Na gazeti la
Tanzania Daima siku moja kabla Ijumaa Oktoba 22 liliripoti kama ifuatavyo;
Mdahalo wa urais kesho
na Mwandishi wetu
TAASISI ya East Africa Business and Media Training Institute kwa kushirikiana na Vox Media Centre imeandaa mdahalo wa mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.
Mkurugenzi wa Vox Media, Juvenalis Ngowi, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa mdahalo huo utafanyika kesho kuanzia saa 12 jioni na kurushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha ITV.
Alisema mdahalo huo utafanyika katika Hoteli ya Movenpic na wananchi wataweza kuuliza mashwali moja kwa moja. Ngowi alieleza kuwa mdahalo huo unatarajiwa kuhudhuriwa na watu 200.
Wagombea urais kwa Tanzania Bara mbali na Dk. Slaa ni Jakaya Kikwete (CCM), Profesa Ibrahim Lipumba (CUF), Peter Mziray (APPT-Maendeleo), Fahmi Dovutwa (UPDP), Mugahywa Muttamwega (TLP) na Hashimu Rungwe (NCCR - Mageuzi).
Huu ni mdahalo kwa pili kuandaliwa na Vox, baada ya ule wa kwanza kufanyika mwanzoni mwa mwaka huu visiwani Zanzibar ambao uliwakutanisha wagombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi.