Mnyauko Fusari kwenye zao la nyanya

Mashima Elias

Member
Dec 22, 2010
18
52
1605512566022.png

Mnyauko Fusari kwenye zao la nyanya.
Mnyauko Fusari (Fusarium Wilt) ni ugonjwa kwenye zao la nyanya, ugonjwa huu pia unaweza kushambulia mazao mengine kama viazi, pilipili, mbilingani, kunde, ndizi n.k, Dalili zake zinaweza kuwa sawia ama tofauti kidogo kwenye kila zao, jambo moja la kuelewa ni kuwa ugonjwa huu una ufanano wa karibu sana na Ugonjwa wa Mnyauko Vitisili (Verticillium Wilt).

Mnyauko Fusari husababishwa na viumbe vya jamii ya Kuvu (Fungi) vinavyoitwa kwa kitaalamu Fusarium Oxysporum, Maeneo mengi yameripoti ugonjwa huu hasa maeneo yale yenye hali ya hewa ya joto, viumbe hivi huishi kwenye udongo wenye wastani wa pH 5 hadi pH 5.6 joto la wastani wa centigredi 28 huwafanya viumbe hawa waendeleze uhai wao lakini pia viumbe hawa kama wakinasa wanaweza kuishi kwenye vifaa vingine vinavyotumika shambani kama Jembe, vifaa vya umwagiliaji kama mabomba, lakini pia viumbe hivi vinaweza kuishi kwenye masalia ya mimea iliyoambukizwa masalia yaliyo juu ya udongo hata yale yaliyofukiwa kwenye udongo hadi kina cha sentimita 100 na vinauwezo wa kuishi kwenye udongo kwa miaka kadhaa, Ukuaji na maisha ya Fusarium Oxysporum huwezeshwa na hali ya joto kwenye Udongo hasa udongo wa Kichanga ulio na Nitrojeni nyingi na Potasiamu kidogo, kwa vile spishi hii huishi kwenye udongo hivyo huingia kwenye mimea kupitia mizizi ya mimea na huenea katika mmea wote kwa njia ya milija ya maji na hasa wakati joto linapokua la wastani wa centigredi 28.

Dalili na Utambuzi wa Mnyauko Fusari kwenye zao la nyanya.
Mnyauko Fusari (Fusarium Wilt) unaweza kushambulia mazao mengine kama viazi, pilipili, mbilingani, kunde, ndizi n.k
Dalili zake zinaweza kuwa sawia ama tofauti kidogo kwenye kila zao na ugonjwa huu una ufanano wa karibu sana na Ugonjwa wa Mnyauko Vitisili (Verticillium Wilt).

Mnyauko Fusari kwenye nyanya mara nyingi husababisha manjano (yellowing) katika jani, njano huanza na majani ya zamani ya chini mara nyingi katika upande mmoja yakifuatiwa na rangi ya kahawia na hatimae kunyauka au kukauka kwa jani na jani kudondoka ama kukatika kirahisi, Mimea iliyoambukizwa mara nyingi hufa kabla ya kukomaa na huonyesha dalili ya kunyauka au kusinyaa hasa wakati wa jua kiasi cha kufanana na mmea uliokosa maji lakini hata ukimwagilia huwa hakuleti tofauti au badiliko lolote, hali hii ni dalili bayana ya ugonjwa huu na hatima yake mmea hufa na ukiung'oa na kupasua kwenye mizizi yake au kwenye vinyweleo utaona rangi ya hudhurungi (dark brown) au kahawia (brown).

Tiba na Udhibiti wa Mnyauko Fusari kwenye zao la nyanya.
Hakuna tiba iliyothibitika ya Mnyauko Fusari, pengine hii ni kutokana na vimelea hivi kuishi kwenye udongo tena kwa miaka kadhaa hali inayoleta ugumu katika kutokomeza ugonjwa huu, lakini kuna mbinu kadhaa za kudhibiti athari au mwendelezo wa spishi inayosababisha ugonjwa huu.

Zifuatazo ni baadhi ya mbinu za kudhibiti Mnyauko Fusari kwenye zao la nyanya.
1. Tumia mbegu zenye ukinzani na ugonjwa huu au mbegu zinazoweza kusitahimili ugonjwa huu (Resistant Varieties) kama kuna historia ya ugonjwa huu kwenye shamba lako ni busara kutafuta mbegu Pinzani na ugonjwa huu na kuzipanda, Watafiti na wazalishaji wa mbegu bora wameweza kuja na mbegu pinzani za ugonjwa huu hivyo itakupasa kuwa na uelewa juu ya maswala ya mbegu na sifa zake, kadhalika hakikisha unatumia mbegu au miche bora, safi na yenye afya.

2. Tibu udongo na vifaa vyako unavyotumia kwenye kilimo hasa ukiwa unataka kusia mbegu yako kwenye kitalu ama kipindi cha kuhudumia miche yako, hakikisha unatibu au kusafisha vifaa vyako vinavyotumika shambani kabla na baada ya kuvitumia hususa ni jembe kwa kuondoo udongo ulioshika kwenye jembe.

3. Ongeza pH. ya udongo wako kutoka 5 hadi 6.5 na 7.0 kwa kuweka chokaa kwenye udongo au mbolea zenye uwezo wa kupandisha pH. ya udongo wako.

4. Epuka majeraha kwenye mimea yako kwani inaweza ikawa ni sehemu ya kuzaliana kwa vimelea vya magonjwa mengine yanayoweza kufanya mimea yako kukosa uwezo wa kuhimili magonjwa na kupelekea kushambuliwa na Mnyauko Fusari

5. Kusanya na teketeza masalia ya nyanya kwa kuchoma moto hasa wakati wa kuandaa shamba na kama kuna mimea iliyoathirika ng'oa na kusanya sehemu moja na choma moto, usifukie masalia au kuyazika aridhini kwani utawafanya vimelea hawa waishi kwa muda mrefu zaidi kwani ndiyo makazi yao.

6. Dhibiti minyoo fundo (Nematodes), wanaweza kuruhusu uingiaji wa vimelea vinavyosababisha Mnyauko Fusari.

7. Lima Kilimo cha Mzunguko. Badilisha zao usilime zao moja au jamii ileile mfululizo kwenye eneo lielile.
Sambamba na hayo ni vyema kufuata kanuni za kilimo bora na ushauri wa wataalamu wa kilimo ili kujihadhari na maabukizi ya ugonjwa huu unaotishia kilimo cha zao la Nyanya.

Imeandaliwa na
Mashima Elias
(Agriculture Field Officer)
Email: mashimae@yahoo.com
 
Dah nikikumbuka hili tatizo lilivyonipotezea mtaji sitamani kulima nyanya tena.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom