Mitandao isitumike kumchafua Rais
Tanzania Daima. 15 Feb, 2012
HIVI karibuni, Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (Necta), lilitangaza matokeo ya kidato cha nne yaliyofanyika nchini mwaka 2011.
Na miongoni mwa wahitimu waliofanya mtihani huo ni mtoto wa Rais Jakaya Kikwete, aliyemaliza katika moja ya shule za sekondari jijini Dar es Salaam.
Kwa bahati mbaya sana, matokeo ya mtoto huyo hayakuwa mazuri licha ya shule yake kufanya vizuri kitaifa katika mitihani hiyo na kuwa moja ya shule kumi bora.
Hoja yetu si kurejea matokeo hayo, bali tungependa kukemea matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii hasa wakati wa kujadili masuala kadhaa na hata mengine ambayo kimsingi ni ya kibinafsi lakini yanahusishwa moja kwa moja na maslahi kwa umma.
Tunasema hivyo kutokana na baadhi ya wachangiaji kwenye mitandao hiyo, kuchukulia matokeo mabaya ya mtoto wa Rais kama suala la kitaifa lenye kuhusishwa na uongozi wa baba yake, na hivyo kumshambulia kiongozi huyo bila sababu ya msingi.
Kwanza, lazima tutambue kuwa kufanya vibaya katika mitihani ni jmabo la bahati mbaya ambalo kimsingi linamuumiza mtahiniwa na vile vile wazazi au walezi wake, lakini tunapaswa kuelewa kuwa mtoto wa Rais ameshindwa kama walivyoshindwa wanafunzi wengine pasipo kujali amesoma shule gani au mzazi ana wadhifa gani.
Pili, tunapaswa kulichukulia jambo hili kama funzo na changamoto kwa elimu yetu, kwani ni watoto wachache sana wa viongozi wetu wakuu wanasoma shule za hapa Tanzania, na kwa ubabaishaji uliyopo kwenye usimamizi wa mitihani bado Rais angeweza kutumia nguvu yake kuhakikisha mwanaye anapendelewa lakini haikuwa hivyo.
Ni vyema wakati wa kujadili na kuchangia maoni hasa kuwahusu watawala wetu, tukazingatia majukumu na wajibu wa msingi tunaowapa viongozi ili watekeleze, na hivyo tunapaswa kuwahukumu kwa kuzingatia mipaka hiyo si kuingilia hata mambo yao binafsi na familia zao.
Mtoto wa Rais kushindwa mtihani si jambo la kutufanya tumtukane baba yake, yeye si malaika kwani huo ndiyo uwezo aliopewa na Mungu na walimu wake wakaongezea ujuzi wao.
Kama hoja ni kwamba kila anayeshindwa mtihani wazazi wake wasakamwe kwa matusi, basi hebu tuwatazame kwanza wa kwetu.
Tunaamini umefika wakati kwa wale wamiliki wa mitandao hiyo kuwa makini na hoja zinazoletwa hewani kujadiliwa na kujifanyia uhakiki kabla ya kuzichapisha, vnginevyo tutajikuta tumegeuka taifa linalovunja haki za msingi za binadamu kwa kuingilia masuala binafsi ya watu wengine.
Kama hoja ni kufeli kwa mtoto wa Rais, basi kafeli kama wale wa kwetu ambao tunawasomesha kwenye shule duni au zile za mamilioni lakini mwisho wa siku hawafaulu, sasa iweje tumwandame kiongozi wetu kwa suala lisilohusiana na kazi tuliyompa?
Tundhani kwa hili Rais alipaswa kusifiwa kuwa si mbinafsi kwa kuwa hakumpeleka mtoto wake kusoma Ulaya kama ambavyo viongozi wengi wa nchi hii wafanyavyo hata kwa watoto wao wasiokuwa na uwezo kimasomo.