Mheshimiwa the Don

Mheshimiwa the Don

26
Mheshimiwa the Don
David Ngocho Samson

Siku ya tatu tangu kutiwa mbaroni kwa Don, kuliibuka sintofahamu kubwa sana kote nchini. Clip ya mazungumzo aliyofanya Machera na Mheshimiwa Mabruki ilikuwa inasambaa kwenye mitandao ya kijamii na kuzua taharuki. Hizo zikiwa ni taarifa ambazo zilipomfikia Machera zilimshitua sana. Clip hiyo ilikuwa itumike mahakamani kama kidhibiti dhidi ya Don, lakini kabla mpango huo kufanyika, tayari ikawa imevujishwa na kuenea kwa kasi na kuzua gumzo kila kona ya nchi.

Machera alijikuta akiitafakari kwa kina. Kwa kila hali ilionekana kuwa watu wa Don walikuwa na njama kubwa kwa kitendo hicho cha kuvujisha sauti na mazungumzo yale. Swali likawa, ni nani na kwa nini alivujisha clip hiyo muhimu ambayo ulikuwa ushahidi mahsusi kwa ajili ya kumtia hatiani Mabruki?

Hakutaka kujiuliza tu, Machera aliamua kufunga safari ya upelelezi. Alihitaji kujua nini hasa kilikuwa kinaendelea nyuma ya mapazia.

Machera akaingia mtandaoni kujaribu kufahamu chanzo cha taarifa ile nyeti. Akiwa bado hajafahamu bado, akakutana na habari nyingine. Kulikuwa na taarifa ya kuandaliwa maandamano makubwa ya kupinga kuchafuliwa kwa jina la Mabruki, waandaaji wakitanabaisha kuwa, sauti ile ilikuwa ya kutengeneza yenye lengo la kumdhalilisha kiongozi wao ambaye tayari walikuwa wanamtarajia kushika hatamu za madaraka katika uchaguzi mkuu uliokuwa unafuata miaka miwili mbeleni, watu hao wakaendelea kudai, hata kukamatwa kwa Mabruki kulikuwa kwa hila.

Taarifa hiyo ikamgutua Machera kutoka kwenye upofu wa ghafla uliokuwa umemkumba, asiweze kuona ukweli katika mwanga halisi. Akabaini njama kubwa ilikuwa inaandaliwa ikilenga kuwahadaa raia kwa kuwaandaa kisaikolojia kulichukua suala la kukamatwa kwa Mabruki kuwa ni njama tu za kisiasa. Hakutaka kuendelea kubaki mtandaoni. Machera akanyanyuka na kuelekea nyumbani kwa Waziri Mabruki, eneo alikomrekodi Mheshimiwa huyo siku tatu zilizopita.

Alipofika eneo hilo, akaonesha vitambulisho vilivyomtambulisha kama afisa upelelezi anayefuatilia habari za kukamatwa kwa Mabruki. Ajabu ikawa kuwa, Mheshimiwa the Don hakuwa na mke wala mtoto isipokuwa wafanyakazi. Walinzi wakampa ushirikiano wa kutosha. Baada ya kuingia ofisini kwa Don, akabaini kitu ambacho hapo awali wakati akihojiana na Mabruki katika mazingira ya hatari kabisa, wakati bastola ikiwa imegusishwa kwenye paji lake la uso, hakuwa amekibaini. Kulikuwa na camera ndogo sana mle ofisini ambayo si rahisi kuiona kwa haraka. Ikampambazukia kuwa, mazungumzo yake na Mabruki aidha yalikuwa mubashara na au yalirekodiwa kwenye computer, au kwenye kifaa chochote chenye uwezo wa kutunza video za cctv camera.

Hata hivyo, ilikuwa wazi kwamba alikuwa amechelewa. Alipofuatilia kwa kina, alibaini kuwa vifaa hivyo vyenye kutunza kumbukumbu za video, havikuwepo tena mahali pake. Server zote zilikuwa zimeondolewa ndani ya jengo la the Don. Hata vile vyumba vilivyokuwa vimejaa ufuska wa Don na watu wake, vilikuwa safi kabisa. Machera akajua ngoma inogile. Watu wa Don walikuwa watu makini.

*†*

Baada ya kikao kikichofanyika ndani ya ukumbi wa Dar Live Mbagala Kati ya Inspekta Matilda na watu wa Don, sasa ulikuwa muda mwafaka wa kuweka mipango kwenye vitendo.

Maandalizi ya kumtoa Mheshimiwa Mabruki kwenye gereza la umma kwa lengo la kumpeleka eneo la siri yalikuwa yamefanyika.

Kwa ajili ya usalama wa Don, lakini pia katika kuepeuka watu wa Don kufanya hila ya kumtorosha the Don katika zile safari za kutoka gerezani kwenda mahakamani, kukiwa pia hofu kuwa gerezani mlikuwa na mamluki wake, ilipangwa na viongozi wa usalama, The Don apelekwe mafichoni na watu wa usalama.

Ikiwa inakaribia saa nane za usiku, gari moja aina ya Nissan Pathfinder lenye namba za usajili PT, ndani yake kukiwa na chemba ndogo ya nondo kwa minajili ya kuhifadhi wahalifu, lilikamata breki nje ya geti la gereza la ukonga. Wanausalama watano waliteremka kwenye gari hilo na kuelekea ndani ya geti hilo. Bila shaka walinzi getini walikuwa na taarifa za ujio wa watu hao. Walionesha vitambulisho vyao, wakaruhusiwa kuingia, huku mmoja kati ya askari wale walinzi akiongozana na wageni hao kuwapeleka kwenye ofisi ya mkuu wa gereza. Hawakuchukua muda ofisini kwa mkuu wa gereza. Wakaongezewa mtu aliyewaongoza kwenda kwenye chumba alimohifadhiwa Mheshimiwa Mabruki.

Mheshimiwa Mabruki akaamrishwa kubadili mavazi. Akavua nguo zake za mahabusu na kuvaa suti yake kali aliyoletewa, iliyofanania sana zile za wanausalama wale. Kwa namna ya ajabu, wanausalama wale wakamshuhudia the Don akitoa tabasamu la ushindi. Wakaondoka naye akiwa mtu huru. Hakufungwa pingu. Walitoka wakiwa wanatembea kama vile Mheshimiwa Mabruki alikuwa sehemu ya wanausalama wale.

*†*

Mheshimiwa Mabruki alipomuona Estivan Brown miongoni mwa maafisa usalama waliofika kumchukua kwa lengo la kumhamisha kwenda safe house, alitabasamu. Awali alikuwa amepenyezewa taarifa kuwa angehamishwa kutoka kwenye chanzo chake cha uhakika mle gerezani, na pia alitonywa kuwa watu wake tayari walikuwa na mpango mahsusi wa kumtorosha katika harakati hizo. Sasa alikuwa na uhakika na uhuru wake.

Kitu ambacho hawakumweleza, ni kwamba miongoni mwa wanausalama wale, walikuwemo pia watu wa usalama, ambao sio miongoni mwa genge lake. Wanausalama wale hawakufahamu kuwa Estivani na mwenzie mmoja walikuwa ni mamluki wa Don. Heri wangelijua!

*†*

Machera alipobaini uwepo wa njama, aliazimu kuchukua tahadhari. Akapiga simu kwa wakubwa kadhaa. Alifahamu kuwa kuna kitu kilikuwa kinatokota hivyo nafsi yake ilimlazimisha kutaka kufahamu zaidi. Simu kadhaa alizopiga zikamjulisha uwepo wa mpango wa kuhamishiwa safe house kwa Mabruki. Akaamua kumpigia simu mkuu wa gereza. La haula lakwata!! Alishachelewa. Mkuu wa gereza akampasha kuwa nusu saa ilikuwa imepita tangu zoezi hilo kutekelezwa. Ilikuwa ni saa tisa na nusu za usiku.

Kusikia hivyo, Machera akajua wazi, The Don alikuwa mbioni kutoroka. Akajaribu kumpigia kiongozi ambaye alijulishwa kuwa anaongoza zoezi hilo la uhamisho. Namba haikuwa hewani. Zoezi la kuwatafuta maafisa wale wengine pia hawakupatikana. Sasa ikawa dhahiri. The Don alikuwa mkimbizi wa mkono wa sheria. Fugitive.

Taarifa hizo zikafikia kwenye ngazi za maamuzi. Machera akakabidhiwa kikosi kwa ajili ya kumuwinda the Don.

Tukutane Tena baadaye!
David
FB_IMG_1591786598873.jpg
 
27
Mheshimiwa the Don
David Samson

Siku mbili baada ya Mheshimiwa Mabruki kutoroshwa, magazeti, vyombo mbalimbali vya habari, na mitandao ya kijamii kote nchini na hata nje ya mipaka ya nchi, vilisheheni taarifa ya kiongozi huyo kutoweka mikononi mwa vyombo vya usalama.

Taarifa hiyo ilinadi kwamba yule kizito aliyekamatwa kwa kuhusishwa na mauaji yaliyokuwa yakiendelea nchini, Mheshimiwa Waziri Mabruki, alikuwa ametoweka pasipo kuacha unyayo, na vyombo vya ulinzi havikuwa na habari wapi kapotelea.

Taarifa hiyo ikalazimu jeshi la polisi kujitokeza hadharani kuelezea suala hilo. Kwa mujibu wa polisi, ilisemekana kwamba mtuhumiwa huyo wa mauaji, ambaye pia alikuwa kiongozi serikalini mheshimiwa Mabruki Ally almaarufu kama The Don alikuwa ametoweka nchini na kwamba polisi walikuwa wanaendelea kumsaka kwa msaada wa Interpol.

Kama polisi walidhani wanatuliza mambo kwa taarifa hiyo, Basi walikuwa wamekosea hesabu. Taarifa hiyo sasa iliuthibitishia umma habari zile za mitandaoni. Ikaibua hisia mchanganyiko miongoni mwa raia. Raia wengi wakatokeza hadharani kudai kulikuwa na njama. Mabruki ambaye hata baada ya kusikika akikiri upuuzi wake, kuna baadhi ya raia walijitokeza barabarani wakiwa na mabango ya kudai haki kwa Mabruki, wakimtetea na kudai amebambikizwa kesi na eti kuwa sauti ile ilikuwa sauti ya kutengenezwa. Wengi wao waliamini huyu ndiye kiongozi aliyefaa kuongoza nchi. Mzalendo nambari moja nchini. Kiongozi waliyemtarajia kukamata usukani wa nchi kwenye uchaguzi mkuu uliokuwa unafuata. Mheshimwa Mabruki – The Don.

Ilidhaniwa pasipo na uhakika, kuwa mheshimiwa huyo alifanikiwa kutoroshwa na watu waliosemekana kuwa ni kikosi mahsusi alichotumia kutekeleza mauaji mbalimbali na matukio mengine ya uhalifu. Hata hivyo, baadaye polisi iliweza kupata miili ya baadhi ya maafisa usalama ambao walikuwa katika kuhakikisha uhamisho wa Mheshimiwa Mabruki. Miili hiyo baaada ya uchunguzi ilionekana kuwa kifo chao kilitokana na sumu ambayo iliwaingia kwa kuvuta hewa.

*†*

Kikosi cha Machera kiliingia kazini. Msako wa kumtafuta Mheshimiwa Mabruki ukashika kasi. Lakini ilibainika wazi, walikuwa tayari wamechelewa sana. Taarifa za uhakika kutokana na upelelezi wao, zilithibitisha kuwa tayari Mabruki alikuwa amepaa kwa ndege binafsi na kuelekea nchini Canada.

Yalipofanyika mazungumzo na serikali ya Canada juu ya kumkamata kiongozi huyo, Canada ilidai kiongozi huyo anayo haki ya kupata hifadhi nchini humo kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa juu ya ukimbizi wa kisiasa. Mabruki na watu wake, walimudu kuigeuza kesi yake kutoka kwenye jinai na kuwa njama za kisiasa kwenye uso wa kimataifa.

Machera akaazimu kuchukua likizo kwa muda.

***

Katika mitaa maarufu kwenye majiji, manispaa na miji kote nchini walijitokeza mitaani raia wengi mamia kwa mamia wakiandamana na kudai taarifa ya kutoweka kwa Don, ilikuwa janja ya serikali kumpoteza kiongozi huyu kama ambavyo ilikuwa inafanya kwa viongozi kadhaa waliopotezwa na watu wasiojulikana.

Maandamano makubwa kabisa kuwahi kutokea yaliratibiwa na viongozi wa vyama vya upinzani na wanaharakati waliokuwa kwenye hati ya malipo kutoka kwa mheshimiwa Mabruki, The Don. Vyombo vya habari vya kimataifa vilitinga nchini na kuweka kambi kuripoti tukio hilo la kihistoria. Mitandao ya kijamii ya Instagram, WhatsApp, Twitter, Facebook na blog mbalimbali ikageuka majukwaa ya siasa. Taarifa za kukashifu serikali zikisambazwa kwa ufanisi kupitia mitandao hiyo.

Picha za maiti, polisi wakiwashughulikia waandamanaji, hekaheka za maandamano, zikasambaa kote ulimwenguni. Kilio kikuu, raia wakikana kuitambua serikali yao, wakitaka iondoke madarakani. Maandamano hayo yakaitia kash-kash serikali ya chama tawala cha Democratic and Developmental Party (DDP). Maadui wa taifa wakitumia mwanya huo kutumia propaganda kuishurutisha serikali kuachia madaraka.

Hali ikawa si hali, kazi zikawa hazifanyiki, vibaka wakitumia fursa kupora mali za watu. Usalama wa watu na mali zao ukiwa mashakani. Mabomu yakalipuka kila kona ya miji yote mikubwa, vifo vya waandamanaji kadha wa kadha vikiripotiwa kwa sauti kubwa na vyombo vya habari vya mabeberu. Hasira za wananchi zikiongezeka. Kukazaliwa makundi mawili yenye uhasama, wafuasi tiifu kwa serikali na wale waliokuwa wafuasi kindaki ndaki wa mheshimiwa waziri, Mabruki Ally. Mauaji ya kisiasa yakiripotiwa kutokana na wananchi kushambuliana. Serikali ikawekwa msalabani. Adui akiwa na nguvu kubwa kutokana na chokochoko za mataifa ya kibeberu ambayo bila shaka yaliona mwanya wa kupenyeza agenda zao.

Ripoti zikatolewa. Takwimu zikapikwa. Rais wa Tanzania akabandikwa majina ya kifedhuli. Nduli, dikteta, gaidi. Sifa zote alizokuwa nazo, zile sifa njema, zikazikwa!

Ajabu!
Hata mawaziri wake wa karibu wakajivua nafasi zao na kujiunga upande wa adui. Ndio. Wale mawaziri njaa, wanaokuwa macho pima palipo na fursa ya wao kunufaika.

Kila dalili ilionesha serikali ya chama tawala ilikuwa mbioni kutoweka. Nao waliona fursa kwa kuwa upande wa adui, upande walioubandika jina 'upande wa wananchi'.

Kuondoa hali ya sintofahamu iliyojitokeza, mzalendo namba moja, rais wa jamhuri akajiuzuru wadhifa wake. Jeshi likakamata nchi na kutangaza kuunda serikali ya mpito huku kukiandaliwa tarehe mpya ya uchaguzi. Mchakato ulipokamilika, rais akakabidhi kijiti cha uraisi kwa mheshimiwa Sebastian Masebo, Waziri wa Mambo ya Ndani, kuongoza serikali ya mpito!

*†*

Mabruki The Don, akiwa anakula kiyoyozi kwenye jumba lake la kifahari huko Ottawa Canada, akaitisha press conference na kutangaza nia ya kugombea uraisi huku akionekana kuungwa mkono na serikali za kibeberu za Marekani, Uingereza, Ufaransa, na umoja wa NATO.

Taarifa hiyo ikaibua maandamano zaidi ya kuunga mkono hoja ya Mabruki huku Tanzania. Tangazo la Mabruki likailaani serikali ya Tanzania kwa kuanza siasa za uchaguzi mapema na kumuundia njama, huku Mabruki akidai serikali hiyo inashindwa kuwahakikishia usalama wananchi wake na kutengeneza habari za kutunga kuwachafua watetezi wa wananchi, hasa yeye. Naam, ni baada ya tangazo hilo ndio kulipoonekana amani ikirejea nchini. The Don akadhihirisha uwezo wa kuamua mustakabali wa amani ya nchi.

***

Katika kijiji cha Tung'aini, pana mto mkubwa uitwao Mesani, bonde la mto huo daima linakuwa na nyasi za kijani ambazo zimewanda mithili ya zulia zuri kwenye sebule ya nyumba ya kifahari.

Hapo alizaliwa kijana Machera, mpelelezi maarufu Tanzania. Leo alionekana akiwa amevalia kofia ya cowboy, fulana ya mikono mirefu na pensi la mifuko mingi, huku miguuni akitinga buti ndefu zinazofikia supu ya ugoko chini kidogo ya goti, akiwa juu ya mgongo wa punda na nyuma yake amekumbatiwa na mrembo mmoja kwa jina Anastazia. Anastazia pia alipendeza vya kutisha. Kichwani kwake kulionekana kofia ya ukindo aina ya sombrero. Alivalia fulana ya kijivu, skin tight jeans na miguuni buti ndefu vile vile zikiimeza jinzi lake. Mikononi walikuwa na ndoano zikiwa zimezamishwa kwenye maji tulivu ya Mto Mesani.

Kwa mbali kulisikika sauti za watu wakifurahia ngoma za jadi aina ya ritungu. Ni msimu wa mavuno na kama ilivyo ada, mavuno ni msimu wa furaha, raha na starehe. Msimu kunapofanyika harusi nyingi. Kipindi kinachoibua mapenzi, na ni msimu ambao wenye mipango yao huiweka kivitendo zaidi.
Mara simu yake ikaanza kuita, kwenye kioo cha Simu hiyo jina la mpigaji likasomeka machoni kwake bayana. Mheshimiwa Raisi!

Asante sana kwa kuwa nami hadi hapa. Huu ni mwisho wa msimu wa kwanza wa simulizi hii, Mheshimiwa the Don. Kufahamu nini kiliendelea, tafadhali usikose nakala yako ya kitabu cha Mheshimiwa the Don ili upate mwendelezo wa msimu wa pili ambao unahitimisha simulizi hii. Taarifa zitakujia baadaye namna ya kupata nakala yako.

David NGOCHO Samson.
[emoji2398]2019
FB_IMG_1591786598873.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom