SIASA chafu za kiharamia ambazo Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimehadharisha hivi karibuni, zimeanza kujidhihirisha baada ya kiongozi mmoja wa chama hicho, kutekwa na wanachama wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kisha kumpeleka msituni na kumfanyia unyama mkubwa.
Wafuasi hao wa CCM wanadaiwa kufanya unyama huo wakiongozwa na viongozi kadhaa wa mikoa ya Manyara na Kilimanjaro ambapo pia walimbana kiongozi huyo katika tawi la Magadirisho, Nuru Maeda, sehemu zake za siri.
Akisimulia kisa kizima cha kitendo hicho cha kutekwa nyara na mbele ya waandishi wa habari jana, Maeda ambaye alikuwa katika maumivu makali, alisema kuwa alikuwa akitoka kwa dada yake, na akiwa njiani alikutana na mwenyekiti wa kitongoji cha Magadirisho ambaye alimuuliza kuwa mkononi alikuwa amebeba nini.
"Nikamwambia nina daftari la wapiga kura, nilikuwa muwazi kwa sababu daftari la wapiga kura si tatizo na ni haki yangu kuwa nalo, yeye akasema kuwa hiyo ni moja ya nyaraka za serikali na kunitaka twende ofisini kwake; akampigia simu mtendaji wa kata, mtendaji yule akamjibu kuwa kama ana daftari hiyo ni haki yake kama kiongozi wala haina tatizo.
"Alipoona kuwa mtendaji hajampatia ushirikiano kama alivyotaka, akaniachia nikaenda nyumbani, kumbe huku nyuma kawapigia simu watu wa CCM," alisema na kuongeza:
"Ghafla nikiwa nyumbani nakunywa chai, wakaja watoto wanasema mwenyekiti wa kitongoji alikuwa ananiita, nikaenda; nilipofika ofisini, muda mfupi wakaja watu wa CCM ambao wengine nawafahamu kwani niliwahi kufanya nao kazi, alikuwepo katibu wa CCM mikoa ya (anaitaja)."
Alidai kuwa walimchukua pale na kumpeleka katika msitu kwenda kumtesa sana, wakampiga na kumminya sana sehemu zake za siri.
"Leo hapa kama isingekuwa kuwajua wale watu nilikuwa nakufa, mpaka sasa ingekuwa habari nyingine. Baadaye nikawaambia kuliko kunitesa wanipeleke kituo cha polisi; nilipofika hapo wakataka kuwa mbele, ndipo OCD akaamuru nipewe kipaumbele kusikilizwa ili ijulikane hasa nini kimetokea, hivi sasa narudi kituoni hapo tena," alisema Maeda.
Akizungumzia tukio hilo katika mkutano wa mwisho kwa siku ya jana kijiji cha Songoro, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Slaa, alionya kuwa matukio ya namna hiyo hayatavumilika tena, akitoa wito kwa Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka bila kupendelea.
Akionekana kushangazwa, alisema ni hatari vitendo vya kihuni kama hivyo kufanywa na chama tawala tena na viongozi wakubwa wa chama hicho.
Dk. Slaa alisema ni ajabu kuwa baada ya miaka yote ya kuwa madarakani CCM imeshindwa kuzungumza mafanikio ya sera zake kwa wananchi kwa vitendo badala yake inaanza kuomba nafasi za uwakilishi ikitaka ‘kuonewa huruma na kufutwa machozi'.
Akimnadi mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari, katika maeneo mbalimbali ya kata za Kikwe, Nkoaranga na Songoro, Dk. Slaa aliwaambia wananchi kuwa wakati wa uchaguzi si wakati wa kufanya propaganda, kueneza majungu na umbea bali ni mahali pa vyama kushindana kwa sera na hoja.
Dk. Slaa aliwaambia wananchi kuwa endapo watamchagua Nassari watakuwa amepata mtu wa kufanya kazi iliyowahi kufanywa na aliyekuwa mmoja wa wapigania uhuru wa Tanganyika, hayati Japhet Kirilo, aliyekwenda kupigania ardhi ya Wameru huko Umoja wa Mataifa (UN).
Naye, Nassari aliwaambia wananchi kuwa chini ya uongozi makini wa CHADEMA, atakwenda bungeni na halmashauri kuisimamia, kuiagiza na kuiwajibisha serikali kwa kuhoji masuala mbalimbali.
Kwa upande wake, meneja kampeni mwenza, Vincent Nyerere, alisema kuwa yuko tayari kujitolea robota zima la vitambaa kwa ajili ya mgombea ubunge wa CCM anayetafuta ridhaa ya wananchi kupata nafasi hiyo nyeti kwa nia ya kufutwa machozi.
"Wananchi kura si kitambaa cha kufuta watu machozi, hivi hapa wangapi wamefiwa na baba zao, mama zao, shangazi zao, wajomba zao, kaka zao, dada zao na ndugu zao wengine wengi tu, lakini CCM na viongozi wake hawajaja hapa kuwaombea ubunge au uongozi wowote wa kuwafuta machozi…mbona hawajapewa ubunge?" alihoji.
|
|