Mkataba wa Bandari: Anayekiri makosa na kuomba msamaha asamehewe kisha twende pamoja

Bams

JF-Expert Member
Oct 19, 2010
16,547
41,060
Yapata mwezi mmoja uliopita, nikiwa Dodoma nilikutana na watu kadhaa, miongoni mwao ni wabunge wawili, mmojawapo aliwahi kuwa Naibu Waziri hapo awali. Hii ni kabla ya hukumu ya mahakama, ni kabla ya waovu kuwakamata watu walioamua kusimama mbele kupigania rasilimali bandari zetu, na ni kabla ya waraka wa Wahashamu Baba Maaskofu. Wabunge hawa walisema wazi kuwa kwa kweli mkataba wa DP haukupelekwa bungeni kwaajili ya kujadiliwa bali ulipelekwa ili ionekane umepitishwa na Bunge, na kwamba ilijulikana kuwa ni mkataba mbaya ndiyo maana walizuiwa kuujadili.

Wabunge hawa wakaeleza kuwa kabla ya mkataba huo kusomwa Bungeni, walitakiwa kuhudhuria kikao cha chama ambako walipewa maelekezo kuwa wanatakiwa kuupitisha. Wakaeleza kuwa hata wabunge walioongea, ni wale waliopangwa kuusifia. Na wanahisi Mdee kupewa nafasi ya kuongea, na kisha kuukosoa huenda Spika hakutegemea kama angefanya hivyo.

Wabunge hawa walionekana kutopendezwa na kile kilichotokea, lakini ni kama watu wanaoona kuwa ni lazima kuwa wanafiki ili maisha yaende.

Kama wabunge wangekuwa wanajitambua, wasingekubali kuburuzwa kwa namna hiyo. Naamini, hata ile namna ya hawa watu walivyopatikana (baadhi kutangazwa bila ya kuchaguliwa, na wengine kwa wizi wa kura), na hulka ya unafiki iliyojengeka ndani ya CCM na hata ndani ya bunge lenyewe, hakuna anayekuwa na ujasiri wa kupinga kitu ambacho nafsi yake haikubaliane naye, na mamlaka zilizowapa huwa ubunge, zinataka.

Kwa hapa tulipofika, ni busara sana kwa wale ambao nafsi zao zinawasuta kutokana na uhusika wao kwenye mkataba ule wa hovyo kabisa, kuuvua uwoga na kuuvaa ujasiri, na kutamka wazi kuwa walikosea na hawakutimiza wajibu wao. Waombe msamaha, nina imani Watanzania watawasamehe, tutasonga mbele pamoja. Hiyo haitajalisha kama anayeomba msamaha kama ni mbunge, ni polisi, ni mwanahabari, ni waziri au kiongozi wa chama.

Kwa Rais Samia, kutangaza tu kuufuta huu mkataba, atakuwa ameomba msamaha kiutuuzima, hata asipotoa kauli ya kuomba msamaha.

Taifa letu ni muhimu kuliko chochote anachoweza kukipata, iwe ni rushwa binafsi au ya kitaasisi. Na tujue kuwa hakuna Taifa pasipo umoja, amani na maelewano.

Baadhi wamekwishaanza kuifuata njia hii. Mbunge wa Bunda, yeye amesema wazi kuwa wala hata kuusoma huo mkataba hakuusoma kwa vile hata lugha iliyotumika, hana ujuzi nayo. Watu wa namna hiyo siyo wa kuwabeza, bali tuwapongeze kwa kujitokeza na kuunena ukweli. Mbunge wa Nkasi, yeye alisema wazi kuwa walikokotwa na kuambiwa wanaenda Dubai, hata hawakuambiwa wanaenda kufanya nini. Kumbe ilikuwa kuipa syndicate uhalali.

Najua ugumu upo zaidi kwa wale wanaotajwa kuhongwa pesa taslim, magari na nyumba. Hawa wana hofu kubwa. Maana kukana hadharani kunaweza kuchukuliwa na waliowahonga kuwa waliwatapeli kwa kuchukua pesa na kuwadanganya kuwa watahakikisha kwa vyovyote mkataba unapitishwa.

Mkataba ni wa hovyo, ni haramu na haufai kwa jamii yoyote. Uharamu wake umenenwa na watu wengi, tena wabobezi sana. Kama kuna yeyote ambaye mpaka leo haoni uhovyo wa mkataba huo basi rushwa aliyopewa, siyo tu itakawa imepofusha akili yake, bali rushwa aliyoila imeua na kuteketeza kabisa akili, dhamira na nafsi yake.

Hongereni ma asanteni Wahashamu Maaskofu, hongera na shukrani sana Madeleka, Mwambukusi, Mdude, Slaa kwa kujitoa sadaka kwaajili ya Watanzania. Asanteni sana TLS, Prof. Shivji, Mzee Butiku na Mzee Warioba, kwa maana hamkupindisha maneno ili kuoulizwa manukato uozo.

Ukweli na wema vinaweza kuchelewa, lakini mwishoni lazima ushindi upatikane.
 
Back
Top Bottom