Miaka 5 ya CCM #Pambana Na Hali Yako

Zitto

Former MP Kigoma Urban
Mar 2, 2007
1,562
10,883
ACT Wazalendo na Bajeti za Serikali ya CCM Awamu ya Tano

1. Mwaka 2016 kukiwa na shamra shamra kubwa za Serikali mpya makisio ya Bajeti yaliongezwa kwa 31%, Chama chetu kilipofanya Uchambuzi wa Bajeti ya Kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano tulihitimisha kuwa #TumeanzaVibaya kwani ongezeko hili litakamua Watu na kuumiza Biashara hatimaye Maisha kuwa magumu.

2. Mwaka 2017 Maisha yakawa magumu sana, mzunguko wa Fedha ulishuka kwa sababu ya kasi ya ukuaji wa ‘money supply- M3 kushuka na Mikopo kwa Sekta binafsi kuanguka mpaka ukuaji hasi. Ulikuwa Mwaka wa #VyumaVimekaza kiasi hata sisi kama Chama hatukufanya Mkutano wa kuchambua Bajeti.

3. Mwaka 2018 tulifanya Ziara kwenye mikoa 16 nchini kutembelea Wananchi katika Kata ambazo ACT Wazalendo ilishinda viti vya Madiwani. Tulikuta hali mbaya sana ya Maisha kwani vipato vya wananchi vilikuwa vimeanguka kutoka na masoko ya bidhaa zao kuanguka, mbaazi, dengu, choroko na mazao yote ya mbogamboga. Mikopo kwa Sekta binafsi kutoka taasisi za Fedha iliendelea kuanguka, mabenki kufungwa ama kuunganishwa na biashara nyingi kufungwa. Tulikuwa #TunavunaTulichopanda

4. Mwaka 2019 tulitaraji kuwa Serikali ingefanya mabadiliko katika mfumo wa Bajeti kwani tayari mashirika ya Fedha ya kimataifa yalianza kuona hali mbaya ya Tanzania kiasi cha IMF kukadiria Uchumi kukua kwa 4% tu. Hata hivyo Serikali iliendelea na mambo yake #YaleYale

5. Mwaka 2020 tumevamiwa na Korona. Sekta ambayo ni Kuku anayetaga mayai ya dhahabu, Sekta ya Utalii, imeumia sana na watu zaidi ya laki 5 kupoteza ajira na Makampuni ya Kitalii kuwa kwenye Hatari ya kufilisika. Tulitaraji Bajeti ya Mwaka huu ingekuwa na Hatua mahususi za kuhami maisha ya watu na Uchumi Lakini imekuwa Bajeti inayohitimisha miaka 5 ya Utawala wa CCM, miaka ya #PambanaNaHaliYako

ACT WAZALENDO

UCHAMBUZI WA BAJETI YA SERIKALI 2020/2021

1.0 Utangulizi

Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano, chini ya Rais John Pombe Magufuli, imewasilisha Bungeni Bajeti yake ya Tano tangu iingie madarakani. Tulipofanya uchambuzi wa Bajeti ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano, Bajeti ya 2016/17, tulieleza kuwa “Bajeti inapaswa kutafsiri maono, malengo, shabaha na ahadi kadha wa kadha ambazo zimekuwa zikitolewa tangu wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015”. Bajeti Nne zimeshatekelezwa, na Bajeti hii ya Tano inatuwezesha kutazama miaka yote 5 ya Awamu ya Tano imekuwa ya namna gani, kama imeweza kutimiza ahadi zake kwa Wananchi na kama hali ya maisha ya Wananchi imekuwa bora au la. Katika uchambuzi wetu huu tunatazama kama Serikali, kupitia Bajeti yake ya Tano, inatekeleza shabaha zake, na kama inaweka rasilimali fedha kwenye vipaumbele vya Wananchi.

Mpaka sasa Serikali inaomba kuidhinishiwa na Bunge Bajeti ya Tano ya Shilingi 34.9 Trilioni, Jumla ya Shilingi Trilioni 126.8 zilikwisha idhinishwa na Bunge katika Bajeti Nne zilizopita.

- 2016/17 shilingi Trilioni 29.5
- 2017/18 shilingi Trilioni 31.7
- 2018/19 shilingi Trilioni 32.5
- 2019/20 shilingi Trilioni 33.1

Kwa Ujumla Bajeti zote Tano za Serikali ya Awamu ya Tano, baada ya hii ya mwaka 2020/2021 kupitishwa na Bunge zitakuwa ni Jumla ya Shilingi Trilioni 162. Je fedha hizi zinaendana na hali halisi ya Maendeleo ya Wananchi? Uchambuzi huu utajibu maswali hayo. Lakini pia tutazama kama Serikali iliweza kutekeleza Bajeti kama ilivyopitishwa na Bunge. Tutatumia Taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Benki Kuu kuonyesha kama Serikali ina uwezo wa kutekeleza Bajeti zake?

2.0 Serikali ya Awamu ya Tano haijawahi kutekeleza Bajeti kwa Ukamilifu

Kwenye Bajeti ya Serikali ya mwaka wa Fedha wa 2016/17 Serikali ilipanga kukusanya shilingi 29.5 trilioni, kwa mujibu wa ripoti ya CAG ya 2016/17, kati ya fedha hizo, Serikali ilikusanya shilingi 25.3 trilioni tu. Na hivyo, kutokufikia lengo la makusanyo kwa 14.33%.

Mwaka 2017/18, jumla ya shilingi 31.7 trilioni zilitarajiwa kukusanywa na zilipitishwa kutumika na Bunge. Serikali iliweza kukusanya kutoka vyanzo vyake vyote shilingi 27.7 trilioni tu. Hivyo kutofikia lengo la makusanyo kwa 12.66%.

Mwaka 2018/19 Jumla ya Shilingi Trilioni 32.5 zilitarajiwa kukusanywa. Lakini kwa mujibu wa Taarifa ya CAG, Serikali ilikusanya shilingi Trilioni 25.8 tu. Hivyo kutofikia lengo la makusanyo kwa 21%.

Mwaka 2019/20 Jumla ya Shilingi Trilioni 33.1 zilitarajiwa kukusanywa. Lakini kwa mujibu wa Taarifa ya Waziri wa Fedha, mpaka Mwezi Aprili, Makusanyo yamefikia shilingi Trilioni 24.85 tu, ikiwa imebakia miezi 2 kabla ya mwaka wa Fedha kuisha. Mpaka Aprili 2020, lengo halijafikiwa kwa 25%.

Makusanyo ya Mapato yote ya Serikali katika mwaka 2018/19 yalikuwa madogo kuliko Bajeti ya mwaka uliotangulia wa 2017/18 kwa Shilingi Trilioni 1.9, yaani chini ya 7% ya Bajeti ya Pili ya Serikali ya Awamu ya Tano. Kwa miaka 3 ya mwanzo ya Serikali ya Awamu ya Tano wastani wa lengo lisilofikiwa ni 16%.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Mwaka ya Benki Kuu ya Tanzania na Kamati ya Bunge ya Bajeti, licha ya Makadiro na Makusanyo halisi tuliyotaja hapo juu, utekelezaji wa Bajeti ya Tanzania chini ya Serikali ya Awamu Tano ni chini ya Asilimia 70.

• Mwaka 2016/17 Bajeti ilitekelezwa kwa 66.5% tu
• Mwaka 2017/18 Bajeti ilitekelezwa kwa 64.5% tu
• Mwaka 2018/19 Bajeti ilitekelezwa kwa 68.6% tu
• Mwaka 2019/2020 Bajeti imetekelezwa kwa 62% tu (mpaka Mwezi Aprili 2020 )

Tunavuna Tulichokipanda?

Uchambuzi wetu unaonyesha kuwa katika mwaka 2016/17 Serikali ilijiwekea lengo kubwa zaidi la Makisio ya Bajeti kuliko uhalisia wa Uchumi wa Nchi yetu. Wakati mwaka 2016/17 Serikali ilikuza makisio kwa 31%, kulinganisha na wastani wa ukuzaji wa Makisio ya Bajeti wa 11% katika miaka miwili ya nyuma. Hivyo sababu ya Serikali kushindwa kufikia malengo ni kuweka makisio makubwa mno bila ushahidi wa takwimu za kutosha kuhusu hali ya uchumi wa nchi. Jambo hili lilisababisha ukamuaji mkubwa wa kodi kwa wafanyabishara, ukamuaji uliosababisha biashara nyingi kufungwa, na ukaleta athari kubwa kwenye uchumi wetu katika mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Licha ya Serikali kutambua makosa yake ya kuweka makisio makubwa mno ya Bajeti yake ya kwanza, kwa kuanza kushusha kasi ya kupandisha makisio kutoka 31% mpaka 7% mwaka 2017/18, na 2% mwaka 2018/19, 2% tena 2019/2020 na 4% 2020/2021 tayari uchumi umeshaharibiwa kwa shughuli za uzalishaji kushuka na hivyo malengo ya makusanyo kuporomoka zaidi kuliko mwaka uliopita.

Katika uchambuzi huu wa Bajeti tunaonyesha kuwa miaka 5 ya Utawala wa CCM imeshindwa kutumia rasilimali Fedha za Nchi kuchochea maendeleo ya Wananchi.

2. Hali ya Uchumi wa Taifa

Eneo hili tutachambua kwa ufupi Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha Bungeni tarehe 11 Juni 2020. Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mwaka 2019 inaonyesha kuwa Pato la Taifa (GDP) limekua kwa 7% kama ilivyokuwa kwa mwaka 2018. Hivyo ukuaji wa uchumi haukuongezeka badi ulibaki pale pale katika viwango vya mwaka uliopita. Kama kawaida kuna mambo muhimu sana ya kuzingatia tunaposoma takwimu za uchumi. Huwa tunarudia mambo haya mara kwa mara na leo tutarudia machache.

1. Sekta zilizoongoza kwa ukuaji uchumi zina mchango mdogo sana kwenye Pato la Taifa.

Shughuli za uchumi zilizoongoza kwa ukuaji ni uchimbaji wa madini na mawe, Ujenzi, Sanaa na Burudani, Usafirishaji na Uhifadhi wa Mizigo (Uchukuzi) na Mawasiliano. Shughuli zote hizi za uchumi zinachangia kidogo kwenye uchumi mzima wa Taifa na hivyo kutokuwa na maana sana katika kukuza uchumi wa wananchi kwani hazina fungamanisho kubwa na uzalishaji wa ajira. Jedwali lifuatalo linaonyesha kwa uwazi juu ya jambo hili:

2. Wakati huohuo, sekta zenye mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa zinakua kwa kiwango kidogo.

Shughuli za uchumi zilizo na mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa zinakua kwa kasi ndogo. Mfano mzuri wa shughuli hizo ni Kilimo na Viwanda. Shughuli zote hizi za uchumi zinachangia sehemu kubwa sana kwenye uchumi mzima wa Taifa, na zinaajiri watu wengi zaidi nchini. Hivyo, kutokukua kwake kwa kiwango kikubwa kunamaanisha kuwa Watanzania wengi hawafaidiki na kasi ya ukuaji wa Uchumi.

Kwa maana hii kasi ya ukuaji wa uchumi hauna maana yeyote kwa wananchi iwapo sekta zinazozalisha ajira nyingi hazikui kwa viwango vikubwa vinavyotakiwa. Ni muhimu kuweka msisitizo kuwa Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano ilifanya kampeni ya uchaguzi wa mwaka 2015 kwa kigezo cha kuwa na Uchumi wa Viwanda lakini takwimu za Serikali yenyewe zinaonyesha kuwa, nanukuu “Mwaka 2019, kasi ya ukuaji wa shughuli za Uzalishaji bidhaa viwandani ilikua asilimia 5.8 ikilinganishwa na asilimia 8.3 mwaka 2018”. Ikumbukwe kuwa Mpango wa Maendeleo wa Pili wa Maendeleo ya Taifa uliweka lengo la sekta ya Viwanda kukua kwa Wastani wa 10% katika ya Mwaka 2016-2021 lengo ambalo halijafikiwa hata katika mwaka mmoja ya Muhula huu wa utawala wa CCM wa miaka 5.

Vile vile, Takwimu za Serikali zimeonyesha kuwa sekta ya viwanda imekuwa ni mwiba sio tu kwenye uzalishaji bali pia kwenye Biashara ya Nje. Kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa, mchango wa sekta ya Viwanda katika mauzo Nje ulipaswa kuongezeka kutoka 24% mwaka 2015 mpaka 30% mwaka 2021. Serikali imeliambia Bunge, nanukuu Thamani ya Mauzo ya Bidhaa za Viwandani ilipungua kwa asimilia 10 na kufikia dola za Marekani 805 mwaka 2019 kutoka dola za Marekani 894.3 mwaka 2018. Bidhaa za Viwanda zilichangia 9% tu ya Mauzo yote Nje na 19.3% ya mapato yote ya bidhaa zisizo asilia mwaka 2019. Msisitizo ni kuwa Wakati Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano inaingia madarakani mwaka 2015 Tanzania iliuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 1.3, hivyo CCM wameporomosha hata kidogo tulichokuwa tunauza Nje.

3. Hasara ya Sakata la Korosho la 2018 imedhihirika

Mwaka 2018 Tanzania iliingia kwenye sakata kubwa la Zao la Korosho ambapo Serikali iliamua kuingilia Soko la Zao hilo, kuchukua mazao ya Wakulima kwa kutumia Jeshi la Wananchi na Wakulima kutolipwa kwa muda mrefu sana. Taarifa ya Serikali ya Mwaka 2019 ilionyesha kuwa Wananchi wa Mikoa inayozalisha Korosho Nchini walivuna Korosho Tani 313,826 na Serikali iliweza kuuza Nje Tani 120,200 za Korosho mwaka huo. Serikali haijawahi kutoa maelezo ya Tani za Korosho ambazo hazikuuzwa nje ya Nchi.

Katika Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Taifa ya Mwaka 2019 Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano imelieleza Bunge kama ifuatavyo, nanukuu “Mwaka 2019, thamani ya mauzo ya Korosho nje iliongezeka na kufikia dola za Marekani milioni 353.1 ikilinganishwa na dola milioni 109.6 mwaka 2018. Hii ilitokana na kuongezeka kwa kiasi cha Korosho kilichouzwa nje kutoka Tani 70,100 mwaka 2018 hadi Tani 295,600 mwaka 2019”. Serikali inapaswa kutoa maelezo kwa Umma ZIPO WAPI TANI 50,100 za Korosho? Serikali pia inapaswa kuwaeleza Wananchi ilifanya nini na Tani 243,000 ambazo hazina maelezo?

Kwa bei za Korosho za Mwaka 2018 Serikali ya CCM Serikali ya imeliingizia Taifa hasara ya Dola za Marekani Milioni 357 sawa na pesa za kitanzania??? kama Mapato ya Fedha za Kigeni ambayo yalipotea kutokana na Serikali kuvuruga soko la Zao la Korosho. Vile vile Nyaraka za Serikali zinaonyesha kuwa Benki ya Kilimo iliwalipa Wakulima Zaidi ya Shilingi Bilioni 600, Fedha ambazo Benki ingezirejesha baada ya Mauzo ya Korosho, lakini Mauzo ya Korosho Nje yaliyofanywa na Serikali kwa mujibu wa Taarifa iliyosomwa Bungeni na Waziri wa Fedha ni Shilingi Bilioni 240 tu kutoka Tani 70,000 zilizouzwa. Benki ya Kilimo itarejesha vipi Mkopo iliyochukua Benki Kuu kwa ajili ya malipo ya Korosho? Hasara ya Shilingi Bilioni 821 (USD 357M) inabebwa na nani? Nani analipa hasara hii kwa Nchi? Nani analipa Fedha za Benki ya Kilimo ilizokopa ili kulipia Korosho? Amri ya kupeleka Jeshi kubeba Korosho ya Wananchi ilitolewa na Mwenyekiti wa CCM, atabeba gharama hizi? Kuna Taarifa za Wastaafu kuhangaishwa mafao yao kwa miaka 2, Fedha hizi ambazo Benki ya Kilimo ilitumia kulipa Wakulima zilichotwa Benki Kuu kutoka akaunti za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii?

3.0 Ukuaji wa Uchumi unaoendeshwa Deni (debt driven growth)

Takwimu za kasi ya ukuaji wa Uchumi zinaonyesha kuwa msukumo wa kiwango cha kukua kwa uchumi wa Tanzania kinatokana na sekta ambazo Serikali imekuwa ikiwekeza kwa nguvu katika miaka 5 iliyopita. Sekta hizo ni Ujenzi, Umeme na Uchukuzi ambazo zimebeba sehemu kubwa ya Bajeti za Serikali tangu Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano iingie Madarakani. Miradi inayotekelezwa katika sekta hizo ni Pamoja na Kufufua Shirika la Ndege ambalo bado linategemea ruzuku ya Serikali kujiendesha, Ujenzi wa Reli ya Kati ambayo haijaanza kuzalisha Mapato kwani mradi bado haujakamilika, Ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere ambalo pia bado halijakamilika na hivyo halizalishi Mapato na Ujenzi wa madaraja, flyovers jijini Dar es Salaam na maeneo mengine ya Nchi. Miradi mingi katika hii inaendeshwa kwa kutumia Mikopo ya kibiashara kutoka mabenki ya Nje. Kwa sababu hiyo Deni la Taifa limeongezeka kwa kasi sana.

Mathalani, Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia Madarakani mwaka 2005, Deni la Nje lilikuwa Dola za Marekani Bilioni 8 na ilipoondoka miaka 10 baadaye Deni hilo lilikuwa limefikia Dola za Marekani Bilioni 15. Hii ni sawa na ongezeko la Deni la Nje la Dola za Marekani Bilioni 7 sawa na ongezeko la 47%.

Hata hivyo, mpaka kufikia Mwezi Machi mwaka 2020 Deni la Nje limefikia Dola za Marekani Bilioni 22.4 sawa na ongezeko la Dola za Marekani Bilioni 7.4 katika kipindi cha miaka 5. Yaani Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano imekopa zaidi ya mikopo yote ambayo Serikali ya CCM Awamu ya Nne ilichukua katika miaka 10 ya uongozi wake.

Madhara makubwa ya ukopaji huu holela ni gharama za kulipa Madeni kuongezeka kama tunavyoona sasa kwenye Mapendekezo ya Bajeti ya Mwaka 2020/21. Gharama za kulipa Madeni zimeongezeka kwa 8% katika ya mwaka 2019/20 – 2020/21 wakati ongezeko la Mapato ya Ndani ya Serikali ni 6% tu. Iwapo miradi ambayo inasababisha Nchi kukopa haitaweza kuzalisha Mapato ya kugharamia malipo ya Madeni, Tanzania inakwenda kugonga ukuta kwa kuondoa Fedha kwenye Huduma muhimu kama Elim una Afya na kuzielekeza kulipa madeni. Katika Bajeti ya mwaka huu Bajeti ya kulipa Deni ni 47% ya Mapato yote ya ndani ya Serikali.

4.0 Bajeti ya Tano ya Serikali 2020/2021

Katika mwaka wa fedha 2020/21, Serikali imependekeza kutumia jumla ya shilingi Trilioni 34.8 ambapo kati ya hizo shilingi trilioni 13 ni za matumizi ya maendeleo sawa na 37% ya Bajeti yote.

Katika Bajeti yote ya mwaka 2020/21, jumla ya shilingi Trilioni 18.3 itatumika kuhudumia Deni la Serikali ( Shs 10.5Tr ) na kulipia mishahara ya Wafanyakazi wa Umma ( Shs 7.8Tr ). Katika Makusanyo yote ya ndani ambayo Serikali itakusanya ambayo ni shilingi Trilioni 23.3 ( Makusanyo ya Kodi na yasiyo ya kikodi ), 79% itatumika kulipa Deni la Taifa na Mishahara. Ni 21% tu ya Makusanyo ya Ndani sawa na shilingi trilioni 5 itakayobakia kwa ajili ya kugharamia matumizi mengineyo ya Serikali (Shs 3.8Tr) na Matumizi ya Maendeleo (Shs 13Tr).

Hivyo Serikali itapaswa kukopa ndani na nje ya nchi ili kutekeleza miradi ya Maendeleo. Ukilinganisha Bajeti ya mwaka 2019/20 na 2020/21 utaona kuwa kasi ya ukuaji wa gharama za kuhudumia Deni la Taifa inaongezeka kwa 8% ilhali kasi ya ukuaji wa Mapato ya Serikali inaongezeka kwa 5.4% tu. Hii ni ishara kuwa madeni ambayo Serikali inayachukua katika kipindi cha miaka 5 iliyopita hayazalishi mapato ya kutosha kuweza kugharamia malipo ya riba na mitaji ya madeni hayo.

Mwaka 2020/2021 Serikali itakopa kutoka Nje jumla ya shilingi Trilioni 2.7 sawa naongezeko la 9% kutoka mikopo ya mwaka uliopita.

Sera ya Mapato: Bajeti ya ‘Hali ya Kawaida’

Katika bajeti ya mwaka 2020/2021, Serikali imependekeza kufanya marekebisho kadhaa kwenye Kodi mbalimbali ili kuweza kufikia malengo ya makusanyo ya kodi. Katika mazingira ya sasa ya Dunia na janga la COVID 19 tulitegemea kuwa Serikali ingependekeza Sera za kikodi ili kuokoa sekta za uchumi ambazo tayari zimeathiriwa na janga la Korona. Kiufupi Bajeti ya Mwaka huu ni Bajeti ya ‘Hali ya Kawaida’.

Sekta ya Utalii imeathiriwa sana na janga la COVID 19 kwa mujibu wa Taarifa kutoka kwa wadau wa Utalii nchini. Hii ni Sekta ambayo inaajiri Watanzania 1.5 milioni na kuchangia 6% ya Pato la Taifa. Hii ni Sekta ambayo mwaka 2019 iliingiza fedha za kigeni Dola za Marekani 2.6 Bilioni, Zaidi ya fedha zilizoingizwa na Dhahabu. Mchango wa Utalii katika Mapato ya Fedha za kigeni ni 27% ya Fedha zote za kigeni ambazo Tanzania ilipata mwaka 2019. Sekta hii ni Kuku anayetaga Yai la dhahabu, lakini Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano haijapendekeza hata hatua moja ya kuilinda dhidi ya janga la Korona. Msimu wa Utalii ambao unaanza sasa tayari umeonyesha kuwa Tanzania haitapata Watalii hata robo ya Watalii wa mwaka 2019. Ajira Zaidi ya milioni moja zitapotea na Serikali kupoteza mapato ya Kodi.

Bajeti ya Mwaka huu ilipaswa kuwa Bajeti ya kuuhami Uchumi. Serikali imepoteza fursa hiyo, madhara yake yatakuwa makubwa sana.

Miaka 5 Migumu sana kwa Wafanyakazi wa Tanzania

Ajira
Serikali imefanya marekebisho kidogo katika mfumo wa kodi za waajiri na wafanyakazi katika Bajeti ya mwaka 2020/21. Marekebisho hayo hayakidhi haja kwani ni kidogo sana na ACT Wazalendo tutapendekeza kiwango kinachopaswa kuwa kutozwa kama Kodi ya Wafanyakazi (PAYE) katika viwango mbalimbali. Hata hivyo, huu ni mwaka wa Tano sasa, Serikali ikishindwa kupandisha mishahara ya wafanyakazi nchini. Bajeti ya mishahara imeongezeka kwa 2.7% mwaka 2020/21 hadi kufikia Shilingi Trilioni 7.8 kutoka shilingi trilioni 7.5 mwaka 2019/20.

Missing points

ACT WAZALENDO TUTAFANYA NINI TUKISHIKA MADARAKA MWAKA 2020?

Bajeti ndogo Mwezi Januari 2021

Huu ni mwaka wa Uchaguzi na hivyo hakuna ushauri ambao tutautoa Serikali ya CCM itausikiliza. Huu ni wakati wa kuwaeleza Wananchi Bajeti yetu itakuwaje baada ya uchaguzi iwapo tutapewa ridhaa ya kuwaongoza Wananchi kwa kuunda Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni dhahiri kuwa baada ya Uchaguzi tutarithi Bajeti ya Serikali ya CCM na lazima tuheshimu mikataba yote ambayo Serikali itakuwa imeingia ikiwemo kuendelea na Baadhi ya Miradi Serikali inatekeleza. Hata hivyo tutafanya marekebisho makubwa ili kutekeleza Miradi ambayo tayari Serikali imeweka Fedha kwa namna ambayo Serikali itashirikisha sekta binafsi na kuchochea uwekezaji binafsi badala ya ushiriki wa Serikali wa asimilia 100. Lengo ni kuhakikisha kuwa tunaokoa Fedha ambazo Serikali imekusanya ili kuzielekeza kwenye huduma muhimu za kijamii na kuhami uchumi dhidi ya madhara ya janga la COVID 19.

Serikali mpya ambayo ACT Wazalendo itakuwa sehemu vyama vitakavyoiunda itafanya Mkutano Maalumu wa Bunge Mwezi Januari mwaka 2021 ambapo Waziri wa Fedha atawasilisha Bungeni Bajeti mpya na kuifuta Bajeti hii ya sasa kwa mujibu wa Sheria. Bajeti hiyo itazingatia mambo makubwa yafuatayo

1. Uchambuzi wa kina kwa kutumia wataalamu wa ndani na wa nje kuhusu namna bora ya kutekeleza Miradi mikubwa kama Reli, Ndege na Umeme kwa ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma kwa kuzingatia muda wa miradi kuanza kuzalisha mapato ya kulipia madeni ya ununuzi/ujenzi wake. Lengo la uchambuzi huu ni kuiondoa Serikali kwenye angalau 50% ya gharama za utekelezaji ili kuelekeza rasilimali Fedha kuhami maisha ya Wananchi.

2. Kutunga será za kikodi ili kuhami sekta ya Utalii na mnyororo wake ambao umeathirika sana na janga la Covid 19. Hii ni pamoja na kulinda Ajira za Wafanyakazi wa Makampuni ya Utalii kwa kutoa ruzuku kwa kampuni zote zitakazoendeleza mikataba na Waajiri na kuruhusu Wafanyakazi waliokosa kazi kulipwa Fao la kukosa Kazi kutoka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii

3. Kuweka vivutio vya kibajeti na kikodi kwenye Miradi yote ya Kilimo cha Umwagiliaji na Viwanda vyote vya kuongeza thamani ya mazao ya Kilimo

4. Kurekebisha Muundo mzima wa Makato kutoka kwenye Mapato ya Waajiri na Wafanyakazi ili kuchochea matumizi kwenye uchumi. Hii ni pamoja na kutambua rasmi kibajeti malimbikizo ya kupanda mishahara kwa Wafanyakazi wa Umma tangu mwaka 2016 na kuweka utaratibu wa kulipa malimbikizo hayo kwa Wafanyakazi wote ikiwemo wale waliostaafu ambao mafao yao yataboreshwa kwa kuzingatia marekebisho ya Mishahara yao.

5. Kuweka mazingira bora ya Mradi muhimu na wa lazima wa Mchuchuma la Liganga kuanza mara moja.

Kwa Upande wa Ajira tunatazamia kuwa:

▪ Serikali itapunguza Kiwango cha Kodi ya Uendelezaji Ujuzi (SDL) mpaka 2% tu. Jambo hilo litawapunguzia gharama za kuajiri waajiri nchini, na litasaidia kupanua wigo wa ajira.

▪ Michango kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii itapunguzwa mpaka 12% kutoka 20% za sasa. Jambo hili litasaidia kushusha gharama za michango kwa waajiri wa sekta binafsi na Serikali kutoka 10% na 15% ya sasa, mpaka 7% tu. Lakini pia itawapunguzia wafanyakazi wa sekta binafsi makato ya 10% ya sasa mpaka 5%, na hivyo kuongeza Kiwango cha Fedha wanachopokea kama mishahara.

▪ Mapendekezo mahususi ya kodi ya mapato (PAYE) ni kama yanavyoonekana katika jedwali hapa chini.

Kwa upande wa Sekta ya Viwanda tunatazamia kuwa
• Serikali italipa malimbikizo ya Marejesho ya Kodi ya VAT kwa wenye viwanda na kwa waagizaji wa Sukari ya Viwandani na kuweka mfumo ambao hapatakuwa na malimbizo tena. Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu itatoa Dhamana ya Serikali (Government Bond) yenye thamani ya marejesho yote na hivyo Benki Kuu kuwalipa wenye Viwanda kwa Mkupuo au wenye Viwanda kuweza ku cash Fedha zao kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Kwa upande wa Sekta ya Kilimo tunatazamia kuwa

• Serikali itarekebisha Bajeti ili kuongeza uwekezaji wa Fedha kwenye Kilimo. Bajeti Mpya itakayoletwa inapaswa kufikia kiwango cha ‘Azimio la Malabo la Umoja wa Afrika’ - linaloelekeza nchi za Afrika kutenga 10% ya Bajeti ya Taifa kwenye Kilimo.

• Serikali itatunga na kusimamia mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka katika sekta ya kilimo (stable fiscal regime for agricultural sector). Mazao yanayotumia gharama za Fedha za kigeni kuyaagiza kutoka nje hasa Sukari na Mafuta ya kula yatapewa kipaumbele cha kipekee, kwa kuweka Fedha za kutosha kwenye MPANGO maalum wa Kilimo cha Miwa, Michikichi na Alizeti, na kufungamanisha mpango huo na ujenzi wa viwanda vya sukari na mafuta ya kula. Serikali itaanza kulipa ruzuku ya gharama za uzalishaji kwa Viwanda vinavyozalisha Bidhaa hizo.

• Serikali itaanzisha Skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima. Skimu hiyo itaweka utaratibu wa kuwapo kwa Fao la Bei ya Mazao (Price Stabilization) na Bima ya Mazao na Mifugo ili kufidia Wakulima pale bei inapoporomoka chini ya gharama za uzalishaji wao. Skimu itahusisha Wavuvi na Wafugaji. Pia Skimu itahusika na utoaji mikopo ya gharama nafuu kwa vikundi vya wakulima au Vyama vya Msingi vya Ushirika ili kununua pembejeo za kilimo na ufugaji, pamoja na kuwa na viwanda vidogo vya usindikaji wa mazao. Serikali itachangia nusu ya Michango ya Wanachama wa Skimu kutoka katika Bajeti ya Serikali.

• Itawekwa tozo ya shilingi 60 kwa kila lita ya Mafuta ya Petroli, Petroli na Mafuta ya Taa ili kugharamia Miradi ya Maendeleo ya Tume ya Umwagliaji nchini kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa Mazao ya Kilimo na ufugaji wa Samaki. Pia miradi mingi ya Umwagiliaji itaendana na miradi ya kufua Umeme wa Maji. Shilingi bilioni 190 zitakusanywa kila mwaka kulingana na matumizi ya sasa ya mafuta. Kwa sasa Tume ya Umwagiliaji ya Taifa imetengewa shilingI bilioni 29 tu.

Kwa upande wa Maji tunatazamia kuwa
• Bajeti ya Miradi ya kusambaza Maji safi na salama kwa Wananchi itaongezwa kwa ongezeko la shilingi 140 ya Ushuru wa Bidhaa Mafuta ya Petroli na Dizeli. Ongezeko hili litaongeza Shilingi Bilioni 486 kwenye Bajeti ya Miradi ya Maji. Fedha yote itapelekwa kwenye Mfuko wa Maji na Wataalamu wa Uchumi watatengeneza mpango wa kukopa mikopo nafuu ya Muda mrefu kwa kutumia Mfuko wa Maji ili kutekeleza miradi endelevu ya kuongeza upelekaji na usambazaji wa maji kwa wananchi, hasa vijijini kwa wakati mmoja nchi nzima. Matumizi ya Nishati jadidifu kama Umeme wa Jua, Umeme wa Upepo na Umeme wa Mfumo wa Maji yenyewe yanayosambazwa yatatiliwa mkazo ili kupunguza gharama za uendeshaji wa miradi ya Maji kwa Wananchi. Ushirika wa Wananchi wa uendeshaji wa miradi wa Maji (Water Users Cooperatives) utapewa kipaumbele na motisha. Lengo ni kumilikisha Maji kwa Wananchi wenyewe.

Kwa Upande wa Elimu tunatazamia kuwa
• Itakuwa imeundwa Tume ya Elimu ili kutazama mfumo Mzima wa Elimu Tanzania kwa kuzingatia kasi kubwa ya ongezeko wa Watu nchini na ujuzi na maarifa wanaotakiwa kuwa nayo kizazi kipya nchini katika kukabiliana na changamoto za maisha ya Dunia inayokuja. Ikumbukwe kuwa Tanzania hivi sasa ina Watoto wanafunzi katika shule za Msingi na Sekondari wapatao Milioni 13 na Idadi hii itaongezeka mpaka Wanafunzi wa Shule za Msingi milioni 15 mwaka 2025. Hii ina Maana Taifa linahitaji vyumba vya madarasa, kuajiri walimu wapya kwa maelfu, viwanja vya michezo, vifaa na walimu wa michezo kwa mamia na uzalishaji wa Vitabu zaidi ya milioni 80. Sio tu tunahitaji Bajeti zaidi kwenye Elimu, bali fikra tofauti kabisa kukabili changamoto hii kubwa ya idade ya Watu.

Tutahitaji Ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi vyenye uwezo wa kuchukua Wanafunzi zaidi ya 5,000 kila kimoja, vyenye vifaa vya kisasa na Wakufunzi katika kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini. Kundi la Wanafunzi milioni 10 walio kwenye Shule za Msingi hivi sasa, na Watoto watakaonza shule kuanzia Januari 2021 lazima wawe Watanzania tofauti kabisa kiujuzi, maarifa na uwezo wa kuikabili Dunia watakapoingia kwenye nguvu kazi ya Taifa baada ya kumaliza masomo yao. Serikali ya ACT Wazalendo haitatumia Fedha za Ndani kuendesha miradi ya Biashara kama vile kununua ndege na kutafuta mikopo kusomesha Watoto wetu. Tutatumia Fedha za Kodi kugharamia Elimu ya Watoto wetu na Fedha za mikopo na sekta binafsi zitatumika kutekeleza miradi ya biashara.
 
Ni uchambuzi mzuri, nadhani watu hawa wapo vizuri kichwani, mwenye hoja kinzani ni bora naye atuwekee uchambuzi wake utakaosheheni mifano na vielelezo kama huu.
 
Ningependekeza wanafunzi waanze kufundishwa IT kuanzia shule ya msingi. Shule ipate computer hata tano, iwe na WiFi, kuwe na mwalimu mwenye taaluma hiyo.

Dunia ya sasa ni kidigital mtoto anamaliza darasa la saba hajui hata kujaza fomu kwa kidigital.
 
Serikali IPI....? Tuongee uhalisia. Laiti kama tungekuwa na uwezekano wa chama kinachotawala kuteuwa P. M kutoka chama chochote hiyo ingekuwa sawa ila kwa mfumo wetu Zitto atabaki kuwa P.M wetu huku mtaani tuu inatosha
Naona corona imevuruga system ya utendaji kazi kwenye halmashauri ya kichwa chako
 
Bia Yetu hajapita huku? Magonjwa Mtambuka je? Mudawote? Stroke? Wadadavuwa? Johnbaptist? Kazi kweli kweli kwa mataahira wa Lumumba
 
Hongera Zitto kwa uchambuni makini. Lakini ccm sawa na mbuzi haizoeleki. Unaweza kuona walivyowanyanyasa wafanyakazi kwa kutowaoengezea mishahara
 
Serikali itapunguza Kiwango cha Kodi ya Uendelezaji Ujuzi (SDL) mpaka 2% tu. Jambo hilo litawapunguzia gharama za kuajiri waajiri nchini, na litasaidia kupanua wigo wa ajira.

Michango kwenye mifuko ya Hifadhi ya Jamii itapunguzwa mpaka 12% kutoka 20% za sasa. Jambo hili litasaidia kushusha gharama za michango kwa waajiri wa sekta binafsi na Serikali kutoka 10% na 15% ya sasa, mpaka 7% tu. Lakini pia itawapunguzia wafanyakazi wa sekta binafsi makato ya 10% ya sasa mpaka 5%, na hivyo kuongeza Kiwango cha Fedha wanachopokea kama mishahara.

Mapendekezo mahususi ya kodi ya mapato (PAYE) ni kama yanavyoonekana katika jedwali hapa chini.

Kwa upande wa Sekta ya Viwanda tunatazamia kuwa
• Serikali italipa malimbikizo ya Marejesho ya Kodi ya VAT kwa wenye viwanda na kwa waagizaji wa Sukari ya Viwandani na kuweka mfumo ambao hapatakuwa na malimbizo tena. Serikali kwa kushirikiana na Benki Kuu itatoa Dhamana ya Serikali (Government Bond) yenye thamani ya marejesho yote na hivyo Benki Kuu kuwalipa wenye Viwanda kwa Mkupuo au wenye Viwanda kuweza ku cash Fedha zao kupitia Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Kwa upande wa Sekta ya Kilimo tunatazamia kuwa

• Serikali itarekebisha Bajeti ili kuongeza uwekezaji wa Fedha kwenye Kilimo. Bajeti Mpya itakayoletwa inapaswa kufikia kiwango cha ‘Azimio la Malabo la Umoja wa Afrika’ - linaloelekeza nchi za Afrika kutenga 10% ya Bajeti ya Taifa kwenye Kilimo.

• Serikali itatunga na kusimamia mfumo wa kodi unaoeleweka na usiotetereka katika sekta ya kilimo (stable fiscal regime for agricultural sector). Mazao yanayotumia gharama za Fedha za kigeni kuyaagiza kutoka nje hasa Sukari na Mafuta ya kula yatapewa kipaumbele cha kipekee, kwa kuweka Fedha za kutosha kwenye MPANGO maalum wa Kilimo cha Miwa, Michikichi na Alizeti, na kufungamanisha mpango huo na ujenzi wa viwanda vya sukari na mafuta ya kula. Serikali itaanza kulipa ruzuku ya gharama za uzalishaji kwa Viwanda vinavyozalisha Bidhaa hizo.

• Serikali itaanzisha Skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa Wakulima. Skimu hiyo itaweka utaratibu wa kuwapo kwa Fao la Bei ya Mazao (Price Stabilization) na Bima ya Mazao na Mifugo ili kufidia Wakulima pale bei inapoporomoka chini ya gharama za uzalishaji wao. Skimu itahusisha Wavuvi na Wafugaji. Pia Skimu itahusika na utoaji mikopo ya gharama nafuu kwa vikundi vya wakulima au Vyama vya Msingi vya Ushirika ili kununua pembejeo za kilimo na ufugaji, pamoja na kuwa na viwanda vidogo vya usindikaji wa mazao. Serikali itachangia nusu ya Michango ya Wanachama wa Skimu kutoka katika Bajeti ya Serikali.

• Itawekwa tozo ya shilingi 60 kwa kila lita ya Mafuta ya Petroli, Petroli na Mafuta ya Taa ili kugharamia Miradi ya Maendeleo ya Tume ya Umwagliaji nchini kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa Mazao ya Kilimo na ufugaji wa Samaki. Pia miradi mingi ya Umwagiliaji itaendana na miradi ya kufua Umeme wa Maji. Shilingi bilioni 190 zitakusanywa kila mwaka kulingana na matumizi ya sasa ya mafuta. Kwa sasa Tume ya Umwagiliaji ya Taifa imetengewa shilingI bilioni 29 tu.

Kwa upande wa Maji tunatazamia kuwa
• Bajeti ya Miradi ya kusambaza Maji safi na salama kwa Wananchi itaongezwa kwa ongezeko la shilingi 140 ya Ushuru wa Bidhaa Mafuta ya Petroli na Dizeli. Ongezeko hili litaongeza Shilingi Bilioni 486 kwenye Bajeti ya Miradi ya Maji. Fedha yote itapelekwa kwenye Mfuko wa Maji na Wataalamu wa Uchumi watatengeneza mpango wa kukopa mikopo nafuu ya Muda mrefu kwa kutumia Mfuko wa Maji ili kutekeleza miradi endelevu ya kuongeza upelekaji na usambazaji wa maji kwa wananchi, hasa vijijini kwa wakati mmoja nchi nzima. Matumizi ya Nishati jadidifu kama Umeme wa Jua, Umeme wa Upepo na Umeme wa Mfumo wa Maji yenyewe yanayosambazwa yatatiliwa mkazo ili kupunguza gharama za uendeshaji wa miradi ya Maji kwa Wananchi. Ushirika wa Wananchi wa uendeshaji wa miradi wa Maji (Water Users Cooperatives) utapewa kipaumbele na motisha. Lengo ni kumilikisha Maji kwa Wananchi wenyewe.

Kwa Upande wa Elimu tunatazamia kuwa
• Itakuwa imeundwa Tume ya Elimu ili kutazama mfumo Mzima wa Elimu Tanzania kwa kuzingatia kasi kubwa ya ongezeko wa Watu nchini na ujuzi na maarifa wanaotakiwa kuwa nayo kizazi kipya nchini katika kukabiliana na changamoto za maisha ya Dunia inayokuja. Ikumbukwe kuwa Tanzania hivi sasa ina Watoto wanafunzi katika shule za Msingi na Sekondari wapatao Milioni 13 na Idadi hii itaongezeka mpaka Wanafunzi wa Shule za Msingi milioni 15 mwaka 2025. Hii ina Maana Taifa linahitaji vyumba vya madarasa, kuajiri walimu wapya kwa maelfu, viwanja vya michezo, vifaa na walimu wa michezo kwa mamia na uzalishaji wa Vitabu zaidi ya milioni 80. Sio tu tunahitaji Bajeti zaidi kwenye Elimu, bali fikra tofauti kabisa kukabili changamoto hii kubwa ya idade ya Watu.

Tutahitaji Ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi vyenye uwezo wa kuchukua Wanafunzi zaidi ya 5,000 kila kimoja, vyenye vifaa vya kisasa na Wakufunzi katika kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa nchini. Kundi la Wanafunzi milioni 10 walio kwenye Shule za Msingi hivi sasa, na Watoto watakaonza shule kuanzia Januari 2021 lazima wawe Watanzania tofauti kabisa kiujuzi, maarifa na uwezo wa kuikabili Dunia watakapoingia kwenye nguvu kazi ya Taifa baada ya kumaliza masomo yao. Serikali ya ACT Wazalendo haitatumia Fedha za Ndani kuendesha miradi ya Biashara kama vile kununua ndege na kutafuta mikopo kusomesha Watoto wetu. Tutatumia Fedha za Kodi kugharamia Elimu ya Watoto wetu na Fedha za mikopo na sekta binafsi zitatumika kutekeleza miradi ya biashara.
Hongera Zitto kwa uchambuzi mzuri wa bajeti.

Serikali ya awamu ya tano kipaumbele chake ni kupambana na wapinzani siyo matatizo yanayowakabili wananchi.

Hivyo kinachoiumiza ccm ni uwepo wa upinzani nchini na siyo matatizo yanayowakabili wananchi wake. Hivyo hatuwezi kutegemea jipya kutoka serikali ambayo kipaumbele chake ni SADISM dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa.

Umeongea vizuri sana kuhusu zao la korosho ambalo serikali imeamua kuliua kwa mikono yake yenyewe. Hii hali inanikumbusha jinsi gani serikali hii hii ya awamu ya tano ilivyoua zao la tumbaku ambalo lilikuwa likiingiza pesa nyingi sana za kigeni na kuboresha maisha ya wakulima.

Serikali ya ccm haina jipya tena la kuweza kuondoa umaskini nchini zaidi ya kuongeza mafukara tu.

Kibaya zaidi ccm hawataki tena kuondoka madarakani kwa sanduku la kura njia pekee ni kuiondoa hata kwa makofi.

Muda hautusubiri tuendelee kupambana.

Sent from my SM-A105F using JamiiForums mobile app
 
Kwanini usiweke na pdf attachment, a long post in JF in one go is not an easy read for everyone.

Kwa wengine ni bora wachukue pdf wasome taratibu kwa kutafakari kuona tofauti na merit ya budget ya serikali kwa kulinganisha na alternative.
 
Back
Top Bottom