Mjukuu akakatisha uhai wa Mama Malcom X………..! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Mjukuu akakatisha uhai wa Mama Malcom X………..!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, Apr 5, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  Apr 5, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280

  23shabaz.jpg
  Hayati Dr. Betty Shabazz

  50334559.jpg
  Malcolm Shabazz akipelekwa mahakamani
  Malcolm.jpg
  Malcolm Shabazz alivyo sasa baada ya kutoka jela
  El%20Hajj.jpg
  Malcolm Akiwa Hija Maka

  Wasomaji wa JF, nimelazimika kuweka makala hii leo badala ya kesho Ijumaa kama ilivyo kawaida kwa sababu nasafiri kwenda Mkwaja Pangani Tanga kwa mapumziko ya msimu wa Pasaka. Nawatakia mapumziko mema ya msimu wa Pasaka.

  Ilikuwa ni majira ya asubuhi ya Juni 1, 1997 katika jiji la NewYork nchini Marekani, kitengo cha kupokea matukio ya dharura kilipokea simu ikiwafahamisha kwamba kuna jengo moja linawaka moto katika eneo la Yonkers.

  Bila kupoteza muda kitengo cha zima moto kilifahamishwa haraka juu ya tukio hilo. Waokoaji walipofika katika eneo hilo walikuta jengo hilo likiwa limezingirwa na moto lakini katika kibaraza cha kuingilia walimuona mwanamke mmoja Mmarekani mwenye asili ya Afrika akiwa amelala chini huku akiwa hajitambui kabisa na alikuwaAmeungua vibaya sana. Alikuwa amevaa gauni lake la kulalia ambalo lilikuwa limeshikana na ngozi ya mwili. mhanga yule alikuwa ni mtu anayefahamika na maarufu sana nchini Marekani. Naye hakuwa mwingine, bali alikuwa ni Dk. Betty Shabazz, mke wa aliyekuwa mpigania haki za watu weusi nchini Marekani Hayati Malik Shabazz aliyekuwa maarufu kwa jina la Malcolm X, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi miaka ya nyuma.

  Ingawa alikuwa hajitambui lakini aliweza kutamka, "Mjukuu wangu, Mjukuu wangu chumbani." Wale askari wa kikosi cha zima moto waliposikia vile wakakimbilia ndani chumbani wakidhani labda mjukuu wake amebaki ndani akiteketea kwa moto. Lakini hata hivyo walipoingia ndani na kuchunguza kwa makini hawakuona mtu yeyote.

  Haraka sana Dk. Betty Shabazz alikimbizwa katika kitengo maalum cha kutibu watu walioathirika na majanga ya moto katika Hospiali ya Jacobi iliyoko jijini New York. Wakati Dk. Betty Shabazz akikimbizwa Hospitalini, Polisi walimuona mjukuu wa mama huyo ambaye alipewa jina la babu yake, la Malcolm Shabazz, aliyekuwa na umri wa miaka 12 akirandaranda pale mtaani huku akiwa na galoni iliyokuwa na mafuta ya taa. Alikuwa akitweta na alionekana kuwa na wasiwasi.

  Malcolm mdogo alichukuliwa na Polisi hadi Hospitali ya Mount Vernon kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya kutokana na hali aliyokutwa nayo kuwa ya kutia shaka. Baada ya vipimo, Daktari alithibitisha kuwa Malcolm alikuwa ni mzima wa afya.

  Baadaye alihojiwa na Polisi na kukiri kuwa ni yeye aliyechoma moto nyumba ya bibi yake na hivyo kumsababishia bibi yake majeraha makubwa ya moto. Ukweli ni kwamba kulikuwa hakuna matumaini ya Dk. Betty Shabazz kupona kutokana na jinsi alivyoungua na moto na hata Daktari mkuu katika kitengo hicho alikiri wazi kuwa yapo matumaini hafifu kwa Dk. Shabazz kupona.

  Akiongea na waandishi wa habari, kwa maneno yake mwenyewe Dk. Bruce Greenstain alisema, "yuko katika hali ngumu sana akipigania maisha yake, kwani kwa jinsi alivyoungua na majeraha aliyoyapata, kwa kweli ni vigumu kwa mtu yeyote kustahimili, kwani ni mbaya zaidi ya kugongwa na gari, ni mbaya zaidi ya kupigwa na risasi."

  Akiendelea kufafanua, Dk. Bruce alisema kuwa, wakati mgumu kabisa katika kumhudumia mtu aliyeungua na moto ni ule wa muda wa masaa 48 tangu mgonjwa afikishwe Hospitalini. Daktari huyo aliongeza kwamba, iwapo mtu ameungua kwa kiwango cha nyuzi 3 ambacho ndicho alichoungua Dk. Shabazz, uwezekano wa kupoteza maisha unakuwa ni mkubwa sana kutokana na kupoteza damu nyingi pamoja na maji ya mwili.
  Dk. Bruce aliendelea kusema kuwa, hata kama Dk. Shabazz atapona lakini itachukua muda ngozi ya mwili wake kurudi katika hali yake ya kawaida. Hata hivyo marafiki wa Dk. Shabazz hawakukata tamaa, kwani pamoja na kuwa katika hali ya kutojitambua, lakini hawakuacha kwenda kumuona na kumjulia hali.
  Miongoni mwa waliokwenda kumuona ni Coretta King, mke wa hayati Mrtin Luther King ambaye naye aliuawa kwa risasi, mwandishi maarufu wa vitabu Mayer Angelou na Promota maarufu wa masumbwi nchini Marekani Don King.

  Akizungumza mara baada ya kumuona Dk. Shabazz, Mayer Angelou ambaye alisafiri akitokea Atlanta na Coretta King pamoja na mabinti wawili wa Dk. Shabazz, alisema, "Ni dada yetu, ndio sababu wote tumekuja hapa kumuona, na kumjulia hali, ingawa bado hajitambui lakini ile kuwa naye hapa inamletea faraja kwa kiasi fulani."

  Hata hivyo licha ya watu maarufu kumtembelea pale Hospitalini, wale waliokosa fursa walituma salaam zao kwa njia mbalimbali. Akipiga simu kutokea jijini London nchini Uingereza, Mchungaji maarufu nchini Marekani Jesse Jackson, alituma salaam zake za pole kwa Dk. Shabazz.

  Naye aaliyekuwa rais wa Marekani wakati huo, Bill Clinton, alituma Fax kutokea jijini Washington akisema kwamba, alipatwa na mshtuko kutokana na tukio hilo. Pia katika Fax yake hiyo Rais Clinton alimuelezea Dk. Shabazz kama mwanamke aliyependa kujiendeleza kielimu na kuwasaidia wanawake na watoto katika kufikia matarajio yao.

  Wiki tatu baadaye tangu Dk. Shabazz apatwe na janga lile la kukusudiwa, pamoja na juhudi za madaktari na sala kutoka kwa watu mbalimbali, alifariki dunia na mjukuu wake moja kwa moja akawa ndiye mtuhumiwa wa mauaji.

  Huo ukawa ndio mwisho wa Dk. Betty Shabazz ambaye mnamo mwaka 1965 akiwa na ujauzito mkubwa wa watoto mapacha huku akiwa ameandamana na mabinti zake wanne alishuhudia mumewe Malik Shabazz almaarufu kama Malcolm X akiuawa kwa risasi wakati wa maandamano ya kisiasa ya kudai haki za watu weusi nchini Marekani yaliyofanyika katika mji wa Harlem.

  Baada ya tukio hilo la kufiwa mume, Baadaye alijifungua mabinti wawili mapacha na kuanzia hapo akawa na mzigo mkubwa kuwalea mabinti zake sita alioachiwa na mumewe ambao ni Attallah, Qubillah, Ilyasah, Gamilah na hao mapacha Malikah na Malaak. Kwa kuzingatia umuhimu wa elimu Dk. Shabazz aliamua kujiendeleza kielimu na kufanikiwa kutunukiwa shahada ya Udaktari wa elimu na akawa akifanya kazi katika taasisi iliyoanzishwa na hayati mumewe iitwayo National of Muslim ambayo ilikuwa inajishughulisha na haki ya kuabudu kwa waislamu weusi.

  Dk. Shabazz alikuwa akielezwa na wanaharakati wa haki za binadamu nchini humo kama Malkia Mweusi na mama mlezi. Wakati mabinti watatu wakiwa wamefuata nyayo za baba yao na wengine wawili wakiwa ni Mameneja uhusiano katika makampuni makubwa nchini humo, binti yake mkubwa aitwae Quibillah ambaye ndiye mama wa mtoto Malcolm alikuwa na matatizo tangu baba yake alipouawa. Wale walio karibu naye wanaamini kuwa bado hajaondokana na jinamizi la kuuawa kwa baba yake huku akishuhudia.
  Akiwa na umri mwa miaka 11 Quibillah aliachana na dini ya wazazi wake ya kiislamu na dini ya Kikristo inayoamini katika amani na isiyoamini katika dhehebu lolote la kikristo na isiyoabudu kwa kufuata mfumo wowote wa madhebu ya Kikristo inayoitwa Quaker. (http://www.bbc.co.uk/religion/religions/christianity/subdivisions/quakers_1.shtml).

  Akizungmzia uamuzi wake huo Quibillah alidai kwamba, hataki kuwa mtoto wa mtu yeyote anayejishughulisha na mambo ya Kimapinduzi. Baadaye alijiengua kutoka katika chuo kikuu alichokuwa akisoma cha Priceton mara tu baada ya mihula miwili. Alipoulizwa sababu ya kufanya hivyo, Quibillah kwa maneno yake mwenyewe alisema, "Mimi sifanani na vile ambavyo watu walidhani nitakuwa, sikuja hapa chuoni na Magwanda pamoja na Buti za Jeshi na wala sizungumzi Kiswahili."

  Akiwa ni binti mwenye akili za ziada lakini na asiye na adabu, Quibillah aliamua kwenda Paris nchini Ufaransa kusoma katika chuo cha Surbonne. Alirejea nchini marekani mwaka mmoja baadaye akiwa hana shahada wala mume lakini akiwa na mtoto mchanga wa kiume ambaye alimpa jina la hayati baba yake Malcolm Shabazz. Baba wa mtoto huyo alikuwa ni Mu-Algeria ambaye alikutana na Quibillah jijini Paris nchini Ufaransa. Lakini mpaka kukua kwa mtoto huyo hakupata kumjua baba yake kwa sababu kulikuwa hakuna mawasiliano kati ya mama yake na huyo baba yake.

  Kwa takriban miaka kumi Quibillah alikuwa akihama kutoka jimbo moja kwenda jingine akiwa na mwanaye huyo, kwani alikuwa akisumbuliwa na msongo wa mawazo pamoja na ulevi wa kupindukia. Mpaka kufikia mwaka 1995 Quibillah alikuwa na hali mbaya sana kimaisha, hadi akawa anaishi kwa msaada wa mfuko wa kijamii wa Minneapolis ambapo pia ilibidi mamlaka ya kulinda haki za watoto imchukuwe mtoto Malcolm kutoka kwa mama yake kwa sababu ya usalama wake kwani walihisi mtoto hatapata matunzo yanavyostahili.
  Baadaye mwaka huo huo, Quibillah alikamatwa kwa kosa la kufanya njama za kutaka kumuuwa Louis Farrakhan, mkuu wa taasisi ya National of Islam, iliyoasisiwa na hayati baba yake Malcolm X.

  Inasemekana Quibillah aliamini kuwa Louis Farrakhan ndiye aliyehusika na na mauaji ya baba yake. Lakini hata hivyo kesi hiyo haikuendelea kwa sababu mtu aliyefichua njama hizo shushushu wa FBI Michael Fitzgerald, licha ya kuwa alikuwa mwanafunzi mwenzie Quibillah, pia walikuwa na uhusiano wa kimapenzi.
  Hivyo ilionekana kuwa kesi hiyo itakuwa na muingiliano wa kimaslahi kwa hiyo waendesha mashtaka wakatengeneza mazingira ya maelewano kwa pande mbili kumaliza shauri lile nje ya mahakama.

  Na hiyo ilikuwa ni baada ya Quibillah kukiri kuhusika na njama hizo na kukubali kupelekwa kwenye kituo cha ushauri nasaha kwa ajili ya kuacha pombe.
  Baada ya kumaliza matibabu ya ushsuri nasaha, rafiki zake Quibillah pamoja na mwanasheria wake Percy Sutton walimtafutia kazi katika kituo kimoja cha redio kilichopo katika mji wa San Antonio jimboni Texas na akawa anaishi chini ya uangalizi wa mtaalamu mmoja wa ushauri nasaha aitwaye Karen Taylor.

  Hata hivyo, hali haikubadilika kwani mnamo Oktoba 1995 askari wa kituo cha Polisi cha San Antonio walipokea simu kutoka kwa mtu ambaye hakutaka kujitambulisha jina lake ambapo aliwajulisha kuwa Quibillah alikuwa amelewa chakari. Polisi walipofika nyumbani kwake walimkuta kweli Quibillah alikuwa amelewa na aliwaambia Polisi kuwa anafikiria kujiuwa. Kutokana na hali hiyo waliyomkuta nayo, ilibidi wamkimbize hospitalini kwa ajili ya kupatiwa tiba ya ushauri nasaha ili aondokane na msongo wa mawazo.

  Wakati huo huo mwanaye Malcolm alipelekwa kwa bibi yake Dk. Betty Shabazz jijini New York, na kuanzia hapo ukawa umeanza ukurasa mwingine, kama vile mchezo wa kuigiza kwa Malcolm kuhamishwa kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Ikawa mara akae kwa bibi yake, na wakati mwingine apelekwe kwa shangazi zake, yaani dada zake Quibillah ambao nao walikuwa wakiishi katika majimbo tofauti tofauti.

  Katika kipindi cha majira ya joto mnamo mwaka 1996, Quibillah alianza uhusiano wa kimapenzi na mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la Theodore Turner. Licha ya tabia ya kikatili aliyokuwa nayo Theodore kiasi cha Polisi kuitwa mara kwa mara nyumbani kwao, kwenda kuamulia ugomvi wa wapenzi hao, lakini mnamo Desemba 1996 wapendanao hao walifunga ndoa na hapo mtoto Malcolm akajiona naye hatimaye anaye baba, japo hakuwa baba yake wa kumzaa.

  Malcolm alikuwa na uhusiano mzuri na baba yake wa kufikia kwani mara nyingi baba yake huyo alikuwa akifuatana naye kwenye mazoezi ya mpira wa kikapu ili kumshuhudia mtoto Malcolm akicheza mchezo huo.
  Mara nyingi Malcolm alikuwa akiwasimulia marafiki zake jinsi baba yake wa kufikia alivyo mwema kwake na anavyompenda. Lakini hata hivyo ndoa ya Quibillah na Theodore haikudumu, ilivunjika baada ya kuishi pamoja kwa kipindi kisichozidi mwezi mmoja tangu wafunge ndoa.

  Hiyo ni baada ya Theodore kurudia vitendo vyake vya kikatili kwa kumsukuma Quibillah nje ya gari lililokuwa likitembea na kutishia kumpiga risasi. Malcolm akawa amechanganyikiwa kwa tukio hilo la kutengena kwa wazazi wake na kuanzia hapo akawa na tabia mbaya. Asubuhi ya Februari 26, 1997, Quibillah Shabazz alipiga simu kituo cha Polisi na kuwaeleza kuwa ametishiwa maisha na mwanaye huyo Malcolm.

  Wakati Polisi walipofika nyumbani kwake, aliwaeleza Polisi kuwa mwanaye huyo anayo matatizo ya kiakili na amekataa matibabu. Naye Malcolm kwa upande wake aliwaeleza Polisi kwamba, alikuwa na hasira kwa sababu mama yake alikuwa amelewa sana na alikataa kumpeleka shule kwa gari.

  Polisi waliamini kuwa, wote mama na mwanaye walikuwa na matatizo ya kaikili yaliyotokana na msongo wa mawazo. Hivyo waliamua kuwapeleka katika Hospitali maalum inayotibu matatizo ya msongo wa mawazo (Depression). Baadaye waliruhusiwa kutoka baada ya kuonesha dalili ya kupata nafuu.

  Mwezi mmoja baadaye Quibillah alipiga simu tena Polisi na kuwaeleza kwamba, yeye na mwanaye hawaelewani kabisa na hivyo alitaka kujua njia sahihi ya kumkabidhi mwanaye huyo kwa mlezi mwingine atakemlea kisheria. Afisa wa Polisi aliyepokea simu hiyo alimshauri ampeleke katika vituo vya kijamii vinavyojishughulisha na kuwalea watoto wasiopata malezi bora kutoka kwa wazazi au walezi wao.

  Lakini hata hivyo Quibillah hakuzingatia ushauri huo na badala yake aliamua kuomba msaada kwa mama yake, Dk. Betty Shabazz ambaye kwa furaha bila kujua kuwa mtoto huyo atamsababishia umauti, alikubali kumpokea mjukuu wake huyo na kuishi naye.
  Kwa ujumla familia yote ya Malcolm X ilifurahishwa na kitendo cha Malcolm mdogo kutengenishwa na mama yake. Hata hivyo hiyo ilikuwa ni kinyume na Malcolm Mwenyewe, kwani hakufurahishwa na kutenganishwa na marafiki zake kwa kupelekwa jimboni New York kuishi na bibi yake, na alikuwa na hasira zaidi kwa kitendo cha kuhamishwa mara kwa mara kutoka mji mmoja hadi mwingine.

  Kutokana na hali hiyo, Malcolm hakupenda kucheza na watoto wenzie, kwani aliogopa kuwa, kama akiwakosea watoto wenzie, bibi yake atamrudisha jimboni Texas kwa mama yake, kitu ambacho hakukipenda. Lakini masikini hali haikuwa kama vile ilivyotarajiwa, mtoto Malcolm akageuka kuwa muuwaji wa bibi yake kwa kumchoma kwa moto akiwa ndani amelala. Baada ya kupata taarifa kuwa mama yake ameunguzwa na moto na mwanaye Malcolm, Quibillah alipanda ndege haraka kuelekea New York na lipofika pale Hospitalini alikolazwa mama yake, muda wote alikuwa akilia pembeni ya kitanda alicholala mama yake hadi macho yakavimba.

  Wakati mwingine alikuwa akienda kwenye jela ya watoto alikohofadhiwa mwanaye akisubiri kusomewa mashitaka ya kujeruhi kwa moto. Mtoto Malcolm alifikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama ya Yonkers hapo mnamo Julai 11, 1997. Mwanasheria aliyekuwa akimtetea Malcolm aliyejulikana kwa jina la Percy Sutton na mama yake Quibillah walionyesha kutoridhishwa kwao na jinsi Malcolm alivyokuwa hatendewi haki na mahakama, waendesha mashtaka na vyombo vya habari.

  "Ni mtoto ambaye amefika kwenye kilele cha matukio ya kutisha katika malezi yake, ni mtoto ambaye ameishi maisha ya tabu kwa kipindi cha miaka yote toka kuzaliwa kwake na ni mtoto ambaye anahitaji uangalizi, ni vigumu kwangu kusema kile alichonieleza zaidi ya kuomba kusamehewa kwa tukio lililotokea." Alisema mwanasheria Sutton.

  Wakati kesi hiyo ilipokuwa ikisikilizwa kwa mara ya kwanza, mtoto Malcolm ambaye alikuwa amebeba uso wa huzuni na kutoamini juu ya tukio lililotokea, aliulizwa na mwendesha mashitaka Barbara Kukowski kama anakumbuka ni kosa gani alilofanya.

  Malcolm kwa kifupi alijibu, "Kuwasha moto"

  Mheshimiwa Jaji Howard Spitz haraka aliingilia kati na kumuonya mwendesha mashitaka Barbara kuwa, si vyema kuingia kwa undani katika suala hilo. Ndipo mwendesha mashitaka huyo akamuuliza Malcolm swali jingine. "Je ni kweli kwa uzembe ulisababisha kifo cha mtu mwingine……. Wakati ukijua dhahiri kuwa kulikuwa na mtu ndani ya nyumba na wewe ukasababisha moto?"
  "Ndiyo" Malcolm alijibu tena kwa kifupi.

  Akiongea na waandishi wa habari, mwanasheria aliyekuwa akimtetea mtoto Malcolm, Percy Sutton, alisema, "Nimeshawahi kuona matukio mengi ya kutisha, lakini tukio hili ni la kusikitisha zaidi."

  Mnamo Agosti 8, 1997, Malcolm alifikishwa kwenye mahakama inayohusika na mashauri ya kifamilia kwa ajili ya kusomewa hukumu. Jaji Spitz aliamuru Malcolm ahifadhiwe katika kituo cha kuchunguza mwenendo wa tabia kwa watoto wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali cha Hillcrest Education Center kwa muda wa miezi 18 muda ambao utakuwa ukiongezwa mpaka atakapotimiza umri wa miaka 18.

  "Unayo changamoto kubwa huko mbeleni katika maisha yako, najua unaweza kujirekebisha na kuwa raia mwema anayeweza kutoa mchango wake katika Taifa. Nakutakia maisha mema na Mungu akubariki." Alisema Mheshimiwa Jaji Spitz.

  Malcolm aliachiwa baada ya miaka minne, ilikuwa ni mwaka 2001. Mnamo mwaka 2003 akihojiwa na gazeti la The New York Times, Malcolm wakati huo akiwa na umri wa miaka 18 alisema kwamba, hakuwa na furaha kuwa mbali na mama yake hivyo aliamua kuwa na tabia mbaya ili kumshawishi bibi yake amrejeshe kwa mama yake lakini mbinu hiyo ikashindikana, na ndio akapata wazo la kuwasha moto ndani ya nyumba. Kwa maneno yake mwenyewe Malcolm alisema:

  "Niliwasha moto kwenye kibaraza na sikudhani kama ungeleta madhara makubwa kiasi kile, lakini hakutakiwa kukimbilia upande ule ambapo moto ulikuwa ukiwaka kwani kulikuwa na mlango mwingine wa kutokea akiwa chumbani kwake. Nafikiri alidhani mimi niko chumbani wakati ule na ndio sababu alikimbilia upande ule wenye moto ili kuniokoa."

  Baada ya kuachiwa Malcolm alikwenda kuishi na mama yake mdogo Ilyasah Shabazz. Alikamatwa kwa kosa la wizi wa dola 100 mwaka 2002. Alipatikana na kosa la uporaji na kufungwa kifungo cha miaka 3 na nusu jela. Malcolm alikamatwa tena mwaka 2006 miezi michache baada ya kutoka jela kwa kosa la kutoboa dirisha la kioo kwenye duka moja kwa nia ya kuiba.

  Mnamo mwaka 2010 alikwenda kuhiji Maka, na kuanzia mwaka 2011 alijiunga na chuo cha John Jay College of Criminal Justice
   
 2. MadameX

  MadameX JF-Expert Member

  #2
  Apr 5, 2012
  Joined: Dec 27, 2009
  Messages: 7,847
  Likes Received: 64
  Trophy Points: 145
  Nitazeeka nasoma hii mkitu anyways...enjoy your stay there...nisalimie shangazi wa pale Mauya
   
 3. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #3
  Apr 5, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Kwa nini Uzeeke? Unaongeza knowledge kwa kusoma simulizi ndefu na wala huzeeki kama unavyodhani.................
   
 4. Twande

  Twande JF-Expert Member

  #4
  Apr 5, 2012
  Joined: Dec 31, 2009
  Messages: 543
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Ooh yes. . mi nimemaliza si unajua ni mdau! inasikitisha sana. . iam still wondering kama huyu kijana atakuja kuwa clean! ni muharifu tu! born that way? au ni maisha aliyoyachagua? hata kama background zinaharibu watu kwa huyu alikuwa na ndugu wenye nafasi na watakatifu angeweza wafuata hao badala ya mama yake! yani maisha haya! poor that mama kifo cha moto!? too sad cjui nisemeje jamani. .
   
 5. Blaki Womani

  Blaki Womani JF-Expert Member

  #5
  Apr 5, 2012
  Joined: Feb 28, 2011
  Messages: 8,460
  Likes Received: 3,715
  Trophy Points: 280
  Nimesoma hadi mwisho inasikisha.amerithi tabia ya baba yake nini hata ajulikani
   
 6. ntogwisangu

  ntogwisangu JF-Expert Member

  #6
  Apr 5, 2012
  Joined: Nov 25, 2011
  Messages: 516
  Likes Received: 25
  Trophy Points: 35
  big up mkuu!!endelea kutupa vitu kama hivi!!!!we need .O.J Simpson story!
   
 7. Mr Rocky

  Mr Rocky JF-Expert Member

  #7
  Apr 5, 2012
  Joined: Oct 10, 2007
  Messages: 15,186
  Likes Received: 570
  Trophy Points: 280
  Inasikitisha
  Ila hata sidhani kuna mabadiliko kwa huyu kijana
  bbado safari ni ndefu sana kwake kubadilika na kuishi maisha ambayo aliombewa na judge
   
 8. NATA

  NATA JF-Expert Member

  #8
  Apr 5, 2012
  Joined: May 10, 2007
  Messages: 4,516
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 135
  Gustavo ndani ya nyumba!

  Thanks inasikitisha lkn maisha ya kijana hayakuwa mazuri hata kidogo.
  Mlezi mlevi amuangalie saa ngapi mwanae.

  Masikini bibi R.I.P
   
 9. TaiJike

  TaiJike JF-Expert Member

  #9
  Apr 5, 2012
  Joined: Dec 14, 2011
  Messages: 1,475
  Likes Received: 174
  Trophy Points: 160
  Ni kisa mkasa wenye kusikisha sana, ingawa wenye funzo tosha kwa vizazi vyetu vya sasa na aina ya malezi wapatayo watoto wetu. Tunatakiwa kuangalia na kuwa makini sana na mambo ambayo yanawazunguka watoto ili wasiweze kuathiriwa kiakili. Mtoto Malcom pamoja na mama yake waliathirika vibaya kiakili kutokana na yale yaliyowazunguka.
   
 10. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #10
  Apr 5, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Kesi ya O J Simpson iko JIKONI..............
   
 11. kitalolo

  kitalolo JF-Expert Member

  #11
  Apr 5, 2012
  Joined: Dec 4, 2006
  Messages: 1,846
  Likes Received: 13
  Trophy Points: 135
  Ngoja kidogo tuko kwenye breking nyiuzi Jukwaa la siasa.
  mauchungu yakiisha ntakuja pita.

  HAPPY HOLLY WEEK AND EASTER
   
 12. M

  MandawaNaManenge Member

  #12
  Apr 5, 2012
  Joined: Jan 27, 2012
  Messages: 80
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 13
  Kwakweli , nimepata vipelemsisimko ( goose-pimples).
  Asante Ndugu Mtambuzi. Salimia Mkwaja na weekend njema.

  Ila jamani hizi familia mparaganyiko nazo kazi!!
   
 13. Mamndenyi

  Mamndenyi JF-Expert Member

  #13
  Apr 5, 2012
  Joined: Apr 11, 2011
  Messages: 29,108
  Likes Received: 6,585
  Trophy Points: 280
  inasikitisha sana,
  mama mzazi hakutimiza wajibu wake kwa mwanaye,
  bibi alitimiza wajibu wake,
  kumbe inabidi kila mtu kuishi na mwanaye, inatoa fundisho,
  asante
  Nakutakia pasaka ya furaha huko milimani uendako.
   
 14. toghocho

  toghocho JF-Expert Member

  #14
  Apr 5, 2012
  Joined: Mar 16, 2011
  Messages: 1,177
  Likes Received: 21
  Trophy Points: 135
  dah!inasikitisha sana, nimeisoma mpaka mwisho, hivi huko marekani life likipinda kidogo tu watu wanakuwa kama wehu, dah hapa bongo watu wamepindiwa lakini waaaaaaaaala, wananpeta tu
   
 15. Bujibuji

  Bujibuji JF-Expert Member

  #15
  Apr 5, 2012
  Joined: Feb 4, 2009
  Messages: 35,336
  Likes Received: 22,188
  Trophy Points: 280
  KAsumba, hamna lolote la maana kwenye uzi huuu
   
 16. BRO LEE

  BRO LEE JF-Expert Member

  #16
  Apr 6, 2012
  Joined: Dec 25, 2011
  Messages: 580
  Likes Received: 42
  Trophy Points: 45
  Nimefurahi sana kusoma kisa hiki kwa undani mkuu, kwani nilikuwa nakifuatilia ktk gazeti la jitambue na ckufanikiwa kupata mtiririko mzuri kama huu.
   
 17. JS

  JS JF-Expert Member

  #17
  Apr 6, 2012
  Joined: Sep 29, 2009
  Messages: 2,065
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Acha wivu........
   
 18. JS

  JS JF-Expert Member

  #18
  Apr 6, 2012
  Joined: Sep 29, 2009
  Messages: 2,065
  Likes Received: 18
  Trophy Points: 135
  Mtambuzi asante sana kwa uzi huu. Nimejifunza kitu leo kuhusu familia ya Malcolm X..huyo mjukuu is a disgrace to the family and mostly to the great name he carries of his grandfather...Mungu amsaidie abadilike...

  Sikukuu njema Mtambuzi
   
 19. mojoki

  mojoki JF-Expert Member

  #19
  Apr 7, 2012
  Joined: Oct 21, 2010
  Messages: 1,333
  Likes Received: 32
  Trophy Points: 145
  hapa majifunza kwamba kumbe wakati mwingine jel haisaidii chochote... Nilidhan akitoka huko atakua amepata mda wa kutosha kuyajutia maisha yake na matendo yake ya nyuma na atajipanga upya kumbe ndo amezidi kuwa chenga
   
 20. m

  mdoe mchaina Senior Member

  #20
  Apr 7, 2012
  Joined: Dec 1, 2011
  Messages: 138
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  asante kiongozi ni story nzuri ni mejifunza mengi kwa maisha ya hawa wapigania haki za watu weusi marekani ila hii ya malcom mdogo sikuwa nayo .mapumziko mema kaka ukifika bweni nisalimie wajukuu wa shehe kombo
   
Loading...