SoC04 Mmomonyoko wa maadili na maendeleo ya Taifa la Tanzania

Tanzania Tuitakayo competition threads
May 23, 2024
14
41
utanguizi.
Mmomonyoko wa maadili si neno geni hata kwa sikio jipya. Ki falsafa mmomonyoko wa maadili ni ukiukwaji wa utamaduni mama uliokuwa sahihi ki msingi; ni kinyume na kila utaratibu wa utu.
Nachelea kusema, Mmomonyoko huu kuna namna tumekwisha kuuhalalisha kama jamii kwa kisingizio cha utandawazi na vichochezi kadha wa kadha.

vyanzo:
Vipo vyanzo vingi vinavyoweza kuchagiza mmomonyoko wa maadili, nitaorodhesha na kuviangazia vichache kwa mapana kadri Mungu atakavyoniwezesha.

chanzo 1. KUIKANA ASILI YA MTANZANIA.
Wazee wa zamani walipo sema, "mkataa kwao ni mtumwa" ni kama walikiongelea kizazi hiki cha hivi sasa. Kizazi kinachoikataa asili ya kuzaliwa na kuiishi asili ya mataifa mengine na kuifanya mfumo wa maisha. Ndio, mtanzania kuamini mgeni ni wa maana kuliko mwenyeji atakaye msitiri taabuni wala si jambo geni. Kuamini Lugha za wenzetu ni bora kuliko kiswahili, si jambo la kushangaza tena. Kufikiri, mavazi yaliyovaliwa na wa huko ughaibuni (mtumba) ni imara na ya mtindo mzuri kuliko ya wabunifu wa ndani ni gonjwa lililowafikia hadi watoto wala hatuichukulii hii kama aibu yetu. Kuamini vyakula vyao ni vya afya kuliko vyetu, kujihimiza mtindo wao huru wa malezi ni bora kuliko wa kwetu; sambamba na kubeba mfumo wao wa mahusiano/familia na kuchagua kuuishi bila kuzingatia hata chembe, nguvu na uimara wetu. Yapo mengi ya kutambulisha na kuelezea namna tumeikana asili ya mtanzania kwa imani tuliyoibeba visisyo, ya utandawazi. Pengine kama si kuikana asili ya mtanzania tungekuwa bado kwenye mstari wetu uliohimiza stara na malezi yenye mafundisho.

chanzo..2. MTOTO WA MWENZAKO.
Wakati wa makuzi yangu, mazingira niliyokulia bado dhana ya "MTOTO WA MWENZAKO NI WAKO," Ilifanya kazi. Hofu ya kutenda mabaya haikuishia kwenye uzio wa nyumbani au mazingira alipo mzazi wangu, popote penye mtu mzima, ni haramu kutenda tofauti na utamaduni wa jamii ile. Kama asipokuadhibu uliyemvunjia heshima, basi utaadhibiwa hata na mgeni asiyekujua na tamati ya yote utabwagwa miguuni kwa wazazi wako ambapo napo utakumbana na adhabu kali. Hali hii imetoweka, kama kuna pahala Tanzania hii, utamaduni huu bado unafanya kazi, basi nipewe shamba nikalime huko maana udongo wake utakuwa na rutuba sana. Zama hizi "mtoto wa mwenzako, ni mkubwa mwenzako" Madhara ya hili kwa jamii inayokua, kutanuka na kuchangamana kimaadili ni makubwa sana. Yako bayana, yameondoa mpaka wa adabu kutoka kwa mtoto kwenda kwa mtu mzima na yamebatilisha 'utu' kutoka kwa mtu mzima kwenda kwa mtoto.

chanzo 3. UMASIKINI.
Kila mmoja atastaajabu ni kwa namna gani umasikini unachangia katika mmomonyoko wa maadili, hata mimi awali kabla sijafanya utafiti wangu mdogo, nilistaajabu. Wacha tutazame hili kwa jicho lisilo na hisia;
Mambo mengi ya kikatili yanayoendele na yaliyowahi kutokea na kuwaacha watu wakiwa watupu wa maneno yalisababishwa na umasikini. Ukisikia mauaji ya Albino, vikongwe, watoto wanawake na baadhi ya mauaji ya wanaume yamehusishwa moja kwa moja na imani za kishirikina ama kigaidi zenye lengo moja tu, kuondoa ama kupunguza umasikini kwa mfanyaji.
Ukisikia baadhi ya matukio ya ubakaji na ulawiti kwa walemavu, wazee na watoto kiini chake ni imani potofu iliyomhamasisha mfanyaji kuwa baada ya kutenda ukatili huo ama mwingine atapunguza ama kuondokana na umasikini. Bila shaka umewahi kusikia biashara ya viungo vya mwili wa binadamu? Bila shaka unaijua biashara ya ngono? Haya ni kwa uchache wa mambo ya kikatili ama matendo yasiyo ya kiutu ambayo hufanywa ili kutafuta kukwamuka kwenye umasikini.

Yanachagiza vipi mmomonyoko wa maadili? Iko hivi, palipopandwa ukatili mara zote humea uharibifu. Palipopandwa tamaa ya kufanikiwa haraka maishani mara zote humea ukatili, iwe wa kimwili ama wa kiakili. Sasa basi kama tutajaza taifa la vijana waliokatiliwa kingono utotoni na hawakupata msaada stahiki, tutakuwa na wazazi wanaoendeleza ukatili kwa watoto wao ama kwa watoto wa wenzao. Tutakuwa na taifa la watu wasioonea haya ushoga na kuupigia chapuo ukahaba. Ndio miaka ijayo ya hiki kizazi kinachosikia na kushuhudia mambo ya kikatili yanayoacha athari hasi ubongoni, itakuwa ni miaka yenye mmomonyoko mkubwa zaidi wa maadili.

chanzo 4.MISINGI.
Katika Biblia, maandiko yanasema, kwenye Zaburi 11:3, Kama misingi ikiharibika, mwenye haki atafanya nini?
Kama wazazi tunaolea sasa hivi ni chimbuko la malezi yasiyolenga tamaduni na asili yetu, huyu mtoto atafanya nini?
Tumehimiza uwepo wa elimu lakini natamani kama tungehimiza kwa ukubwa huo huo umuhimu wa maarifa kwenye kila pembe, haswa hii ya mahusiano na malezi.

Wazazi wengi wa kisasa wamesoma na hata wale ambao hawajasoma basi wamekuja kuuelewa umuhimu wa elimu, asilimia kubwa watoto wanapata elimu ya darasani. Elimu hii ni elimu jumuishi, vinakutana vichwa elfu tano kutoka itikadi na tamaduni tofauti. Kama mtoto hajapandwa mbegu ya msingi ya maadili bora, ni wazi ataiga. Hapo kwenye kuiga sasa ndo kuna kasheshe. Yeye ni kama debe tupu, anajazwa chochote kijacho kutoka kwa yoyote.. Na hapa ndipo tunapata mlipuko wa misingi ovu endelevu. Ukisikiliza hadithi za mashoga watano, mmoja kaanzia shuleni, hii ni tafiti ndogo niliifanya kibinafsi.
Maana yake ni nini?
Unapeleka mtoto shule akiwa na maswali mengi ya kiukuaji na kijinsia yaliyokosa majibu ya kueleweka, anaenda kupandikizwa majibu hasi yanayomjengea msingi mbovu... hii ni kwa sababu hakuwa na msingi wowote mama.

chanzo 5. AFYA YA AKILI.
Kutokana na mapana ya upatikanaji na usambaaji wa taarifa, ugunduzi wa ongezeko la matatizo ya afya akili umebainishwa.
Swali ni je! Afya ya akili ina uhusiano gani na mmomonyoko wa maadili?

Nachelea kusema kwa asilimia fulani tumejikuta katikati kama taifa la watu wanaopuuza sana. Kwa sababu nyingi mfanowe ni:
Upatikanaji duni na makini wa elimu ya afya ya akili, shinikizo la kitaaluma na uamini kwenye janga hili.
Sijui kama ni imani tu, au ni namna yetu na nguvu ndani yetu vimetuchagulia kutoamini uwepo mkubwa sana wa tatizo hili. Fikiria, kwa akili ya kawaida, malezi na utamaduni wetu, ni maamuzi mepesi binti kujifanya mwanaume? Hapa siongelei suala la homoni, naongelea suala la maamuzi halisi. Ni maamuzi tu ya kawaida mwanaume kukubali kuolewa na kuwa mke? Tukitoa suala la tamaa, umasikini na ushawishi mbaya, ni maamuzi madogo hayo? Ni maamuzi ya kufanywa na binti au kijana wa kiume mwenye utimamu na nguvu ya kimaamuzi akilini? Tatizo la afya ya akili lina mchango mkubwa kwenye mmomonyoko wa maadili, haiingii akilini, mtoto ambaye hajaathirika na lolote ubongoni kumtukana au kumpiga mzazi wake. Haiingii akilini, mtu timamu mwenye imani na elimu kumgeuza mtoto wake wa damu kichezeo cha ngono. Tatizo la afya ya akili ni halisi.

Tayari nimeangazia mambo matano ambayo kwa namna moja ama nyingine ni vichocheo vya mmomonyoko wa maadili, katika vyanyo hivyo, kila kimoja kinapiga kwa namna yake maendeleo ya Taifa letu. Na hapa sote tunakubaliana, hakutakuwa na taifa lenye maendeleo endelevu kama hakutakuwa na kizazi chanya na chenye maadili kwenye Taifa husika.

NINI KIFANYIKE?
Yapo mengi sana ya kufanya, lakini mimi nitasimama na hivyo vipengele nilivyochagua kuviangazia.

kifanyike. 1.KUIKATAA ASILI;
(a)Kwenye mtaala wa elimu katika somo la maarifa ya jamii kufanyiwe matengenezo. Kwanini somo la maarifa ya jamii lisijikite kwenye kufundisha maarifa yaliyoasisiwa na mababu na yakawa na tija kwa vizazi nyuma yetu? Kwanini ile misemo ya kiswahili iliyokanya, onya na kuleta hofu ya ubaya isitengenezewe masomo na yakatumika kuwajenga watoto kuukulia utamaduni wa mtanzania? Maswali haya mawili yakipata majibu chanya yanaweza kupunguza mzigo wa mada vitabuni zisizojenga chochote cha zama hizi. Kadri ulimwengu unavyopambazuka, kama nchi tunapaswa kupambazuka pia. Tuna kila sababu ya kuachana na masomo ya kufikirika na badala yake yawekwe masomo halisi yanayoishi. Asili, malezi na utamaduni wenye kubeba ile asili nzuri ya mtanzania uwekwe kwenye mtaala wa elimu yetu. Elimu ya ujamaa irejeshwe ikiwa imeboreshwa, kuna namna ilichochea utu.

(b) Tanzania tunalima pamba yenye ubora wa kuiuza kimataifa ama sivyo? Kwanini viziwepo viwanda vya kuchakata pamba na tuuze vitambaa huko kwa wenzetu kama wao watufanyiavyo? Kwanini serikali isione kuna haja ya kuwekeza kwenye viwanda ghafi badala ya kuua ubunifu wa watu wa ndani? Kama kutakuwa na kiwanda kikubwa hapa nchini, kinachozalisha vitambaa, mfano vya pamba yetu halisi kama ilivyo kwa vichache vinavyotengeneza kanga na vitenge visivyokidhi soko na kupelekea uagizwaji mkubwa wa vitenge kutoka China basi pengine tayari tungekuwa na vazi la asili kutoka kwenye zao linalolimwa nchini kwetu. Tazama China, kuna viwanda vingi na vinavyozalisha kwa urahisi bila vikwazo, usumbufu wala mlundikano wa kodi, kitu kilicholipa taifa lile wageni wengi wanaoenda kuilipa kodi bila kulazimishwa wanunuapo bidhaa kutoka China. Vipi kama wawekezaji wa ndani wangepewa vipaumbele na urahisi wa ufanyaji kazi? Vipi kama wangekopesheka bila hekaheka nyingi? Ni wazi ingekuwa rahisi kukabiliana na mtumba ambao kwa asilimia fulani unavalika mno kutokana na kuuzwa bei chee. Ni ngumu sana kumvua mtu nguo na usimpe ya kuvaa. Wapo mafundi na wabunifu wazuri mno nchini, kama tungekuwa na viwanda vikubwa vya mali ghafi tungeweza kukuza pato la taifa kwa kuuza nguo za kitanzania kwenye masoko yetu na kuhamasisha uvaaji mzuri. Nikupashe tu, wakongomani na watu kutoka mataifa mbalimbali pembezoni na ndani ya Afrika mashariki, huja kununua nguo na bidhaa za mavazi hapa Tanzania zilizoranguliwa China, Uturiki na mataifa mengine. Vipi kama tungekuwa na bidhaa hizo tena zenye ubora na bei nzuri zilizozalishwa hapa hapa nchini? Mbali na kukuza pato la taifa tungekuwa na cha kuwapa wanaoamini mavazi kutoka nje ni mazuri zaidi. Tungekuwa na kipimo cha kimaadili kuanzia kwenye mavazi.

(c) Bado nchi ina mashamba mengi na mapori nje ya yale ya hifadhi. Kwanini basi kilimo cha asili kisipewe nafasi? Kwanini wananchi wenye uwezl wa kulima wasipewe mashamba walime japo vile vya msimu? Kwa rutuba tuliyonayo hakuna mtanzania ambaye angetakiwa kununua mchele uliolimwa nchini kwake elfu nne, wala mahindi kwa elfu mbili na miatano. Hakungetakiwa kabisa kuwepo mfumuko wa bei ya sukari hadi kufikia kilo elfu 5. Mashamba yapo, kwanini msiwape watu au kampuni za wazawa ziyalime? Watu wanathamini vyakula kutoka nje kwa kudanganyana swala la ubora ila ukweli ni kwamba gharama ya chakula Kinacholimwa hapa Tanzania ni kubwakuliko kununua ya kigeni. Serikali iangalie, kuna ulazima gani wa kuweka kodi kubwa kwenye nyama inayozalishwa hapa hapa nchini? Hivi kweli kuna ulazima wowote wa kilo ya nyama ya ng'ombe kuuzwa elfu 12?

Najua kuna watu wanauliza jambo hili lina uhusiano gani na mmomonyoko wa maadili, ni hivi:
Mazoea hujenga tabia, na tabia ikijengeka ni rahisi sana kuambukizika. Mtu atanza kuona nguo kutoka uturuki ndio nzuri, atafuata kuona maindi kutoka marekani ndio ya gharama nafuu, ataanza kuamini, samaki kutoka Pacific ndio zenye madini muhimu mwilini, taratibu atajivua utanzania na kuanza kuamini hakuna jema linaloweza kutoka Tanzania. Nini kitafuata?
Imani chanzo chake si ni kusikia? Ushawishi ukienea na kuhakikisha mahitaji yote matatu muhimu ya mwanadamu ni kutoka nchi za watu ni nini kitamfanya mtu huyu asiamini ushoga ni haki ya binadamu? Ni jambo gani jema kuhusu Tanzania utaliongea kwake akaliamini? Tutazame sana katika kutengeneza/kuiboresha asili mama na kuifanya ipendwe na watanzania.

kifanyike 2.MTOTO WA MTU NI WAKO.
Natamani iundwe kampeni maalumu kabisa itakayosimamiwa na wizara ya jinsia maendeleo na watoto, isemayo MTOTO WA MWENZAKO NI MTOTO WAKO.
Kampeni hii ilenge sana kwenye kutoa elimu kwa mwanamke, mwanaume na kijana, juu ya utu na ubinadamu wetu.
Elimu isiwe ile ya nadharia tu, iwe elimu inayotekelezeka ki mfumo na kiutendajì. Kampeni ishikiwe bango na vyombo vyote vya habari, kampeni ishikiwe bango na imani zote za kidini. Na kila ipigwapo ngoma hiyo, itoe sauti isemayo MTOTO WA MWENZAKO NI WAKO.
Hakuna kitu hujenga ama kubomoa kama imani, kama mtu atajengewa imani hasi, hakika itageuka maisha yake na kama mtu akijengewa imani chanya hakika ataiishi.. Imani ya kumfanya mtu mzima kuhisi kila mtoto ni mtoto wake itasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili. Itapunguza sana ubakaji na ulawiti wa watoto. Itapunguza unywaji pombe na utumiaji wa madawa ya kulevya kwa sababu hakuna pahala pa kujificha. Itapunguza ukatili majumbani haswa kwa mabinti wa kazi. Itahimiza walimu kufundisha kwa moyo kama zamani. ITACHOCHEA UTU. kila mtu ataanza kujiona mwenye jukumu juu ya nafsi ya mtu mwingine na zaidi ya yote itatengeneza kizazi ama jamii yenye UPENDO.

kifanyike 3.UMASIKINI.
(a)Kuwe na mfumo wezeshi wa elimu ambao haumfanyi msomi kuwa tegemezi na mzembe. Kila taaluma itolewayo itolewe kwa mfumo wa utendaji tena, wenye kuendana na zama hizi za teknolojia.
Sasa si kama zamani kwamba umasikini unaletwa na ujinga, sikuhizi wapo wenye elimu isiyo na maarifa ya kuwakwamua kwenye umasikini. Nauangalia mfumo uliotumika kuijenga China kwa jicho la kipekee. Wachina sio watu wavivu wa kutaka kaa tu ofisini. Mchina hata akija hapa nchini kama Injinia mkubwa lazima utakutana naye kwenye kazi. Maana yake ni nini? Mfumo wa elimu usikomae na maksi za karatasini bali ziangazie uwezo wa ndani wa kiutendaji. Uwepo ufadhili wa moja kwa moja wa serikali kwenye masomo ya fani na ufundi. Kuwe na uhuru kwa mtoto aliyemaliza elimu ya msingi kuchagua kuendelea na madarasa ama kusaidiwa kulea na kuendelezwa kitaaluma kwenye kipaji alichonacho. Taifa la kesho lenye akili mnemba linahitaji uwezo wa asili wa mwanadamu kutengeneza kitu kipya. Utajiri uko ndani ya vitu vipya.

(b).. Huwezi kuumaliza umasikini kama utasimama upande mmoja. Kumekuwa na wimbi kubwa mno la mmomonyoko wa maadili lililochochewa kwa kiasi kikubwa na watu maarufu (waliotambulishwa na vipaji) Umewahi kujiuliza kwa nini?
Wacha nijibu kwa mtazamo binafsi,
Ukifuatilia historia ya wasanii wengi ni watu waliojiumba ama kuumbwa na watu fulani kuwa wasanii. Mtu aliyejiweka mwenyewe, kwa kupitia mateso na maumivu mahali fulani kuna ulimbukeni lazima anakuwa nao. Kuna kiburi tu anakipata, asipopewa elimu, anawaaminisha walio nyuma yake pesa inanunua kila kitu. Asipokuwa mtovu wa nidhamu, anaweza kutumia pesa kupotosha na dhana ya umasikini kuacha madoa ikasimama kidedea. Kama kungalikuwepo mkono wa serikali katika kulea na kuendeleza vipaji vya watoto na vijana basi hivi leo Mimi ningetimiza ndoto ya kuwa mwandishi mkubwa bila maumivu.
Hao wasanii ambao tayari ni (self mae) wapewe elimu juu ya kuwa kioo cha jamii, watuondolee huu msemo wa MASIKINI AKIPATA MATAKO HULIA MBWATA.
Naiomba serikali yangu tukufu.
Ianze kuamini na kutengeneza mikakati bora ya kulea na kuviwezesha vipaji kuchanua. Ukifuatilia taifa kama Uturuki kwa sasa hivi pato lake kubwa la kigeni linatokana na kazi za sanaa na fasihi. Kuna waandishi wazuri sana, kuna wana muziki wenye tungo za kimaadili na kitamaduni, kuna wacheza ngoma za asili, kuna waigizaji wenye vipaji vya kushangaza ila wamebaki kuwa masikini kwa sababu hakuna njia. Serikali itengeneze njia. Iwekeze kwenye sekta zinazohusisha sanaa na fasihi, kuna namna huku kunaweza kupunguza umasikini. Lakini umasikini upungue katika dhima sahihi na sio ya kuuza utu upate kitu.
Mifumo ya kuukimbiza umasikini ipo lukuki ni swala la "Tunalea kizazi gani? Kipaji bila maarifa ni kama kutwishwa gunia la misumari kwenye paji la uso. Serikali iandae mfumo wezeshi wa maarifa kwa watu wenye karama na vipaji mbalimbali. Mfumo huo ujumuishe elimu juu ya kipaji, msaada wa kuingia sokoni na elimu juu ya umaarufu. Umasikini ukipungua mmomonyoko wa maadili utanyong'onyea. Hakutakuwa na wa kumdhalilisha mwenzake kama ki viwango tutakaribiana. Wapeni nafasi wenye jitihada.

kifanyike 4.MISINGI
Jambo kubwa na muhimu la kufanyika hapa ni kujengwa upya kwa misingi. Haiwezi kuwa rahisi lakini inawezekana kwa sababu bado kuna watoto na wanazaliwa wengine. Inawezekana kwa sababu bado kuna vijana ambao wanaweza kufundishika.
Elimu ya malezi iende sambamba na elimu ya ujana. Ikiwezekana mtoto kwanzia kidato cha kwanza ajifunze malezi. Ndani ya kujifunza malezi atapata kwana kujiona yeye kama mtoto ni wapi anakosea na ajapokuwa mtu mzima atapaswa asikosee wapi. Elimu ya malezi na mahusiano kwa wenzetu tunaowaigaiga ni kitu cha mazingatio mno. Wanaamini malezi mabaya ni chanzo cha mahusiano mabaya. Ni vyema elimu ya malezi iwepo na itolewe kwa weledi. Kwenye malezi ndipo ulipo msingi.
Serikali itoe nafasi kwa wabobezi wa malezi kutoa madarasa ya malezi kupitia vyombo vya habari. Kumshawishi mtoto kuharibika ni rahisi sana kama hajui kuwa anakwenda kuharibika ila kumshawishi mtoto mwenye misingi imara ya kitabia iliyokumbatwa na hofu ya Mungu ni ngumu mno. Elimu ya malezi ni muhimu sana kwa hizi zama. Huu utandawazi na teknolojia vitumike kukuza maarifa yenye tija.
Msingi mzuri wa malezi ni chanzo kizuri cha mahusiano binafsi na mahusiano ya mtu na jamii yake.


kifanyike 5.AFYA YA AKILI.
Naiomba serikali yangu tukufu ikubaliane na ongezeko la janga hili na ichukuwe hatua. Wakati mwingine mmomonyoko wa maadili unachochewa na baadhi ya magonjwa ya akili yasiyo na athari za moja kwa moja.
Moja ya vipimo ambavyo vinahitajika na ikiwezekana vipigiwe chapuo kufanyika mara kwa mara ni kipimo cha afya ya akili. Tuko na wazazi walioathiriwa na 'trauma' za utotoni na wanawapeleka huko huko watoto wao bila kujua. Taifa salama lenye maendeleo linataka watu wenye afya njema ya akili.

HITIMISHO;
Mmomonyoko wa maadili unao uwezo wa kulipa taifa umasikini, maradhi na udumaavu. Hii ni kwa sababu, kadri maadili yanavyomomonyoka watu huacha njia zao na kufuata zisizofaa. Wengine huingiliana kinyume na mapenzi ya Mungu na kuishia kuambukizana magonjwa, wengine huingiliana na wanyama na kuishia kuibua magonjwa mapya. Kwenye magonjwa tunapoteza nguvu kazi ya taifa. Kwenye kukosa nguvu kazi tunapoteza rasilimali watu, na hapo taifa litazidi kuwa masikini.
Mmomonyoko wa maadili huhalalisha udhalimu, mfano ushoga na usagaji. Taifa lenye wanaume mashoga na wanawake wasagaji haliwezi kukua litadumaa tu. Kwa sababu kwanza ni chukizo kwa Mungu. Niiombe serikali, iwekeze nguvu kwenye kutoa elimu na maarifa pamoja na kuurejesha utamaduni wetu uliochochea sana uwepo wa maadili.

MAARIFA SAHIHI YATAPUNGUZA NA MWISHO YATAMALIZA MMOMONYOKO WA MAADILI
 
Kuamini vyakula vyao ni vya afya kuliko vyetu
Inasikitisha, watanzania tunaweza kuvipata vyakula na vinywaji vilivyoandaliwa kiasili lakini cha kishangaza tunapoteza pesa kushadadia vyakula ambavyo nje wanakula watu wasio na kipato cha kula vyakula asili (organic). Vitu kama pitzza burger soda chips kule kwa wenzetu ni fast food za wasio na muda.

sambamba na kubeba mfumo wao wa mahusiano/familia na kuchagua kuuishi bila kuzingatia hata chembe, nguvu na uimara wetu
Wangejua wazungu wenyewe wametafiti na wakaona kuwa mahusiano imara ya karibu ndio cha msingi zaidi maishani. Tunaowaiga ujinga wameshasanuka.

Ndio miaka ijayo ya hiki kizazi kinachosikia na kushuhudia mambo ya kikatili yanayoacha athari hasi ubongoni, itakuwa ni miaka yenye mmomonyoko mkubwa zaidi wa maadili
Hatujachelewa, tufanye tusifike huko kama Marekani anavyohangaika na tatizo la 'serial killers' chanzo mojawapo ni watoto kuishi ukatili na kukataliwa au kutothaminiwa kwa mtu binafsi hadi anaamua kuukataa utu, kuukataa ubinadamu na kuvaa unyama. HATARI. Na haiishii kwake tu, ni jamii nzima. Rejea panya road.

kila mtu ataanza kujiona mwenye jukumu juu ya nafsi ya mtu mwingine na zaidi ya yote
🤗

Serikali itengeneze njia. Iwekeze kwenye sekta zinazohusisha sanaa na fasihi, kuna namna huku kunaweza kupunguza umasikini. Lakini umasikini upungue katika dhima sahihi na sio ya kuuza utu upate kitu.
Nakubaliana na wewe. Serikali inaweza kutengeneza timu ya kuchunguza script za filamu na mashairi. Na yule anayetengeneza kitu kinachojenga jamii basi anapatiwa ruzuku maana amefanya kazi ya manufaa kwa jamii. Public interest calls for public funding. Na kinyume chake pia. Anayeharibu jamii ni kumpiga faini kali.

Niiombe serikali, iwekeze nguvu kwenye kutoa elimu na maarifa pamoja na kuurejesha utamaduni wetu uliochochea sana uwepo wa maadili.

MAARIFA SAHIHI YATAPUNGUZA NA MWISHO YATAMALIZA MMOMONYOKO WA MAADILI
Ahsante sana. Tuangalie maendeleo ya kiakili na kimaadili ya taifa kwa umakini. Watu wenye akili njema ni taifa jema kiotomati
 
Back
Top Bottom