SEHEMU YA 53
Theo akaanza kumbembeleza, alichomwambia ni kwamba hakuwa akimsaliti, asingeweza kufanya hivyo maishani mwake, alimpenda kuliko mtu yeyote yule katika dunia hii, asingeweza kufanya kitu cha kipumbavu kama kile.
“Kumbe yule ni nani?” aliuliza Violeth.
“Ni video mpya! Nitaachia video mbili hivi karibuni mpenzi! Picha nimeziruhusu ziwekwe kama kiki ila hiyo ni video mpya,” alisema Theo.
“Yaani picha hizo ni kiki?”
“Ndiyo mpenzi! Siwezi kukusaliti, na kama nimekukosea naomba unisamehe!” alisema Theo huku akitoa sauti ya kutia huruma mno.
Kwa jinsi alivyokuwa akimpenda mume wake, Violeth akaamua kukubaliana naye, alihitaji kuona mwisho wa kila kitu ungekuwa nini.
Alichokifanya Theo ni kuangalia picha zile, akatunga wimbo harakaharaka, akamuomba Iyanya warekodi video kwenye maeneo yaleyale tena huku akiwa amevaa nguo zilezile.
Hiyo haikuwa kazi, wimbo ulikamilika na hatimaye video kushutiwa na kisha kuanza kupandishwa vipande vichache.
Kila mtu aliyeziona picha zile, akashtuka, wengi wakaanza kujilaumu kwa kumtukana Theo na wakati picha zile zilikuwa ni za kwenye video yake mpya.
Watu wengi wakaanza kuwalaumu watu waliokuwa wamsambaza picha zile kwa lengo la kumchafua Theo ambaye alionekana kupendana na mke wake kupita kawaida.
Na ili kuongezea, kwenye akaunti yake akaandika maneno mengi ya kuwalaumu watu kusambaza picha zile pasipo kuuliza kilichokuwa kikiendelea kwani ndoa yake ilitetemeshwa kutokana na picha zile zilizokuwa zimesambazwa.
Mpaka kufikia hapo, kichwa chake kikawa na akili zaidi, aligundua kwamba alikuwa akifuatilia hivyo kufanya mambo yake kwa siri kubwa kabisa.
Penzi likazidi kukua mpaka ilipofika siku ya kurudi nchini Tanzania. Aliporudi na kuonana na mke wake, akamfuata na kumkumbatia, alimng’ang’ania kwa nguvu kiasi kwamba hakuwa amefanya jambo lolote lile.
Alimwambia jinsi alivyokuwa akimpenda, hakukuwa na mwanamke mwingine zaidi yake katika maisha yake. Violeth aliridhika maneno ya mume wake na kuamini kwamba hakukuwa na jambo baya lolote lile ambalo lilitokea huko Afrika Kusini.