SEHEMU YA 62
Huo ulikuwa ni muda wa majonzi mazito, Theo alikuwa na maumivu makali moyoni mwake, kila alipokuwa akimwangalia mke wake, alisikia maumivu makali mno.
Alikaa na mkewe ndani ya chumba alicholazwa mtoto wao, mioyo yao ilikuwa na maumivu makali, kile kilichotokea kiliuma kupita kawaida. Baada ya saa kadhaa, wakaitwa ndani ya chumba cha daktari na kuambiwa kilichokuwa kikiendelea kwa mtoto wao.
Kwa Rachel jambo hilo lilionekana kuwa jipya, lilimuuma mno lakini kwa Theo halikuwa jipya, alilifahamu kwa kuwa aliambiwa kabla ila hakutaka kumwambia mke wake kwa kuwa aliamini angekuwa na majonzi zaidi.
“Niliambiwa hivyo na daktari,” alisema Theo maneno yaliyomfanya Violeth kushtuka kwani hakuamini kama mume wake alilifahamu hilo ila hakutaka kumwambia.
“Ulilifahamu? Kwa nini hukuniambia?” aliuliza Violeth huku akionekana kukasirishwa na kile alichokisema Theo.
Hakutaka kumficha, alimwambia ukweli kwamba hakufanya hivyo kwa kuwa alikubaliana na daktari anyamaze kwani endapo angemwambia kila kitu basi asingeweza kuvumilia kutokana na kile kilichotokea kwa mtoto mwingine.
Violeth hakutaka kuelewa, kwake aliona kama alisalitiwa lakini Theo alimwambia kila kitu, na alifanya vile kwa ajili yake kwani endapo angemwambia basi angeharibu kila kitu.
“Ni ushauri kutoka kwa daktari kwani hata mimi nilitamani sana kukwambia,” alisema Theo, alijitetea sana.
“Kwa hiyo hukutaka kuniambia kabisa!”
“Nilifuata ushauri wa daktari! Mke wangu, huu si muda wa lawama tenaa tunatakiwa kuungana kwa ajili ya afya ya mtoto wetu,” alisema Theo huku akimwangalia mke wake huyo.
Violeth hakutakiwa kulalamika kwa lolote lile, kile kilichofanyika kilikuwa ni kwa ajili yake hivyo kutakiwa kusahau na kuangalia afya ya Rachel tu.
Daktari huyo akawaambia kwamba matibabu juu ya misuli ya moyo wa Rachel yalitakiwa kufanyika nchini India, kwa nchi kama Tanzania ambayo ilikuwa na wataalamu wadogo ingekuwa vigumu sana kufanyika.