Misamaha ya kusalimisha silaha haramu ni kila mwaka?

Misamaha ya kusalimisha silaha haramu ni kila mwaka?

Elias Msuya

Platinum Member
Joined
Dec 23, 2011
Posts
238
Reaction score
942
hq720.jpg
Wakati Jeshi la Polisi nchini likitangaza msamaha wa miezi mwili wa kutoshtakiwa kwa watu wote wanaomiliki silaha kinyume, imebainika kuwa misamaha hiyo imekuwa ikitolewa mara kwa mara kiasi cha kuibua hoja ya usalama wa wananchi ikiwa watu hao wanajimilikisha silaha na baadaye kupata misamaha.

Akizungumza Septemba Mosi 2025, Msemaji wa Jeshi la Polisi, DCP David Misime amesema msamaha umetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa, chini ya Kifungu cha 66 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015, kwamba silaha zikabidhiwe Vituo vya Polisi, Ofisi za Serikali za Mitaa, au kwa Watendaji wa Kata na Shehia.

Amewataka wanaomiliki silaha haramu wajisalimishe kuanzia Septemba 1, 2025 hadi Oktoba 31, 2025 katika vituo vya Polisi vilivyotajwa na kutangazwa na Serikali.

Ametoa taarifa hiyo, wakati kukiwa na taarifa kuwa kuna kontena la silaha lililoingizwa nchini kupitia bandari ya Dar es Salaam. Hata hivyo, Misime amekanusha taarifa hizo akisema taarifa hizo ni za uongo.

Misime amebainisha kuwa kuwa uchunguzi wa Jeshi hilo haujathibitisha jambo hilo, na kuwaonya watu wanaotumia mitandao ya mijamii kuzusha taarifa za uongo kwa nia ya kihalifu.

Misamaha kila mara

Hii si mara ya kwanza kwa Jeshi la Polisi kutangaza msamaha kwa wanaomiliki silaha kwa njia haramu. Kwa nyakati tofauti watu hao wamekuwa wakitangaziwa misamaha, japo haijulikani kama silaha zote huwa zinasalimishwa.

Juni 28, 2024, Msemaji wa Polisi, David Misime alitoa taarifa akiwataka wananchi kusalimisha silaha zilizokuwa zinamilikiwa kihalali na ndugu zao ambao kwa sasa ni Marehemu, ili silaha hizo zisilete madhara katika jamii na kusema kuendelea kuhifadhi silaha hizo nyumbani ni kinyume cha sharia.

Alionya kwamba, atakayepatikana akimiliki silaha hizo akikutwa na hatia Mahakamani anaweza kufungwa miaka 15 jela au faini ya Sh milioni 10 au vyote kwa pamoja.

Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 55 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015 ni kwamba mmiliki wa silaha mara anapofariki, ndugu wa marehemu wanapaswa kuisalimisha silaha hiyo katika kituo cha Polisi kilicho karibu wakati taratibu za mirathi na umilikishwaji kwa Mtu mwingine kwa mujibu wa sheria zikiendelea.

Oktoba 16, 2024, aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoani Kigoma, SACP Filemon Makungu aliwataka wananchi ambao hawajasalimisha silaha zao kufanya hivyo kwani muda wa kusalimisha ukiisha msako mkali utaanza ili kuwabaini wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.

Makungu alikuwa akieleza mafanikio ya misako na operesheni mbalimbali zilizofanyika kuanzia Septemba 17 mwaka huu hadi Oktoba 14 2024, akisema tangu kuanza kwa usalimishaji wa silaha kwa hiari ni mwananchi mmoja pekee ambae amesalimisha silaha aina ya AK 47 aliyokuwa akimiliki kinyume na sheria.

Mwaka 2023 nao kulikuwa na misamaha kwa wanaomiliki silaha haramu.

Oktoba 5, 2023, Jeshi la Polisi lilitoa taarifa ya kuwakumbusha wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kuendelea kutumia vizuri msamaha uliotolewa na Serikali ambapo atakayesalimisha kwa hiari hatachukuliwa hatua yeyote wala kuulizwa maswali.

Msamaha huo ulianza toka Septemba 1, 2023 na mwisho ni Oktoba 31, 2023, ambapo wananchi walitakiwa kurejesha silaha zikiwamo zile za wamiliki waliofariki ambazo ndugu zao bado wanazo majumbani.

Taarifa hiyo ilisema wanaliomiliki silaha kinyume cha sheria wanaposalimisha kwa hiari, faida yake ni kutokukamatwa na kufikishwa mahakamani.

“Endapo silaha hizo hazitasalimishwa katika muda wa msamaha uliotolewa na Serikali, operesheni ya nchi nzima itakapoanza wanaomiliki silaha hizo watakamatwa na kufikishwa mahakamani na wakipatikana na hatia kifungo chake ni miaka 15 jela au faini ya shilingi milioni 10 au vyote kwa pamoja,” ilisema taarifa hiyo.

Agosti 30, 2023 Msemaji wa Jeshi hilo SACP David Misime alitoa taarifa akiwataka wale wote wanaomiliki silaha haramu kuzisalimisha kuanzia Septemba, 1 hadi Oktoba 31 mwaka huu.

Agizo hilo lilifuatia msamaha wa kutoshtakiwa kwa wale wote watakaozisalimisha silaha hizo uliotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mhandisi Hamad Masauni chini ya Kifungu cha 64 cha Sheria ya Udhibiti wa Silaha na Risasi ya Mwaka 2015, Sura ya 223.

Kupitia taarifa iliyotolewa leo na, imesema kufanya hivyo ni kudhibiti uzagaaji wa silaha haramu kama ilivyokuwa makubaliano ya 2018 ya udhibiti wa silaha hizo.

Mwaka 2022, Serikali ilitoa pia misamaha kwa wamiliki haramu wa silaha.

Jeshi la Polisi latangaza msamaha kwa watakao salimisha silaha haramu. Septemba 5, 2022 huyo huyo alitoa taarifa akisema kulikuwa na kampeni maalum inayojulikana kama Msamaha wa Afrika iliyohusisha usalimishaji wa silaha haramu kwa hiari zinazomilikiwa na baadhi ya watu kinyume cha sheria, ama kwa kutokujua taratibu za kisheria za umiliki wa silaha hizo.

Mwaka 2022 Jeshi la Polisi liliteketeza silaha haramu 6,208 ambazo zilikusanywa wakati wa kampeni maalum ya wananchi kusalimisha silaha hizo.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini, alilitaka Jeshi la Polisi nchini kuongeza nguvu kudhibiti uingizaji silaha haramu ili kusaidia kupunguza matukio ya uvunjifu wa amani yanayo chochewa na ongezeko la silaha haramu nchini.

Mwaka 2021, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla aliwataka majambazi na wahalifu kujisalimisha polisi na kukabidhi silaha zao huku akitangaza operesheni ya kuwasaka popote walipo.

Alitoa kauli hiyo leo Jumanne Mei 25, 2021 baada ya kikao chake na makamanda wa polisi huku akirejea matukio yaliyotokea hivi karibuni likiwemo la Mbezi ambapo Jimmy Kibiti aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akitoka benki na kuporwa Sh4 milioni na la jana la mfanyabiashara kujeruhiwa kwa risasi eneo la Mabibo.

Misamaha hiyo ilikuwepo kwa muda mrefu. Kwa mfano Julai 26, 2013, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete aliwaonya wanaomiliki silaha kiharamu. Akizungumza katika mkutano wa hadhara wilayani Ngara Mkoa wa Kagera, Rais Kikwete alitoa wiki mbili kwa majambazi kusalimisha silaha na kujisalimisha.

"Nimechoka tutafanya operesheni kubwa ambayo haijawahi kutokea Kagera, Geita na KigomA kwa kuvishirikisha vyombo vyote vya ulinzi mnavyovijua, akivitaja, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi na Idara ya Usalama wa Taifa.

Zaidi Soma
 
Back
Top Bottom