SEHEMU YA HOTUBA YA DR SLAA ALIYOWASILISHA BUNGENNI
"Pamoja na Taarifa ya Ufisadi ndani ya BOT pia hakuna hatua yeyote iliyochukuliwa kuhusu maeneo mengine tuliyoyaibua mathalan Ufisadi kupitia Kampuni ya Meremeta na Tangold. Waziri wa Fedha ambaye ndiye mwenye dhamana na makampuni hayo katika majibu yake siku ya ijumaa amerusha maswala hayo kwa Mawaziri wa Kisekta. Inawezekana Serikali inasubiri Bunge liunde tena Kamati Teule nyingine kwa lengo la kupitia makampuni haya ambayo umiliki wake umegubikwa na utata mkubwa kutokana na Meremeta kuandikishwa Uingereza ikiwa na Hati ya Usajili na 3424504 ya Tarehe 19 August,1997 na kupata Hati ya Kutimiza Masharti (Certificate of Compliance) nchini Tanzania kama Tawi la Kampuni ya Kigeni yenye na 32755 ya tarehe 3 Oktoba, 1997. Kinachoshangaza katika Kampuni hii ni kuwa wenye hisa wake tofauti na Bunge lilivyoelezwa mara nyingi, ni Triennex(PTY) Ltd ya Afrika Kusini yenye hisa asilimia 50%, Msajili wa Hazina mwenye hisa asilimia 50% kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Kampuni mbili za London Law Services Ltd wa Temple Avenue, wenye hisa 1% na London Law Secretarial Services Ltd ambao anuani yao ni sawa na hao wenzao, nao pia wana hisa 1%. Hii Meremeta hasa ni ya nani, na hawa London Law Services na London Secretarial Services ni akina nani hasa. Kampuni ya Meremeta ina hisa asilimia ngapi? Haya ni mambo yanatufanya tuwe na mashaka makubwa sana. Hivi Serikali inaogopa nini kuweka mambo haya wazi hadharani, angalau kwa Kamati husika ya Bunge basi ili kama kuna sababu ya msingi wawakilishi wa Wananchi waweze kufahamu.
Vivyo hivyo kwa Kampuni ya Tangold ambayo ilisajiliwa katika kisiwa cha Mauritius tarehe 05 April,2005 Ikiwa na Hati ya Usajili na 553334 na kupata Global Business Licence( C2/ GBL) tarehe 08 April,2005. na kupata Hati ya Kutimiza Masharti hapa nchini tarehe 20 February 2006. Hata hivyo Mhe. Spika, Taarifa zilizoko ni kuwa Tangold imekuwa na akaunti NBC Corporate Branch, no. 0lll03024840 iliyofunguliwa Tarehe 1 January, 2003, yaani miaka miwili kabla Kampuni hiyo haiijasajiliwa Mauritius na takriban miaka 4 tangu imepata Hati ya Kutimiza Masharti Tanzania. Ni kwa vipi, kampuni hii kufanya kazi wakati Bunge lilijulishwa na Mhe. Waziri Karamagi kuwa ndiyo iliyorithi Meremeta baada ya Meremeta kufilisika? Mhe. Spika haya maswali yanahitaji kujibiwa kinagaubaga ili kuwarudishia Watanzania imani kuhusu kinachojiri na usalama wa Rasilimali na fedha zao. Waziri Mkuu ndiye mtu stahiki wa kurudisha imani hii kama Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, baada ya Waziri wa Fedha kushindwa kutoa majibu ya kuridhisha jana. Isitoshe, Makampuni haya tangu yaliposajiliwa nchi za nje na hata hapa Tanzania japo yamekuwa na akaunti katika Benki za nje na za Ndani Hesabu zao hazijakaguliwa na chombo chochote hadi leo (hatujui kama itakuwa imekaguliwa na CAG katika Taarifa ya BOT ya 2007/2008 ambayo haijawasilishwa Bungeni bado).
Wahusika wa Tangold ni Bodi ya Wakurugenzi ambayo ni viongozi au waliokuwa viongozi waandamizi katika Serikali. Wakurugenzi hao ni pamoja na hayati Daudi Balali aliyekuwa Governor wa Benki Kuu (BOT), Andrew Chenge aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Gray Mgonja, Katibu Mkuu-Wizara ya Fedha, Patrick Rutabanzibwa- Katibu Mkuu-Maji na Vincent Mrisho-Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu."
MIMI SWALI LANGU HAPA NI KWAMBA MBONA KWENYE HAO WANAHISA WA MEREMETA SIONI JESHI? CHA KUSHANGAZA ZAIDI JESHI HUWA HALIFANYI WALA HALIJIHUSISHI NA BISHARA, KAZI YA JESJI NI KULINDA NA KUHAKIKISHA TAIFA NI SALAMA, SASA JESHI NALO SIKUHIZI LIMEJIINGIZA KWENYE KUANZISHA MAKAMPUNI? WAZIRI MKUU BADO HAJATOA MAJIBU HAPO. TUNAOMBA WAZIRI MKUU AJIBU HOJA KAMA ILIVOULIZWA NA DR SLAA KWENYE HOTUBA YAKE HAPO JUU