na Sitta Tumma, Mwanza
RAIS Jakaya Kikwete ametoa sh milioni 10 kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa Maendeleo ya Elimu katika Jimbo Nyamagana jijini Mwanza.
Hatua ya Rais Kikwete kutoa kitita hicho cha fedha, imeonyesha kufungua milango kwa wanasiasa wengine kushiriki kuchangia maendeleo ya wananchi bila kujali itikadi zao za kisiasa.
Rais Kikwete alichangia fedha hizo juzi usiku, wakati wa harambee ya ufunguzi wa mfuko huo katika jimbo hilo linaloongozwa na mbunge Ezekiel Wenje (CHADEMA), iliyofanyika jijini hapa.
Harambee hiyo ambayo iliongozwa na mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (akiwa ni mgeni rasmi) ilifanikiwa kupata zaidi ya sh milioni 50 huku Zitto akiipiga mnada saa yake na kununuliwa kwa sh milioni 1.7.
Mbali na Rais Kikwete kutoa mchango huo, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbrod Slaa alichangia sh milioni tano, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, sh milioni mbili, Zitto sh milioni moja na Wenje milioni tatu.
Baadhi ya wabunge wengine wa CHADEMA waliotuma michango yao kwa kupitia kwa mgeni rasmi, Zitto ni pamoja na Gres Kiwelu sh 300,000, Muhonga Saidi sh 200,000, Rayah Ibrahim sh 200,000, na wengine wengi, huku Naibu Meya wa jiji la Mwanza, Charles Chinchibela (CHADEMA), akichangia sh 200,000.
Baadhi ya wafanyabiashara wa jijini Mwanza waliochangia kufanikisha harambee hiyo ni pamoja na mfanyabiashara maarufu Joseph Madirisha ambaye alitoa sh milioni moja pamoja na wengine kadhaa waliochangia kupitia mtandao wa Facebook ya Zitto ambao walitoa euro 1,000 na sh 600,000. Akizungumza katika harambee hiyo ya kuchangia Mfuko wa Maendeleo ya Elimu jimbo la Nyamagana, Zitto aliwataka wanasiasa kuacha hulka ya kususia shughuli za maendeleo, kwani wakati huu si wa siasa bali ni kupigania maendeleo ya wananchi wote kwa ujumla.