Mesaki: Mhadhiri aliyepata shahada ya uzamivu kwa kutafiti uchawi

LIKUD

JF-Expert Member
Dec 26, 2012
15,115
27,105
Mesaki: Mhadhiri aliyepata shahada ya uzamivu kwa kutafiti uchawi
APR 16, 2012by RAIA MWEMAin
Mmoja wa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Simeon Mesaki alitunukiwa shahada yake ya uzamivu (Ph.D) kutokana na utafiti wake kuhusu uchawi na mauaji ya kishirikina katika Tanzania. Huo ulikuwa mwaka 1993, wakati akisomea shahada hiyo katika Chuo Kikuu cha Minnesota, nchini Marekani. Katika makala hii Mwandishi Wetu, ARISTARIKO KONGA, anapitia utafiti huo, kwa ruksa ya mtafiti mwenyewe.

“Hii ni tasnifu (dissertation) inayohusu mwanzo, maendeleo ya kihistoria na hadhi ya sasa ya imani na vitendo vya uchawi katika Tanzania. Hoja kuu ni kwamba uchawi ni matokeo ya hali halisi inayowakanganya watawala wasomi katika Afrika…Kwa mfano nchi inakabiliwa na mauaji dhidi ya watuhumiwa wa uchawi…Kwa kukataa kukubali uchawi upo, watawala wanajikuta wanapoteza uwezo wa kuudhibiti uchawi, na kwa hakika, kusaidia raia kushughulika na tatizo hilo kwa ukamilifu.

Lakini pia kwa kukabiliana nalo moja kwa moja, wanajikuta wanahamasisha watu kuwa na imani zaidi kuwa tatizo hilo lipo…Kwa mfano, kwa kuwahamisha watuhumiwa wa uchawi kutoka eneo moja kwenda jingine, na kuhubiri zaidi kuhusu uchawi, kila mmoja anajikuta analitambua tatizo hilo.

Fumbo hapa ni kwamba, uchawi unadidimiza maendeleo, wakati shughuli za kimaendeleo zinatoa baadhi ya mazingira yanayopalilia shughuli za kichawi. Mtanziko (dilemma) ni kwamba shughuli za maendeleo ambazo zinaweza kuwa muhimu katika kuondoa sababu za uchawi, kama vile umasikini na maradhi, huzaa sababu nyingine pia, kama vile mmomonyoko wa mamlaka za kijadi na inda dhidi ya wale wanaofaidi zaidi maendeleo.

Uhamasishaji wa juhudi za kimaendeleo huweza kupunguza baadhi ya sababu za uchawi, lakini pia huzaa sababu nyingine za uchawi. Kwa hiyo, baadhi ya wanawake katika eneo la kati-mashariki ya Tanzania, walishindwa kufaidika na mpango wa shule za awali kwa kuwa walihofia baadhi ya wenzao, walikuwa ‘wakiwaroga’ baadhi ya watoto wao.

Kwa upande mwingine, matukio kadhaa (katika Afrika) yanayohusu mafanikio ya wakulima, wafanyabiashara au wanasiasa, yamehusishwa na vitendo vya ushirikina. Kwa ujumla, uchawi unatoa changamoto kwa utendaji wa kimahakama na kitamaduni wa watawala, na hata uwezo wa mamlaka ya dola.

Utafiti huu unatoa hali ya utata, ukihoji kwamba uchawi unawagusa pia watawala, na si tu kwamba unawakatisha tamaa ya kutawala, lakini pia unatoa changamoto kwao kwa kutetea maisha ya kisasa. Hakika, kadri jinsi ninavyofikiria kuhusu ushirikina, ndivyo ninavyogundua kuwa hii ni sehemu ya tatizo la utambulisho-tafsiri ya kitamaduni, ya kuwa watu wa kisasa.

Kuna sababu tatu zinazotambua kuwa uchawi kama sababu katika mahusiano kwenye nchi nyingi za Afrika na watu wao. Kwanza,… tangu uhuru, uchawi umechukuwa nafasi muhimu katika jamii kwenye nchi nyingi baada ya ukoloni katika Afrika.

Pili, kutokana na silika, usiri na muandamano wa imani na vitendo kama hivyo, changamoto zinazokabiliana na mataifa mapya ni nyingi. Kadri imani hizo zinavyokosa muundo, ndivyo zinavyosalia kuwa ni za kificho. Kwa hiyo, inakuwa vigumu zaidi kwa vyombo vya dola kudhibiti vitendo vya kishirikina. Uchawi unaonekana kuwa ni kitu kilichofungwa na kinachosambazwa kwa makusudi kwa vitendo. Kutokana na hali hiyo, kunakuwa na matatizo kadhaa. Kwa upande moja, uchawi tangu asili, umehusishwa na vitendo vya kukashifu.

Hadhi yake, uchawi kama ni hali ya ‘kukosa maendeleo’ imewashawishi viongozi wengi wa Afrika kuendeleza uwepo wake bila kutoa kauli zozote. Kutokana na hali hiyo, hakujakuwapo na miradi yoyote ya kimaendeleo, iliyolenga kuutokomeza ushirikina. Miradi ya maendeleo inasemekana imeathiriwa katika hatua tofauti na watu walioko kwenye mzingo wa uchawi.

Kwa hiyo, uchawi ni aina fulani ya ujinga au ujivuniaji wa tamaduni unaowageuza baadhi ya watu kuingia kwenye uchawi? Nafasi ya uchawi katika jamii na juhudi za kuudhibiti zinatoa mtanziko (dilemma).

Kwa mfano, baadhi ya viongozi husita kukemea au kuchukia imani kama hizo, kwa kuwa, wakati fulani wao wenyewe huhusika katika vitendo hivyo. Matokeo yake, hakuna msisitizo wowote katika kupambana na tatizo hilo, kwa kuwa sera rasmi haitambui, wakati huo huo, inaonekana kukubalika kama ni mila na desturi.

Tatu, migongano inayochipuka kutokana na sheria ya uchawi iliyorithiwa, bado inaendelea kuongezeka katika nchi nyingi, wakati nguvu ya kung’ang’ania imani hizo inazidi kuwa kubwa kutokana na matatizo ya kijamii na kiuchumi yanayotoa mboji nzuri kwa imani hizo. Sehemu ya tatizo inaonekana kuzama katika dhana ya kukosa uelewa au kushabikia ukubwa wa imani katika uchawi, ambazo zimejikita katika jamii zilizo nyuma kisayansi.

Kwa upande mwingine, ni kuwa wale ambao hunyakua fursa ya woga dhidi ya uchawi ni katika harakati za kujinufaisha kiuchumi na kisiasa.

Wamisionari wametambua ukubwa wa tatizo la uchawi na mambo mengine yanayoambatana nao, kwa kuwa mambo hayo yanaweka vigingi katika kuwahubiria watu au kupanda wasiwasi miongoni mwa watu waliobadili dini zao.

Tangu miaka ya 1970 wamisionari wamechukua hatua, kwa kutumia mfumo wa mikutano na machapisho. Wamelenga zaidi mtazamo wao katika masuala hayo na athari zake katika mpango wao. Kwa mfano, mkutano kuhusu ‘Imani na Uponyaji’ ulifanyika Yaounde, Cameroon, Septemba 10 hadi 13, 1972 na mwingine ulioitwa Episcopal Conference on Africa and Madagascar (SECAM), ulifanyika mjini Rome, mwaka 1975. Kusanyiko hilo lilivuta hisia za maaskofu wote waliohudhuria, kwamba kuna haja ya kufanya utafiti kuhusu masuala ya uchawi. Chapisho lililoitwa "Who is Who in African Witchcraft", lilitokana na mkutano huo.

Hivi leo uchawi umebakia kuwa kitu kinachoonekana katika jamii. Umekuwa ukijadiliwa katika vyombo vya habari. Wanasiasa na watawala wanaukataa. Ni kitu cha wazi katika mahakama na ni sehemu ya mazungumzo ya umma wa Tanzania. Katika matukio mengine, uchawi unaweza ukachukuliwa kwa mzaha, lakini katika matukio mengi, mtu kuhusishwa na uchawi kunahofiwa kutokana na madhara yake kuwa makubwa.

Kwa hiyo, kwa sehemu kama za Wasukuma, kuhusishwa na uchawi kunaweza kufikia hatua ya kifo cha upanga, wakati katika maeneo ya pwani ya Rufiji, mauaji ya kishirikina yanasababisha mtu kupanda cheo katika himaya ya wachawi.

Katika soka ya Tanzania, viwango vikubwa vya fedha hufuata mkondo wake kwa watu wanaosadikiwa kuwa ni wataalam wa uchawi, ambao hutumia uganguzi, matambiko na dawa kali, ili kuziroga timu pinzani na kushinda.

Wakati mwingine, wazazi wengi huchukua hatua ili kuwalinda watoto wao kwa kuwavisha mizigo ya hirizi ili kuukimbiza uchawi.

Kuna kufanana na tofauti za uchawi kutokana na jamii ya Tanzania ilivyotapakaa.

Mwishoni mwa 1986 nilianza masomo katika Chuo Kikuu cha Minnesota, ili kuvaa silaha zote zinazohitajika kufanya utafiti wa suala la kukanganya kama hili la uchawi. Tangu wakati huo, nimekuwa nikiendeleza maoni yangu kuhusu suala hilo, kama ni hali halisi ya kihistoria na lina nafasi yake katika jamii ya sasa ya Tanzania. Niliweka wazi mawazo na hoja zangu kuhusu suala hilo, katika mtihani wangu wa awali wa mahojiano ya mdomo, mwaka 1989. Hilo lilifuatiwa na utafiti katika maktaba na nyaraka, na uchunguzi wa nje ya maktaba, nilioufanya katika Tanzania.

Nilikusanya mambo ya kihistoria kutoka Rhodes House huko Oxford, vile vile kutoka School of Oriental and African Studies katika Chuo Kikuu cha London, Nyaraka za Taifa nchini Tanzania pamoja na sehemu ya East African ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Nilipitia magazeti na majarida katika Tanzania, na pia kitengo cha majarida katika Chuo Kikuu cha Minnesota na kufaidika na mpango wa mikopo baina ya maktaba katika Chuo Kikuu hicho.

Nilikusanya takwimu huko Rufiji, Dar es Salaam, Mwanza na Shinyanga, nikiwahoji watu mbali mbali, wakiwamo mahakimu, viongozi wa dini na wananchi wa kawaida. Uzoefu wangu ulinipa fursa kurejea nyuma na kufanya tafakuri mpya kuhusu dhana nzima ya uchawi, kama mtafiti na mwanaanthropolojia ( akishughulikia elimu ya binadamu, hasa inayohusu habari zinazohusu asili na maendeleo yake ya awali).

Nilijikuta nimegawanyika kati ya taaluma yangu, ambayo inasisitiza maarifa na maadili ni mambo ya mpito yanayotawaliwa na uwezo wa ubongo na wakati, kwa upande mmoja, na umuhimu wa kwenda sawa na jambo hili na kisha kuisaidia nchi kushughulikia suala la uchawi, kwa upande mwingine.

Nilipata fursa ya kuwasilisha matokeo ya utafiti wangu katika semina, mjini Dar es Salaam na Uingereza (katika vyuo vikuu vya Hull na Cambridge). Pamoja na takwimu nilizokuwa nimezisheheni, sasa naweza kuelezea tatizo la uchawi kwa kujiamini, ingawa sidai kuwa ninatoa ukweli wote au majibu yasiyo na maswali ya ziada.

Utafiti wangu ulihusu mtazamo wa uchawi kabla ya ukoloni katika jamii za Kiafrika. Niliangalia masuala ya utawala na sheria ili kuua imani za uchawi wakati wa ukoloni katika Tanganyika na madhara yake.

Niliangalia pia jukumu lililofanywa na waganga wa jadi waliokuwa maarufu kwa kupambana na uchawi wakati wa ukoloni. Nilifikiria zaidi kupeleleza kuhusu nafasi ya uchawi katika Tanzania ya sasa, jambo ambalo liliniongoza kwenda kuchunguza mauaji ya kishirikina katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga.

Najaribu kuweka wazi baadhi ya dhana potofu kuhusu uchawi katika jamii za jadi za Kiafrika. Kwa kurejea msimamo mbaya wa Uingereza kuhusu uchawi, naiona sheria dhidi ya uchawi kama mpango mkubwa wa kuidhibiti jamii. Ilikuwa dhahiri kwamba sheria ya uchawi, iliyolenga kurekebisha imani hiyo maarufu, ilishindwa kufanya kazi, na badala yake ikawa imeweka msingi wake kwa kuchukua nafasi kubwa baada ya uhuru.

Hivi sasa uchawi ni hali halisi na hata kuwa wazi katika jamii ambako kunadhibitiwa na Sheria ya Uchawi. Kwa hakika, sheria hii, ikiwa na utata mwingi, si chombo sahihi cha kushughulikia suala tete na gumu kama uchawi. Kutokana na sababu hii, makundi ya wauaji wa kulipwa, yamekuwa wakipata fursa ya kufanya mauaji huko Usukumani.

Katika utafiti huu ninaeleza kuwa kuendelea kuwapo kwa uchawi katika Tanzania ya sasa, ni lazima kuchanganuliwe kwa kutazama historia.

Uzoefu binafsi ni kwamba nimeingiwa shauku katika suala la uchawi kama mwana taaluma, mmoja wa wanazuoni, na kimsingi, kama Mtanzania.

Wakati nikijua kawaida ya kutatiza kwa mambo ya uchawi, nitasimulia baadhi ya matukio ambayo nimekumbana nayo, yanayohusishwa na uchawi. Kadri ninavyosimulia matukio haya yaliyonipata, ninavuta hisia kuhusu hofu kuu inayotokana na uchawi.

Nikiwa mwanaanthropolojia, nikiongozwa na msimamo, ninayakumbuka matukio haya kwa kuwa yaliathiri ufahamu wangu kuhusu ushirikina.

Kwa upande wa kisiasa, mwaka 1982/83, nilikuwa ndiye mwenyekiti wa CCM (Chama Cha Mapinduzi), tawi la kijiji changu, Changanyikeni, kilichopo kilometa mbili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako nilikuwa nafundisha. Kijiji ambacho ninaishi si cha kawaida kutokana na mchanganyiko wake.

Jina la Changanyikeni linatokana na hali halisi ya mchanganyiko wa wakazi wake. Kinajumuisha watu kutoka makabila mbali mbali. Lakini cha muhimu zaidi, nusu ya wakazi wake ni wasomi wazuri. Wakazi wengi wana elimu zaidi ya ile ya msingi na baadhi wana shahada za vyuo vikuu. Kwa hakika, wengi hufanya kazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (kama ilivyokuwa kwangu).

Matokeo yake, tawi letu la CCM lilikuwa la kipekee, kwa kuwa wajumbe wote wa Kamati ya Utendaji, walikuwa wahitimu wa vyuo vikuu. Katika tukio moja nililazimika kuita mkutano wa Kamati kujadili imani iliyokuwapo miongoni mwa watu, kwamba kijiji kilikuwa kimekumbwa na uchawi, na kuelezea matakwa ya muda mrefu ya baadhi ya wakazi kutaka mganga, aletwe kijijini hapo, kisha awaumbue wachawi.

Umuhimu wa hali hiyo ulikuwa ni kwamba mtaalam, aitwaye Tekelo, tayari alikuwa akifanya kazi zake katika kijiji cha jirani, na kwa hiyo ilidaiwa kwamba tusiikose fursa hiyo. Kamati yetu ilikuwa na wajumbe saba, na wengi wangeamua kuhusu jambo hilo.

Tulijadili hasara na faida za kumwita mganga, na kwa hakika kumlipa (kama alama ya makubaliano). Mwishowe kura zilizopigwa zilikuwa sawa kabla ya mimi kupiga yangu. Nilipiga kura ya kukataa kumwita mtu huyo, aliyedaiwa ni mtalaam.

Uamuzi huu ulikuwa na maana ya mambo kadhaa. Kwanza, tulichelea kukigawa kijiji chetu katika makundi tofauti ya wenye kuamini na wasioamini. Pia jambo hilo lingetufikisha katika kuwindana kwa uchawi, jambo ambalo nilikuwa naamini hatukuwa tayari nalo.Tekelo alikuwa na historia ya kuwa chanzo ya misuguano baina ya serikali na waganga wa jadi, ambao walikuwa wakidai kazi zao zitambuliwe rasmi.

Hatimaye Tekelo alipigwa marufuku kufanya kazi zake, amri ambayo ilitolewa na serikali huko wilayani Bagamoyo, kwa kuwa alikuwa akihofiwa kuwa ni tishio kwa umoja wa eneo hilo.

Tukio jingine linahusu chanzo cha uhusiano wa kihasama baina ya dada yangu na mama mdogo. Kwa juhudi zangu, dada alipata cheti cha ualimu wa shule za msingi, na amekuwa ni mwalimu tangu mwaka 1978, katika shule iliyoko maili tano kutoka nyumbani kwetu.

Dada yangu ambaye ni mtoto wa nne katika familia ya watoto kumi, waliozaliwa kwa mama na baba mmoja, hajaolewa lakini ana mabinti watatu. Mtoto wa kwanza ni wa kawaida na anasoma katika shule ya sekondari katika kijiji tulichozaliwa. Mtoto wa mwisho pia ni wa kawaida, lakini pacha wake wa kiume alifariki dunia wakati wa kuzaliwa.

Kwa bahati mbaya, mtoto wa pili wa dada yangu huyo si binti wa kawaida. Anaonekana hawezi kusema kwa ufasaha. Mwaka 1992, niliambiwa kuwa dada yangu huyo alikwenda kumwona mpiga ramli, ili kufahamu ni kwa nini mtoto wake ana ulemavu huo. Mpiga ramli alimtaja mama mdogo kuwa ndiye aliyesababisha hali ya bintiye.

Madhara ya jambo hili la ramli ni kwamba dada na mama mdogo walivunja kabisa mawasiliano. Hakika walikuwa maadui. Ili kufanya hali kuwa ngumu zaidi, mama mdogo naye alikwenda kutafuta sababu ni kwa nini mwanawe pekee wa kiume aliyesoma, ambaye nilisaidia kumsomesha, hajaweza kuwatembelea wazazi wake kwa miaka kumi. Aliambiwa na mganga kwamba, mama yangu mzazi amempa laana mwanawe, ili asiwe na kumbukumbu ya kurejea nyumbani.

Ili kufanya mambo kuwa mabaya zaidi, dada yangu alimhamisha binti yake wa kwanza, kutoka shule ya bweni, kwenda shule ya kutwa karibu na kijiji chetu, ili asiwe na chaguo jingine zaidi ya kukaa nyumbani kwetu, makazi ambayo yako jirani na ya mama mdogo.

Nilipowatembelea wazazi wangu kwa mara ya mwisho, niliweza kubaini chuki iliyokuwapo kati ya makazi hayo mawili, lakini nilishindwa kuliweka bayana suala hilo kutokana na ukosefu wa ushahidi na ujasiri wa kuuliza kuhusu suala hilo, kwa kuwa kungesababisha madhara kadhaa.

Tukio jingine linalohusiana na uchawi, lilijitokeza likihusu dada yangu mwingine aliyeishi Dar es Salaam, akifanya kazi katika mradi wa kilimo, unaofadhiliwa na nchi za kigeni. Dada yangu (Nitamwita Wasiwasi), aliyekuwa na umri wa miaka 26, alikuwa hajaolewa na hakuwa na watoto. Aliishi katika chumba kimoja na dada yetu wa kwanza, aliyekuwa na umri wa miaka 42, ambaye alifanya kazi kama mpishi katika taasisi ya elimu. Dada yetu mkubwa pia hakuwa ameolewa ingawa alikuwa na watoto wanne.

Wakati mmoja, mapema Januari 1992, Wasiwasi aliamua kuondoka na kwenda kuishi na kaka yangu, aliyekuwa anaishi katikati ya Jiji la Dar es Salaam, katika nyumba yenye vyumba vitatu vya kulala, aliyopangishiwa na mwajiri wake. Kaka yangu alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha dawa. Hakuwa ameoa na wala hakuwa na watoto.

Wasiwasi alipewa chumba kwa ajili ya matumizi binafsi, ambapo aliweza kujipikia na kumpikia kaka yangu pamoja na ndugu yetu mwingine, ambaye pia wakati mwingine alikuwa akiishi katika nyumba hiyo.

Usiku mmoja, umeme ulikatika ghafla na Wasiwasi alikimbia kutoka kwenye jengo hilo. Mwishowe tulimkuta akiwa hospitali ambako aligundulika kuwa alikuwa amepatwa na wazimu. Baada ya siku moja ya kulazwa hospitali, alirejea kwenda kuishi na dada yake.

Itaendelea
 
Back
Top Bottom