51 -52
Taarifa juu ya mrembo aliyeshinda taji la Chang’ombe Alice Majaliwa mpaka kuingia kambini sasa ikawa imechukuwa sura mpya kichwani kwa Baba yake halisi Alice,Majaliwa pamoja na mkewe Juliana. Picha mbali mbali kupitia magazeti na hata habari kutoka kwa majirani waliokuwa wakiishi nao waliweza kuzitembeza taarifa mpaka kuwafikia moja kwa moja. Ingawa Mama yake halisi na Alice, Juliana alipigwa sana na mumewe kipindi cha nyuma wakati bado wanaishi na Alice hali iliyompelekea Mama huyo kutoroka na kumuacha Alice akiwa bado mdogo na baba yake nakufanyiwa vitendo vibaya vya kubakwa na mzee wake mpaka kufikia hatua ya Alice kumtoroka Baba yake akiwa bado mdogo nakutokomea kusikojulikana. Na sasa Mama yake halisi Alice,Juliana alikuwa wa kwanza kurudisha moyo kwa kurudi nyumbani kwake baada ya kuvumilia sana kwa kipindi cha mwezi mmoj na nusu akiwa kijijini kwao Kondoa. Alirudi nyumbani kwake kwa lengo moja tu nalo ni kuishi ama kumchukuwa na mwanae Alice. Alihuzunika sana baada ya kukuta Alice katoroka na kumuacha Baba yake akiwa katika hali mbaya ya kuishiwa nguvu kwa kutokula kwa siku tano. Tumbo lake lilikuwa limejaa pombe kali zile za kienyeji. Juliana hakuwa na kazi yeyote lakini kupitia kwa majirani na wasamalia wema alifanikiwa kumtibu mumewe mpaka akawa katika hali yake japokuwa tayari mwili wake Majaliwa ulikuwa katika hatari kutokana na kuingiliwa na ugonjwa wa kansa ya ngozi. Maisha yalizidi kuwa magumu zaidi. Baadhi ya majirani wakashauri wamtafute mtoto wao huenda wakapata msaada wowote kutoka kwake. Siku, wiki mpaka miezi ikakatika kwa kuhaha bila kuwa na dalili zozote za kumpata Alice kutokana na Jiji la Dar es salaam kuwa kubwa sana. Hatimaye baada ya kuhangaika kwa muda mrefu bila kuambulia chochote wakafanikiwa kuelekezwa ofisi za waratibu wa mashindano ya miss Tanzania. Walianzia safari yao ya kutoka Tandale kwa mtogole walipokuwa wakiishi kwa mguu mpaka Posta zilipo ofisi na kwabahati wakamkuta mlinzi ambaye aliwaelekeza moja kwa moja ofisini. Walimkuta mwakilishi mmoja wapo akiwa bado yupo ofisini na si mwingine bali alikuwa ni John Mapunda.
“Samahani Baba eti hapa ndio ofisi za wale wanaoshiriki mashindano ya miss Tanzania..??”
Majaliwa alijikaza na kumuuliza John kwa sauti ya upole huku kifua kikimbana kwa kukohoa. John aliwaangalia mara mbili mbili kwa jicho la dharau.
“Ni nani kawaelekeza mje hapa..?? Hapa hatutoi msaada wa aina yeyote zaidi ya kujishughulisha na maswala ya urembo, kwani hamjaelekezwa hapo chini mapokezi..??”
”hapana Baba, hapo mapokezi hatukumuona mtu na ni mlinzi ndio katuelekeza hapa moja kwa moja. Sisi hatupo hapa kwa ajili ya msaada wa kifedha. Tupo hapa kwa shida moja tu..??”
“shida gani..? wakati naona kabisa sura zenu zimekaa na ugonjwa . Maana namuona hata huyo mzee kababuka mwili wote huku kashikilia bahasha kubwa sijui ndio mafaili ya hospitali..?? Muwe waelewa hapa siyo hospitali jamani..? Na mlinzi yupi amewaruhusu nyie watu msiye na akili ya kufikiria..??”
Hasira sasa zikawa zimempanda John na kuinuka katika kile kiti alichokuwa amekikalia huku akiinuka na kuranda randa mule ofisini. Alijua fika kuwa wanahitaji msaada tu wa kifedha kutikana na hali zao walizokuja nazo kuanzia miili yao mpaka mavazi. Juliana alikuwa amevaa khanga zilizopauka na kuchanika huku mumewe, Majaliwa akiwa katika vazi lenye rangi ya kahawia lililoshonwa shonwa kila pembe huku likiwa halina kola kabisa.
“Baba sisi ni wazazi wa Alice majaliwa. Mimi ni Baba yake mzazi, naitwa Majaliwa.. Na tupo hapa kwa ajili ya kuonana na mwanetu Alice twende naye nyumbani..”
John alipigwa na butwaa kwa muda. Hakutaka kabisa kuamini maneno yale. Kwanza kutokana nakujua kuwa Alice na marehemu Angel walikuwa mtu na mdogo wake na wala hawakuwa na wazazi na ndio maana Angel alizikwa chini ya manispaa. John aliendelea kukaa kimya kwa takribani dakika tano nzima huku akiendelea kuwatolea macho wazazi halisi wa Alice. Baba halisi wa Alice, Majaliwa alionekana kukasirika sana kwa kudhalilishwa kuwa ni omba omba. Aliitoa bahasha aliokuwa ameishika kisha akachomoa picha ndogo iliokuwa ikimuonesha Alice akiwa amebebwa na Baba yake huyo enzi za utoto huku pembeni yake akiwa mkewe, Juliana kisha ile picha akaiweka mezani kwa John kuhakikisha kuwa wao ni wazazi halisi wa Alice.
“Alice mwenyewe huyu hapa Baba. Embu tunakuomba sana utuelekeze yupo wapi kwa sasa..?”
John alibaki na kigugumizi kwa alichokiona kupitia ile picha. Ni kweli alikuwa Alice yule aliyemfahamu. Yule alice ambaye alimchukulia kama mtoto wake wa kufikia. Aliyeishi naye kwa muda mrefu tangu Angel afariki.
“Embu niwaulize kitu wazee wangu..? Hivi mnajua Angel alipo..?”
“Baba, sisi huyo Angel wala hatumjui kabisa. Sisi ni wazazi wa Alice ambaye unamuona katika hiyo picha..”
“Sawa nimewaelewa. Ni kwamba hivi ninavyoonge leo ndio kilele cha mashindano haya ya miss Tanzania ambayo yatafanyika ukumbi wa Diamond Jubilee pale upanga. Kwa sasa hamtaweza kumuona huyo Alice mpaka mashindano yaishe usiku. Hivyo cha kuwasaidia tukutane wote usiku pale Diamond Jubilee kuanzia saa mbili..”
“Ndio wapi huko baba..??”
“Hampajui..? kwani nyie mnaishi wapi..?”
“Baba sie tupo tunaishi Tandale kwa Mtogole na hapa unapotuona tumekuja mjiini kwa miguu kwani hata nauli yenyewe kwetu ni shida Baba..!!”
“Sasa cha kuwasaidia hapa naondoka muda huu kwenda kwangu hivyo nitawapitisha hapo ukumbini mchana huu na itawabidi mpaka muda wa mashindano saa mbili usiku ufike. Kuhusu kuingia ukumbini msijali nitawasaidia kuingia na kuwatafutia sehemu nzuri tu ya kukaa wote wawili kwa kuwa hamna uwezo wa kulipia kiingilio..”
Katika maisha ya John kamwe hakupenda kuwasaidia watu ambao hawana uwezo. Roho mbaya na ya kikatili aliyoumbiwa nayo sasa ikawa inajionesha kwa wazazi halisi wa Alice. Alijitahidi kuvumilia kwa kuwapakiza kwenye gari lake na kisha kuwapitisha mpaka hapo ukumbi wa Diamond Jubilee. Halafu yeye akaelekea kwake kujiandaa. Njia nzima ilikuwa ni ya ushindi kwa John. Furaha yake kubwa ilikuwa ni kwa Jamila ambaye alikuwa akimuumiza kichwa endapo akimpa ushindi, Alice atachukuliaje.
“Asante sana Mungu kwa kunionesha njia. Alice achukuliwe tu na wazazi wake akaishi nao. Nashukuru mipango yangu sasa imekamilika na tayari nimewahonga majaji wote na hivyo namsubiria kwa hamu Jamila wangu kuwa mshindi usiku wa leo.”
*************
Ule urafiki ambao ulijijenga toka siku ya kwanza walipoingia kambini kati ya Jamila na Alice sasa ukawa umevunjika rasmi. Japo walikuwa wanakaa chumba kimoja lakini sasa wakageuka kuwa maadui kama vile chui na paka. Ni jamila ndio aliovunja uhusiano rasmi ambao ulikuwa ni wa kufa na kuzikana kati yao. Ilikuwa ni siku moja kabla hakujafikia kilele cha mashindano ya kumtafuta mrembo wa Tanzania. Dharau na kejeli kutoka kwa Jamila zilimchefua sana Alice. Jamila alijivunia kutembea na Baba yake Alice japo alitambua kuwa ni Baba yake mzazi halisi. Ile ahadi ambayo Jamila aliahidiwa kutoka kwa John kuwa mshindi wa kwanza katika mashindano ya mrembo wa Tanzania sasa ikawa imemuingia vilivyo masikioni mwa Alice. Alice alijiona mkosaji duniani. Aliumia sana moyo. Machozii mengi ya hasira yaliokuwa yakimtiririka mithili ya maji yanaofuata mkondo sasa yakawa yamesalimiana na sakafu yote. Nusu ya sakafu ilienea machozi ya Alice. Usiku kutwa alikuwa hana furaha wala kuamini kama Jamila angeweza kumgeuka na kutembea na Baba yake. Kumbukumbu zake zilimrudisha mbali sana toka alipoachwa na Dada yake wa kufikia marehemu Angel. Ndipo akamjua rasmi Baba yake wa kufikia, John. John alimuhaidi kumpenda kwa njia zote na kumfanya kuwa na furaha wakati wote. Tabasamu likaanza kutawala tena katika nyuso yake huku kumbukumbu zikimleta mpaka kwenye tukio alilofanyiwa na Baba yake huyo wa kufikia, John. Tukio la yeye kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya mrembo wa Chang’ombe lilimfariji. Kitendo cha yeye kutangazwa mshindi wa kwanza na kuzawadiwa nyumba pamoja na kiasi cha shilingi milioni mbili. Alijikuta yale maumivu yakipozwa na hilo tukio huku akiwa bado kwenye kona ya kitanda amesimama akimuangalia Jamila. Alijikuta hasira inamrudia tena kwa mara ya pili. Sasa akawa anaongea peke yake huku Jamila kapitiwa na usingizi hajitambui.
“Baba kweli furaha yangu ulioniahidi ndio hii..?? Kwanini umeamua kunifanyia hivi Baba yangu..?”
Uvumilivu wa wiki nzima aliokuwa akivumilia sasa ukawa umefikia tamati. Alice alijikuta akichukuwa simu yake nakuanza kubonyeza namba za simu kumpigia Baba yake wa kufikia,John. Simu iliita sana bila kupokelewa. Alijaribu zaidi ya mara tano lakini haikupokelewa. Halmashauri ya kichwa chake ikapambanua nakuamua kumpigia simu Mama yake wa kufikia, Janet. Akapokea ile simu.
“Mama..??, najua wewe ni mzima tu wa afya..!!”
“Vipi tena mwanangu kwani kuna nini..??”
“Mama..?? Baba yangu uko naye usiku huu..??”.
“Ndio niko naye hapa kalala..!!”
“Pliiz mama..!!, tena pliiz..!! embu nipe niongee naye..?”
“Hapana mwanangu hata mimi ni mzazi wako waweza kuniambia tu. Tuliza kwanza hizo jazba ulizonazo kisha niambie nini kimekusibu mpaka unapiga simu usiku huu tena ukiwa katika hasira..?”
Janet alioonesha kushtushwa sana na na ile simu iliopigwa na alice usiku. Katu hakuwahi kumsikia Alice akipiga simu usiku wa manane tena akiwa katika hali ya jazba. Pia Alice huwa hana tabia sana ya kumpigia simu baba yake zaidi ya kupitia kwanza kwa Mama yake hata kama anashida. Alichokifanya Janet, aliiweka simu yake sauti ya juu kisha akamuamsha mumewe apokee ile simu. Kwa usingizi ambao ulikuwa umemtawala John, alishtuka huku akiwa hajitambui vizuri nakupokea ile simu.
“Enh hujambo mwanangu..??, vipi usiku huu nini tena..?”
“Nakupenda sana Baba yangu. Najua unajua kesho ndio kilele cha mashindano yetu Baba. Nakuomba niwe mshindi nakuomba sana Baba yangu..”
Alice alijikuta akiishiwa nguvu nakuongea maneno ambayo hakuyapangilia vizuri katika akili yake. Lengo lake kubwa ni kumwambia ukweli juu ya Jamila kuwa mimba aliokua nayo Jamila si ya kwake kama anavyodhania.
“Mwanangu..?, kesho jitahiidi sana na tayari nimeandaa ushindi utaenda kwako..”
Hasira kali zikamzidia Alice nakujikuta akiikata ile simu. Alikuwa ameshachoshwa na uongo wa Baba yake huyo wa kufikia, John. Aliona anadanganywa wakati ushahidi anao kwa Jamila. Alijikuta kile kidonda chake cha moyo kikizidi kuuma. Alichokifanya aliizima simu yake kisha akaenda moja kwa moja kwenye kabati la vipodozi. Kabati ambalo lilitawaliwa na vipodozi vyake na vya jamila. Aliichukua chupa ya paffyumu yake ambayo Jamila alikuwa akiipenda sana kisha akaipasua chini nakubakiwa na kipande cha chupa chenye ncha kali. Alisogelea mpaka eneo la kitanda pembeni kabisa alipokuwa amelala Jamila fofofo na kisha akauchukuwa mto na kumfunika nao Jamila usoni mpaka maeneo ya mdomoni. Jamila alitapatapa sana lakini kutokana na nguvu za hasira alizokuwa nazo Alice alijikuta akiuchukua mkono wake uliokuwa na kile kipande cha chupa nakukipeleka mpaka tumboni mwa jamila nakumchoma nacho. Alirudia hivyo hivyo kama mara tatu kuingiza tumboni na kutoa huku mkono mmoja akiwa na mto uliomziba Jamila uso na mdomo asiweze kutoa makelele.