alisema daktari aliyeitwa James Mchana huku akimwangalia Dilunga usoni, kwa jinsi alivyolia sana, macho yake yalivyovimba, hata yeye mwenyewe alijisikia uchungu moyoni mwake.

“Ninataka kumuona mke wangu dokta,” alisema Dilunga huku akimwangalia daktari kwa macho ya kuomba sana.

“Kwa leo! Haiwezekani!” alisema daktari huku akimwangalia mwanaume huyo aliyevalia sare za jeshi la polisi huku akiwa na nyote za kutosha.

Hakuwa na hamu ya kuondoka hospitalini hapo lakini kwa sababu daktari alimwambia alitakiwa kuondoka, alitakiwa kufanya hivyo haraka.

Ni ndani ya dakika kadhaa, waandishi wa habari wakafika mahali hapo, walihitaji kujua kilichotokea, kila aliyesikia kulikuwa na bomu lililokuwa limelipuka nyumbani kwa Miraji alishangaa, ilikuwa ni vigumu kwa bomu kutegwa mahali hapo kwa kuwa kuliaminika kuwa na ulinzi mkubwa, na kubwa zaidi ni kwamba siku hiyo kulikuwa na viongozi wengi wa jeshi la polisi akiwemo IGP mwenyewe.

Miraji na mkewe ndiyo walikuwa watu pekee waliofariki dunia katika sherehe hiyo huku watu wengine wakijeruhiwa vibaya. Watu hao waliojeruhiwa kidogo alikuwemo IGP aliyeitwa Godlove Gideon, Mrakibu wa Polisi (SP) Awadhi Salumu, Sajini Meja wa Polisi (RSM) Bupe Christopher na Kamishina Msaidizi na Mwandamizi wa Polisi (S.A.C.P) Jackson Dikwe na watu wengine wachache.

Hao wote waliletwa hospitalini hapo, walikuwa na majeraha madogo tu. Walichukuliwa na kupewa huduma na madaktari waliokuwa hapo na baada ya kumaliza, wakaruhusiwa na kumfuata Dilunga na kuanza kumpa pole.

“Dilunga! Pole sana,” alisema Awadhi huku akimwangalia Dilunga aliyekuwa amesimama pembeni ya Dk. Mchana ambaye alimtaka kwenda nyumbani kupumzika.

Hakuitikia, alimwangalia rafiki yake huyo, bado alikuwa na majonzi moyoni mwake, hakupoa, suala la mke wake lilikuwa kubwa mno, asingeweza kupata faraja kwa urahisi kama ilivyoonekana.

Wote hao wanne walimfariji lakini hakufarijika, wakaamua kutoka ndani kwa lengo la kuondoka. Waandishi wa habari ambao walifika hapo kwa lengo la kuwahoji, walizuiliwa na polisi kadhaa, hawakutakiwa kuwasogelea kwani mambo yalionekana kuharibika kabisa, kulikuwa na hali ya hatari kila kona.

Wote watano wakaingia ndani ya gari na kuondoka huku Dilunga akionekana kuwa kwenye hali ya majonzi kupita kawaida.
Upande wa pili, tukio la kulipuka kwa bomu hilo nyumbani kwa Miraji na kumuua yeye na mkewe ilikuwa stori kubwa kwa usiku huo.

Kila kona nchini Tanzania kulikuwa na maswali mengi kuhusu tukio hilo, lilikuwa moja ya matukio makubwa kutokea mwaka huo, yaani kila kona watu walikuwa wakilizungumzia hilo tu.

Kwenye mitandao ya kijamii kila mmoja alihoji, lilikuwa jambo lisilowezekana kwa bomu hilo kulipuka katika sherehe iliyowakutanisha viongozi kadhaa wa jeshi la polisi Tanzania, yaani kwa kulipuka kwa bomu hilo kulimaanisha Tanzania haikuwa salama, kama viongozi wa polisi walilipuliwa kwa bomu, vipi kuhusu wao wananchi?

“Polisi tu wamelipuliwa! Vipi kuhusu sisi?” aliuliza mwanaume mmoja kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, watu wengi walitoa mawazo yao na jambo kubwa lililogundulika ni kwamba Tanzania kwa kipindi hicho hakukuwa na ulinzi wa kutosha.
Habari hiyo ilitangazwa kwenye kila chombo cha habari. BBC, AlJazeera, Dotch Welle na vyombo vingine vya kimataifa walikuwa wakitangaza kuhusu habari hiyo, lilikuwa tukio la kushangaza ambalo liliibua maswali mengi vichwani mwa watu wengi.

“Ilikuwaje?” hilo ndilo swali ambalo kila mmoja alijiuliza, mbaya zaidi, hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa na jibu lolote lile.

Kumbuka kitabu kinaendelea kupatikana kwa sh. 10,000/= kwa wakazi wa Dar na 15,000/= kwa watu wa mikoani wakiwemo Zanzibar.

Wasiliana nami kwa namba 0718069269.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom