SEHEMU YA 27
Alipofika nje, akamwambia dereva wake kwamba alitakiwa kuendesha gari kwa mwendo wa kasi kuelekea katika Hoteli ya Bavaria. Safari hiyo iliwachukue dakika tano tu, walipofika, akaelekea huko chumbani na kumkuta Fareed akiwa kitandani.
“Nimekuja harakaharaka kama nimepaa,” alisema Bwana Saed huku akivua koti lake na kumfuata Fareed pale alipokaa.
**** Akili ya Godfrey ilikuwa ikimfikiria Fareed tu, kila alipokaa, kichwa chake kilikuwa kwa mwanaume huyo tata. Kikaoni hakuwa na furaha, kila alipokaa alikuwa akimfikiria kiasi kwamba wakati mwingine alijiona kama mgonjwa kwa jinsi aliyokuwa amechanganyikiwa kwa penzi lake.
Siku hiyo hali ilionekana kuwa tofauti kabisa, kila alipokuwa, mara kwa mara alikuwa akisumbuliwa na Fareed kwa kutumiwa meseji na hata wakati mwingine video lakini siku hiyo, alikaa mwanzo wa kikao mpaka mwisho hakukuwa na meseji yoyote aliyokuwa ametumiwa.
Akahisi kwamba kuna tatizo, akahisi kwamba Fareed alikuwa na mwanaume mwingine, moyo wake uliumia, ukamchoma kupita kawaida, hakutaka kukubali, akaanza kumpigia simu, cha ajabu simu ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
“Mbona hapokei simu? Kuna nini? Au yupo na mwanaume mwingine? Au kuna mwenzangu kamuona akirandaranda akamteka, hapana! Ni lazima niwahi kurudi,” alisema Fareed huku akionekana kuchanganyikiwa hasa.
Hakukuwa na raha kikaoni hapo, muda wote kichwa chake kilivurugika, kwa kile kilichokuwa kimetokea cha kutokutumiwa meseji kiliuchanganya moyo wake, hivyo alipotoka kikaoni, moja kwa moja akaingia ndani ya gari alilolikodi kulitumia na kurudi hotelini.
Hakuchukua muda mrefu, akafika na moja kwa moja kuteremka na kuanza kuelekea humo. Alikimbia kama mtu aliyekuwa na haraka fulani, alipoingia ndani ya chumba hicho, hakumuona Fareed, akaelekea bafuni, napo hakuwepo na kila alipompigia simu, iliita bila kupokelewa, uso wake ukavimba kwa hasira.
“Huyu malaya atakuwa ananisaliti! Atakuwa amelala na mwanaume mwingine,” alijisemea huku akionekana kuwa na hasira kali mno.
Aliendelea kumpigia simu, haikuwa ikipokelewa na mwisho wa siku kutokupatikana kabisa, alichanganyikiwa na moyo wake kujawa na hasira kali.