Mikoa yetu katika Ilani za CCM na CHADEMA

Oct 6, 2020
27
50
Wakati watanzania wakiendelea kutafakari kable ya kuamua watakichagua chama gani kushika dola, miongoni mwa mambo yanayoweza kuwaongoza ni namna ambavyo vyama vya siasa vimezingatia mahitaji ya maeneo wanamoishi wapigakura, na hivyo kata, wilaya na/au mikoa yao. Mbali na kuangalia mahitaji ya maeneno, inatarajiwa vyama hivi katika mitarajio yake, vina mipango ya kuendesha miradi ya maendeleo ambayo ni mahususi katika mkoa Fulani. Makala haya yanaangazia ilani za vyama viwili vyenye nguvu zaidi nchini, kuona ni kitu gani vyama hivi vikipewa dhamana vitafanya nini mkoa gani. Kama vina masuala viliyoyataja, basi ni rahisi kwa watekelezaji wa ilani hizi kuzigatua kwa ajili ya mkoa mmoja mmoja.

Arusha ni mkoa umetajwa mara 55 katika ilani ya CCM ikiwa ni Pamoja na kwamba, chama kitakomesha matumizi ya bangi na mirungi katika mkoa huo, na kwamba maghala makubwa ya kuhifadhi chakula katika mkoa huo yatakarabatiwa, na vituo vya kuchakata mazao kwa ajili ya mauzo ya nje vitajengwa. Hata hivyo ilani ya CHADEMA haiutaji mkoa huu.

Dar es salaam imetajwa mara 85 katika ilani ya CCM, ikieleza Pamoja na mengine kwamba yatafunguliwa matawi ya benki ya maendeleo katika mkoa huu kwa ajili ya kuwahudumia watu wa vipato vya chini ambapo mikopo nafuu itapatikana kwa ajili ya wakulima na wengine. Katika ilani ya CHADEMA, Dar es Salaam imetajwa mara 7. Hapo chama hiki kinaeleza kusidio lake la kuongeza ufanisi wa bandari jijini, kuanzishwa kwa mamlaka ya halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, ili wakazi wanufaike, ajira ziongezeke na pato liinuke.

Dodoma imetajwa mara 116 katika ilani ya CCM, ambako maendeleo ya ushirika wa kilimo yataendelea kujengwa na maeneo ya wajasiriamali wadogo wadogo yatatengwa. Vijana watajengewa uwezo katika mkoa huo na kupatiwa vifaa vya uzalishaji mali. Makao makuu ya nchi hayaongelewi kwenye ilani ya CHADEMA.

Geita ni mkoa uliotajwa mara 36 katika ilani ya CCM. Inaelezwa mkoa huu umejengewa skimu ya kilimo cha umwagiliaji, na barabara ya Geita – Bukoli – Kahama ya kilometa 107 itajengwa. Ilani ya CHADEMA haikuona haja ya kuutaja mkoa huu.

Iringa inajitokeza mara 49 katika ilani ya CCM. Huko mashamba yaliyoathiriwa na tindikali yatarejeshewa rutuba na kutapunguzwa upotevu wa mazao baada ya kuzalishwa shambani. Huu ni mkoa ambao kilichoandikwa katika ilani ya CHADEMA kiliusahau.

Kagera umetajwa mara 22 katika ilani ya CCM. Katika mkoa huu CCM inaeleza kuwa imefanikiwa kurejesha mali za ushirika zilizoporwa na wachache, na kwamba daraja la Kitengule linaendelea kujengwa, na ujenzi wa daraja la Kalebe utaanza. Hakuna jina Kagera katika mipango ya kiilani ya CHADEMA.

Katavi ni mkoa uliotajwa mara 10 na Chama cha Mapinduzi. Mkoa huu utapata ukarabati wa daraja la Ugalla, daraja la Mirumba litaanza kujengwa na ni miongoni mwa mikoa mipya itakayojengewa hospitali kubwa za rufaa. Mkoa huu haujalengwa katika ilani ya CHADEMA.

Kigoma umetajwa na CCM mara 39, ambako vyama 12 vya ushirika vya michikichi vimefufuliwa, na wakala wa elimu ya mafunzo ya uvuvi wanaimarishwa huko Kibirizi. Aidha, Maragarasi juu katika barabara ya Buhigwe-Kitanga – Kumsegwa kutajengwa daraja. Kigoma haimo kwenye ilani ya CHADEMA.

Kilimanjaro inaonekana mara 15 katika ilani ya CCM. Huko kunatajwa mradi uliofanyika wa kufungwa kwa rada za kisasa na jengo jipya la abiria katika uwanja wa kimataifa wa ndege, lakini bado kuna mpango wa kununua rada ya hali ya hewa na kuifunga mkoani humo. Huu mkoa umetajwa mara moja katika ilani ya CHADEMA inapoongelea kushughulikia majanga, na kwamba serikali itakuwa mfariji mkuu watu wanapopata majanga kama vile mafuriko.

Lindi unajitokeza mara 41 katika ilani ya chama cha wakulima na wafanyakazi. CCM inataja ilivyofanikiwa katika kuanzishwa kwa vyama viwili vya ushirika mkoani humo. Mkoani humo, eneo la Nyegendi kutaanzishwa kituo cha kuzalisha vifaranga vya samaki kama sehemu ya mpango wa chama wa kustawisha viumbe-maji. Lilipotafutwa jina la mkoa huu katika ilani ya CHADEMA, halikuonekana.

Manyara ipo mara 23 kwenye ilani ya CCM. Ila baadhi ya kurasa, kilichotajwa ni Lake Manyara. Miwa ya mkoani humo imetajwa, na viwanda vitatu vya SIDO vilivyoanzishwa huko, na upembuzi yakinifu wa kiwanja cha ndege cha Manyara utafanyika. Uchunguzi wa ilani haukupata neno Manyara kwenye ilani ya CHADEMA.

Mara ni mkoa uliotajwa takribani mara 15 katika ilani ya CCM. Huko chama hiki kinakumbuka kujengwa kwa mahakama kuu mkoani humo, na jinsi kamati ya maafa ya mkoa ilivyofanywa kuwa imara zaidi. Kumejengwa pia jengo la huduma za dharura za kitabibu. Mkoa huu nao haumo kwenye ilani ya CHADEMA.

Mbeya imeandikwa mara 44 katika ilani ya CCM. Huko watumiaji wa madawa ya kulevya watapewa matibabu na serikali, na kutaanzishwa vituo vyenye kuweza kutoa huduma kama once stop centres, kadhalika madampo yatajengwa ili kuimarisha usafi wa mazingira na afya za wananchi. Ilani ya CHADEMA haiusemei mkoa huu.

Morogoro unahesabika mara 47 ndani ya ilani ya chama tawala. Ni mkoa ambao ccm inaweka kumbukumbu kwenye ilani, kwamba tafiti zikiwemo za maendeleo ya utamaduni, mil ana desturi zimefanyika huko, na mafunzo ya kuboresha utendaji katika elimu yatafanyika katika mikoa kadhaa ikiwemo Morogoro. Jina la mkoa huu linajitokea mara mbili kwenye ilani ya CHADEMA, ikiwa inakiongelea Chuo Kikuu cha Sokoine kinachopatikana mkoani humo, na kwamba kitashauriwa kuwa na mtaala wa kilimo cha oganiki.

Mtwara unatajwa na CCM mara 58 kwa kukumbuka kwamba ni mkoa ambao umekuwa mwenyeji mzuri wa mikutano ya mahusiano mwema na nchi jirani, kama vile Msumbiji, na unatajwa mpango wa kuboresha maeneo ya kuvinjari na utalii katika mkoa huo. Ilani ya CHADEMA inautaja pia mkoa huu mara mbili, hususan inapoongelea lengo lake la kuongeza ufanisi wa bandari ya Mtwara.

Mwanza upo mara 81 kwenye ilani ya chama cha rangi za kijani na njano. Katika mkoa huo, CCM inajivunia kukarabatiwa kwa uwanja wa Nyamagana, hapa ikitaja maendeleo katika sekta ya michezo. Katika mkoa huu seriali ya CCm itaendelea kutoa elimu ya kukabiliana na majanga. Watanzania watakuwa wanaelewa sababu hasa ya hili. Mwanza nao, hautajwi na watunga ilani wa CHADEMA.

Njombe ambao ni mmoja wa mikoa mpya, jina lake limekumbukwa na CCM mara 34. Huko kutajengwa stand ya mabasi katika jitihada za chama za kuboresha usafiri. Kumekamilishwa makazi ya wakuu wa mikoa, na mahakama ya hakimu mkazi imekamilika. Mkoa umepewa zana muhimu za kiutawala. Jina Njombe halimo kwenye ilani ya CHADEMA.

Pwani ni jina la mkoa linalopatikana mara 33 (si lazima kwamba unaotajwa ni mkoa huo au ukanda wa pwani) katika ilani ya CCM. Huko kutawekwa Pamoja na mambo mengine, mkakati wa kuhifadhi mazingira katika ukanda husika, elimu ya matumizi endelevu ya rasilimali itatolewa, na jamii zitajengewa uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Neno pwani linaonekana mara 4 katika ilani ya CHADEMA, ambapo chama hiki kinataja kuendeleza uvuvi, na kitakavyosimamia uvunaji wa rasilimali nyingine za majini.

Rukwa umetajwa mara 8 katika ilani ya chama tawala. Ni mkoa ambao chama kimeendelea kutoa elimu ya kukabiliana na majanga, na ili kukabili ukame mkoani humo ujenzi wa bwawa kubwa umeanza, hususan bwawa ka Nkasi. Rukwa hausemewi kwenye ilani ya CHADEMA.

Ruvuma umeorodheshwa mara 19 katika ilani ya CCM. Huko kumekuwa na uboreshaji wa usimamizi wa serikali za mitaa, na kutajengwa ghala jipya la kuhifadhia vifaa tiba na madawa. Kama kwa mikoa mingine, ilani ya CHADEMA iko kimya kuhusu Ruvuma.

Shinyanga ipo mara 31 kwenye kurasa za ilani ya CCM. Huko kutaboreshwa makazi ya wazee wetu katika kituo cha Kolandoto. Na huko serikali ya CCM ilifanikiwa kuboresha machinjio kwani mkoa huu una uzalishaji mkubwa wa nyama. Shinyanga hautajwi na chama cha Demokrasia na Maendeleo.

Simiyu ni mkoa uliotajwa mara 20 na CCM. Huko, serikali ya chama hiki imetoa mwongozo thabiti wa uwekezaji, na mradi mkubwa wa maji umeanza kutekelezwa ili kuyakabili mabadiliko ya tabianchi. Huu ni mkoa ambao haujaongelewa kwenye ilani ya CHADEMA.

Singida umetajwa mara 33 na chama cha mapinduzi, ukiwa umepangiwa kupelekewa kikamilifu maji toka ziwa Victoria, na umetajwa pia uboreshaji wa hospitali ya rufaa uliofanyika mkoani humo. Hakuna neno Singida, kwenye ilani ya CHADEMA.

Songwe ni jina linalotajwa na CCM mara 24. Huko, serikali ya chama hiki ilifanikisha kuanza kwa uchimbaji wa makaa yam awe, eneo liitwalo Kabulo. Izingatiwe kwamba, kutajwa kwa Songwe kumehusisha pia uwanja wa ndege ulioko mkoani Mbeya. Ilani ya CHADEMA iko kimya pia kuhusu jina la mkoa huu.

Tabora inatokea mara 42 kwenye ilani ya CCM. Huko miradi inayoahidiwa na CCM ni Pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa, kati ya Tabor ana Makutupora, na Isaka na Kigoma. Na mji wa Tabora umeelekea kwenye ‘utoronto’ kwa kuwekewa taa za nguvu za jua barabarani. Mkoa huu hautajwi katika ilani ya CHADEMA.

Tanga nayo imetajwa takribani mara 50 na CCM huku kuendelea kujengwa kwa daraja zuri kabisa la Pangani kukibainishwa, na ujenzi tarajiwa wa barabara ya Utofu hadi Majanimapana na Dunga Mwembeni. Aisha bandari na reli zitaendelea kukarabatiwa huko. CHADEMA kinakusudia pia kuboresha bandari ya Tanga, hivyo kimeutaja mkoa huu mara mbili.

Mjini magharibi umetajwa mara 5 katika ilani ya CCM. Kwamba huko, serikali ya CCM ilifanikiwa kuimarisha ulinzi katika sekta ya utalii, na huko CCM ikishinda itajenga sekondari yenye dakhalia! Hakuna jina la mkoa huu katika ilani ya CHADEMA.

Kaskazini Pemba haujatajwa moja kwa moja katika ilani ya CCM, ila miradi ya maendeleo ya kisiwa cha Pemba imetajwa mara nyingi, ikiwa ni Pamoja na hospitali ya Micheweni. CHADEMA kinaitaja Pemba mara moja, kama eneo kutakakoanzishwa eneo maalum la miradi ya ujasiriamali.

Kusini Pemba kumetajwa na CCM mara 2, ambapo kusidio ni kuimarisha vivutio vya utalii huko, na kujengwa kwa ofisi ya ukaguzi wa elimu mkoani humo. Hakuna mahali mkoa huu umetajwa kipekee katika ilani ya CHADEMA.

Kaskazini Unguja nako kumetajwa moja kwa moja katika ilani ya CCM mara 3. Kwamba mkoani humo mradi wa ofisi ya kukagua elimu unatjwa na kutaanzishwa jaa la kusarifu taka. Hakuna neno Unguja katika ilani ya CHADEMA.

Kusini Unguja nako kunatokea mara 3 kwenye ilani ya CCM. Huko kunatajwa juhudi za kutokomezwa magonjwa kama malaria na kipindupindu, na masuala ya utafiti. Ilani ya CHADEMA haiutaji kabisa mkoa huu.

Yamkini CCM imeitaja mikoa yote hii kwa sababu ina kazi iliyofanyika na ina mipango mipya kwa ajili ya maendeleo linganifu ya mikoa yote na inaheshimu ugatuzi katika kuitekeleza. Hivyo, itakuwa rahisi kama CCM ikishinda, watendaji wa mikoa husika hawatababaika katika kujua chama kinataka wafanye nini katika maeneno husika. Aidha pengine, CHADEMA hakikuitaja mikoa mingi ya taifa hili kwa sababu ya mtindo kiliouchagua wa uandishi wa ilani au kwakuwa kinakusudia kuigawanya Tanzania katika majimbo ya kiutawala. Asomaye na achague, kwa ilani hizi, mtu wa mkoa gani anachagua wagombea gani.
fullsizeoutput_1.jpeg
 
Back
Top Bottom