SEHEMU YA 125
“Ila ni mbali sana.”
“Ndiyo! Ila mwezi mzima nao ni mwingi mno,” alisema Fareed.
Hawakuwa na jinsi, hakukuwa na uwezekano wa kuwahi huko, ilikuwa ni lazima watumie mwezi mzima mpaka kufika nchini humo. Hawakuwa na hofu, walichojua ni kwamba walikuwa katika mikono salama na kusingekuwa na tatizo lolote lile.
Hawakutaka kujiuliza sana kuhusu mabegi madogo ambayo waliambiwa kwamba ni lazima waingie nayo nchini Marekani na kukutana na mtu ambaye aliwaambia kwamba wangekutana naye. Walimwamini Mustapha, kila mtu ambaye walikutanishwa naye, walimwamini kwa asilimia mia moja.
Safari ikaanza, ilikuwa ni ndefu na yenye kuchosha mno lakini hawakujali. Wiki ya kwanza ikakatika wakiwa majini, ya pili, ya tatu mpaka ya nne bado walikuwa njiani kuelekea nchini Marekani kwa kupitia katika Bahari ya Atlantiki.
Baada ya kupita siku ishirini na nane, wakaingia katika Visiwa vya Puerto Rico ambapo walipokelewa kinyemela na Waarabu wengine na kupelekwa katika nyumba moja kubwa na kutulia huko.
Bado waliendelea kuwaona Waarabu kuwa watu wema, hawakujua mpango mzito waliokuwa nao watu hao, hawakujua kama walikuwa wakienda kutolewa mhanga pasipo wao kujua.
Hapo Puerto Rico walikaa kwa siku mbili kisha kuondoka na kuelekea nchin Cuba ambapo hapo wakakutana na Waarabu wengine waliowaunganisha kwa baadhi ya wanajeshi na kuambiwa lengo la watu hao kufika hapo.
Kutokana na uadui mkubwa baina ya Marekani na Cuba, mipango ikaanza kusukwa upya, ilikuwa ni lazima Marekani ilipuliwe kwa mara nyingine tena na watu hao ndiyo waliowafanyia mpango Fareed na wenzake kuingia nchini Marekani kinyemela kabisa, njia walizokuwa wakitumia Wacuba hasa wauza unga na kutulia jijini New York.
“Kesho mtaelekea katika Kituo cha Pennslyvania, hapo kuna treni itakuja, kuna mtu atawaletea tiketi na nyie kuondoka, popote mtakapokwenda mtajua kivyenuvyenu, cha msingi tumekwishawaleta Marekani, sasa kutafuta maisha ni juu yenu,” alisema Mustapha huku akiwaangalia.
“Tunashukuru sana!” waliitikia huku wakiwa na furaha.
“Kesho ndiyo mtakwenda. Jiandaeni!”
“Sawa.”