Halisi,
Naifungua makala ya salehe, ili iwe rahisi kutambua ninachosema.
Salehe anamalizia kuwa Muungwana hujibu yale anayotuhumiwa (Angalau).
Salehe UUNGWANA si kuvaa suti na tai, Waswahili husema "Ada ya mja Muungwana ni VITENDO" ukichanganya hicho cha kukaa kimnya na vingine vingi huyo Mtu si Muungwana bali kinyume chake, neno sitaliandika nina hakika wote tunalifahamu, kwa hiyo wakati wa kuliita Chepe kwa jina lake umefika tuache kuliita Koleo.
KATIKATI ya wiki hii kulikuwapo taarifa za kukamatwa kwa vijana wa Wilaya ya Kinondoni, hasa eneo la Kawe, kwa madai ya kumzomea Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, kwa kumuita fisadi.
Vijana hao waliona njia sahihi ya kufikisha ujumbe wao kwa Rais mstaafu huyo ni kwa kumzomea na kumwita fisadi, kwa sababu wasingeweza kupata nafasi ya kwenda Seaview kuzungumza naye.
Wangeweza vipi kuipata nafasi hiyo wakati hata vyombo vya habari ambavyo vina ukaribu na mwanasiasa huyo kila kukicha vimekuwa vikitafuta nafasi hiyo bila mafanikio, hivyo kuendelea kuandika matendo ya kifisadi aliyoyafanya kiongozi mstaafu huyo bila upande wa pili kujibu mapigo hayo.
Hivi sasa ni rahisi zaidi kupanga miadi ya Rais Jakaya Kikwete, na kuzungumza naye kuliko kuweka miadi hiyo na Mkapa, ambaye moja kati ya taaluma alizonazo ni uandishi wa habari, ambao unaeleza wazi kuwa mtu maarufu siku zote ni habari.
Habari yoyote iliyojificha ndiyo wananchi wana kiu nayo zaidi kuliko zile za kupikwa au kuandaliwa kwa lengo la kujisafisha au kuficha ukweli fulani ama kwa makusudi au bahati mbaya.
Vijana waliomzomea Mkapa walikuwa sahihi kwani hawaoni kama serikali yao ina juhudi za dhati za kumuwajibisha kiongozi huyo na wenzake waliotumia madaraka yao vibaya kwa kujineemesha.
Mkapa, aitwe nani kwa kuingia mikataba mibovu ya madini, kubariki uuzwaji wa nyumba za serikali, kuongeza mkataba wa TICTS kinyume na taratibu, kutowawajibisha watendaji wake walioelekea kulega lega katika kazi.
Tanesco kila siku hutoa sh milioni 146 kuilipa Kampuni ya Tanpower Resources Limited ambayo inaaminika kuwa inamilikiwa na Mkapa na Daniel Yona, ambao waliingia mkataba wa kinyonyaji wenye lengo la kujinufaisha zaidi.
Watanzania ambao wanaishi vijijini na hawapati huduma ya umeme kutokana na Tanesco kutokuwa na uwezo huo kwa sababu ya kulipa madeni mengi kwa kampuni zilizoingia mikataba mibovu wanamwonaje na watamwitaje Mkapa?
Si yeye na Mramba ndio walioidhinisha ununuaji wa rada ya kijeshi mwaka 2002, ambayo Tanzania ililanguliwa mara mbili ya bei halisi, yote hiyo ikiwa na lengo la kuchukua teni pasenti yao. Bila shaka vijana wale hawakukosea kumwita Mkapa fisadi, si tunaona hata Marekani, Rais George Bush, anaitwa gaidi kutokana na sera ya kuzivamia nchi nyingine kwa kisingizio cha kupingana na ugaidi.
Mbona polisi hawakumkamata Dk. Slaa, Mrema, Mbowe, Mbatia, Kimaro na wengineo wengi wenye nafasi zao katika siasa ya nchi hii walioweka wazi na kutaja majina ya viongozi akiwemo Rais Kikwete wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
Je, wanasiasa waliotaja listi ya viongozi mafisadi wapo juu ya sheria na hawaguswi, isipokuwa wale vijana wasio na mbele wala nyuma ndio wapo chini ya sheria na wanagusika kirahisi?
Kama utaratibu huu wa kuanza kuwakamata watu kwa kuwaita majina fulani wenzao umeidhinishwa, basi ni vema ukaanzia kwa viongozi wenyewe, kwani wao ndio vinara wa kuyakuza majina hayo. Kwa mtindo huu kila mtu atakamatwa, maana hakuna hata mtu mmoja asiyetamka neno ufisadi katika nchi hii kwa hivi sasa.
Ingawa taarifa za kukamatwa kwa vijana hao kwa kutenda kosa hilo zimekanushwa na Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Jamal Rwambow, aliyebainisha kwamba, si kweli kuwa waliwakamata vijana hao kwa kosa hilo, bali inawezekana walifanya kosa jingine.
Alisema ni kawaida jeshi lake hufanya operesheni mbalimbali katika wilaya hiyo kwa lengo la kupunguza vitendo vya kihalifu, hivyo kuna uwezekano vijana hao walikutwa na makosa mengine na watu wakaamua kuyakuza mambo kwa kudai wamekamatwa kwa kosa la kumwita Mkapa fisadi.
Pamoja na majibu hayo, lakini bado kuna taarifa kuwa baada ya kuona jamii itakuja juu endapo itabainika wamekamatwa kwa kosa hilo, Polisi wameamua kubadilisha kibao kuwa waliokamatwa walikutwa na bangi.
Kama taarifa hizo ni za kweli, Polisi wamekosea na dhamira zao zitakuja kuwasuta au kuwashitaki siku za usoni, kwa kufanya uonevu kwa watu walio sahihi kuwaita majina wanayostahili watu fulani.
Mkapa analazimika kuitwa hivyo, kwani hakuna kumbukumbu zinazoonyesha alishawahi kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma zinazomkabili ili jamii ijue mbivu na mbichi, bali amekuwa kimya kwa kile kinachotafsiriwa kuwa watu wanaopiga kelele hawamkoseshi usingizi.
Ni kweli hizi ni kelele za chura hazimzuii ngombe kunywa maji, lakini kwa muungwana ni lazima angalau angepaza sauti yake juu ya kile kinachosemwa juu yake.
Kulindana na kuoneana aibu kwa watendaji wa serikali hasa wanaofanya vibaya, ndiko kunakowasababisha wananchi kuanza kuwaita viongozi wetu majina ya aibu na ya kudhalilisha.
Serikali isipobadilika kuna kila dalili wananchi siku za usoni wakachukua hatua kali zaidi ya hizo na hata ikiwezekana kuwapiga mawe viongozi wa aina hiyo.
Waswahili walishaweka bayana kuwa usipoziba ufa utajenga kuta.