Chenge, kisha Mkapa
Mwandishi Wetu Aprili 23, 2008
Raia Mwema~Muungwana ni Kitendo
KUTUHUMIWA kwa ufisadi na hatimaye kujiuzulu kwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, kumefungua njia ya umma kuhoji uadilifu wa viongozi wa siasa akiwamo Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa.
Raia Mwema imeambiwa kwamba ukweli kwamba Chenge ndiye aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wote wa Serikali ya Mkapa, unatosha kuhoji uadilifu wa rais huyo mstaafu kwa kuwa Chenge ndiye aliyekuwa mshauri wake mkuu katika masuala ya Serikali.
Sasa tanapitia upya mikataba ya madini, lakini mikataba ya aina hiyo na mingine, kama wa IPTL na TANESCO, ilipitishwa wakati wa Mkapa na Chenge.
Kwamba sasa Chenge amekubali kukaa kando baada ya tuhuma hii moja tu ya rada, maana yake ni kwamba kama tunataka kama nchi tunaweza sasa kuanza kuhoji mikataba mingine tujue huko nako ni fedha kiasi gani ziliingia katika mifuko binafsi, anasema mwanasiasa mmoja ambaye aliomba asitajwe.
Mwanasiasa huyo na wengine kadhaa, walikuwa wakizungumzia hatua ya waziri Chenge kutangaza kujiuzulu siku chache tu baada ya tuhuma dhidi yake kuandikwa katika magazeti ya Uingereza, akidaiwa kuwa alihusika katika kupokea fedha zipatazo bilioni moja kwa shilingi za Tanzania, zilizotokana na ununuzi wa rada kutoka katika kampuni ya BAe ya Uingereza.
Chenge baada ya kufika nchini akitokea ziarani China, alikanusha kuwa anahusika katika tuhuma hizo, na akasema kwamba hata hivyo, fedha hizo zilikuwa ni vijisenti tu kwa viwango vyake na kwamba tuhuma hizo zisingemfanya ajiuzulu.
Raia Mwema imefahamishwa kwamba suala hilo si dogo kama ambavyo Chenge alijaribu kuliweka, ukweli ni kwamba ni unyeti huo uliofanya yeye arejee nchini kabla ya wenzake waliokuwa naye ziarani China.
Hilo si suala dogo. Japo aliondoka wakati tayari akiwa amekwisha kuhojiwa, mambo yalipopamba moto ilibidi aambiwe arudi huku wengine wakiendelea na safari katika ngwe iliyokuwa imebaki, anasema ofisa mmoja mwandamizi ndani ya chama tawala, Chama Cha Mapinduzi akieleza kwamba kundi jingine alilokuwa ameandamana nalo Chenge liliendelea na safari ya Ulaya wakati yeye akirejea.
Lakini habari zinasema pia kuhusishwa kwa Mkapa katika mtiririko huo wa Chenge kunatokana na ukweli kwamba kama alivyo Mkapa, Chenge naye anatumia huduma za wakili Joseph Mbuna, mwenye uhusiano wa kibiashara na kifamilia na rais huyo mstaafu.
Pamoja na kwamba zimekuwapo jitihada za kumuepusha Mkapa zinazoelekezwa kwa Chenge na wanasiasa wengine, kuingia kwa Mbuna katika utetezi huo kunaelezwa kuwa kutaibua ambo mazito zaidi yaliyokuwa yamejificha.
Mbali ya kuwa pamoja na familia ya Mkapa katika kampuni tata ya Kiwira Coal Mines, Mbuna anaunganishwa na familia ya rais huyo mstaafu kutokana na watoto wao wawili kuoana na hatimaye kuwa pamoja na wazazi wao katika biashara mbalimbali, ambazo zimekuwa zikichunguzwa.
Rada inayomtia matatani Chenge na Mkapa ilifika nchini mwaka 2002, baada ya mchakato wa ununuzi huo kufanyika kuanzia mwaka 1999, ukiwahusisha viongozi mbalimbali, akiwamo Mkapa na watendaji wa idara mbalimbali serikalini.
Mkapa, ambaye aliingia madarakani mwaka 1995 akiwa mmoja wa viongozi waliobebwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, kwa bendera ya kuwa ni mtu safi (Mr.Clean), sasa yu katika wakati mgumu kutokana na kuibuka kwa tuhuma mbalimbali, ambazo sasa kuna kila dalili kwamba hawezi kuzikwepa na nyingine zinamuelekea moja kwa moja.
Mkapa kama kiongozi mkuu, amekuwa akitajwa kuhusika na ubadhirifu Benki Kuu (BoT) ambako sasa kunaaminika kuwa mabilioni ya fedha yalichotwa chini ya kivuli cha shughuli nyeti za nchi.
Kwingine anakotajwa Mkapa ni katika kampuni ya Meremeta, ambayo kuwako kwake kumekuwa kukiichanganya sana Serikali.
Vyanzo kadhaa vya habari vinasema Rais Mstaafu Mkapa alishinikiza na kuidhinisha kuanzishwa kwa kampuni hiyo tata inayohusishwa na upotevu wa Sh. bilioni 155. Tayari Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), Ludovick Utouh, ametamka kwamba ofisi yake haijawahi kukagua hesabu za Meremeta Gold, na kampuni hiyo haimo katika orodha ya makampuni yanayomilikiwa na Serikali ama kwamba Serikali ina hisa humo.
kizungumza katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma, CAG, Utouh, alisema wazi kwamba Meremeta haimo katika orodha ya makampuni na mashirika ya umma ambayo yamewahi kukaguliwa na ofisi yake, hoja ambayo inapinga ile iliyopata kusema kwamba Meremeta ni mali ya umma.
Utata huo unaongezwa na taarifa za kwamba serikali kupitia Msajili wa Hazina ilitoa cheti cha kuithibitisha Meremeta kuwa kampuni ya umma tokea Oktoba mosi, 1997, baada ya kudaiwa kwamba serikali ilikuwa na hisa katika kampuni hiyo, hisa zilizoshikiliwa na watendaji wakuu serikalini, ambao hata hivyo hadi sasa wanaendelea kuzishikilia baada ya baadhi yao ama kuondolewa au kubadilishwa nafasi zao. Hao ni pamoja na Chenge ambaye amekuwa Mkurugenzi wa Tangold, ambayo ilichukua nafasi ya Meremeta iliyofilisiwa.
Habari zinasema kwamba tayari uchunguzi wa kina umekwisha kuanza kufuatilia, hasa zilikokwenda fedha hizo kiasi cha Sh. bilioni 155, zikiwa ni nyingi zaidi ya zile zilizochotwa BoT kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA). Sakata la EPA linahusisha Sh. bilioni 133.
Wakati haya yote yakifahamika, baadhi ya wabunge wamesema kwamba kujiuzulu kwa Chenge Jumapili iliyopita, ni jambo ambalo walikuwa wanalitarajia, na kwamba amechelewa mno kuchukua hatua hiyo.
Wamesema haikuwa sahihi kwa Chenge kusubiri hadi anyooshewe kidole.
Eneo mojawapo ambalo baadhi ya wabunge wamesema walikuwa na mashaka na utendaji wa Chenge, hasa kutokana na mikataba mingi mibovu, ambayo nchi iliingia wakati Chenge akikalia kiti cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Wabunge wengine walisema kwamba kujiuzulu pekee hakutoshi, bali ni kwenda mbali zaidi kwa kujivua nyadhifa za CCM na nyingine zilizoko nje ya uwaziri. Chenge ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na Kamati Kuu.
Wakati kujiuzulu kwa Chenge bado hakujapoa wala kufutika kwenye kumbukumbu za watu, wapinzani nao wamepeleka hati zao za kuomba kukagua daftari la mali na madeni ya viongozi mbali mbali, akiwamo Rais Mstaafu Mkapa na Chenge mwenyewe.
Katika ombi lao kwa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wanataka pia kukagua daftari hilo kuona mali za Rais Jakaya Kikwete, Mbunge wa Rombo, Basil Mramba, Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, Mbunge wa Musoma Vijijini Nimrod Mkono, Waziri Mkuu aliyejiuzulu Edward Lowassa na aliyekuwa Gavana wa BoT Daud Balali.
Wengine ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Patrick Rutabanzibwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini (aliyejiuzulu), Nazir Karamagi.