SI siri tena kwamba Tanzania imegubikwa na ufisadi wa kutisha, mkubwa na wa aina yake Afrika Mashariki, kama si bara zima la Afrika.
Ufisadi huu, ulioanzia awamu zilizopita zilizobinafsisha kila kitu kilichokuwa cha Umma, kwa usiri mkubwa, mizengwe na kwa bei ya kutupa, umeongeza kasi jinsi siku zilivyopita.
Kipindi hicho, tumeshuhudia kashfa kubwa kubwa za ufisadi zenye kuatamiwa kwa machukizo ya Umma, kama ile ya Independent Power Tanzania Ltd (IPTL/TANESCO), ambapo nchi imeporwa mabilioni ya fedha kwa mkataba tata wa umeme wa miaka 20 kuanzia mwaka 1999. Chini ya mkataba huu, nchi imetupwa gizani kwa kukosa umeme, lakini inaendelea kuilipa IPTL zaidi ya 5bn/= kwa mwezi bila kujali, umeme uwepo au usiwepo; tutumie au tusitumie, kwa sababu mkataba wa mwaka 1995 unaelekeza hivyo. Walioliingiza Taifa katika mkenge huu wanafahamika kwa vyeo na kwa majina; lakini wapo huru, wanapeta.
Kashfa nyingine zenye kuangamiza ustawi wa Taifa ni pamoja na zile za EPA, ununuzi wa rada na ndege ya Rais; ubinafsishaji wa NBC na uuzaji wa nyumba za Serikali; mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, Richmond/Dowans, mikataba mibovu ya madini; Loliondo, na ufujaji wa zaidi ya bilioni 150/= za mfuko wa kuwezesha uagizaji bidhaa (CIS), kwa kutaja chache tu.
Na kama tusingeshituka, manyang'au hawa walikuwa wamepania pia kuhujumu mifuko ya Akiba ya wafanyakazi kwa kujichotoa mabilioni ya fedha kwa njia ya ushiriki katika vitega uchumi vya mifuko hiyo. Na ingawa ufisadi huu unafahamika vizuri, na wahusika wanajulikana kwa Serikali (ikiwamo Serikali ya awamu ya nne), juhudi zimeendelea kufanywa kuatamia uchafu huo, na wahusika kuoshwa kwa sabuni kali ili, kwa hadaa kubwa, waweze kumeremeta machoni mwa Umma.
Hizo ndizo zilikuwa enzi za mwanzo kabisa za utamaduni wa kukwapua mali ya umma miongoni mwa wanasiasa na watawala, kwa kushirikiana na kada ya wafanyabiashara, kuota mizizi.
Utafiti makini umeonesha kwamba, katika juhudi za kujiponya, wahujumu hao ama wamekimbilia kunyakua (kupora) nafasi za kisiasa ili wapate kinga ya kisiasa, au wamegeuka kuwa wafadhili wakubwa wa Chama Tawala na kampeni za uchaguzi ili walindwe na kusafishwa.
Lakini pamoja na hayo, licha ya chama tawala na Serikali kujitahidi kuzisafisha kashfa mbalimbali za ufisadi ziweze kumeremeta, kashfa moja kabambe nchini, ya mradi wa Mgodi wa Meremeta, imeshindwa kumeremeta. Kushindwa kwa juhudi za Serikali hivi karibuni za kuisafisha Meremeta ili imeremete zimepelekea Bunge kuitaka Serikali iwasilishe hesabu za Kampuni hiyo kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zikaguliwe ili kukata mzizi wa fitina.
Hata hivyo, pamoja na Agizo hili la chombo hicho cha kutunga Sheria, chenye jukumu pia la Kikatiba la kusimamia utendaji kazi wa Serikali, hesabu za Kampuni hiyo hazijakaguliwa wala kuwasilishwa kwa CAG. "Nitakagua nini wakati sijapata hesabu zenyenyewe kutoka Serikalini ….. siwezi kufanya ukaguzi wowote", alinukuliwa akisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG), Ludovick Utouh, akilalama hivi karibuni, juu ya Serikali kukataa kutii Agizo la Bunge, kwa hofu inayofahamika.
Serikali kwa upande wake, inaonekana kuiatamia kashfa hii kwa madai kwamba siri za Meremeta hazizungumziki, na hesabu zake hazikaguliki kwa sababu zinahusu mambo ya usalama wa Taifa. Kuna ukweli gani juu ya madai haya? Je, Meremeta ni mradi wa Serikali? Kwa misingi ipi; na kwa kiwango gani?. Hebu tuchimbue kidogo kuusaka ukweli.
Kampuni ya Meremeta, ambayo inadaiwa haijasajiliwa chini ya Ofisi ya Hazina kama kampuni au shirika, tayari imechota malipo tata zaidi ya 155 bn/= zilizolipwa na Benki Kuu (BOT) kwa Kampuni ya Nedcor Trade Service, baada ya udhamini wa Kampuni yenye hisa ya Triennex (PTY) limited ya Afrika Kusini. Malipo haya na mengine, kama tutakavyoona badaye, ndiyo yaliyozua utata na Bunge kuagiza mahesabu yakaguliwa.
Katika makala haya, tutaona na kufahamu kama ni kweli kampuni ya Meremeta ni ubia wa Serikali na Kampuni ya Triennex, unaohusisha Jeshi la Ulinzi, kama inavyodaiwa, na pia kuhusisha Usalama wa Taifa. Tutaona ni kwa vipi, makampuni mengine kama Deep Green Finance na Tangold (yanavyoguswa na kashfa hii) yalivyoingia; na kwa nini Serikali inajiuma mdomo na kukunja mikono yanapotajwa.
Inaelekea kwamba Serikali ya Awamu ya Nne, haihusiki sana na sakata hili, japo inalijua fika; lakini imejitahidi kuliatamia bila mafanikio kwa njia ya "kufunika kombe mwanaharamu apite".
Lakini ifahamike kwa misingi ya sheria kwamba, kitendo cha mtu kufunika kombe au kuatamia kosa lililotendwa na mtu mwingine, kwa lengo la kumwepusha mtu huyo mwingine sheria isichukue mkondo wake dhidi ya mtu huyo; au kosa alilotenda lisijulikane, kinamfanya mtu huyo mwenye kutaka kumwokoa huyo mtu mwingine na yeye kuwa mshiriki wa kosa hilo kwa kiwango sawa na cha mtuhumiwa halisi wa kosa. Kwa hiyo, viongozi wanaowalinda au kuwasafisha mafisadi wana hatia ya ufisadi ule ule wa wale wanaojaribu kuwaokoa.
Huu ndio utamaduni wa kulindana kwa maovu, unaoshika kasi nchini kwa machukizo ya Umma; kana kwamba viongozi na washirika wao wana kinga ya kimsahafu (Luka 12:32) kwamba, "Msiogope, enyi kundi dogo; kwa kuwa baba yenu (mfumo wa kifisadi) ameona vema kuwapa ule ufalme - (wa ulaji?)"
Hebu tuziangalie sasa Meremeta, Deep Green na Tangold, Kampuni zinazolindwa na mfumo wa utawala wa nchi kwa maumivu na chukizo kubwa kwa wananchi; tuone kama kweli shughuli zake zina chembe ya Usalama wa Taifa.
Kampuni ya Meremeta iliandikishwa na kusajiliwa nchini Uingereza Agosti 9, 1999 (kisiwa cha Isle of Man) na kupewa namba ya Usajili 3424504; lakini Serikali yetu inadai ni ubia kati ya Serikali ya Tanzania yenye asilimia 50 ya hisa, na Kampuni ya Triennex ya Afrika Kusini, inayomiliki hisa asilimia 50 pia.
Utata unaongezeka pale inapodaiwa kuwa, Makampuni ya London Law Serivices Ltd, na London Law Secretarial Ltd, nayo ni wanahisa wa Meremeta.
Madhumuni ya Kampuni hiyo yanaelezwa kuwa ni kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo nchini, pamoja na kuwasaidia zana za kufanyia kazi. Swali linalojitokeza hima hapa ni kwa vipi kampuni inayomilikiwa na Serikali, na ambayo shughuli zake zinafanyika hapa hapa nchini na kwa misingi ya Usalama wa Taifa, iandikishwe na kusajiliwa katika nchi ya kigeni?
Kati ya mwaka 2003 na 2005, Kampuni hii ilitelekeza wajibu na madhumuni ya kuanzishwa kwake na kuanza kuchimba dhahabu yenyewe huko Buhemba, Musoma. Hapo ndipo hadithi ya Meremeta kuhusisha Usalama wa Taifa ilipoanza; hapo ndipo hadithi ya Meremeta kujihusisha kusaidia kiwanda cha magari cha Jeshi cha Nyumbu (Kibaha ) ilipoanza kupikwa na kusikika.
Ikumbukwe kuwa, katika kipindi hicho (2003 – 2005), kiwanda cha Nyumbu kilipangiwa fedha kutoka serikalini jumla ya Sh. 950 milioni, kwa ajili ya kutengeneza magari 21 ya kijeshi, kwa wastani wa 45.2m/= kwa kila gari, na hakukuwa na fedha zaidi zilizoingia kutoka vyanzo vingine kipindi hicho.
Ukweli juu ya kwamba Mradi wa Meremeta haukuhusika kwa namna yoyote ile na Jeshi la Wananchi, unathibitishwa pia na Waziri wa Ulinzi, Philemon Sarungi, katika hotuba yake ya Bajeti ya 2004/2005, aliposema: "Mradi wa Buhemba umejengwa katika eneo lililokuwa Kambi ya Jeshi, na shughuli za uchimbaji na uzalishaji zinasimamiwa na Idara ya Madini".
Kile tu kwamba mradi huo ulijengwa mahali ambapo zamani ilikuwa Kambi ya Jeshi, hakufanyi uwe Mradi wa Jeshi wenye kuhusishwa na Usalama wa Taifa. Ukweli ni kwamba, Mgodi mpya wa Buhemba ulijengwa kwa rand milioni 240 (dola 56m) na Kampuni ya WBHO (Pty) Ltd ya Afrika Kusini, na ulikamilika mwaka 2000. Ujenzi huo ulifanywa kwa niaba ya Meremeta na Triennex (Kampuni zote tata), na si kwa niaba ya Serikali ya Tanzania. Ulizihusisha pia kampuni za kigeni za Jefferies and Green na Time Mining, zote za Afrika Kusini.
Niharakishe kusema hapa kwamba, mmoja wa wanahisa wakubwa wa Kampuni ya Time Mining (TM), alikuwa mama mmoja Mtanzania mke wa mmoja wa vigogo nchini ambaye ndiye pia aliyeileta kampuni hiyo nchini kuja kusimamia na kuendesha Mgodi wa Meremeta, eti kwa niaba ya Serikali ya Tanzania.
Cha kushangaza hapa pia ni kwamba, wengi wa watumishi wa nje (expatriates) wa Kampuni ya Ukaguzi ya Alex Stewarts ya mjini Washington, iliyoletwa Tanzania kukagua mauzo ya nchi za nje ya dhahabu kwa makampuni ya madini nchini, ndio hao hao waliokuwa watumishi pia wa Kampuni ya Time Mining.
Kama kweli serikali ilikuwa na maslahi katika Meremeta, kwa nini iliruhusu mtu binafsi kusajili kampuni binafsi ya kigeni kusimamia mradi huu? Hatutazungumzia sana suala la Alex Stewarts hapa, kwa sababu liko mahakamani, likiwahusisha mawaziri wa zamani na katibu mkuu msitaafu.
Baada ya kukomba dhahabu yote huko Buhemba na Buhemba Kusini, Nyamongo na Magunga, mwaka 2006, Meremeta ilitangazwa kuwa ilikuwa inafanya kazi kwa hasara, na ikaundwa Tume ya Serikali ya watu watano, kuchunguza matatizo ya Kampuni hiyo. Wazito na Waheshimiwa sana waliokuwa katika Tume hiyo, ni Daudi Balali – Gavana wa BOT na Mwenyekiti wa Tume; Gray Mgonja, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, na Patrick Rutabanzibwa, wakati huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.
Wengine walikuwa ni Vincent Mrisho, Katibu Mkuu, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa; Andrew Chenge, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, na Michael G. Garner, kama Mshauri huru wa Tume, ambaye alikuwa pia ndiye Mshauri wa Benki ya Nedbank, yenye uhusiano na Kampuni ya Nedcor Trade Service, iliyochota bilioni 155/- kutoka Benki Kuu katika mazingira ya kutatanisha.
Tume hiyo ilipendekeza kusitishwa kwa shughuli za Kampuni ya Meremeta za kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo, jukumu ambalo tayari ilikwishalitelekeza tangu mwaka 2003, na kujiingiza katika uchimbaji na umiliki wa migodi.
Tume ilipendekeza pia kuanzishwa kwa Kampuni mpya yenye jukumu la kusimamia na kuendesha Mgodi wa Buhemba yenye kumilikiwa na Serikali asilimia kwa mia. Kwa lugha nyingine ni kwamba, baada ya kung'atuka kwa Meremeta, Serikali iliamua kusimamia yenyewe Mradi huo wa dhahabu kupitia chombo au taasisi teule.
Na kwa uzito wa mapendekezo ya Tume hiyo ya Balali, Meremeta ilifilisiwa, ambapo mali na madeni yake yalichukuliwa na Kampuni mpya ya "Tangold," inayodaiwa kumilikiwa na Serikali kwa asilimia mia. Na ingawa Meremeta (halisi) ilifungwa rasmi mwaka 2006 nchini Uingereza, shughuli zake hazikukoma nchini Tanzania wakati huo, kama tutakavyoona baadaye katika makala haya.
Hapa kuna utata mwingine, kwamba kumbukumbu zinaonyesha kuwa, Kampuni ya Tangold ilianzishwa katika Visiwa vya Mauritius, Aprili 4, 2005; na kupewa Leseni ya Biashara Aprili 8, 2005 kama kampuni binafsi. Lakini kumbukumbu nyingine zinaonyesha kuwa, Tangold ilifungua Akaunti ya Benki Namba 011103024852, Tawi la Corporate Drive la NBC, Dar es Salaam, Januari 1, 2003; kabla hata Tume ya Balali na wenzake haijaundwa kutatua tatizo la Meremeta.
Taarifa nyingine zimeonyesha zaidi kuwa, kampuni hiyo ni ya kigeni iliyosajiliwa nchini Mauritius na kupewa leseni nchini Tanzania, Februari 20, 2005 kama tawi la kampuni ya kigeni; na ilianza kupatiwa fedha na BOT Agosti 1, 2005 kwa kazi isiyojulikana.
Je, ina maana kwamba Tangold ilikuwapo nchini Tanzania kabla ya kuanzishwa nchini Mauritius mwaka 2005, au ni aina fulani tu ya usanii? Hata kama ilikuwapo, iliwezaje kufungua akaunti benki, Januari 1, 2003 ambayo ilikuwa Sikukuu ya Kitaifa ya Mwaka mpya?. Kama ilikuwapo, kwa nini Tume ilipendekeza kuundwa kwa kampuni ambayo tayari ilikuwapo? Nini tofauti kati ya Tangold iliyofungua akaunti Januari 2003, na Tangold iliyosajiliwa Mauritius April 4, 2005 kurithi Meremeta?
Ingawa mapendekezo ya Tume na tamko la Serikali yalikuwa kwamba, kampuni hiyo mpya (Tangold) imilikiwe kwa asilimia mia na Serikali, utekelezaji wake ulikuwa ni kinyume chake; ambapo inaelekea wajumbe wa Tume iliyoundwa kuchunguza matatizo ya Meremeta, ndio waliogeuzwa kuwa Wakurugenzi wa Kampuni hiyo mpya. Hao wanatajwa (kwa baadhi majina yao kuongezwa herufi moja ya katikati), kuwa ni Daudi Balali, Gray S. Mgonja, Andrew Chenge, Patrick J. W. Rutabanzibwa na Vicent F. Mrisho.
Inawezekana, kwa mtazamo wa enzi hizo na kwa kusudi hilo, kwamba hao watano ndio walikuwa Serikali yenyewe; lakini kifungu cha saba (7) cha Katiba ya Kampuni ya Tangold kinatibua dhana yote hiyo, kinaposema, "Wenye hisa ya Kampuni wanaweza kurithisha hisa zao kwa ndugu zao".
Je, ni kweli Tangold ilikuwa inamilikiwa na Serikali asilimia mia kama ilivyopendekeza Tume ya Balali, na pia kwa mujibu wa tamko la Serikali? Ni ndugu wapi hao wa Serikali (kama kweli Serikali ina ndugu!) waliostahili kurithishwa hisa za Serikali?
Haya ni maswali magumu, na tunashawishika kuamini kwamba, Tangold haikumilikiwa na Serikali asilimia mia; bali ilikuwa kampuni binafsi iliyorithishwa mali za kampuni ya Meremeta.
Wakati matatizo ya Meremeta yakiendelea, na wakati huo huo tayari mapendekezo ya Tume ya Balali ya watu watano yakiwa yameanza kufanyiwa kazi, Machi 18, 2004, iliundwa Kampuni nyingine iitwayo "Deep Green Finance" (DGF) ambayo madhumuni na shughuli zake hazijafahamika vizuri mpaka sasa. Wakurugenzi wa DGF walikuwa ni Mark Ross Weston wa New Zealand; Antón Taljaard wa Afrika Kusini, na Rudolf Van Schalkwyk, pia wa Afrika Kusini.
Wanahisa wa DGF walitajwa kuwa ni Protase R. G. Ishengoma, Stella Ndikimi wa kampuni ya uwakili ya IMMA, ya jijini Dar es Salaam; Benki ya Nedbank Africa Investment Ltd ya Afrika Kusini (ambayo mshauri wake, Michael G. Garner, ndiye pia aliyekuwa Mshauri huru wa Tume ya watu watano, iliyochunguza matatizo ya Meremeta na kupendekeza kuundwa kwa Tangold), na Kampuni ya SBM Nedcor Holdings, ambayo haijafahamika bado, kama ina uhusiano wowote na Kampuni ya Nedcor Trade Service, iliyolipwa na BOT malipo tata ya zaidi ya Sh. 155 bn/= kwa niaba ya Meremeta.
Wakurugenzi hao watatu wa Deep Green Finance, ndio waliokuwa maofisa pia wa NedBank; na jina la Deep Green limetumiwa mara nyingi na NedBank katika miradi yake ya kijamii.
Haifahamiki pia ni kwa vipi na kwa njia ipi, Watanzania pekee wawili, Protase Ishengoma na Stella Ndikimi, walitembelewa na ngekewa ya kununua hisa za kampuni yenye kumilikiwa na wageni kama hii (DGF); na kama ni kweli inavyodaiwa, kwamba hatimaye walichukua hisa (kwa njia ya kuhamishia au kununua) katika Nedbank Ltd na Nedbank Africa Investments, Aprili 15, 2004.
Kama ilivyokuwa kwa kampuni ya Tangold, iliyofungua akaunti siku ya Sikukuu ya mwaka mpya; ndivyo ilivyokuwa pia kwa kampuni ya Deep Green Finance, iliyofungua akaunti Benki ya NBC, Na. 011103024840, tawi hilo hilo la Corporate Drive; safari hii ilikuwa Sikukuu (ya mapunziko) ya Mei Mosi, 2004.
Kuna utata kuhusu utoaji wa namba za akaunti za benki hiyo, kwamba akaunti ya Tangold, namba 011103024852, iliyofunguliwa Januari 1, 2003, ni kubwa (kwa akaunti 12 zaidi), ikilinganishwa na Akaunti Namba 01110302840 ya Deep Green Finance, iliyofunguliwa zaidi ya mwaka mmoja baadaye, Mei 1, 2004. Je, ni utaratibu wa NBC kutoa namba za akaunti kuanzia na namba za juu, kushuka chini? Kama sivyo, basi kuna uwalakini unaotufanya tuamini kwamba kulikuwa na hitilafu ikizingatiwa pia kwamba akaunti zote mbili zilifunguliwa siku za mapumziko ya Sikukuu za kitaifa.
Toka Mei 1, 2004 akaunti ya Tangold ilipofunguliwa, hadi Julai 31, 2005 (zaidi ya mwaka mmoja), hapakuwa na shughuli za DGF zilizoingiza fedha katika akaunti hiyo, hadi Agosti 1, 2005 ilipoanza kupokea mabilioni ya fedha kutoka ama Benki Kuu, Deep Green Finance au Tangold, kwenda ama Deep Green Finance, Tangold, Meremeta, IMMA Advocates au kusikojulikana.
Wakati tunaelezwa kwamba Tangold ilianzishwa Aprili 5, 2005 na kupewa leseni ya biashara Aprili 8, 2005 kuchukua nafasi ya Meremeta, na mali na madeni ya Meremeta kuhamishiwa au kuchukuliwa na kampuni mpya, kwa maana kwamba Meremeta ilikuwa imefilisiwa na kufungwa; lakini kumbukumbu zinaonyesha kwamba, Oktoba 12, 2005, jumla ya 1,690,500,000/= zilihamishwa kutoka Tangold kwenda kampuni (mfu?) ya Meremeta; na vivyo hivyo Novemba 23, (555,300,048/=) na Deseaba 12 (551,060,000/=). Iliwezekanaje Meremeta kulipwa fedha hizo wakati ilikwishafilisiwa? Nani aliifufua?
Kwa kifupi, kati ya Agosti 1, 2005 na Desemba 21, 2006, jumla ya 32bn/= zilihamishwa kutoka Benki Kuu kwenda Deep Green Finance na Tangold; mbali na zile zilizopelekwa kusikojulikana.
Tunashawishika kuamini kwamba, Deep Green Finance iliundwa kurahisisha na kuhakikisha utoroshaji wa fedha za Meremeta na Tangold kwenda nje ya nchi na si kwa sababu nyingine yoyote ile.
Baada ya mahesabu hayo, na kuonekana kwamba Mradi wa Tangold hauwezi kuendelea, Serikali iliuza haki za Mgodi huo kwa Kampuni ya "Rand Gold" ya Afrika Kusini, kwa bei ya chini ya soko, na kusababisha hasara ya dola za Kimarekani milioni 100; na pia kulipa dola milioni 132 pamoja na adhabu na riba, kutokana na Serikali (BOT) kudhamini wakopaji/wawekezaji waliofilisika na kutupa mzigo kwa Serikali kuyalipa.
Tangu kuundwa kwa Kampuni ya Meremeta, hadi kuundwa na kufilisika kwa Kampuni ya Tangold, licha ya kuruhusu uporaji mkubwa wa mabilioni ya fedha na rasilimali, ilisababisha pia hasara ya jumla ya dola za Kimarekani milioni 232, sawa na 232bn/= wakati huo, kwa njia ya kifisadi. Malipo hayo yalifanyika Oktoba 2005, mwezi mmoja tu kabla ya Rais Benjamín Mkapa kumaliza awamu yake.
Kwa hiyo wanaodai kwamba kashfa ya Meremeta haizungumziki, eti kwa sababu inagusa mambo ya Usalama wa Taifa, wajichunguze kwanza kabla hawajanena; kisha watueleze hayo wanayatoa wapi; vinginevyo tutawahesabu Wasaliti wa Taifa hili.
Na kwa nini tusalimu amri kwa taarifa za uongo, wakati nchi yetu inageuzwa "Shamba la Bibi" kwa ulafi wa wachache wa ndani, wakishirikiana na wahujumu uchumi wa kimataifa?.
King'aracho ni dhahabu, lakini si kila king'aracho au kimeremetacho ni dhahabu. Kashfa ya Mradi wa dhahabu wa Meremeta ni mfano wa ufisadi uliokithiri nchini, kiasi kwamba hata upambwe kwa lugha ya vito na kufukiziwa ubani, hauwezi kumeremeta wala kunukia. Wale makuwadi wa ufisadi nchini, wanaodhani kwamba wanaweza kutudanganya tukadanganyika, wajue kwamba wanajaribu kutemea mate mbingu, na hivyo hawawezi kukwepa kuchafua nyuso zao.
Chanzo: Raia Mwema