MUUAJI MWENYE BARAKOA - 27
Sultan Uwezo

+255
Kuulizwa maswali mengi kulimfanya kijana huyu kuondoka sehemu hii akiamini kuwa kuelezea tukio hili kwa mtu asiyemfahamu ni kujitengenezea ushahidi mbele ya vyombo vya sheria. Lilifika gari maalum ambalo lilizichukua pikipiki zile na kuondoka nazo huku maafisa wa Jeshi la Polisi wakiendelea kukusanya taarifa za ajali ile kutoka kwa mashuhuda wa tukio.
"Nikiwa nimesimama naongea na simu nilisikia mlio nyuma yangu ambao ulinifanya nikatishe kuongea na simu nikakimbia kuja lakini cha ajabu nilimshuhudia mmoja wa watu ambao bila shaka alikuwa ni dereva wa moja ya pikipiki akiifuata pikipiki ile ya rangi nyeusi na kumuinua dereva wake akaondoka naye na hawakufika hatua hata tatu ilitokea taxi iliyowabeba na kuondoka kasi." Shuhuda huyu alielezea.
" Hukuweza kumtambua mmoja wao kati yao wawili?"
" Ningewafahamu vipi wakati nilikuwa nafanya yangu ndipo niliposikia kishindo cha ajali hii lakini Taxi iliyowachukua ilielekea upande huu." Shuhuda huyu alionesha upande wa kulia wa barabara. Maafisa hawa waliendelea kukusanya taarifa za ajali hiyo ambayo iliwachanganya sana kutokana na waliokuwa wakiendesha kutopatikana eneo la tukio.
" Vipi umeambulia chochote ulikopita wewe? Maana mimi bado naona chenga chenga tu sioni picha halisi." Afisa mmoja alimuuliza mwenzake wakiwa wameegemea gari lao wakipitia taarifa zao.
"Inaonekana hii ajali iliandaliwa na mmoja wao na ndiyo maana hata baada ya kutokea aliinuka haraka akamfuata mlengwa na kuondoka naye kwa usafiri ambao aliuandaa." Mwenzake naye alitoa ufafanuzi wake kutokana na kile alichokipata kwa mashuhuda.
"Inspector Oso naanza kuipata picha hapa, inavyoonekana mtekaji alishaandaa mazingira ya kufanikisha zoezi lake na ndiyo maana gari lililowabeba lilikuwa linasubiri hapa."
"Naanza kukuelewa hebu twende eneo la tukio tukauchore mchoro pale pale." Inspector Oso alimwambia mwenzake na kuelekea katikati ya barabara.
Baada ya kufika pale katikati waliuchora mchoro wao wa namna ajali ilivyotokea na mpaka kupelekea mtekaji kufanikisha zoezi lake bila kutambulika.
" Hapa mtekaji alitumia akili kubwa sana kitu kinachovutia zaidi ni namna gani aliweza kupenya katikati ya wanashiriki wa shindano bila kushtukiwa? Hivyo ninachokiona hapa ni kwenda kuwahoji waandaaji wa mashindano haya wanaweza kuwa na majibu ya maswali yetu." Mmoja wa Maafisa ambaye alikuwa ndiye kiongozi wa zoezi hilo alitoa wazo ambalo waliona lina mashiko hivyo walirudi kwenye gari na kuondoka kuelekea chuoni.
***
Alifungua macho yake na kujikuta akiwa kafungwa kamba kwenye vyuma vilivyo ndani ya chumba chenye giza na alipojaribu kujitingisha mikono yake akajikuta akichomwa na vitu vyenye ncha kali.
"Niko wapi hapa?" Jennifer aliuliza swali ambalo lilimfikia moja kwa moja Catherine ambaye alikuwa akiongea na simu nje ya chumba hicho na kumfanya kurudi ndani.
"Ooh Malkia umezinduka? Karibu sana kwenye dunia ya giza." Sauti ile ilimfanya Jennifer kugeuza kichwa na kujaribu kuangalia kama atayathibitisha masikio yake ambayo yalimpa taarifa ya sauti hiyo.
"Usihangaike kutaka kunijua mimi ni nani." Catherine aliwasha taa iliyokuwa karibu na kiti ambacho alikalia ambayo ilimfanya kuonekana vizuri.
"Haaa wewe si mama Mchungaji?" Jennifer alimuuliza baada ya kuiona sura yake vizuri.
"Yes wala hujakosea mwanangu mimi ndiye na hutakosea ukiniita Catherine." Alimjibu akiinuka kitini kumfuata.
"Kwanini umeniteka mama yangu?" Jennifer alimuuliza.
"Unaka kujua sababu ya kukuteka Jennifer?" Catherine alimuuliza.
"Ndiyo maana nikifikiria sijawahi kukukosea hata siku moja mama yangu." Jennifer alimjibu.
"Nisikilize binti yangu nimefanya hivi baada ya marehemu mama yako kushirikiana na mume wangu kufanya ambayo walifanya huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za kanisa."
"Una maana gani kusema hayo?" Jennifer alimuuliza.
"Labda nikuulize swali dogo tu Jennifer, hivi wewe ni mtoto wa nani?" Catherine alimuuliza akiwa nyuma yake akiishikashika kamba iliyokuwa ikining'inia.
"Mimi?" Jennifer alimuuliza.
"Ndiyo wewe kwani tuko wangapi hapa ndani?" Catherine alimuuliza.
"Mimi si ni mtoto wa Otago Mathew?" Jennifer alimjibu.
"Uko sahihi Jennifer lakini na mimi nikikuambia kuwa wewe si zao la Otago utaamini?" Catherine alimuuliza.
" Kivipi mama Mchungaji?" Jennifer alimuuliza.
" Sina jibu la moja kwa moja lakini kuna simu nakwenda kuipiga hapa na hii ndiyo itakupa ukweli Jennifer." Catherine aliipiga simu ya Mchungaji Rodney Hauser huku akirudi kwenye kiti.
" Naongea na nani tafadhali?" Mchungaji Rodney Hauser alimuuliza baada ya kupokea simu kwa sababu Catherine alitumia simu yenye usajili mwingine ambayo Mchungaji hakuwa nayo.
"Ongea naye huyu mtu anza kwa kujitambulisha." Catherine alimwambia Jennifer akimkabidhi simu ambayo ilikuwa loudspeaker.
"Haloo!!" Jennifer aliita.
"Haloo , haloo ya nini nimeuliza naongea na nani?" Mchungaji aliuliza kwa hasira.
"Naitwa Jennifer na wewe ni nani?" Jennifer alimuuliza.
"Jennifer? Jennifer gani?"
"Jennifer Otago." Jennifer alimjibu.
Lakini kabla hajaongea kingine chochote Catherine alimnyang'anya simu Jennifer na kutoka nayo nje ya kile chumba na kwenda kumkabidhi kijana wake aliyeshirikiana naye kwenye utekaji huo.
"Jennifer, Jennifer!!" Mchungaji Rodney aliendelea kuita.
"Unaonekana unampenda huyu binti yako au nakosea?" Kijana huyo aliuliza akiwa anaingia ndani alimo Jennifer.
"Binti yangu? Kwani wewe ni nani?" Mchungaji Rodney alimuuliza mtu huyo.
"Mimi ni mfanyabiashara wa watu kama Jennifer." Alimjibu akimgeukia Catherine kuona kama anakwenda sawa na Catherine akamuonesha dole kuashiria kuwa yuko sawa.
"Mfanyabiashara kivipi?" Mchungaji Rodney alimuuliza.
"Naomba unisikilize vizuri wewe Mchungaji Uchwara mikononi ninaye mwanao Jennifer najua unampenda vizuri sana hivyo basi ili usikutane na jina jingine la huyu mtoto fuata maelekezo yetu."
"Isiwe umemteka binti wa watu wewe?" Mchungaji aliuliza lakini kabla hajafanya chochote kile simu ilikatwa.
Kisha alimkabidhi simu Catherine ambaye alikuwa kamtolea macho Jennifer.
"Mbona siwaelewi? Mimi sina kosa lolote ambalo nimelifanya kwenu naomba mniachie tafadhali." Jennifer aliomba msaada akiwa anatokwa machozi.
"Nakufungua kamba lakini utaendelea kuwa chini ya uangalizi wetu ndani ya hili pango. Umeelewa?" Catherine alimwambia Jennifer.
"Mama yangu naomba uniachie nikaungane na wenzangu chuoni."
"Chuoni? Chuo gani hicho? Kuhusu chuo kwa sasa hesabu ziro mpaka zoezi langu likamilike." Alimjibu huku kijana wake akimfungua kamba.
Akiwa amesimama akimuangalia kijana wake anavyomfungua kamba Jennifer mara simu yake iliita na baada ya kuiangalia ilikuwa namba ngeni hivyo aliipokea na kuweka sauti ya juu (loudspeaker) kisha akamkabidhi Jennifer hebu ongea na hii simu.
"Halo, ha...halooo...." Jennifer alipokea.
"Naombeni msimfanye chochote mwanangu na kama kuna mnachohitaji tafadhali niambieni mimi lakini msimtese mwanangu."
"Ba..ba...baba ni wewe?" Jennifer aliuliza baada ya kuijua sauti ya Otago.
"Mwanangu Jennifer ni wewe? Vipi hawajakufanya chochote hao watekaji?" Otago Mathew alimuuliza binti yake.
"Ha...ha...hapana huyu ni....." Lakini kabla hajaongea chochote alikutana na kofi ambalo lilimpeleka chini.
"Unataka kumwambia nini baba yako? Jiangalie wewe." Catherine alimwambia akimkabidhi simu kijana wake.
"Kuna nini tena mwanangu?" Otago aliuliza baada ya kusikia mzozo upande wa pili wa simu.
"Jiangalie wewe kiumbe acha kufuatilia mambo yasiyo kuhusu na kama unamhitaji binti yako akiwa salama funga domo lako na subiri simu yetu kinyume chake utapokea taarifa mbaya za mwanao" Alikata simu na kumkabidhi Catherine ambaye aliipokea na kuiweka mfukoni kisha alimfuata Jennifer pale chini alipokuwa kalala akilia.
"Jennifer ukijitia kujuajua utaishia kuyaonja mauti ambayo hayata kuwa na mliaji."
"Naomba unisamehe mama sirudii tena." Akiendelea kulia pale chini.
"Unatakiwa kuwa mpole tofauti na hapo utajuta si umeona simu ya pili imekuja wakati sisi tulipiga kwa mwingine? Hivi ndivyo watu wanavyokuwa hawana subira Jennifer hivyo unatakiwa kuwa mpole." Catherine alimwambia Jennifer aliyekuwa akijikongoja kuinuka.
***
"Niambie Daktari wangu, Wanaendeleaje wagonjwa wangu?" Martin alimuuliza Daktari anayewashughulikia wakina Seynabou.
"Wanaendelea vizuri sema huyu wa kuitwa Adoyee itamchukua muda kupona majeraha yake kutokana na namna ambavyo alishambuliwa lakini huyu Seynabou muda wowote atakuwa sawa." Alimjibu.
"Hawa wengine?" Martin aliuliza akionesha waliko wakina Awadh waliko.
"Wale hawana tatizo wako vizuri tu sema niliyekuwa nina wasiwasi naye alikuwa yule Soud lakini vipimo vimeniridhisha yuko vizuri." Daktari alimjibu Martin.
"Vizuri kumbe wewe endelea kuwashughulikia wakina Adoyee wacha mimi nikafanye yangu." Martin alimwambia akielekea ndani kwake.
"Sasa wacha mimi nirudi kituoni nikaendelee na shughuli nitarudi baadaye kuwaangalia." Daktari alimuaga Martin ambaye alimpa tu ishara akiingia ndani.
"Nipe taarifa Martin." Ulikuwa ujumbe ambao uliingia kwenye simu ya Martin akiketi ofisini kwake. Aliusoma kisha akaona aujibu. "Makamanda wanaendelea kuimarika kila dakika." Lakini akakumbuka kitu hivyo akaona wacha amuulize Catherine.
"Kuna tukio la kutekwa kwa mmoja wa wanamichezo kutoka Chuo kikuu cha Lagos, vipi umeipata hiyo?" Alimaliza na kuutuma.
"Nimeipata hiyo sijui ni nani atakuwa amefanya hilo tukio kwa kweli na kwa anavyoonekana alijiandaa iweje asikamatwe?" Catherine alimjibu.
"Du mimi nilijua ni wewe, sasa iweje unashangaa?" Martin alimuuliza.
"Hivi huyu mwanamke hausiki kweli?" Martin alijiuliza swali akilifungua kabati kuchukua nyaraka zake.
"Hivi kaka Martin sisi si tunaruhusiwa kuanza mazoezi kama ulivyosema jana?" Jumbe alimuuliza Martin.
"Tunaweza kuanza lakini wacha kwanza tupate taarifa ya mwisho ya Daktari ili ikiwezekana tuanze pamoja na wakina Seynabou." Alimjibu.
"Sawa kaka lakini vipi kuhusu ile taarifa ya Lagos umewasiliana na Madam?"
"Yeye mwenyewe anashangaa kama sisi sijui mhusika ni nani?" Martin alimjibu akipitia nyaraka moja baada ya nyingine.
"Naomba Jumbe na Awadh waanze safari kesho kuja Nigeria kuna kazi nataka ikamilike ndani ya siku nne zijazo." Ni ujumbe uliotumwa kwa Martin na Catherine.
"Kesho? Na huko kuna kazi gani?" Alijiuliza swali baada ya kuusoma ujumbe huo. Akaona wacha ampigie moja kwa moja.
"Madam sijauelewa ujumbe wako." Martin alimwambia baada ya simu kupokelewa.
"Ni hivi, huku nimefanya tukio la kwanza mliloliona kwenye vyombo vya habari lakini katika pitapita yangu kwenye 'app' nimeiotea namba ya mzee Malick ikiwa kama kilometa hamsini tu kutoka nilipo hivyo ninataka kuifanya hiyo kazi kabla hajashtuka." Catherine alimjibu.
" Kwa hilo ondoa shaka wataanza safari alfajiri." Martin alimjibu.
" Na iwe hivyo aisee." Catherine alisisitiza na kukata simu. Martin alitoka na kuwaita wakina Awadh na kuwaeleza kila kitu kama alivyoambiwa na Catherine hivyo akawataka wafanye maandalizi ya safari.
JE NI NINI KITATOKEA KATIKA KITIMUTIMU HIKI?
TUKUTANE KATIKA SEHEMU INAYOFUATA.
Sent using
Jamii Forums mobile app