SEHEMU YA 50
Juke hakuamini alichokiona, ni kweli aliziona picha kadhaa zikimuonyesha Theo akiwa na mwanamke mwingine akila raha. Kama alivyoumia rafiki yake na yeye pia aliumia, hakuamini kama mwanaume huyo angeweza kumsaliti mke wake kutokana na matatizo waliyokuwa wamepitia.
Juke hakuwa na cha kufanya zaidi ya kumbembeleza rafiki yake huyo kwa kumwambia kwamba kusingekuwa na jambo baya, lile alilokuwa akipitia lilikuwa ni mtihani ambao alitakiwa kupambana nao kuhakikisha anaushinda kwani kwenye kila maisha ya ndoa jambo kama hilo lilikuwa linatokea mno.
Picha zile hazikuwa siri tena, kila mtu aliziona, wengi hawakuamini kama Theo angechukua hatua ya kumsaliti mke wake aliyekuwa kipenzi cha Watanzania wengi.
Walioumizwa walikuwa wengi mno, kila mtu akaanza kuandika hisia zake kwenye akaunti yake.
Hakukuwa na mtu aliyemsapoti kwa upumbavu aliokuwa ameufanya, wengi walikuwa wakimlaumu kwa kuwa alitoka kwenye matatizo baada ya mtoto wao mmoja kufariki dunia, kwenye miezi michache waliyokuwa wameishi baada ya hapo alitakiwa kumfariji sana mke wake lakini si kumtesa kama alivyokuwa amefanya.
“Ndiyo maana huwa ninasema wanaume wote ni mbuzi!” alisema mwanamke mmoja, alionekana kuwa na hasira mno.
“Yaani hata mume wako?” aliuliza mwingine kwa utani.
“Tena yule ndiyo beberu kabisa. Yaani hawa wanaume jamani wanatuumiza mno,” alisema mwanamke huyo.
Hiyo ndiyo ilikuwa habari ya siku nzima, kulikuwa na maneno mengi yaliyokuwa yakizungumzwa, wengi walihitaji kusikia kutoka kwa Theo, angesema nini kutokana na zile picha zilizokuwa zikionekana ambazo zilipigwa kwa siri kubwa.
Kwenye akaunti yake, hakuposti picha yoyote ile. Muda wote wale wadaku walikuwa wakitembea huko lakini hakukuwa na kitu chochote kile. Walijaribu kumpigia simu yake, haikuwa ikipatikana, ilizimwa na hata wakati ambao ilikuwa ikiita haikuwa ikipokelewa.
Kule nchini Afrika Kusini kama kawaida Theo alikuwa akila raha na Iyanya, alimpenda mno msichana huyo, kwake, alikuwa kila kitu, alimsahau mke wake na hata kumpigia simu hakufanya hivyo kabisa.