Magazetini
JF-Expert Member
- Aug 16, 2014
- 593
- 1,713
MFANYABIASHARA wa Arusha anayemiliki kampuni ya Tanzania Bush Camp yenye kambi za watalii katika hifadhi za Serengeti mkoani Mara na Manyara iliyopo katika mikoa ya Arusha na Manyara, Timoth Mroki (36) amejiua kwa kujipiga risasi tatu kifuani akiwa katika baa maarufu ya Arusha Raha iliyopo eneo la Shams, jijini hapa.
Kisa cha kujiua kwake kimetajwa ni kusababisha ajali, baada ya kuligonga gari lingine katika eneo la Mbauda wakati akitoka katika makazi yake yaliyopo eneo la Kwa Mrombo, jijini hapa.
Alifikwa na mauti katika tukio lililotokea kati ya saa 1:30 na saa 2:00 usiku, ndani ya baa hiyo.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Mroki alifika katika baa hiyo baada ya kufanikiwa kuwatishia kwa risasi waendesha bodaboda waliokuwa wamemzingira katika eneo la ajali na kisha kuondoka kwa kasi kwa gari lake aina ya Nissan Navara.
"Alipiga risasi mbili hewani waliokuwa wamemzunguka wakanywea, akatumia mwanya huo kukimbia na moja kwa moja akafika Arusha Raha pengine kwa lengo la kujificha, na hapo akaanza kunywa…
"Ingawa inaonekana alikotoka alikunywa kidogo, alipofika Arusha Raha alikunywa haraka pombe mbili kali aina ya Valuu (Valeur) na wakati anamalizia ya tatu, akajikuta anazingirwa tena na wale waendesha bodaboda," anasema mtoa habari huyo na kuongeza kuwa, baada ya kufyatua tena risasi mbili nyingine hewani, lakini bila ya dalili ya watu hao kutishika, ndipo akaamua kujimiminia risasi.
Habari zaidi zinasema wakati anazingirwa, naye akijihami kwa risasi wasamaria wakiwa katika harakati za kupiga simu Polisi walishtukia wakiingia katika eneo la tukio lakini tayari Mroki alikuwa ameshajitoa uhai baada ya kujimiminia risasi kifuani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatusa Sabas hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, ingawa Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi ya wilaya ya Arusha imekiri kuwepo kwa tukio hilo, lakini chanzo chetu kikikataa kutajwa jina gazetini kwa kuwa si wasemaji wa matukio ya polisi mkoani Arusha.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
=============================================================================================================
UPDATESPolisi wachunguza kifo cha mfanyabiashara Arusha
KAMANDA wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas amesema mfanyabiashara wa nyumba za muda za wageni wa kitalii Bush Camp, Timoth Mroki (36) alijiua kwa kujipiga risasi kifuani kwa kutumia bastola yake aina ya KEL –TEC, yenye namba za usajili HCB21.
Amesema chanzo cha tukio hilo, bado hakijajulikana na Polisi inaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo chake. Alisema hayo katika taarifa yake kwa waandishi wa habari, jana.
Kamanda Sabas alieleza kwamba kabla ya tukio hilo, Mroki alikuwa anaendesha gari lenye namba za usajili T222CMX, Isuzu Double Cabin, lililokuwa likitoka maeneo ya Mbauda kuelekea mjini.
Alisema kutokana na msongamano mkubwa wa magari, Mroki aliamua kutanua barabara ili kukwepa foleni huku akiwa katika mwendo kasi.
Alipofika maeneo ya Shams, aligongana na gari kubwa la mizigo, mali ya kampuni ya Gupta, aina ya MAN yenye namba za usajili T548 BRL, lililokuwa linaendeshwa na Ally Ibrahimu (52), ambapo ajali hiyo ilisababishwa kung'oa bampa la mbele la gari kubwa.
Kamanda alisema pamoja na kusababisha ajali hiyo, Mroki aliendelea na safari yake, ndipo madereva wa pikipiki (bodaboda), walimfukuza na kufanikiwa kumkamata huko Ngarenaro eneo la kona ya Nairobi.
Aliporudi eneo la tukio na kuulizwa kwa nini amesababisha ajali, aliamua kutoa bastola yake na kufyatua risasi mbili hewani na hatimaye risasi ya tatu alijipiga kifuani kisha kuanguka chini.
CHANZO: Habari Leo