Kuna watu waliiulizia hii hotuba aliyotoa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania Samson Luhigo kuhusu ubinafsishaji wa bandari.
UKARIBISHO
Mheshimiwa Rais,
Nami napenda kuchukua fursa hii kukukaribisha wewe tena hapa THA na mahsusi Bandari ya Mtwara.
Ni furaha na faraja kutembelewa na Mwenyekiti wa wenye hisa katika shughuli unayoendesha.Uwe ni meneja au mfanya kazi. Inakupa wakati mzuri wa kujitathmini lakini pia wenye hisa kuweza kukutathmini.Inakipa fursa pia kiwanda kutoa maelezo kwa wenye hisa kuhusu shuguli za kiwanda. Leo Mheshimiwa tuna furaha kupata fursa hii.
Katika dakika chache ambazo nimepewa na Uongozi wa Mkoa ninapenda kueleza machache kuhusu THA kwa ujumla,machache kuhusu zoezi la ubinafsishaji, na Maono ya Mamlaka ya Bandari kuhusu Bandari ya Mtwara.
THA Kwa Ujumla
Kwa ujumla biashara ya Bandari hairidhishi kwani shehena inayopitia kwenye bandari zetu imeendelea kupungua, hivyo mapato
kuendelea kupungua. Kwa kuwa gharama zisizoepukika zinazidi kuongezeka faida inazidi kudorora, na ukizingatia ya kwamba mabawa ya kiuchumi ya Mamlaka yamekuwa yakikatwa kikatili na zoezi la ubinafsishaji, faida imekuwa ikiporomoka.
Ninaamini, kwa sababu nimekusikia ukitamka hadharani kwamba kituo cha kontena kimekuwa na ufanisi mkubwa kiutendaji kazi. Hii imesababishwa na mambo mawili muhimu.
La kwanza ni upanuzi wa lango la Bandari ya Dar Es Salaam ulioziwezesha meli kuingia na kutoka masaa 24 bila kujali usiku au kupwa kwa maji hivyo kupunguza wakati wa meli kukaa bandarini kwa masaa 12 hadi 24.
La Pili ni Ubinafsishaji
Mheshimiwa Rais, nimetafakari sana na nimeamua kwamba kama ningelizaliwa mwanamke na Mungu akanipa umbile la kutamanika la kumshawishi mwanamme yeyote kunioa nisingeolewa na Mtanzania hata kama yeye ni Rais.Nimemuona kijana mmoja wa kigeni maarufu na hodari. Ningelihakikisha kwamba huyo tu ndiye amenioa. Jina lake Ubinafsishaji. Ana umbile zuri hivyo anapendeka, ana uwezo wa kufanya lolote ambalo waswahili wa kitanzania hawawezi kuthubutu. Kijana huyu hodari. Ninasikia, ninaamini na wewe Mheshimiwa Rais, umelisikia hili kwamba siku moja aliikunjia uso Ikulu yako, wakalipa bill za umeme haraka haraka. Kijana wa Kitanzania angelidiriki hivyo angelijikuta kaburini. Na kama angelizikwa Dar es Salaam si kwenye makaburi ya heshima kama Kinondoni.
Kijana huyo wa kigeni nasikia akatoka Ikulu akaenda akawakunjia uso Makao Makuu ya Jeshi, haraka wakalipa bili za umeme. Kijana wa kitanzania ambaye angelidiriki Kufanya hivyo angelikufa kwa kuruka kichura.
Kijana huyo akatoka hapo akenda kwa kitinda mimba kipenzi wa watanzania akamkunjia uso, naye sasa nasikia analipa bili za umeme. Mswahili wa kitanzania angelidiriki kufanya hivyo angelishitakiwa kwa kuhujumu muungano. Asingelipata hata muda wa kulitambua rungu ambalo lingemlamba.
Mheshimiwa Rais, ningelikuwa binti mzuri nisingeolewa na Mtanzania ningeliolewa na kijana mzuri wa kigeni aitwaye ubinafsishaji.
Ninachotaka kusema Mheshimiwa Rais, ni kwamba sehemu kubwa ya kile kinachoonekana kuwa ni mafanikio ya ubinfsishwaji kinatokana na wabinafsishaji kuruhusiwa kile ambacho Menejimenti za kitanzania haziruhusiwi kufanya.
Nimeyasema hayo Mheshimiwa Rais awali ya kutamka kwamba kimekuwa na ongezeko kubwa la ufanisi wa Kituo cha Kontena. Kasi ya kupakua na kupakia Makontena imeongezeka karibu mara mbili, na muda wa Makontena kukaa bandarini umefupishwa kutoka siku 14 hadi siku 2.
Hii imetokana na ongezeko la teknolojia, uwezo wa kimenejimenti na la muhimu sana , uhuru wa kufanya maamuzi bila kuingiliwa.
Mheshimiwa, ninapenda kuipongeza Serikali yako kwa mafanikio haya ambayo pia nimesikia mara kwa mara ukiyataja katika hotuba zako.
Mheshimiwa Rais, tunasoma katika Biblia kwamba Mfalme Daudi alikuwa na mtoto aliyempenda sana. Alipougua Mfalme akafunga na kuomba Mungu amponye. Hatimaye mtoto akafa. Watumishi wa Daudi kwa kuona alivyokuwa na majonzi wakati wa ugonjwa wa mtoto wakaogopa kwenda kumuarifu Daudi kuhusu kifo cha mtoto.
Mheshimiwa Rais, kwa sababu za kibinadamu inawezekana washauri wako wamekueleza tu ufanisi unaotokana na ubinfsishwaji wa kituo cha Kontena. Ninahakika ungelikuwa unazo habari nyengine, kwa tabia yako ya uwazi na ujasiri ungelikuwa sambamba na kusifu mafanikio ya ubinafsishaji wa Kituo cha Kontena ungelikuwa unawaarifu watanzania machungu ambayo imebidi wayameze.
Mwaka kabla ya ubinafsishaji wa Kituo cha Kontena, 1999/2000, faida baada ya kodi ilikuwa karibu Shs. 10b, katika mwaka wa ubinafsishaji wa Kituo, 2000/2001, faida ilishuka hadi Shs. 4b. Hesabu za 2001/2002 ambazo zimewasilishwa kwa wakaguzi zinaashiria kwamba faida baada ya kodi itaporomoka kwa kishindo hadi Shs. 0.04b.
Sababu kubwa ni mapato duni yaliyoko kwenye mkataba wa ubinafsishaji wa Kituo cha Kontena ambacho ndicho kilikuwa mhimili wa mapato ya Mamlaka, kuongezeka kwa gharama zisizoepukika, na uzito wa madeni ya Mamlaka kwa Serikali.
Wakati wa kutekeleza mradi wa Maendeleo ya Bandari ya Dar es Salaam, Serikali ilikubaliana na World Bank kwamba kwa sababu Mamlaka ya Bandari ni Shirika la kibiashara isingepewa fedha za Maendeleo na Serikali bali ikopeshwe hata kama Serikali inapewa fedha hizi bure na wahisani. Hivyo fedha zote ambazo Serikali ilipewa na wahisani ama kwa riba ndogo sana au bure, Serikali ikaikopesha Mamlaka ya Bandari kwa riba ya 11%. Mwaka 1985 riba hii ilionekana ni nafuu ukilinganisha na riba zingine. Sasa hivi riba hii ni juu mno na ingawa ilikuwa na nia nzuri imegeuka kuwa mzigo kwa Mamlaka na hivyo kuwa ni kikwazo katika ushindani. Tumeomba kwa miaka mingi sasa Serikali ipunguze hii riba lakini kutokana na ufinyu wa mapato ya Serikali, Hazina wamekuwa wanalisikia ombi hili lakini hawalielewi.
Ilikuongeza ushindani wa bandari zetu na ili kuiwezesha Mamlaka ya Bandari tunaomba tena Serikali yetu ilitazame suala hili upya. Hasa kwa kuwa hata kama tumeamua kufanya biashara ya bandari inapokuja kwenye kugharamia miundo, mbinu wawekezaji pekee inawezekana wasimudu na hivyo kuitaka Mamlaka ya Bandari kuchangia. Hivyo Mamlaka ya Bandari sharti iwezeshwe kujenga uwezo huo.
Zoezi la ubinafsishaji
Kuhusu ubinafsishaji wa vitengo vilivyobakia vya Mamlaka, ukiondoa Kituo cha Kontena, zoezi linaendelea vizuri. Mshauri aliyeteuliwa na PSRC amekamilisha mapendekezo ya namna ya kuibinafsisha Mamlaka ya Bandari, TCFB na NASACO. PSRC wamekwisha wasilisha taarifa kwa Wizara ya Mawasiliano na Uchukuzi ya maamuzi ya Serikali.
Katika awamu hii ninapenda kuishukuru na kuipongeza Kamisheni yako, PSRC, kwa kuwa tumeona mabadiliko makubwa katika mtazamo, hisia, na ushirikiano wao.
Katika awamu ya kwanza, Menejimenti ilionekana kama haijui lolote, na wanaojua kila kitu ni washauri wa kigeni tu na kila lililo tamkwa na washauri wa kigeni ni amri ya Mungu. Kama wengine mna la kusema subiri kiama. Kulikuwa na washauri wa kigeni kule ambao mara nyengine tulikuwa tunashawishika kuamini kwamba wamejipanga kabisa na makampuni ya nje kuelekeza mambo yende vipi.
Hali sasa imebadilika Kamisheni yako imebadilika na kufikia maamuzi yaliyo na manufaa zaidi. Tunatamani tungelianza upya sasa, lakini Mheshimiwa, tusililie maziwa yaliyomwagika tugange yajayo.
Katika kuganga yajayo yapo mambo kadhaa ambayo pamoja na Kamisheni yako kuyatafakari, lakini kwa sababu ya historia ya Mtanzania na utamaduni wake inawezekana hata yakifika mezani kwako yatakuwa ni rojorojo sana kiasi kwamba utayapita bila kuyaona.
Masuala hayo ni mafao ya wafanyakazi, ushirikishwaji wa wafanyakazi katika zoezi la ubinafsishaji na hatima ya nyumba za kuishi za wafanya kazi.
Ingawa Serikali katika matamshi mbali mbali imetamka kwamba mashirika yaliyo na uwezo tu yenye uwezo wa kutoa mkono wa kwaheri ndiyo yatakayoruhusiwa kutoa mkono wa kwaheri, Kamisheni imechelea kuthibitisha kauli hii katika majadiliano mbali mbali.
Hili linawapa wasiwasi wafanyakazi hasa ikizingatiwa kwamba Mamlaka walioitumikia kwa uaminifu inao uwezo na kwamba wenzao wasiopungua 3000 wamepunguzwa, retrenched, kwa kupewa mkono wa kwaheri kwa misingi ile ile ambayo wenzao waliokuwa retrenched mapema walipewa.
Mheshimiwa Rais, tukiri ya kwamba wakati tulipoanza zoezi la ubinafsishaji sera ya jinsi gani Mtanzania wa kawaida angelishiriki katika zoezi hili haikueleweka kwa wengi na wala nina mashaka kama sasa hivi hali hii imebadilika. Ninaamini Serikali yako ilikuwa inalifanyia kazi suala hili ili hata watekelezaji kama Ka