Morogoro: Machinga watamba vituo vya 'Daladala', masoko yakibaki matupu

Morogoro: Machinga watamba vituo vya 'Daladala', masoko yakibaki matupu

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
30
Reaction score
25
Karibu vituo vyote vya mabasi madogo ya abiria (maarufu kama daladala) katika Manispaa ya Morogoro, ni kawaida kukutana na wafanyabiashara wadogo (wamachinga) wakitembeza bidhaa zao mikononi.

Huwafuata wateja huku na huko, wakitangaza bidhaa kwa sauti za kuvutia ili kuwashawishi wanunuzi kabla ya safari kuanza au baada ya kushuka. Bidhaa hizo huanzia matunda, maji ya kunywa, vitafunwa hadi vifaa vidogo vya matumizi ya kila siku. Taswira hii imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya wakazi wa Morogoro, lakini pia inaibua mjadala mpana kuhusu nafasi ya masoko rasmi na ufanisi wake.

Kwa kiasi kikubwa, uwepo wa wamachinga katika vituo vya daladala unaashiria changamoto ya masoko kutotumika ipasavyo. Badala ya wafanyabiashara hao kufanyia biashara zao ndani ya masoko yaliyojengwa na halmashauri, wengi wao wamehamia kwenye vituo vya daladala ambako kuna uhakika wa kupata wateja kwa haraka zaidi.
WhatsApp Image 2026-07-02 at 10.04.22 (3).jpeg
Hali hii imekuwa kichocheo cha wadau mbalimbali katika Manispaa ya Morogoro kupendekeza njia mbadala za kukabiliana na biashara holela, huku wakisisitiza umuhimu wa kuunganisha mifumo ya usafiri na masoko pamoja na kuwashirikisha wamachinga wenyewe.

Katika kutafuta suluhu ya kudumu, wadau wa maendeleo wakiwemo wataalamu wa biashara na mipango miji wameishauri Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuachana na mbinu za nguvu za kuwaondoa wafanyabiashara hao barabarani, ambazo zimeonekana kushindwa kutoa matokeo ya kudumu.

Badala yake, wanasisitiza matumizi ya mbinu jumuishi zinazozingatia uhalisia wa mahitaji ya wafanyabiashara na tabia ya wateja, huku wakiipa umuhimu hoja ya kujenga masoko karibu na vituo vya mabasi au kuweka vituo vya mabasi katibu na masoko yalikojengwa.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi na biashara kutoka kampuni ya JWD Agribusiness, Bw. Emmanuel Paschal, anasema changamoto siyo uwepo wa majengo ya masoko bali ni mfumo mzima wa biashara. Anaeleza kuwa masoko kama Machinga Complex na Azimio yanapaswa kuunganishwa moja kwa moja na vituo vya daladala ili kuvutia wateja kwa urahisi.

“Tatizo si majengo, bali ni mfumo. Masoko yasipounganishwa na usafiri, wateja na mahitaji halisi ya wafanyabiashara, yatabaki kuwa magofu,” anasisitiza Paschal. Aidha, Paschal anapendekeza uwezekano wa kufunga baadhi ya barabara nyakati za jioni ili zitumike kama masoko ya muda.
WhatsApp Image 2026-07-02 at 10.04.22 (4).jpeg
Anasema utaratibu huu tayari unatumika katika baadhi ya manispaa nchini, ambako barabara hubadilishwa kuwa maeneo ya biashara wakati wa jioni na kurudi katika matumizi ya kawaida asubuhi. Mbinu hii, kwa mujibu wake, inaweza kutoa suluhu ya muda mfupi huku mipango ya muda mrefu ikiendelea.

Ushirikishwaji wa wadau
Kwa upande wake, Meneja wa Maendeleo ya Kilimo Biashara katika Chemba ya Biashara (TCCIA), Bw. Kastas Paschal, anaona ushirikishwaji wa wamachinga kuwa msingi muhimu wa mafanikio ya mipango yoyote inayolenga kuwahamisha au kuwaboresha wafanyabiashara hao.

“Mipango inayolenga kutafuta suluhu za wamachinga isipowashirikisha walengwa ni kupoteza muda na fedha za umma, kwa kuwa miradi inayotekelezwa kama ujenzi wa masoko hushindwa kutumika,” anasema.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mtaalamu wa mipango miji kutoka Chuo cha Ardhi Morogoro, Yusuf Abdalah, anayesisitiza umuhimu wa kuzingatia usawa katika utekelezaji wa sheria. Anasema mamlaka zinapaswa kwanza kuhakikisha zinatenga na kuandaa maeneo rafiki kwa wafanyabiashara wadogo kabla ya kuanza kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.

Mtazamo mpya
Kwa mtazamo mpana, suala la wamachinga linapaswa kutazamwa kama sehemu ya uchumi jumuishi badala ya kero. Bw. Emmanuel Joseph kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI anaeleza kuwa sekta isiyo rasmi ina mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, hivyo urasimishaji wake ni jambo lisiloepukika.

Naye Vedasto Sitta kutoka Tume ya Mipango anasisitiza kuwa wamachinga wanapaswa kuingizwa katika mifumo rasmi ya uchumi ili kusaidia kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025–2050.

“Machinga hawapaswi kuonekana kama kero, bali kama sehemu ya mnyororo wa uchumi. Kuwajumuisha kutasaidia taifa kufikia malengo yake ya uchumi jumuishi,” anasema.

Hasara ya mapato
Takwimu za Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro zinaonyesha kuwa masoko ni chanzo muhimu cha mapato, yakichangia takribani Sh. bilioni 4 kwa mwaka, kiwango ambacho kinaathirika kwa mamlaka kupoteza sehemu ya mapato hayo, pale biashara zinapofanyika maeneo yasiyo rasmi.

Mkuu wa Divisheni ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika manispaa hiyo, Bw. John Kulunge, anasema sababu kubwa inayowafanya wafanyabiashara kuacha masoko ni ukosefu wa subra kutokana na mitaji midogo.

“Wafanyabiashara wengi wanahitaji kuuza kila siku. Akiwa sokoni na hajapata wateja, anakimbilia barabarani ambako kuna uhakika wa mauzo ya haraka,” anafafanua na kuongeza: “Wafanyabiashara wengi wanakwepa masoko rasmi.”

Anaongeza kuwa ili Morogoro ipate hadhi ya jiji, mapato ya ndani yanapaswa kuongezeka kutoka shilingi bilioni 17 hadi zaidi ya bilioni 20 kwa mwaka, hivyo kutotumika kwa masoko rasmi, kunaweza kuwa moja ya sababu za kukawiza kufikiwa kwa hadhi hiyo inayotamaniwa.

Hatua za Manispaa
Katika kukabiliana na hali hiyo, Manispaa ya Morogoro imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kutenga shilingi milioni 312 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa soko la Mawewezi ili liweze kuchukua wafanyabiashara wengi zaidi. Pia kuna mpango wa kuboresha soko la Nane Nane ili liweze kuwahudumia zaidi wauzaji wa matunda na mbogamboga.

Mbali na hayo, halmashauri inapanga kuweka vituo vya bajaji na daladala karibu na soko la Machinga Complex lililopo Fire, kwa lengo la kulifanya kuwa kitovu cha biashara kinachovutia wateja na wafanyabiashara kwa wakati mmoja.

Kadhalika imekuwa ikichukua hatua za kuwakamata machinga wanofanya biashara nje ya masoko na kuwafikisha mahakamani wafanyabiashara kadhaa kwa kosa la kufanya biashara kinyume cha sheria, ambapo kila mmoja alitozwa faini ya shilingi 100,000. Hata hivyo, baada ya muda, wengi wao hurudi tena barabarani.

Kwa ujumla, hali ya wamachinga kujaa katika vituo vya daladala inaonesha hitaji la maboresho ya kimfumo badala ya hatua za muda mfupi. Ushirikishwaji wa wadau, uboreshaji wa miundombinu ya usafiri na upangaji bora wa masoko ni mambo muhimu yanayoweza kusaidia kubadili taswira ya biashara katika Manispaa ya Morogoro.

Ikiwa mapendekezo haya yatazingatiwa, si tu kwamba yataongeza matumizi ya masoko rasmi bali pia yataimarisha mapato ya halmashauri, kuboresha mpangilio wa mji na kuinua kipato cha wafanyabiashara wadogo. Mwishowe, suluhu ya biashara holela Morogoro iko katika kuunganisha watu, mifumo na mahitaji halisi ya kiuchumi kwa njia jumuishi na endelevu.

ANDIKO LA: Farida Mangube, Morogoro
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
 
Ukiona hivyo maana yake planners wa serikali siyo practitioners wanajua makaratasi zaidi kuliko mambo ya field, kama wangeshirikisha wadau kwenye planning pengine hilo tatizo lingekuwepo
 
Back
Top Bottom