Mpango mauaji ya Wayne Derek Lotter ulivyosukwa na kutekelezwa jijini Dar

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,117
1670855503512.png

Agosti 16, 2017 jiji la Dar es Salaam na dunia kwa ujumla lilipokea taarifa ya kusikitisha ya kifo cha Wayne Lotter, Mkurugenzi wa Taasisi ya Protected Area Management System (PAMS), inayojishughulisha na harakati za kupambana na ujangili chini ya mwamvuli wa utetezi na uhifadhi wa wanyama pori.

Lotter ambaye anatambulika Tanzania kama Mwanaharakati wa Tembo alikutwa na umauti baada ya kupigwa risasi karibu na eneo la makazi yake la Baobab Village, Masaki, Dar es Salaam alikokuwa anaishi. Siku ya tukio, Lotter na Mkurugenzi mwenza wa PAMS ambaye hakutajwa jina walikuwa wakitoka jijini Arusha katika harakati zao za kazi.

Walipofika karibu na eneo hilo walikutana na majambazi ambao waliwavamia na baadaye walimpiga risasi Lotter. Tukio hilo kama yalivyo matukio mengine ya uhalifu liliingiza Jeshi la Polisi katika uchunguzi ili kubaini wahusika wa tukio ambapo takribani watuhumiwa 22 walikamatwa kabla ya kuchujwa kwa sababu mbalimbali na kubaki 11 waliokwenda hadi mwisho walipohukumiwa kunyongwa hadi kufa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyoketi kusikiliza shauri hilo chini ya Jaji Leyla Mgonya.

Washtakiwa hao ni Rahma Mwinyi, Nduimana Ogiste, Godfrey Salamba, Chambie Ally, Allan Mafue, Ismail Mohamed, Leonard Makoi, Ayoub Kiholi, Abuu Mkingie, Habonimana Nyandwi na Michael Kwavava. Ni katika hukumu hiyo ndipo maelezo ya wahusika wa mauaji hayo yanapobainisha mpango mzima ulivyofanyika mpaka kutekeleza mauaji ya mwanaharakati huyo.

Mpango ulianzia jijini Arusha kwa mshtakiwa wa nane, Leonard Makoi ambaye katika ushaihidi ndiye anaonekana kuratibu mpango mzima kuanzia mwanzo. Makoi kwenye maelezo ya onyo alieleza kushiriki kutafuta watu wa kutekeleza mpango huo kuanzia mwanzoni.

Alikaririwa akisema: “Ni kwamba, mwaka 2017 mwezi wa saba tarehe sikumbuki, alinipigia simu mzee mmoja anayeitwa Machips, jina kamili silifahamu (akimaanisha mshtakiwa wa saba, Ismail Mohamed). Akaniambia kuna biashara anataka aongee na mimi.

“Majira ya saa saba usiku nilienda tukakutana na Mzee Machips, akaniambia kuna kazi ya Dar es Salaam. Nilipomuuliza ni kazi gani akaniambia kuna Mzungu anayehusika na meno ya tembo anatakiwa auwawe. “Akaniambia kama kuna watu wanaweza kufanya hiyo kazi niongee nao, tukubaliane ili kazi ifanyike. Baada ya kuniambia hivyo nilimweleza kwamba kuna kijana anaitwa Karama anaweza akafanikisha hiyo kazi,” alieleza katika sehemu ya maelezo yake.

Kwa mujibu wa maelezo yake walikubaliana na Karama ambaye baada ya makubaliano alimpigia akimtaka amtumie fedha kwa ajili ya maandalizi ya kazi hiyo.

“Baadaye Karama alinipigia simu akaniambia nimtumie pesa Sh milioni tatu kwa ajili ya kununua bunduki ya kufanyia kazi. Niliwasiliana na Mzee Machips akanipa hiyo pesa nikaituma kwa njia ya basi la Kilimanjaro Express. “Mwezi wa nane tarehe sikumbuki mwaka 2017. Ile kazi ilikuwa imekaribia na Mzee Machipsi alinipa pesa Sh milioni 58, nikaenda nazo Dar es Salaam kwa ajili ya kuwalipa akina Karama na wenzake akiwemo Gody na Mrundi ambae simfahamu kwa jina. “Ile kazi ilifanyika yule Mzungu akauwawa. Baada ya kazi kesho yake nilimpigia Karama akaja maeneo ya Ubungo katika hoteli ya Blue Pearl, nikamkabidhi kibegi kikiwa na Sh milioni 52 na kiasi kilichobaki, Sh milioni 6 nikabaki nacho, nikarudi Arusha,” alieleza.

Karama ambaye hakuwa mmoja washtakiwa mahakamani aliendelea kutajwa katika maelezo ya washtakiwa wengine kwamba ndiye aliyeratibu mpango huo kwa asilimia kubwa ikiwa ni pamoja kutafuta silaha, kuwahifadhi na kufanya nao vikao vya kuratibu mpango huo nyumbani kwake.

Katika maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Nduimana Ogiste, raia wa Burundi, alieleza namna alivyowasiliana na Karama ambaye alimtaarifu kuhusu mpango wa mauaji uliopangwa kufanyika Dar es Salaam na kuthibitisha kuwa alitumiwa shilingi milioni tatu kwa ajili ya kununua silaha.

Yeye alikiri pia kupokelewa na Karama alipowasili Stendi ya mabasi Ubungo kutoka Burundi na kupelekwa kuishi nyumbani kwake (Karama) Temeke.

Alikiri pia kushiriki vikao mbalimali vilivyofanyika kwa Karama kwa lengo la kupanga na kutekeleza mauaji ya Lotter.

Agosti 16, 2017 Lotter na Mkurugenzi mwenza wa PAMS walikuwa wakisafiri kutoka Arusha kuelekea Dar es Salaam kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) bila kujua kuwa walikuwa katika mpango wa kuuawa kwani nyuma yao kulikuwa na mtu anayetoa taarifa za safari yao na mbele yao katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), kulikuwa na watu wanaowasubiri kutekeleza uharamia juu yao.

Kati yao walikuwa ni watu wanaowafahamu, yaani madereva wao wanaowatumia katika safari zao mara zote yaani Chambie Ally na Daudi Kwavava.

Chambie yeye alishiriki mpango huo kutokea Arusha ambapo alitoa taarifa ya kuondoka kwa Lotter Kiwanja cha Ndege wa Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA) kuelekea Kiwanja cha Ndege cha Julius Nyerere (JNIA) na Kwavava alishiriki mpango huo kwa kwenda kuwapokea na kuhakikisha anarahisisha mazingira ya kutekeleza mauaji hayo.

Saa chache kabla ya kwenda JNIA kuwapokea Lotter na mwenzake, Kwavava kwa mujibu wa ushahidi inaelezwa kwamba alipitia dukani kwa mshtakiwa wa sita, Allan Mafue ambaye anatajwa kuwa alifadhili mpango huo wa mauaji na ndiye aliyemlipa Ogiste ujira wake wa Sh milioni 20 kutokana na kazi aliyofanya katika mpango huo.

Kwavava alienda kuonana na Mafue kwa ajili ya maelekezo ya mwisho ya utekelezaji wa mpango wao. Tukio hilo pia lilithibitishwa na Ogiste ambaye kwenye maelezo yake alieleza kuwa alimshuhudia Kwavava akiingia dukani kwa Mafue ambako alikaa kwa dakika thelathini kwa ajili ya kukamilisha mpango huo.

“Walikaa kama dakika thelathini au zaidi, baadaye walitoka na yule mzee aliondoka. Karama aliniambia, tuingie ndani ya gari. Tulipoingia alisema kazi ipo. Na yule mzee aliyekuwa naye (akimaanisha Kwavava) ndiye dereva atakayemchukua Mzungu uwanja wa ndege. Wameshaongea naye walipoingia ndani kwa Mafue, tuliondoka kwenda uwanja wa ndege.” Ushahidi ulionesha kwamba walipofika JNIA, Kwavava aliwapokea Lotter na mwenzake na safari ya kuelekea Masaki ilianza bila Lotter kujua kwamba nyuma yao Karama na Ogiste walikuwa wakiwafuatilia kwa kutumia gari aina ya Toyota IST kwa lengo la kuwaua.

Katikati yao dereva wa bodaboda, Ayoub Kiholi alikuwa akihakikisha usalama wa wauaji kwa kujiweka tayari kuwaokoa dhidi ya askari polisi na kuhakikisha hawavurugi mpango wao.

Awali katika maelezo yake, Kwavava alisema kuwa Agosti 16, 2017 akiwa amewabeba abiria wake kutoka JNIA, walifika katika makutano ya barabara ya Haile Sellassie ambako gari aina ya Toyota IST yenye paa jeusi iliwazuia kwa mbele na wakashuka watu wawili wenye silaha kuelekea kwenye gari yake.

Alisema mmoja wao alifyatua risasi na kumpiga Lotter karibu na kidevu huku akimwacha mwenzake ambaye ndiye aliyekuwa karibu zaidi.

Kwavava alitoa maelezo hayo kana kwamba alikuwa hajui chochote kuhusu mpango huo mpaka pale uchunguzi wa wa polisi ulipokuja kumbaini kwamba alishiriki na kumtia nguvuni.

Washtakiwa wengine kama Rahma wanaingia katika kesi hii kwa kushiriki njama za mauaji ambapo ushahidi ulionesha alishiriki kuwahifadhi na kuwaandalia chakula wahalifu walioshiriki mpango huo nyumbani kwa kaka yake Karama ambaye alikuwa akiishi naye huko Temeke Pia Rahma, kwa mujibu wa ushahidi alishiriki kuficha silaha zilizotumika kutekeleza mpango huo kwa kwenda kuzizika katika makaburi ya Ngazija Upanga, Dar es Salaam baada ya kusikia kuwa kaka yake alichukuliwa na watu wasiojulikana na yeye kuhisi kuwa amekamatwa na polisi.

Ingawa haikujitokeza waziwazi sababu ya kumuua Lotter, lakini inaaminika ni kutokana na harakati za kupambana na majangili.

===============

Desemba 2, 2022 ilitolewa hukumu ya kihistoria na Mahakama Kuu masjala kuu ya Dar es Salaam iliyowahukumu washtakiwa 11 kunyongwa hadi kufa kwa kumuua mwanaharakati wa mapambano ya ujangili, Wayne Dereck Lotter.

Lakini unafahamu zilitengwa Sh58 milioni kwa ajili ya kutekeleza mauaji hayo? na unafahamu muuaji aliyefyatua risasi iliyomuua Wayne alikodiwa kutoka Burundi na akalipwa Sh20 milioni? Na unafahamu silaha zilinunuliwa kwa Sh3 milioni?

Mbali na hayo, unafahamu madereva teksi wawili ambao waliaminiwa sana na Wayne aliyekuwa raia wa Afrika Kusini ndio walioshiriki kusuka mipango ya kumuua tajiri yao waliyemzoea kwa karibu miaka 10 mfululizo?

Basi kuyafahamu yote hayo, fuatilia mfululizo wa matoleo ya makala katika gazeti hili ambapo tutakuletea mwanzo mwisho wa tukio hilo, kesi ilivyoendeshwa hadi kufikia uamuzi wa washtakiwa 11 kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa.

Katika sehemu hii ya kwanza, tutaangalia tangu marehemu ambaye ni mkurugenzi wa taasisi ya Protected Area Management System (PAMS) na mkurugenzi mwenza walivyoondoka Arusha hadi anauawa Dar es Salaam.

Usiku wa Agosti 16, 2017, Wayne akiwa na mkurugenzi mwenza wa Pams walisafiri kutoka Arusha kwenda Dar es Salaam kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) pasipokujua kuna kifo kinamsubiri.

Hakufahamu kama dereva aliyemchukua kutoka Arusha mjini kwenda KIA ambaye wamemfahamu kwa miaka mingi na dereva teksi atakayewapokea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jullius Nyerere (JNIA), Jijini Dar es Salaam, wamekula njama ya kumuua.

Baada ya kutua JNIA, walipokelewa na dereva teksi wa siku zote anayewapokea aitwaye Michael Daud Kwavava ambaye wamemfahamu kwa zaidi ya miaka 10, aliwachukua kuelekea Babao Village ambako ndipo walipokuwa wakielekea.

Wakiwa njiani walipofika katika njiapanda ya Barabara ya Kaole na Haile Selassie katika eneo la Masaki, walizuiwa kwa mbele na gari lingine na kwa mshtuko ndani ya gari hiyo walishuka watu walioonekana ni majambazi.

Majambazi wawili walilisogelea gari lao na mmoja akachukua kompyuta mpakato (laptop) zao na baadhi ya nyaraka ambazo walikuwa wakizifanyia kazi, mmoja alikuwa na silaha na alimfyatulia risasi mwanaharakati huyo. Baadaye majambazi hao waliokuwa na gari aina ya Toyota IST, walitokomea kusikojulikana na Wayne alikimbizwa hospitali ya Sally International ambayo haikuwa mbali na eneo la tukio, lakini tayari alikuwa amefariki dunia.

Baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza upelelezi kuwabaini nani wanaoshukiwa kuhusika na mauaji hayo na washukiwa 18 walikamatwa wakiwamo raia wawili wa Burundi na mwanamke Rahma Mwinyi. Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani na katika usikilizwaji wa shauri hilo Mahakama Kuu walipangwa kuanzia mshtakiwa wa kwanza Khalid Mwinyi au Banyata, hadi mshtakiwa wa 18, Almas Swedi maarufu kwa jina la Malcom.

Wengine kuanzia namba mbili walikuwa ni Rahma Mwinyi au Baby, Nduimana Ogisye ambaye ni raia wa Burundi, Godfrey Salamba, Chambie Ally, Allan Mafue, Ismail Mohamed au Machips, Leonard Makoi na Ayoub Seleman Kiholi.

Mbali na washtakiwa hao, walikuwepo Joseph Lukoa, Gaudence Matemu, Abuu Mkingie, Habonimana Nywandwi au Ogistee ambaye ni raia wa Burundi na Michael Kwavava aliyekuwa dereva teksi aliyewabeba Wayner kutoka JKIA.

Wengine katika orodha hiyo ni Emannuel Sonde, Kelvine Soko, Samia Hujat na Almas Swedi au Malcom na wote walikanusha mashtaka matatu ya kula njama kufanya mauaji na kumuua kwa kukusudia Wayne.

Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo na Jaji Leila Mgonya, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akawasilisha maombi kwa njia ya chemba ambayo yalikubaliwa, kwamba kesi iendeshwe faragha ili kulinda mashahidi.

Kutokana na ombi hilo ambalo lilikubaliwa na Jaji Lameck Mlacha katika uamuzi wake wa Desemba 8, 2020, mashahidi wote 32 waliotoa ushahidi walitambuliwa kwa vifupisho vya maneno AA hadi AZ na BA hadi BF 32.

Katika ushahidi huo, upande wa Jamhuri ulikuwa na mawakili wa Serikali saba wakiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Yamiko Mlekano na mahakama ilipokea pia vielelezo 43 yakiwamo maelezo ya ungamo ya baadhi ya washtakiwa.

Mathalan katika mahojiano yaliyorekodiwa, mshtakiwa wa tatu ananukuliwa akieleza namna alivyoelezwa kuwa mzungu (Wayne) angekuja na usafiri wa ndege siku hiyo huku mwingine akinukuliwa akielezea mgawo wa fedha ulivyokuwa.

Ni katika maelezo hayo ya ungamo, unakuta simulizi za mshtakiwa wa nne, Salamba anavyoeleza walivyokwenda JNIA baada ya mauaji na mshtakiwa wa tatu aliyemfyatulia risasi marehemu, alikabidhiwa mgawo wake wa Sh20 milioni.

“Huyo Allan Mafue alitoa Sh20 milioni ambazo alikabidhiwa Zebedayo kama mgawo wake katika nafasi yake ya uuaji kama alivyoahidiwa, baada ya hapo tulimrudisha Zebedayo Temeke nyumbani kwa Fahami Karama,” anaeleza. Maelezo mengine ni ya mshtakiwa wanane, Makoi anayesema katika maelezo yake “Ni kwamba mwaka 2017 mwezi wa saba tarehe sikumbuki alinipigia simu mzee mmoja anayeitwa Machips jina kamili silifahamu akaniambia kuna biashara.

“Nilimuuliza ni kazi gani akaniambia kuna mzungu anayehusika na meno ya tembo anatakiwa auawe. Akaniambia kama kuna watu wanaweza kufanya hizo kazi niongee nao, ili tukubaliane kazi ifanyike,” ananukuliwa Makoi akisema.

Shahidi wa kwanza

Shahidi wa kwanza aliyetambulika kama AA ambaye ni daktari anayefanya kazi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili anasema Agosti 19, 2017 alisaidiana na daktari mwenzake ndio walioufanyia uchunguzi mwili wa Wayne.

Katika uchunguzi huo walibaini marehemu alikuwa na jeraha karibu na mdomo na walipochunguza zaidi ndani waliona kipande cha chuma ambacho waliamini ni risasi ilipenya hadi mkono wa kushoto wa marehemu. Kutokana na risasi hiyo, mfumo wa upumuaji ulizibwa na damu na kwamba sababu za haraka za kifo ilisababishwa na kukosa hewa katika mfumo wa upumuaji kutokana na kuganda kwa damu.

Baada ya uchunguzi huo aliandaa ripoti ya uchunguzi ambayo ilipokelwa mahakamani kama kama kielelezo namba moja.

SEHEMU YA PILI

Katika sehemu ya pili, tunaendelea kukuletea ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri ambao kwa njia moja ama nyingine walishiriki katika kushuhudia tukio au kufanya upelelezi uliofanikisha kujulikana ukweli wa mauaji ya Wayne.

Shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri aliyetambuliwa kama AB, ambaye ni mmoja wa wakurugenzi watano wa Pams Foundation, alisema siku ya tukio alijulishwa na mkurugenzi mwenzake kwamba wamevamiwa eneo la Masaki.

Mkurugenzi huyo ndiye aliyekuwa amesafiri pamoja na Wayne kutoka Arusha hadi KIA na baadaye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), alisema walivamiwa eneo hilo wakitokea uwanja wa ndege na baadaye alikwenda haraka hospitali ya Sally International.

Shahidi huyo aliithibitishia mahakama kuuona mwili wa Wayne pale Sally International, lakini wakati huo ilikuwa tayari imethibitishwa kuwa amefariki dunia na ndiye pia aliyeutambua mwili wa Wayne katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kabla ya kufanyika uchunguzi (post mortem).

Shahidi wa tatu, nne na tano

Shahidi wa tatu ambaye kama waliomtangulia naye alipewa kifupisho cha AC na ni mtaalamu wa uchunguzi wa kisayansi kutoka Forensic Bureau, yeye aliieleza mahakama kuwa Desemba 13, 2017 alipokea vitu vinne avifanyie kazi.

Vitu hivyo ni silaha mbili, risasi ndogo 162, risasi kubwa moja na bomu la kurushwa kwa mkono na vitu hivyo viliambatana na barua kutoka ofisi ya RCO Kinondoni ikimtaka achunguze kama silaha hizo zilikuwa zinafanya kazi sawa sawa.

Barua ya pili ilikuwa na sampuli za maganda mawili ya risasi yaliyotumika kutoka silaha aina ya Uzi-Gun na kichwa kimoja cha risasi na ilimtaka kuchunguza sampuli hizo zilifyatuliwa kutoka kwenye silaha gani kati ya Uzi-Gun au Riffle Marker 4.

Baada ya uchunguzi wa kina, aliiambia mahakama kuwa aligundua silaha zile zilikuwa zinafanya kazi barabara na hata lile bomu la kurushwa kwa mkono na kwamba maganda na kichwa cha risasi vilifyatuliwa kutoka silaha aina ya Uzi-Gun.

Vitu hivyo pamoja na nyaraka vilipokelewa kama vielelezo namba 2 hadi 15.

Shahidi wa nne kama AD ambaye ni Ofisa wa Polisi aliieleza mahakama kuwa ndiye polisi wa kwanza kwenda eneo la tukio na huko alikutana na dereva teksi (Kwavava-mshtakiwa wa 14) ambaye alikuwa amewabeba wazungu hao.

Akiwa hapo aliona gari alilokuwa akiendesha dereva teksi huyo na alipata nafasi ya kumuuliza dereva nini kilichotokea, na baadaye alikwenda Hospitali ya Sally International lakini alipofika huko alielezwa Wayne alishafariki.

Baada ya hapo alirudi eneo la tukio ambako katika uchunguzi alifanikiwa kupata maganda mawili ya risasi yaliyotumika, moja aliliokota ardhini na lingine likiwa ndani ya teksi iliyokuwa imembeba Wayne na mkurugenzi mwenza wake.

Pia alisema baada ya kufanya yote hayo, Agosti 19, 2017 alishiriki na kushuhudia uchunguzi wa mwili wa Wayne katika Hospitali ya Muhimbili na akiwa kizimbani alimtambua mshtakiwa wa 14, Kwavava aliyekuwa dereva teksi.

Shahidi wa tano aliyetambuliwa kama AE ambaye anafanya kazi katika Dry Clearner ya Isnashir iliyopo mtaa wa Bibi Titi, Kinondoni na anakumbuka Septemba 19, 2017 wakimuomba ashuhudie upekuzi katika makaburi ya Ngazija.

Hapo makaburini anakumbuka kumuona msichana ambaye baadaye alikuja kumtambua mahakamani kama mshtakiwa wa pili, Rahma na mtu mwingine aliyemtaja kama Mzee Maganga ambaye ni mhudumu wa makaburi.

Akiwa hapo alimsikia mshtakiwa huyo wa pili akiulizwa na polisi ni wapi walipochimbia silaha na baada ya kuonyesha kwa ishara, ndipo Mzee Maganga aliwaambia polisi walihamisha mzigo huo hadi eneo la kona makaburini.

Anasema Mzee Maganga alichukua jembe na kuchimba ambapo alishuhudia mfuko wa kiroba ulitolewa na ndani yake kulikuwa na begi jeusi na lilipofunguliwa kulikutwa silaha mbili na bomu na birika yenye rangi ya bluu bahari.

Birika hiyo ilipofunguliwa kulikutwa soksi zilizokuwa na risasi na zilikuwa risasi kama 160 baada ya kuhesabiwa na alikiri kusaini hati ya ukamataji mali na akiwa hapo alimuona polisi mmoja akipiga picha vitu vyote vilivyopatikana hapo.

Ushahidi wa shahidi wa sita

Shahihi huyu, Ofisa wa Polisi aliyepewa utambulisho AF, aliieleza mahakama kuwa Septemba 16, 2017 kati ya saa 6:00 na saa 6:30 mchana alipata taarifa kutoka kwa msiri kuwa mmoja wa washukiwa wa mauaji yuko Kasoro Guest House.

AF ambaye anafanya kazi katika kikosi kazi cha makosa makubwa Polisi Chang’ombe, Dar es Salaam anasema alikwenda katika nyumba hiyo ya kulala wageni na kufanikiwa kumkamata mshukiwa ambaye katika kesi hiyo ni Rahma.

Shahidi huyo alieleza kuwa alimkuta na pasi ya kusafiria yenye jina la Rahma Almasi na kumpeleka kituo cha Polisi Oysterbay, lakini baadaye aliitwa tena aungane na timu ya makachero kwamba Rahma amekiri na yuko tayari kuonyesha silaha.

Wakiwa katika makaburi ya Ngazija, kulifukuliwa mfuko wa kiroba ambao ndani yake kulikuwa na begi jeusi na ndani yake kulikuwa na vitu vitatu ambavyo ni kitenge, mfuko mweusi na birika (thermos) yenye rangi ya bluu bahari.

Ndani ya vitu hivyo kulikutwa silaha aina ya Uzi-Gun yenye namba 084912 na bunduki aina ya Rifle ambayo haikuwa na namba za utambulisho na pia kulikuwa na bomu la kurusha kwa mkono na risasi 167 huku 162 zikiwa za Uzi-Gun.

Katika maswali ya dodoso (cross examination), shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa alikuwa na taarifa kuwa mshtakiwa huyo wa pili, Rahma alikuwa mbioni kuondoka nchini kwenda Comoro kulingana na taarifa alizopewa na msiri wake.

ITAENDELEA KESHO
 
Bado kesi haieleweki yupo wapi Karama? ameuawa? amefichwa? sababu za kuuawa kwa Lotter? nani aliyefadhili hizo hela?
katika watuhumiwa 22 ,hukumu iliyotolewa watuhumiwa 11 wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa akiwemo karama huku wengine wakiachiwa kuwa huru ,halafu kama unakumbuka kuna rubani mmoja alipotea huko tunduru na ndege ndogo mwaka Jana ni muendelezo WA kupoteza ushahidi Kwa sababu inasemekana baadhi ya mawaziri wapo kwenye hilo janga
 
Kuna watu walisomea na kubobea kufanya uchunguzi.

Huezi fanya mauaji watu wasikukamate. Lazima utaacha trace ambayo ndo itasababisha wewe kukamatwa.

Labda uue mbuzi wa jirani yako.
Hao watu waliosome na kubobea kufanya uchunguzi hawawezi kutumiwa na majambazi ili kuondoa traces zote?
Kwa teknolojianya kibongo mi naona ni rahisi sana, na majambazi wengi tu wanaua na kudunda mtaani.
 
Rahma na dereva bodaboda wameonewa,kupika chakula watu wanaoukuja nyumbani kwa kakaake sidhan kama wamehusika na mauaji,hata kama alificha silaha ni ktk hali ya kawaida ya kujihami,anahitaji mwanasheria mzuri,kuna watu wanastahili kunyongwa ila siyo rahma na dereva wa bodaboda,halafu hajasema hizo milion 58 zilitoks kwanani na zilienda kwa lengo gani ikiwa huyo mrundi alipewa milioni 20 na myu mwingine
 
swala la ujangiri ni mtambuka,mdogo wake Rost pamoja na yule mbunge wa Shy walihusishwa na ujangiri mambo yalizimwa kiaina,mambo haya huwa kuna wakubwa nyuma yake,na utawala huu ndo utawala wa ujangiri wa kuvuna pembe za ndovu.
Zama za kuvuna tembo hizi....nakumbuka enzi za jk ilibaki kidogo tu waishe tubaki kuwasoma kwenye vitabu
 
Mzungu atakuwa kaondoka na wengi kama kweli hawa watu 11 watanyongwa. Ni jambo la ajabu sana ukifikiria roho ya Mzungu mmoja Kaburu ni sawa na roho za Waafrika 11 Wazawa au tuseme 12 pamoja na Karama. Hukumu ya ajabu sana hii.
 
Rahma na dereva bodaboda wameonewa,kupika chakula watu wanaoukuja nyumbani kwa kakaake sidhan kama wamehusika na mauaji,hata kama alificha silaha ni ktk hali ya kawaida ya kujihami,anahitaji mwanasheria mzuri,kuna watu wanastahili kunyongwa ila siyo rahma na dereva wa bodaboda,halafu hajasema hizo milion 58 zilitoks kwanani na zilienda kwa lengo gani ikiwa huyo mrundi alipewa milioni 20 na myu mwingine
Zilitoka kwa Ismail machips
 
Back
Top Bottom