SEHEMU YA 97
“Ooh! Nitakuweepo huko, nitakuja peke yangu kuonana nawe,” aliandika Fareed.
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Niahidi kama tutakuwa wote!”
“Nakuahidi!”
Moyo wa Maria ukaridhika, hakuamini kama hatimaye mwanaume huyo alikubaliana naye kwamba wangeonana na kufanya mambo yao. Moyo wake ukawa na furaha tele, akajitupa kitandani huku akiiona dunia yote kuwa yake kwani kile alichotaka kukisikia ndicho alichoambiwa na mwanaume huyo.
“Nitalala naye na kumuonyeshea kwa nini yule babu amepagawa kwa penzi langu,” alisema Maria na kujilaza kitandani huku akiisubiri kesho ifike, waondoke kuelekea Misri ambapo huko angeonana na mwanaume huyo.
**** Keith hakutaka kukaa sana na mpenzi wake nchini Italia, alichokifanya ni kuondoka na kuelekea katika Mji wa Giza, nchini Misri kwa ajili ya kuyatazama mapiramidi yaliyokuwa nchini humo.
Njiani, bado walionyesheana mapenzi ya dhati, walikuwa wakibusiana sana lakini mawazo ya Maria hayakuwa hapo, alimfanyia mwanaume huyo kila kitu lakini moyo wake, kichwa chake, vyote vilikuwa vikimfikiria Fareed, mwanaume ambaye hakujua kama alikuwa akitoka kimapenzi na mpenzi wake.
Ndege haikuchukua muda mrefu ikafika nchini Misri ndani ya Jiji la Cairo ambapo hapo wakachukua basi lililowapeleka mpaka katika Mji wa El Giza. Macho ya Maria yalishangaa, hakuamini kile alichokuwa kikiona, aliyaona mapiramidi makubwa ambayo alikuwa akiyasoma kwenye vitabu na wakati mwingine kuyaangalia kwenye televisheni.
Alishangaa mno, wakati mwingine alitamani kulia kwani furaha aliyokuwa nayo kipindi hicho ilikuwa kubwa sana. Akamkumbatia mpenzi wake, Keith na kumshukuru sana kwa kumsafisha macho kwa kumpeleka nchini Misri.
“Tutakwenda kule kesho, leo tulale hotelini,” alisema Keith, wakati huo waliyaona mapiramidi yale yakiwa mbali kabisa.
Walipoingia hotelini, kama kawaida wakaanza kucheza michezo ya kimahaba kitandani, kila mmoja alimtamani mwenzake, kila mmoja alihitaji sana kuwa na mwenzake wakati huo.
Japokuwa Maria alijitoa sana kama ilivyo kawaida yake lakini kichwa chake hakikuacha kumfikiria Fareed, kwake, mwanaume huyo alikuwa kila kitu, alikichanganya kichwa chake, muda mwingi alikuwa na mawazo tele juu yake.