OMBAOMBA ALIYEUZA WANAE- 3
NYUMBANI kwa mama Emiliana, Modester aliishi vizuri sana, yaani utadhani alikuwa ni mtoto wa pale. Hakunyanyaswa wala kusemwa tofauti, zaidi alipewa mahitaji yote muhimu kama walivyopata kina Emiliana na Jackson.
“Tumuandikishe shule?” Siku moja mzee Lauliani, baba wa familia ile alimwambia mkewe.
“Mh!” Mama Emiliana aliguna. “Na umri huo, atakubali kweli?”
“Zungumza naye, anapaswa tu kukubali…akafute ujinga!”
Mama Emiliana alizungumza na Modester juu ya jambo hilo la kuandikishwa tena shule ya msingi baada ya kukatisha masomo Singida akiwa darasa la pili, jambo ambalo hakulitegemea, Modester alilipokea kwa furaha sana jambo hilo.
Akaandikishwa shule.
Akiwa shuleni alikuwa anafanya vizuri sana. Zaidi akawa anawafundisha wanafunzi wenzake ubaoni pale ambapo mwalimu hakuwa darasani. Walimu wakamuona ni kichwa, wakamrukisha madarasa.
Darasa la kwanza alilisoma muhula mmoja, muhula mwingine akausoma akiwa darasa la pili. Ikawa hivyo katika miaka iliyofuata, katika mwaka wa tatu Bi Modester akawa amefika darasa la sita. Mwaka wa nne alipoingia darasa la saba, aliingia pamoja na Emiliana!
Kwenye mtihani wa kumaliza shule ya msingi wawili hao walifaulu pamoja, tena walipangwa shule moja.
Kutokana na kusoma shule moja na kuishi pamoja nyumbani Modester na Emiliana walitokea kuwa marafiki wakubwa sana, walioshirikiana kwenye mambo mengi, na pia walidokezana juu ya siri zao.
Kwa upande wa Jackson, kina Modester wakiwa kidato cha pili, yeye alimaliza kidato cha nne, na matokeo yalipotoka alikuwa amefaulu kujiunga kidato cha tano nje ya jiji, kwa hiyo baada ya kwenda shuleni muda mwingi wakawa mbali naye, walikutana kipindi cha likizo.
Miaka ikasonga mbele, Modester na Emiliana wakamaliza kidato cha nne, wakati Jackson yeye akimaliza cha sita. Bahati mbaya hakufaulu kwenda chuo kikuu. Baba yake mzee Lauliani alimtafutia nafasi jeshini alikokuwa na jamaa zake wanaofahamiana.
Akaenda huko.
Kina Emiliana na Modester walipomaliza kidato cha sita, walifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mlimani. Modester akisomea masuala ya saikolojia na mwenzie akisota na sheria!
Wakati huo, Jackson alikuwa mwajiriwa jeshini, kwa muda wa miaka miwili, na alifanyia kazi katika kituo cha Lugalo!
***
WAKIWA chuoni mwaka wa kwanza, Emiliana tayari alikuwa amekwisha jihusisha kwenye masuala ya mapenzi, na kila kitu alikuwa akimueleza Modester, lakini jambo la kushangaza mpaka wakati huo hakuwahi kusikia hata siku moja mwenzie huyo akimueleza juu ya kuwa na mpenzi ama kuvutiwa na kijana yeyote!
Ilibidi amuulize.
Ilikuwa ni katika jioni moja, siku moja kabla ya Sikukuu ya Pasaka, wakiwa chumbani kwao, Modester akiwa amejilaza kitandani akipitia pitia baadhi ya mambo aliyokuwa ameyaandika kwenye diary yake, na Emiliana akiwa anakunja nguo.
“Inamaana,” aliaanza kwa kuvuta usikivu. Modester akamtupia macho. “Mpaka sasa hujawahi kukutana na kijana akakupenda, nawe ukampenda?”
Nt’see!
Modester alicheua kite cha kutolitegemea swali lile.
“Nilifikiri unataka kuongea kitu cha maana…kumbe huo upuuzi!” alimjibu.
“Kwa hiyo uhusiano wa mapenzi kwako ni upuuzi?” Emiliana alimuuliza kwa sauti ya kushushua akisimama kuendelea kufanya kile alichokuwa anakifanya.
“Kwa sasa…ni upuuzi, na sitaki kujihusisha nao.”
Emiliana alitabasamu.
“Na sisi tunaojihusisha nao ni wapuuzi?”
“No…sijamaanisha hivyo, kwangu ndio upuuzi, kwa wengine unaweza kuwa jambo la msingi…ntajuaje!”
“Na, je?” Emiliana aliendelea akizungumza kwa pozi; “Akitokea kijana mzuuri ambaye hujawahi kumuona duniani, mrefu, aliyejazia, mwenye kifua kipana, anayezungumza kwa besi na kila sifa unazozipenda…bado utamkatalia, kisa kwa sasa mapenzi ni upuuzi kwako?”
Modester alifunga diary yake ile iliyokuwa mikononi.
“Emmy!” Akaita akisajili tabasamu hafifu. “Unanjaa eeeh?” Alimuuliza, “na kijana wa namna hiyo utampata wapi?”
“Wapo…” Emmy alizungumza akiyazungusha macho yake kwa maringo.
“As long as kwa sasa mapenzi ni upuuzi kwangu…hata aje nani, sitaweza kumkubalia mpaka pale nitakapokuwa tayari…baada ya kumaliza masomo na kupata kazi!”
Emmy aliguna.
“Haya…nitakuona!” Akamwambia akiweka nguo ile aliyokuwa ameishika kabatini.
“Utajijua mwenyewe!”
Modester alisema akimpuuzia kwa kuchukua simu yake na kubofya.
Baada ya nusu saa toka wafanye mazungumzo hayo, ndipo walipokaa mezani kwa ajili ya chakula cha usiku. Walikuwepo wawili hao, mzee Laulian, mkewe na mfanyakazi wa ndani waliyezoea kumuita kwa jina la Dada!
Wakiendelea kula huku wakifanya mazungumzo, Emiliana aliropoka;
“Pasaka ya mwaka huu mbaya kweli…!”
Watu wale waliokaa pamoja naye wakamtazama.
“Ubaya wake?” Mama yake alimuuliza.
“Hakuna ahadi yoyote ya kutolewa out…kutoka kwa baba,” alisema kwa sauti ya chini kwa mtindo wa utani.
Wote mezani pale wakacheka wakimtazama mzee Laulian.
Mzee Laulian alitafuna chakula kilichokuwa mdomoni na kumeza, kisha akajitetea;
“Si’ kwa sababu kaka yenu ndiye atawatoa!”
“Mh!” Emilliana aliguna. “Kaka mwenyewe huyo, tangu awe mwanajeshi anaonekana mwaka hadi mwaka…tutamuonea wapi sie?”
“Kesho anakuja…” Mama yake alimpasha.
“Kaka Jackson kesho anakuja?” Modester alijikuta akivutika kwenye mazungumzo yale na kuuliza.
“Ndio…alisema atakuja kula sikukuu nasi, na atawatoa out!”
“Eeeh! Bora…nilikuwa nimemkumbuka kweli,” Modester alisema.
“Kwa hiyo kutakuwa na out, usijali juu ya hilo Emmy…” Mzee Laulian alizungumza kwa kusisistiza akimtaza binti yake yule machepele.
“Sasa hapo Pasaka itanoga…eeeh?” mama yake naye alimuuliza.
Mezani pale wote walimtazama, Emiliana akainamisha kichwa chini akitabasamu.
Wote wakacheka!
“KAKA Jackson ameamua kutufanyia surprise…maana sio kawaida yake kupanga kuja bila kutujulisha.” Emiliana alimwambia Modester walipoingia chumbani kwao baada ya chakula.
“Si’kajua kesho sikukuu ni lazima tu atatukuta nyumbani!”
“Ahaaa! Na kweli!”
Kilijengeka kimya kifupi. Kisha Emiliana akakivunja kimya hicho.
“Kuhusu kesho sijui itakuwaje…?” Alisema akionyesha hali ya kuchanganyikiwa.
“Kuhusu nini?” Modester alimuuliza.
“Sidhani kama nitatoka na kaka Jack…”
Modester alimakinika naye.
“Kwa nini hudhani…wewe sindiye uliyekuwa unazungumzia habari za out, pale mezani?!”
“Nilikuwa nafurahisha genge…baada ya kuona baba hana mpango wa kututoa…lakini nina mtoko na Chris!” Alisema akimtaja mpenzi wake aitwae Christopher ambaye Modester alimfahamu.
Modester aliguna.
“Sasa utafanyaje ili kaka Jack akuelewe. Kuja kwake ni kwa ajili yetu. Halafu wewe umwambie kwamba hutoki…atakuelewa kweli?”
“Mh!... Sijui nifanyeje! Na kumkacha Chris siwezi…hili amenisisitiza kweli yaani, nami nilimpa uhakika kuwa nitakuwa naye…”
“Aaah!…utajua mwenyewe utakavyo handle!”
Modester alionyesha kumpuuzia.
“Ona…” Emiliana akamvuta usikivu tena. “Tutatoka wote kama kawaida, halafu tukiwa njiani nitamuomba kaka Jackson kwa kumdanganya kuwa kuna rafiki yangu anashughuli muhimu na alinisisitiza niwepo…wewe utoke naye…halafu nitajitahidi kabla nyie hamjarudi nyumbani tuonane na kurudi wote!”
Modester alipandisha mabega na kuyashusha.
“Utaongea naye!” Alimwambia mwenzie yule.
***
SIKU hiyo ya Pasaka ilikuwa ni yenye heka heka sana. Modester na mama Emiliana, ndio waliokwenda kanisani, Emiliana alipoamka alidai hajisikii vizuri, na akataka abaki nyumbani, kukichangamka amsaidie dada wa kazi nyumbani pale kuandaa chakula.
Majira ya saa sita za mchana ndipo kina Modester walipotoka kanisani. Wakaungana na Emiliana na dada wa kazi jikoni kuandaa chakula.
Hadi saa nane wakati Jackson anafika chakula kilikuwa kipo tayari, familia ile kwa pamoja na jamaa kadhaa ambao walikuwa wamealikwa kujumuika kwenye sikukuu hiyo inayosherehekewa na baadhi ya Wakristo, kila mwaka baada ya mfungo wa Kwarezima walikaa mezani pamoja kwa ajili ya chakula.
Wakiwa mezani hapo, wakiendelea kupata chakula waliendelea pia na mazungumzo mbalimbali.
“Ila kaka Jack na we’ uoe sasa!” Mama wa kuropoka Emiliana, aliropoka.
Watu mezani pale walicheka wengine wakitabasamu.
“Emmy…wewe hunaga staha?!” Mosdester alimuuliza mwenzie kwa kumshangaa.
“No… sisi ni dada zake inabidi tumwambia, sikukuu kama hizi, hatupaswi kuhangaika majikoni peke yetu, inabidi tuwe na wifi anayekuja tunakomaa naye…”
Watu waliendelea kutabasamu, Modester naye alitikisa kichwa huku anatabasamu.
“Nitaoa tu mdogo wangu…very soon!” Jackson alisema.
“Ila hakikisha wifi yetu awe mzuri kuliko sisi!”
“Jamani!” Modester aling’aka kwa mshangao kutokana na kauli ile ya Emiliana.
“Ndio,” Emiliana alidakia kwa msisitizo. “Akituletea kibwengu bwengu tunakitimulia mbali!”
Wakazidi kucheka.
Na mazungumzo yakaendelea yaliyotawaliwa na utani mwingi.
Baada ya chakula na kupumzika sebureni, mida ya saa kumi Jackson aliwaambia Emiliana na Modester wajiandae ili awatoe out!
Wawili hao walielekea chumbani kwao mbio mbio kwa furaha.
Wakaoga na kujiandaa.
Walivaa mavazi yao mahususii waliyoyatenga kwa ajili ya mitoko ya mara moja moja. Kama huo!
Modester aliyekuwa mrefu wa wastani, alipigilia gauni la kitenge cha Makenzi, alilolishona kwa mtindo wa nguva ya chini. Mtindo huo wa ushonaji ulilifanya gauni hilo liushika vyema mwili wake uliojazia na kutengeneza muinuko mahususii chini ya mgongo wake. Liliishia maeneo ya mapajani, likaacha sehemu kubwa ya miguu yake iliyoshiba, wazi. Rangi ya gauni hilo ilimkaa vyema kutokana na rangi yake ya mwili na ilishabihiana na rangi ya pochi ndogo aliyoishika mkoni. Kichwani hakuwa amesuka, alikuwa na nywele fupi, alizozilisha vyema mafuta yaliyozipendezesha.
Modester alivutia.
Miwani ya jua aliyoitupia machoni ilimpendezesha zaidi. Ikamfanya aonekana mfano wa staa wa filamu. Viatu vya chini alivyoweka miguuni navyo vikampa chati, akaonekana mwanamke asiye na mambo mengi, lakini mzuri halafu simple!
Kwa upande wa machepele Emiliana, naye alivaa gauni la kitenge, lakini cha Java, alichokishonesha kwa mtindo wa mwanamke nyonga. Lilimkaa vyema kutokana na umbo lake jembamba. Kichwani, alikuwa amesuka nywele zake kwa mtindo wa serfe, alibeba mkoba wa rangi nyeusi, na miguuni alivaa viatu vyeusi vya mchuchumio.
Wote kwa pamoja walijipulizia manukato, ila yenye harufu zinazotofautiana.
Wakatoka chumbani Na kuelekea sebureni, alikokuwa amekaa Jackson peke yake.
Jackson kuwaona, alipigwa na butwaa.
Hasa akimakinika na Modester.
Alivutia mno.
Moyo wake ukamdunda.
Ukamjuza pia msichana huyo alikuwa ni mzuri aliyejaaliwa umbo na sura. Lakini upande mmoja wa nafsi yake ukamhoji; mbona uzuri huo alikuwa hajawahi kuuona kwa namna ya kipekee kama siku hiyo?
Upande mwengine wa nafsi hiyo ukajibu; pengine ni kwa sababu nina muda sijamtia machoni…lakini ni mzuri!
“Mmependeza sana…” Hatimaye alijikuta akizungumza akishindwa kulificha hilo moyoni.
Wasichana wale walitabasamu.
“Asante,” Modester alijibu.
“Sasa kwa kupendeza huku…usije ukatwambia unatupeleka Coco Beach, sisi siyo watoto!” Emiliana asiyekaukiwa kauli za masishara alimwambia kaka yake yule.
Jackson alibasamu.
“Yani huyu…!” Modester alisema akitikisa kichwa!
“Ghafla nimepata shida ya kujiuliza wapi niwapeleke…” Jackson naye alisema kwa masihara.
“Kwani mwanzo ulipanga utupeleke wapi?” Modester alimuuliza.
“Nilipanga tupitie Mlimani City, tununue Ice Cream, kisha twende Slipway!”
“Unaona sasa…!” Emiliana alisema kwa masihara.
“Unaona nini…mbona haina shida!” Modester alisema kwa uhakika.
“Twendeni bwana, nilikuwa natania.”
Jackson alisimama.
“Na mama yupo wapi?” Emiliana alimuuliza kakaye.
“Atakuwa huko uani na Dada.”
“Ngoja nikamuage.”
“Niagie na mimi Emmy!” Modester alimwambia.
“Twende tu akuone ulivyopendeza.”
“We’naye…” Modester alizungumza akicheka. Kisha akamfuata Emiliana nyuma. Wakaenda kumuaga mwanamke huyo na kisha wakaelekea kwenye safari hiyo ya mtoka wa jioni.
Ni katika mtoko huo ndipo vita kali ilipoanzia baina ya Modester na Jackson. Ni vita iliyoihusisha baadaye familia ya mzee Laulian, iliyomlea Modester tangu akiwa na umri wa miaka kumi na moja.
Ikasababisha maafa makubwa sana yaliyodumu kwenye maisha ya wahusika hao na familia zao!
Ukaribu uliojengwa katika kipindi chote hicho, ukafa!
ITAENDELEA