BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,124
Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Tanzania
RAIS Mstaafu, Benjamin Mkapa haachi kujuta kutokana na baadhi ya yale aliyoyatenda kwenye utawala wake, anaomba Watanzania wamsamehe, anaandika Wolfram Mwalongo.
Kinachomfanya kujuta ni hatua ya utawala wake kukabidhi ‘injini ya uchumi’ wa taifa hili kwa wawekezaji chini ya ‘sera ya ubinafsishaji.’ Mkapa alikabidhi mashirika ya umma mikononi mwa wawekezaji bila kuwa na mkakati wa kusimamia ili sera yake iwe na tija kwa taifa.
Rais Mkapa alihudumia nchi hii kama rais kuanzia mwaka 1995 hadi 2005. Alipokea madaraka hayo kutoka kwa Rais Ali Hassan Mwingi aliyehudumia nchi kuanzia 1985 mpaka 1995, aliyeanza kuhudumia taifa hili kwenye ngazi hiyo ni Mwalimu Julius K. Nyerere tangu Uhuru 1961.
Akiwa kwenye Tamasha la Nane la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofayika kwenye Ukumbi wa Nkurumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana Mkapa amekiri kwamba, hatua ya kuleta sera ya ubinafsishaji bila kuweka chombo maalum cha kudhibiti kumesababisha hasara.
Si mara ya kwanza kiongozi huyo mstaafu kusema maneno hayo hasa anapozungumzia maswala mazito katika utawala wake.
“Kukosekana kuundwa mfumo mzuri wa udhibiti kumesababisha kuwepo kwa watu waliotumia fursa hiyo kwa maendeleo yao binafsi na si kwa Taifa.
“Kwenye uongozi wangu kitu ambacho mpaka sasa ninajuitia ni kuanzisha sera ya ubinafsishaji na kushindwa kuweka mfumo au chombo cha kuudhibiti,”amesema Mkapa.
Mara kadhaa wachumi wa kitaifa wamekuwa wakikosoa utawala wa Mkapa kwa kuita wawekezaji na kuwapa ‘mali’ za taifa katika misingi mibovu ya uangalizi wake na kusababisha kuteketea kwa mali hizo. Miongoni mwayo ni viwanda, mashirika ya umma pamoja na Benki.
Mkapa kwenye tamasha hilo amesema “kuhusu ubinafsishaji huo ndio kitu naweza kukiri nilikosea na ninachoweza kuwaomba Watanzania msamaha.”
Mashiriki mengi ya umma pamoja na viwanda vilivyokabidhiwa kwa wawekezaji kutoka nje vilikufa na wengine kutumia mali hizo za taifa katika kujipatia mikopo na kufanya mambo mengine nje ya malengo yaliyokusudiwa.
Hata hivyo, Mkapa amesema “nilifanya kosa lakini hatuwezi kusema ubinafsishaji haufai kwa sababu ulisaidia kuleta mabadiliko na na kuongeza uzalishaji katika mashirika yaliyokuwa yameshindwa kuendeshwa na serikali.”
Ametoa mfano kwamba, “wakati mimi naingia madarakani viwanda vya sukari vya Mtibwa, Kagera, na Kilombero vilikuwa vikizalisha tani 120,000 hadi 130,000 lakini wakati naondoka niliacha vinazalisha tani 300,000.
“Mtibwa ilikuwa imeishakufa kabisa, lakini tuliweza kukirudisha na baada ya mimi kuondoka vimeendelea kuzalisha lakini inashangaza kuona miaka 17 wameshindwa kuongeza uzalishaji.”
Hata hivyo Mpaka alirudisha lawama kwa Watanzania kwamba, wana hulka ya kuzungumzia zaidi watu kuliko kuzungumzia sera na kuziboresha ili ziwe na tija kwa taifa.
Kwenye hotaba yake Mpaka amesema kuwa, Mwalimu Nyerere alishughulishwa katika kutafuta maendeleo ya Watanzania na kwamba, hakupinga ubinafsishaji kwenye taifa hili.
“Mwalimu Nyerere alikubali dhana ya ujasiriamali, uwekezaji, ushindani, ubunifu, ufanisi na utengenezaji wa faida vitu ambavyo viko sambamba na Ubepari,” amesema Mkapa na kuongeza;
“Vitu alikuwa anavitaka Mwalimu ni baadhi ya mambo mabaya ya Ubepari ikiwemo unyonyaji na mgawanyo wa faida usio sawa na ndio maana akaweka Azimio la Arusha akilenga kuwa na jamii ya usawa isiyo na unyonyaji.”
Akizungumzia ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) amesema, Mwalimu Nyerere aliona faida za ubinafsishaji na kwamba, aliona umuhimu wa kuibinafsisha benki hiyo.
“Kuhusu NBC Mwalimu si kwamba alikuwa anapinga kuibinafsisha bali ni namna ambavyo inaweza kuwanufaisha wananchi baada ya kuibinafsisha,” amesema Mkapa.