Posted Date::11/22/2007
Tiba MOI:Aliyepasuliwa mguu badala ya kichwa, afariki
Jackson Odoyo na Andrew Msechu
Mwananchi
EMMANUEL Mgaya (19), aliyefanyiwa upasuaji wa kichwa Jumatatu wiki hii baada awali kufanyiwa wa mguu kimakosa, katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), amefariki dunia jana asubuhi.
Mara baada ya Mgaya kufanyiwa upasuaji wa kichwa, hali yake ilibadilika na kuwa mbaya kisha kulazwa chumba cha wagonjwa mahututi (ICU), hadi mauti yalipomfika jana saa 2:30 asubuhi.
Awali Mgaya alifanyiwa upasuaji wa mguu badala ya kichwa na Emmanuel Didas ya kichwa badala ya mguu, Novemba mosi mwaka huu katika taasisi hiyo.
Akizunguza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu muda mfupi baada ya Mgaya kufariki dunia, mmoja wa wauguzi wa MOI, alisema hali ya mgonjwa huyo, ilianza kuwa mbaya juzi mchana.
Alisema jana asubuhi mapema alipofika kazini, alimkuta akipumua kwa shida, hali iliyoonyesha alikuwa amezidiwa.
Aliongeza kuwa, baadaye madaktari wanaomuhudumia waliwasili katika chumba hicho na kugungua hali yake ilikuwa ni mbaya zaidi.
Hali ya mgonjwa huyo ilianza kuwa mbaya tangu jana (Juzi)mchana na niliporudi kazini leo (jana)alfajiri nilikuta hali yake imebadilika kiasi cha kunipa wasiwasi, lakini madaktari walifika muda mfupi badaye na kumpa huduma za haraka japo hazikuweza kumsaidia, ? alisema muuguzi huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini kwa kuwa si msemaji.
Kwa mujibu wa chanzo, jitihada za kuokoa maisha ya Mgaya zilishindika majira ya saa 2:30 mgonjwa huyo alifariki dunia.
Hata baadhi ya madaktari waliozungumza na Mwananchi walithibitisha kwamba Mgaya amefariki dunia.
Kifo cha Mgaya kimetushutua sana kwa sababu tangu alipofanyiwa upasuaji wa mara ya kwanza kila daktari wa taasisi hii alijaaribu kumsaidia kwa karibu, alisema daktari huyo.
Waliongeza kwamba hata Mkurugenzi Mkuu wa MOI, Profesa Laurent Museru, amesikitishwa sana na kifo hicho na kulazimika kuitisha kikao cha dharura kujadili namna ya kufikisha taarifa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kwa ndugu wa marehemu huyo.
Akizungumza na Mwananchi, Profesa Museru amethibitisha kutokea kwa kifo cha Mgaya.
Ni kweli Mgaya alifariki dunia leo (jana) asubuhi na tumeshawajulisha ndugu zake pamoja kutoa taarifa wizarani, pia mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti,alisema Profesa Museru.
Alisema kwamba utaratibu wa maziko yake, utafahamika baada ya kuwasiliana na ndugu zake. Mgaya ni mwenyeji wa Mkoa wa Iringa.
Habari za kifo cha Mgaya, si tu zimewashtusha wafanyakazi wa MOI, pia Waziri wa Afya, kimesema chanzo chetu cha habari.
Mgaya alifikishwa katika taasisi hiyo, Oktoba 28, mwaka huu akitokea mkoani Iringa na kufanyiwa uchunguzi wa kina kuhusu matatizo yake na madaktari kushauri afanyiwe upasuaji wa kichwa.
Mwanzoni mwa mwezi huu, badala ya kufanyiwa upasuaji wa kichwa, alifanyiwa upasuaji wa mguu, huku Didas akifanyiwa wa kichwa badala ya mguu.
Kwa sasa Didas amelazwa ICU katika taasisi hiyo huku kukiwa na habari kwamba amepoza upande wa kulia wa mwili.
Tokea Didas amefanyiwa upasuaji huo tata, hajaamka, wala hajaongea na kadri siku zinavyokwenda hali yake, inazidi kuwa mbaya.
Baada ya tukio hilo, Prof Museru aliamriwa na Bodi ya MOI, kuunda tume ya kuchunguza upasuaji huo na kutekeleza hilo, Novemba 2 mwaka huu.
Tume ilikamilisha kazi yake Novemba 13, na kuikabidhi Bod Novemba 15, na Bodi kuipeleka kwa Waziri Novemba 16.
Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyusa ameahidi kutoa taarifa ya Tume hiyo iliyoundwa kuchunguza sakata la upasuaji huo.
Taarifa iliyopatikana jana kutoka katika wizara yake, ilifahamisha kuwa, Profesa Mwakyusa anatarajiwa kutoa taarifa hiyo leo saa 4.00 wizarani hapo.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi vifaa vya upimaji kwa ajili ya wagonjwa wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) jijini Dar es Salaam jana, Mwakyusa aliahidi kutoa taarifa hiyo leo, baada ya kumalizia maandalizi ya mwisho.
Naombeni munivumilie kwa leo, ninamalizia utaratibu wa kuitoa, ila nitaitoa kesho , siewezi kuzungumza lolote leo kwa kuwa ninaweza kuzungumza nusu nusu, nivumilieni kama mlivyonivumilia tangu nilipowaomba kufanya hivyo nilivyokuwa Bungeni Dodoma, Waziri huyo aliwaambia wanahabari waliotaka kujua hatma ya taarifa hiyo.
Alisisitiza kuwa, subira ni suala la msingi, hivyo wanachi hawana budi kusubiri kwa muda ili waweze kupata taarifa iliyokamilika.
Awali Prof Mwakyusa, alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari, akisema taarifa hiyo angeitoa juzi, lakini kwa sababu zisizojulikana, alishindwa kufanya hivyo.