SEHEMU YA 72
Hakukaa na kutulia, muda mwingi alikuwa akisimama na kutembea huku na kule, alionekana kufikiria mambo mengi na kitu pekee ambacho alihisi mke wake ni kwamba mume wake huyo alikuwa akiifikiria hali ya mtoto wao kumbe haikuwa hivyo kabisa.
“Iyanya! Haiwezekani! Leo ni lazima nije kulala na wewe,’ alijisemea Theo akiwa ndani ya chumba alicholazwa mtoto wake.
Muda mwingine alikuwa akikisogelea kitanda kile na kumwangalia mtoto wake, alikuwa akipitia kwenye matatizo makubwa lakini kutokana na kuwa na tamaa ya kulala na mwanamke ambaye alihisi kuwa na uzuri kuliko wote katika dunia hii, hakutaka kujali kabisa.
Mtoto Rachel aliendelea kuwa vilevile, hakuongea kitu, hakutingishika, hakulia wala kufanya kitu chochote kile. Mke wake, Violeth alikuwa akilia tu, kila alipomwangalia mtoto wake kitandani pale aliumia kupita kawaida.
“Mke wangu! Hutakiwi kulia, hiyo ni kumchulia mtoto,” alisema Theo huku akimwangalia mke wake.
“Moyo wangu unauma mume wangu!” “Najua! Ngoja nikakutafutie chakula,” alisema Theo, alifanya hivyo kwa kuwa alihitaji kuondoka hapo hospitalini na kwenda kumuona Iyanya hotelini.
“Hapana! Sijisikii kula.
Naomba ubaki nami, nitakula kesho asubuhi,” alisema mke wake maneno ambayo yalimuumiza mno kwani alitamani sana kuondoka, hakutaka kubaki mahali hapo hata kidogo.
“Hapana mke wangu! Ni lazima ule kwa afya yako, hata kama hujisikii njaa,” alisema Theo huku akimwangalia mke wake.
Hakutaka kubaki hapo hospitalini, alimwambia mke wake kwamba ni lazima aondoke mahali hapo na kwenda kumtafutia chakula. Japokuwa Violeth alikataa lakini hakuwa na jinsi na kwa sababu mume wake aling’ang’ania, hakuwa na jinsi.
Theo akaondoka, njiani alikuwa akikimbia. Hoteli ambayo alimchukulia chumba Iyanya haukuwa mbali kutoka hapo alipokuwa. Alitamani kuwa na kasi zaidi na muda mwingine alitamani hata kupaa.
Mhemko wa kuwa na Iyanya ulimshika mno, hakutaka kusikia la mtu yeyote yule na aliuahidi moyo wake kwamba siku hiyo ingekuwa ni ya hatari, ilikuwa ni lazima Iyanya ajutie uamuzi wake wa kwenda India.