MKEMIA Mkuu wa Serikali, Dk. Ernest Mashimba, amefariki dunia usiku wa kuamkia jana akiwa katika Hoteli ya Lushoto Executive Lodge aliyokuwa amefikia mkoani Tanga.
Akizungumza kwa njia ya simu na Tanzania Daima, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Liberatus Sababs alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, na kusema marehemu alifariki jana akiwa usingizini.
Alisema wahudumu wa hotel hiyo, waligundua kutokea kwa kifo hicho majira ya saa 4 jana, wakati wakitaka kufanya usafi wa vyumba baada ya
kugonga muda bila majibu kujibiwa, hali iliyosababisha watoe taarifa kwa uongozi wa juu wa hoteli hiyo ambao uliamua kuchukua funguo za akiba na kwenda kufungua mlango.
Kamanda Sabas alisema uchunguzi zaidi kuhusu kifo hicho unaendelea na taarifa rasmi itatolewa leo.
Habari za kuaminika zinasema, Dk. Mashimba alikuwepo Lushoto kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za binti yake anayesoma Shule ya Sekondari ya Wasichana Kifungilo, ambapo alialikwa kama mzazi rasmi, aliyewakilisha wazazi wa wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne mwaka huu.
Katika hutuba yake, aliyoisoma kwa niaba ya wazazi, Dk Mashimba alisisizita watoto wa kike kupewa kipaumbele katika elimu, kwani ikiwa wataelimishwa wanayo nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko.
Alitoa mifano, mbalimbali ya baadhi ya wanawake walofanya vizuri katika uongozi baada ya kushika nafasi za juu akitoa mfano wa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha Rose Migiro.
Katika hafla hiyo, marehemu aliahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni moja kwa ajili ya intaneti shuleni hapo.
Pia katika sherehe hizo, Dk. Mashimba alinunua gazeti lililoandikwa na wanafunzi kwa sh 100,000 huku akitoa sh 50,000 kwa ajili ya motisha kwa walimu wa shule hiyo.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima.