Kutoka Dodoma Sifa Lubasi anaripoti, kwamba Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Pudenciana Kikwembe (44), kutoka Mkoa wa Katavi, amevamiwa na kuporwa fedha na kadi tatu za benki wakati akiwa kwenye baa ya Lady May barabara ya Iringa mjini humo.
Akisimulia tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen, alisema kuwa tukio hilo lilitokea saa 8.30 usiku wa kuamkia jana kwenye baa hiyo. Alisema mtu asiyefahamika, alivamia baa hiyo akiwa na gobori na kumpiga risasi ya mguu mkaanga chipsi, Ally Kubula (22). Alisema baada ya kumjeruhi mkaanga chipsi huyo ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma akitibiwa majeraha, alipora mikoba miwili; mmoja ukiwa wa Mbunge huyo wenye dola 600 za Marekani, Sh 180,000 na kadi za benki za NMB, CRDB na NBC.
Pia alipora mkoba mwingine wa Sharon Tuli, rafiki wa Mbunge huyo, ukiwa na simu mbili na Sh 100,000. Kamanda alisema juhudi za kumsaka mtu huyo zinaendelea na Jeshi la Polisi linatoa rai kwa wananchi kupitia sera ya Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi, kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuhakikisha wanabainika na kuchukuliwa hatua stahiki.
Kupitia mtandao wa kompyuta, Mbunge huyo alikiri kuporwa fedha na kadi za benki. Ni kweli kwamba tukio hilo lilitokea jana (juzi) saa 2.30 usiku katika baa ya Lady May Pub, iliyoko barabara ya Iringa
nilifika mahali hapo kupata chakula na kuzungumza na wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zilizoko Dodoma wanaotoka Rukwa na Katavi kuhusu mambo mbalimbali, alisema Mbunge.
Habari Leo