SEHEMU YA 68
Theo hakuwa na jinsi, moyo wake ulijisikia huzuni nzito lakini alitakiwa kukubaliana na kile alichoambiwa na mpenzi wake kwamba alifiwa na hivyo kwenda msibani kwa lengo la kuungana na familia yake.
Alisubiri huku akiwa na hamu tele ya kumuona Iyanya kwa mara nyingine tena. Wakati mwingine alitamani kuona kila kitu kilichotokea kilikuwa ndoto ambapo baada ya muda fulani angeshtuka na kujikuta akiwa nchini Tanzania, kitandani pamoja na msichana huyo mrembo.
Uzuri wa Violeth ulipotea kabisa machoni mwake, hakumpenda, alimzoea, alimuona kuwa mwanamke wa kawaida sana.
Alimthamini lakini hakutaka kufanya naye kitu chochote kile, na tena katika kipindi hicho ambacho mtoto wao alikuwa akiumwa, alimshukuru Mungu kwa kuwa kusingekuwa na uwezekano wa kuonana naye kimwili tena mpaka pale ambapo mtoto huyo angepona kabisa.
*** “Upo wapi?” lilikuwa swali la kwanza kwa msichana Iyanya, aliulizwa na mwanaume mmoja, bilionea mkubwa nchini Afrika Kusini.
“Tanzania!”
“Unafanya nini huko? Nimekutafuta sana, simu zako haupatikani mpaka WhatsApp. Ninataka kuonana nawe, unakumbuka kwamba kesho ni siku yake ya kuzaliwa?” aliuliza mwanaume huyo.
Iyanya alishtuka, hakuamini alichokisikia, alikuwa na mambo mengi ya kufanya kiasi kwamba hakukumbuka hilo.
Alinyamaza kwa muda, ni kama alipigwa na bumbuwazi kusikia mwanaume huyo alimwambia hivyo, alifikiria kwa sekunde kadhaa, akaligundua hilo.
“Mungu wangu! Nilisahau kabisa,” alisema Iyanya.
“Njoo Afrika Kusini haraka, nina zawadi yako kabambe,” alisema mwanaume huyo.
“Zawadi gani?”
“Wewe njoo utaikuta huku,” alisema mwanaume huyo na kukata simu.
Iyanya alitulia na kufikiria alichokuwa akiambiwa. Mwanaume ambaye alimpigia simu aliitwa Dickson Makusa, alikuwa miongoni mwa wanaume waliokuwa na pesa nchini humo.
Makusa alimpenda sana Iyanya, katika maisha yake alifanya mapenzi na wanawake wengi warembo, aliwapenda, aliwapa pesa lakini mwenye alikiri kwamba hakukuwa na msichana ambaye alimpenda kwa moyo wote kama Iyanya.