Baada ya kikao cha Dodoma, katibu mkuu wa CCM bw. Wilson Mukama ameendeleza ngonjera kuwa mafisadi hawajasafishwa na kwamba watashughulikiwa. Nikiangalia ambavyo CCM imekuwa ikiwakumbatia mafisadi huku ikiendeleza kauli za kujivua gamba, inanifanya nikumbuke hadithi ya zamani ya "fisi na ngozi iliyokwamia shingoni"
Fisi alikuwa amealikwa kwa wakwe ambako alirimiwa ipasavyo. Alichinjiwa ngombe akala sawasawa. Kesho yake akifunga safari ya kurudi, kwa tamaa ya nyama aliomba apewe ngozi aende nayo. Alipofikiri namna ya kuibeba akatoboa tundu na kuingiza shingo yake na safari ikaanza. Ilipofika mchana kwa vile kulikuwa na jua kali, ngozi ikaanza kukauka na kumkaba koo. Hata hivyo kwa tamaa ya nyama hakutaka kuchomoa kichwa hata baada ya kuonywa na wasafiri wengine njiani. Matokeo yake ngozi ikazidi kukauka na kumkaba zaidi na hakuweza kutoa kichwa na hivyo akafa nayo.
Nionacho mimi ni CCM inayokufa na magamba yake yanayokaukia shingoni kwa vile hawataki kuchomoa kichwa na kuachana nayo. CCM wanajua vema wanavyofaidika na magamba (mafisadi) hayo. Hivyo kwa tamaa yao wanasubiria kifo ambacho ni dhahiri kutokea hata kabla ya uchaguzi wa 2015.
Kwa kifupi, kauli ya Mukama haina mshiko.
Nawasilisha