Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna, Suleiman Kova akionyesha picha ya Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya REGIONAL CARGO SERVICES LTD,ABDULKADIR S/O KASSIM ABDI, Miaka 38, Mkazi wa Temeke Mikoroshini ambaye anatuhumiwa kwa kutoa makontena 329 kwenye bandari kavu ya AZAM (AZAM ICD) bila kulipia kodi anayetafutwa na jeshi hilo pia ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni za ?JAS EXPRESS FREIGHT LTD? na ?XL CLEARING AND FOWARDING Co. LTD? ambazo zote zilitumika kutoa makontena hayo. Ameonyesha picha ya mtuhumiwa huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
JESHI la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa 40 ambao wanahojiwa kwa tuhuma za kula njama na kuikosesha serikali mapato. Uchunguzi unafanywa kwa pamoja na maafisa wa Jeshi la Polisi na Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) kwa lengo la kubaini jinsi ambavyo makontena 329 na mengine 2489 yalivyotolewa bandarini kinyume cha taratibu.
Kati ya hao, watuhumiwa 26 ni watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)na watumishi 03 kutoka Bandari kavu (ICD) YA AZAM wanatuhumiwa kuhusika na upotevu wa makontena 329. Aidha, watuhumiwa 11 ambao ni watumishi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kwa kuhusika na upotevu wa makontena 2489.
Uchunguzi unaoendelea pia unahusisha kupitia kumbukumbu mbalimbali na kadhia za forodha ili kubaini mtindo uliotumika na kuwabaini wote waliohusika katika mchakato huo. Makontena 329 yaligundulika kukosekana kwenye ICD ya AZAM kuanzia mwezi Julai hadi Novemba 2015, wakati makontena 2489 yaligundulika kutolewa Bandarini kuanzia Mwezi Machi mpaka Septemba, Mwaka 2014 kinyume cha taratibu kwa lengo la kukwepa kodi na ushuru.
Uchunguzi bado unaendelea ili kuwabaini wote wanaohusika na hatimaye majalada ya kesi yatapelekwa kwa mwanasheria wa serikali ili watuhumiwa watakaobainika kuhusika na makosa mbalimbali wafikishwe mahakamani.