Zak Malang
JF-Expert Member
- Dec 30, 2008
- 5,404
- 234
- Yadaiwa ni mkono wa mtu
- Aliugua gonjwa la ajabu
- Alikataa kubadili nia hiyo
- Jiji la Mwanza lazizima
Mwanamke aliyekuwa ametangaza nia ya kuomba uteuzi wa kugombea ubunge katika jimbo la Busega kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Magu, Mkoa wa Mwanza katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, mwaka huu, Nsega Aloyce Ntobi, amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha.
Kifo cha Nsega kimezua mjadala katika Jiji la Mwanza huku baadhi ya wakazi wakikihusisha na nia yake ya kutaka kugombea wadhifa huo wa kisiasa.
Habari zinasema kuwa Nsega alifariki usiku wa kuamkia juzi jijini Mwanza, wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando baada ya kuugua ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.
Kifo hicho kimeghubikwa na utata huku baadhi ya wananchi wakidai kuwa kuna mkono wa wanasiasa kadhaa.
Taarifa mpya inasema kuwa mgombea ubunge wa Busega, Nsega amepata ugonjwa huo siku mbili tu baada ya kukutana na (mwanasiasa ambaye jina tunalihifadhi) akiombwa ajitoe kwenye mchakato na yeye kukataa, kilidai chanzo kimoja cha habari.
Habari zinadai kuwa saa chache kabla ya kuugua, Nsega alikutana na mwanasiasa mmoja aliyekuwa na nia ya kugombea ubunge katika jimbo hilo kwa ajili ya mazungumzo yaliyohusu mchakato wa kugombea ubunge katika Jimbo la Busega.
Inadaiwa kuwa Nsega ambaye ni mkazi wa Pasiansi jijini Mwanza, alikimbizwa Bugando kwa ajili ya matibabu Aprili 28, mwaka huu.
Kabla ya kukukutana na mwanasiasa huyo, aliwahi kumtumia message(ujumbe mfupi wa maneno) akimsihi ajiondoe kwenye kinyanganyiro cha kugombea ubunge katika jimbo la Busega. Hata hivyo, Nsega alikataa, kilidai chanzo kingine cha habari kwa njia ya simu jana.
Chanzo hicho kilifafanua kada huyo wa CCM aliendelea kufanya mawasiliano na marehemu na kwamba baadaye walikutana kwa ajili ya mazungumzo zaidi.
Kwa mujibu wa habari hizo, Nsega alivyorudi nyumbani alijifungia chumbani kwake na hakuwa na uwezo wa kuzungumza. Hata hivyo, haijafahamika Nsega alikutana wapi na mwanasiasa huyo.
Hata hivyo, mmoja wa ndugu wa marehemu huyo (jina tunalo), jana alithibitisha kwamba Nsega amefariki dunia na kuongeza kuwa marehemu ameacha watoto kadhaa.
Alisema kuwa mwili wa marehemu bado umehifadhiwa Bugando ukisubiri kusafirishwa kwenda katika kijiji cha Nsora wilayani Magu kwa mazishi, ambayo yamepangwa kufanyika Jumamosi.
Mwili utaondolewa Bugando keshokutwa (kesho) hadi nyumbani kwa marehemu, Pasiansi kwa ajili ya kuagwa na baadaye kusafirishwa kwenda Nsora-Magu kwa ajili ya mazishi siku ya Jumamosi, alisema ndugu huyo.
Mwenyekiti wa CCM mkoani Mwanza, Clement Mabina, alithibitisha kwa njia ya simu kutokea kwa kifo hicho.
Mabina ambaye ni Diwani wa Kata ya Kisesa wilayani Magu, alizungumza jana na Nipashe baada ya Katibu wa CCM mkoani Mwanza, Rajabu Kundya, kutopatikana ofisini na simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa. Ndiyo, hata mimi nimesikia hivyo. Nilipigiwa simu na ndugu yake mmoja jana (juzi) kwamba Nsega amefariki na kwamba aliugua ugonjwa wa kuvua nguo na kubaki uchi, alisema Mabina.
Mabina pia alithibitisha kuwa kabla ya mauti, Nsega alikuwa amejitambulisha kwake kuwa alikuwa na nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Busega katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Alishafika hata kwangu kunieleza kuwa atagombea, kwa hiyo ninaamini hata ofisi ya Katibu wa CCM mkoa ina taarifa kama hizo, alisema Mabina.
Mwandishi wa habari hizi alifika nyumbani kwa marehemu Iloganzala ambako alikuta umati wa waombolezaji wakiwemo wana-CCM.
Kwa kweli tumeupokea msiba huu kwa masikitiko makubwa. Hadi mauti, Nsega alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilemela.
Aidha, alikuwa katibu wa tawi la CCM Pasiansi Magharibi, alisema Katibu Mwenezi wa CCM tawi la Iloganzala Magharibi, Emmanuel Magoti, na kuongeza kwamba:
Ni kweli alikuwa ametangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Busega. Ni juzi tu walikuja wazee ambao ni wana-CCM wakihitaji picha yake kwa ajili ya kutengeneza vipeperushi. Magoti alisema kuwa jina la Nsega ni chimbuko la jina na Jimbo la Busega.
Magoti alithibitisha kuwa mazishi yatafanyika Jumamosi katika kijiji cha Nsora wilayani Magu, baada ya shughuli za maombi kufanyika nyumbani kwa marehemu.
CHANZO: NIPASHE