Mbinu za kutokuchepuka kwa karne ya 21 - 22

MBINU ZA KUTOKUCHEPUKA KWA KARNE 21 - 22

Kwa Mkono wa, Robert Heriel.

Ikiwa wewe ni mvivu soma kwa urefu wa kamba za akili yako.

Hakuna mtu mwenye akili timamu, muadilifu na aliyestaarabika anayependa kuchepuka. Ni wazi kuwa kuchepuka ni ishara ya mtu kujidharau, kujidhalilisha, kumuasi Mungu na kuitambulisha vibaya jamii atokayo. Hapana shaka watu wote wanaochepuka hujikuta katika dhiki, taabu na majuto makuu hasa pale akili njema zikiwarejea. Hata hivyo, watu waovu huona fahari kutenda uovu, hivyo sio ajabu kusikia mtu akijisifia kuwa yeye anachepuka.

Kuchepuka ni ishara ya kutoridhika, kuwa na tamaa mbaya, kutojielewa na kushindwa kujizuia kihisia, kimwili na kiakili. Mtu anayeshindwa kujizuia au kujitawala ni mbaya zaidi kuliko mnyama wa mwituni.
Bila kujali nani anayechepuka, iwe mimi, au wewe, au yule, au mtu awaye yeyote yule, hata kama ni mzazi, kiongozi wa aina yoyote ile, ilimradi tuu anachepuka basi mtu huyo kajidharau, na ni mdharauliwa, kajitukana nafsi yake.

Kwa nini uchepuke?
Hakuna sababu yoyote ya kuchepuka isipokuwa sababu ya kushindwa kujitawala, kujidharau, kujitukana, tamaa mbaya n.k.
Mwanaume anayoruhusa ya kuoa mwanamke zaidi ya mmoja, kwa nini uchepuke?
Ikiwa unajijua kabisa mwili wako hautaridhika na mwanamke mmoja kwa nini uwe na mwanamke mmoja?
Ikiwa ulijua wazi kuwa mwanamke mmoja hakutoshi, kwa nini usingemmtaarifu huyo mkeo kuwa unamuoa lakini utaongeza mwanamke mwingine siku zijazo, ili usijemdhulumu huko mbeleni kwa kutomwambia haya mapema.

Mtu anayechepuka hana utofauti mkubwa na FISI, tamaa mbaya, mtu asiyeridhika na kitu alichokuwa nacho, anataka na vingine zaidi.

Mwanamke anayechepuka hujiabisha yeye mwenyewe, na kumdhalilisha na Mama yake, kwani ni kawaida kwa mtoto wa kike kurithi kwa sehemu kubwa mambo ya Mama yake. Hivyo mwanamke unapochepuka unajaribu kuieleza jamii na watu wanaokuzunguka kuwa Mama yako alikuwa na tabia mbaya. Huwa naamini, ikiwa mama hakuwa malaya basi 90% watoto wake wakike hawatakuwa Malaya. Lakini ikiwa mama alikuwa hajatulia iwe kwa siri au kwa wazi basi 90% ya watoto wake wa kike lazima wasitulie, lazima wawe viruka njia.

Niliwahi kuambiwa na Mzee mmoja pale kijijini kwetu Makanya,, tukiwa tunacheza mchezo wa Bao, kuwa; nikitaka kuoa mwanamke yoyote yule basi nitazame tabia na muonekano wa Mama mkwe. Kwani vile mama mkwe alivyo ndivyo kwa 90% mtoto wake atakavyokuwa. Mzee yule nilimbishia lakini akaniambia niwe mtulivu nikue niyaone. Hiyo ilikuwa miaka kumi na tatu iliyopita.

Ni nadra sana Baba kumshauri mwanaye wa kiume au wakike jambo baya, ila ni jambo la kawaida na rahisi kwa Mama kumshauri vibaya mwanaye wa kike au wakiume. Hata ndoa nyingi za sasa huvunjwa na kina mama mkwe kuliko Baba mkwe. Ni rahisi kwa mama mkwe kumshauri binti yake aende kwa waganga wa kienyeji ili amtengeneze mumewe(wewe hapo) ila haijawahi kutokea Baba mkwe akamshauri binti yake mambo ya namna hiyo. Hii ni kusema, ikiwa Mama mkwe ni mpumbavu hakuwa mke mwema kwa Baba mkwe wako, basi kuna uwezekano mkubwa mke wako naye akakupiga Knockout.

Nikirejea kwenye mada, leo tutaangazia mbinu madhubuti zitakazo kufanya usichepuke iwe ni mwanaume au mwanamke. Mbinu hizo ni kama ifuatavyo;

1. MJUE SANA MUNGU
Hii ndio mbinu ya kuu kabisa inayobeba zingine. Kumjua Mungu ni kujijua wewe mwenyewe, huwezi kujijua pasipo kumjua aliyekuumba. Ukishamjua Mungu basi utakuwa umeshajijua. Ukishamjua Mungu lazima utamheshimu na kumtii. Kumheshimu Mungu ni kujiheshimu wewe mwenyewe na wengine. Ukiweza kumtii Mungu basi umeweza kila kitu kwenye maisha ikiwemo kuweza kutiisha mwili, hisia, akili na roho yako. Pia utaweza kuyatiisha maisha yako yaende vile utakavyo. Kumtii Mungu ni kujipa mamlaka ya kutawala Dunia yako.
Kumjua Mungu ni kujiweka huru kweli kweli, kutokumjua ni kujigeuza mtumwa na mateka. Hakuna aliyehuru pasipo kuwa na Mungu. Kumjua Mungu kutakufanya automatic uwe na upendo, utajipenda mwenyewe, utapenda mkeo/mumeo, watoto na watu wengine pasipo kuwaumiza. Kutomjua Mungu kutakufanya usiwe na Upendo, hautapenda mkeo/mumeo wala watoto achilia mbali watu wengine. Kumpenda Mungu kutakufanya maisha yakupende, nawe utauafurahia.

Ukitaka usichepuke kwa mkeo/mumeo basi jambo rahisi kuliko yote ni kumjua Mungu.
i/ Jua Mungu ni nani ili ujue wewe ni nani
ii/ Jua Mungu anapenda nini ili ujue chakupenda
iii/ Jua Mungu anachukia nini ili ujue chakuchukia
iv/ Jua Mungu anatawalaje ili uje utatawalaje mambo aliyokupa
v/ Jua Mungu anahukumu vipi ili ujue utahukumuje
vi/ Jua Mungu anafanyaje kazi ili ujue kazi zako nawe utafanyaje
vii/ Jua Mungu anasemaje ili ujue cha kusema
viii/ Jua kusudi la Mungu kutoa baraka fulani ili ujue namna ya kutumia baraka hizo
ix/ Jua Mungu hana second chance ili ujue kutumia Golden chance akupazo
x/ Jua Kwa nini Mungu anaishi milele ili ujue namna ya kuishi miaka mingi

Ukishamjua Mungu basi kuchepuka itakuwa hadithi kwako.

2. OA MWANAMKE MZURI SANA UNAYEMPENDA/ OLEWA NA MWANAUME MZURI SANA UNAYEMPENDA. UPENDO + UZURI
Tayari ushamju Mungu automatic utakuwa umeshajijua wewe ni nani, unapenda nini na nini haupendi, unajielewa sasa.
Utajua yupi ni mwanamke/mwanaume mzuri wa kufaa kuwa naye kwenye maisha. Macho yako hayatakudanganya kwa vile unayaelewa, moyo wako hautakuhadaa kwa sababu tayari unaujua ukoje. Akili yako haitakuyumbisha kwa sababu unaijua.
Usipojielewa basi huwezi muelewa hata yule uliyeamua kumuoa/kuolewa naye.

Iangalie akili, hisia, roho yako ni wakati gani ipo real ndipo uchagua mwenza wa maisha. Akili, hisia, na roho vikiwa real ndio utajua mke/mume mzuri wa kukuoa/kuolewa naye. Ninakuambia kabisa kuwa sio kila muda akili, moyo na roho yako inakuwa Real, kuna wakati ina-pretend kutaka jambo fulani kumbe haitaki. Sishangai mtu akihangaika miaka nenda rudi kutafuta jambo fulani lakini akilipata analiona ni lakawaida au kulichukia kabisa. Ni kwa sababu akili, hisia na roho yake ili-Pretend na kumdanganya inataka kitu fulani kumbe sio kweli..

Akili, Moyo na Roho viki-Pretend kutaka jambo fulani, hiyo huitwa TAMAA. Akili, Moyo, Roho ikihitaji jambo fulani kiukweli kabisa, hiyo huitwa UPENDO.
Tamaa haidumu lakini Upendo unadumu. Tamaa furaha yake niwa muda, upendo furaha yake ni ya milele.

Uzuri wa mwanamke/ mwanaume unayetaka akuoea/uolewe naye unatofautiana baina ya mtu na mtu. Hata hivyo zingatia akili yako ikiwa Real ili mapenzi yenu iwe Real na kudhalisha Ndoa Real. Lakini akili , moyo na roho viki-pretend, ukajichanganya kuingia kwenye mapenzi, basi mapenzi yenu yatatawaliwa na ku-pretend, mwishowe ndoa yenu nayo itakuwa ya ku-Pretend.

Ndoa ya Real haihitaji Kitchen party, haihitaji Kungwi, wala mafunzo ya aina yoyote yale. Ndoa real,, wanandoa wanajikuta automatic wanalandana na kutimiziana mahitaji yao kikamilifu kabisa. Yaani mambo yanaenda yenyewe tuu. ndoa Real hazina mshauri, kwani zinajiendesha zenyewe kutokana zipo Automatic. Upendo haufundishwi, upendo haupo artificial, upendo ni natural. Kumwambia mwanamke amfanyia mumeo moja, mbili, tatu ni dalili kuwa huyo mke hampendi mume wake hivyo hajui amfanye nini. Mtu unayempenda lazima utajua cha kumfanyia automatic.

Lakini Ndoa za Ku-pretend ndio zinahitaji sijui Kitchen Party, sijui Kungwi na mafunzo kede kede. Ndoa za Ku-pretend zipo Manual, lazima washauri wawepo waziongoze, mambo hayaendi pasipo kuuliza kwa watu wengine. Wanandoa kwa sehemu kubwa hawalandani, hivyo magomvi ya mara kwa mara lazima yawepo.
Siku hizi Somo wapo wengi wakuwafunda kinadada, jambo ambalo linadhihirisha kuwa ndoa nyingi siku hizi ni ndoa za Ku-pretend. Mwanamke anayekupenda hawezi kufundishwa namna ya kukuhudumia wewe kama mume wake. Mwanaume anayekupenda hafundishwi namna ya kukutunza wewe kama mke wake.

Watu wote waliowahi kupenda wataungana na mimi kuwa ni ngumu sana kuchepuka/kumsaliti mtu unayempenda. Kwanza yeye ndio unamuona kila kitu wengine unawaona katuni tuu. Mwanamke anayempenda mume wake Real kabisa pasipo ku-pretend dalili namba moja kabisa ni lazima atawadharau wanaume wengine. Na hii hutokea kwenye First Love kwa wanawake wengi. Sio ajabu mwanamke akawa anaringa sana na kuwanyali vijana wanaomuita akiwa kwenye first love. First love is a real love.

Uzuri wa mwenza wako ni kile kinachokushtua uonapo wanawake, mathalani;
i, Mshtuko wa maumbile kama vile Makalio na nyonga kubwa, ukiona unashtuka uonapo wanawake wa namna hii basi jua hao ndio ugonjwa wako. Usijeoa mwanamke nje ya wenye sifa hizo. Oa mwanamke mwenye matako makubwa na nyonga nene ikiwa ndio furaha yako, ndoa ni furaha sio sehemu ya kujitolea au kuoneana huruma.
Wanawake wembamba na warefu, ikiwa ndio mshtuko wako uwaonapo, basi oa mmoja wapo kati ya hao.
Halikadhalika na wanawake size ya kati, na wengineo.

ii/ Mshtuko wa Rangi na kimo
Ikiwa unashtuliwa ukiona wanawake wenye rangi nyeusi kama mkaa, moyo unaminywa ukiwaona. Oa hao. Oa mwanamke mwenye rangi inayoshtua moyo wako na kulegeza misuli ya macho yako. Ndoa ni uwanja wa kushtuana. Kama haushtuliwi basi hiyo ni hatari kubwa
Au mwanamke mweupe ikiwa ndio mshtuko wako oa.
Wengine mishtuko yetu ni maji ya kunde mtelezo. Kila mmoja apambane na hali yake.

Mishtuko mingine inaweza kuwa kwenye macho, sauti, uchogo au komwe, mdomo, tabasamu, sura zuri au kawaida ua ugwadu, nywele n.k

Oa/ Olewa na mtu mzuri kabisa unayempenda na anayekuchanganya ukimtazama, moyo wako haubaki kama ulivyo lazima uvuje damu na kupoteza Frequency za kudunda.

3. RUHUSU URAFIKI NA HUYO MUME/MKE UNAYEMPENDA ALIYEKUOA.
Upendo ni urafiki, ushampenda na amekuwa mpenzi/ mke au mume wako. Kile kilichopo moyoni kiruhusu usikizuie. Kilichopo moyoni ni Urafiki. Hapana shaka ukimpenda mtu unajikuta unataka kila kitu ukijuacho naye akijue. Unajikuta unaropoka hata visivyoropokwa, hio ndio maana halisi ya Upendo. Mtu anayekupenda kamwe hana ubavu wa kukuficha jambo lolote. Kumficha umpendaye ni dalili ya kuwa una-pretend mapenzi. Kwenye ku-pretend ndio anaoubavu wa kumficha mwenza wake. Kwenye upendo lazima mambo yawe wazi kabisa.

Watu wanaopenda ni kawaida kuwa WAMBEYA, kuambia umbeya wao kwa wao ni kitu cha kawaaida, kwenye stori zao. Kuna wakati mwanaume anaweza kutaka kumsimulia mke wake jinsi anavyotongoza huko mitaani hahahaaa! Ogopa watu wanaopendana kabisa. Ndio maana haishauriwi kuwashauri wapendanao kwani unaweza jikuta linakurudia wewe mwenyewe. Yaani umshauri shoga ako amuache mume wake, Loooh! hakika habari hizo utazikuta kwa shemeji yako. Au umwambie mwanaume ubaya wa mke wake anayempenda, hakika unachokitafuta utakipata.
Watu wanaopendana wanapiga Stori, wanacheka pamoja, wanataniana kama watoto wadogo, hakuna yale mambo ya kujifanya siriaz, ati mkoloni, peleka ukoloni wako kwa Baba yako huko. Mbuzi wewe.

Mkishapenda kila mmoja anakuwa huru na mwenzake, upendo ni uhuru. Mwanamke anaouwezo wa kumwambia mume wake kuwa hajaridhika na hajafika kileleni, lakini atasema hayo kirafiki na watajua namna ya kutafuta suluhu. Kwenye upendo wa kweli hakuna asiyetosheka au kuridhishwa na mwenzake. Mwanamke atakuwa huru kumwambia mume wake jinsi ya kumridhisha wawapo kitandani. Wapi ashike kwa namna gani, wapi asishike kwa namna ipi, aende slow au Faster, atulie au aendelee. Hao ni Marafiki wanaambiana ukweli, na ukweli unaraha yake kwenye mapenzi.

Lakini ukijidai kumnunia mkeo hakika na kuambia hata umpakie Mkongo au uwe na uume wa aina gani, kamwe hauwezi mridhisha mke wako kitandani. Mkeo anahitaji upendo, upendo ndio urafiki, awe huru na wewe, lakini ukijifanya mbabe nakuhakikishia lazima uvune ulichokipanda.

Watu wengi wanasema wanawake hawaeleweki jambo ambalo sio kweli, wanawake ni binadamu kama walivyo binadamu wengine. Mwanamke haeleweki hasa ukimnyima Uhuru. Mtu asiye na uhuru kamwe hawezi eleweka kwa sababu atakuwa mnafiki. Lakini mtu huru anaeleweka kwa sababu yupo real hana haja ya kuwa mnafiki. Maneno haya yote narejelea hoja ya Urafiki wa kweli baina ya mume na mke.

Mfanye mkeo au mume kuwa rafiki yako. Kuchepuka itakuwa ndoto. Atakuwa huru kwako kujieleza kwa chochote kile kinachomsibu, hata kama anamtamani mwanamke/mwanaume mwingine atakuambia ukitaka, muhimu uwe jasiri na mstahimilivu kwani huo ndio ukweli. Kisha mjue namna ya kukabiliana na hisia hizo za tamaa ya mmoja wenu.

Hatuwezi kujidanganya kuwa mioyo yetu haitamani watu wengine, ni uongo. Sisi wanaume ndio tunatamaa zaidi, lakini hata wanawake pia wanatamaa. Hivyo inapotokea ukatamani basi kuwa huru kujieleza kwa mkeo au mumeo ili mjue mtasaidiana vipi kuepusha balaa. Kuficha haitasaidia kitu.

4. TAFUTENI MALI KISHA ZITUMIENI WOTE MKITUMIA NAFSI YA KWANZA WINGI
Gawaneni majukumu, au shirikianeni kwa pamoja, tumieni nafsi ya kwanza wingi mfanyapo na msemapo. Kwa mfano, tumeamua kununua Gari jipya litakalotusaidia hapa nyumbani. Na sio kusema; Nimeamua kununua gari jipya litakalowasiadia hapa nyumbani. Kauli ya wingi kwenye umoja ni kauli ya ushirikiano. Hata kama wewe ndio umetoa pesa iwe mke au mume, kauli za nafsi ya kwanza wingi isikauke nyumbani kwenu. Jambo hili tumelitoa kwa MUNGU wetu aliyemkuu. Hapo alipoumba mbingu na nchi, alipendelea kusema " natufanye mtu kwa mfano wetu" kana kwamba wapo wengi, lakini hiyo ni kauli ya kushirikiana.

Upendo unandana na wajibu. Baraka zote zitumike kwa manufaa ya wanafamilia. Mke anabaraka zake, na Mume anazo baraka zake, halikadhalika na watoto. Neno baraka hapa linarejelea Majaliwa kutoka kwa Muumba, kama vile Vipaji na karama, elimu na ujuzi, maumbile, vyeo na mamlaka. Mke anaweza kuwa na vipaji vikubwa kuliko mume, basi vinaweza kutumika kuiletea familia mali, tumezoea wanaume wakiwa na vipaji zaidi ya wanawake lakini leo sitaongelea hayo. Mke anaweza kuwa ameajiriwa udaktari alafu mume akawa Polisi. Mali zote zichumwe na kurudishwa kwenye familia.

Hata hivyo kuchuma mali ni jambo moja na kutumia mali ni jambo jingine. Matumizi ya mali yasilenge kumkandamiza mwingine, hata hivyo kwenye upendo sio rahisi ubinafsi kujipenyeza

5. WAJUE MAADUI ZENU.
Adui huweza kuwa yeyote yule katika familia yenu. Anaweza kuwa rafiki, ndugu, wazazi, majirani au hata wafanyakazi wenzako.
Hata hivyo wapo maadui wa aina mbalimbali, wapo maadui wa kiuchumi, maadui wa kimapenzi, maadui kiroho, hawa ndio maadui wakuu wanaoangusha ndoa nyingi hivyo lazima uwafahamu mapema kabla mechi haijafika mbali.
Licha ya ubaya wa adui lakini faida kubwa ya adui ni Kupima upendo wenu na kuwaimarisha kama mtakuwa imara.

MAADUI WA KIUCHUMI
Hawa ni wale maadui ambao wanazorotesha uchumi wenu, aidha wanadhulumu mali zenu, wanawapunja mishahara, au kuwaibia mali zenu, pia watu wote wanaomtaka mmoja wenu afukuzwe kazi hivyo wanamfanyia fitna na kumuwekea mizengwe hao ni adui wa familia.
Inafahamika kuwa moja ya nguzo za familia ni uchumi mbali na Upendo, pasipo uchumi imara ni mara chache sana kukawepo na familia imara. Ndio maana msingi mkuu wa sheria za Mungu ni upendo, na Kufanya kazi ni sehemu ya Upendo, hivyo unapoidhoofisha nguzo ya upendo ambayo ni kazi inayoleta uchumi wa familia ni kuiangusha familia.

Ukiona mtu yeyote anayechezea kazi yako jua huyo anacheza na upendo wako, anacheza na familia yako, anacheza na mke/mume na watoto wako. Kazi ndio uchumi ambapo ni sehemu ya upendo.
Mtu akitengua nguzo ya kazi kwenye upendo wenu ujue amebakisha padogo sana kuwaangamiza. Kupenda kazi, ni kumpenda mkeo/mumeo na watoto wako. Hata hivyo kazi isiwe sehemu ya kuvunja familia bali iwe sehemu ya kuiimarisha.

MAADUI WA KIMAPENZI
Hawa ni wale wapima upepo, kuona ni kweli mnapendana, kutaka kujua kile unachokipata kwa mkeo/mumeo. Kundi hili halina nguvu sana ikiwa mnapendana sana, yaani upendo wenu unanguvu. Lakini kundi hili ni hatari ikiwa litapata nafasi kidogo tuu.
Wanaume tunatamani sana wanawake wazuri wenye mivuto ya kimahaba. Kiukweli hawa ni vipimo halisi ikiwa tunapenda wake zetu. Kikawaida thamani ya mwanamke unayemtamani huwa kubwa kabla hujaongea naye. Uzuri wa mwanamke unayemtamani ni pale umuonapo akipita au akiongea na wetu wengine. Lakini baada ya kuzungumza naye thamani yake automatik inashuka kabla hata hujaenda kufanya naye mapenzi.

Huwa nawaambiaga watu, ikiwa umemtamani mwanamke mwingine na ukataka kuchepuka naye, basi namna bora ya kujizuia ni kumtongoza mwanamke huyo na kumzoea haraka, usifanye haraka kulala naye, kaa hata miezi mitatu kabla hujalala naye utajikuta unamzoea na ule uzuri uliokuwa unauona mwanzoni umeyeyuka kisha utashangaa kumbe hata mke wako anamzidi kwa kila kitu.

Mwanamke ukishahisi mumeo ananyemelea mwanamke mwingine, usipaniki, huo ndio wakati wa kulinda mapenzi yako. Vaa vizuri kwa miezi mitatu mfululizo, ukiwa Sex na romatic, huku ukichunguza mienendo ya mumeo. Nakuhakikisha hatachepuka.

Uzuri wa mwanamke ambaye sio mke wako ni pale kabla hujaongea naye, ukishaongea naye thamani yake inashuka, wanaume wengi watakubaliana na mimi.

Hata hivyo hii ni tofauti na kwa Mwanamke.
Mwanamke tamaa yake huwa mbali ukilinganisha na mwanaume. Tamaa ya mwanamke ni mpaka ivutwe na mwanaume. Mwanamke hawezi kuwa na hisia za kimapenzi kwa sekunde kama tulivyo wanaume. Mwanamke anahitaji mazoea na ukaribu ili hisia zake ziweze kuvutika upande wa pili. Hata hivyo wapo wanawake exceptional ambao huweza kutamani mwanaume kwa sekunde ingawaje hawa ni wachache sana, na wengi huitwa MALAYA. Malaya ni mwanamke mwenye tabia ya kiume ya tamaa ya ngono.

Mwanamke ili asichepuke lazima asiwe na ukaribu na mazoea na wanaume hasa wale wenye mshtuko wake wa moyo. Mwanaume mwenye akili ni kawaida kumzuia mke wake na ukaribu na wanaume hasa wenye mishtuo ya moyo wake, wacheshi, wajanja wa mdomoni, na wenye sifa za kuvutia mwanamke.

Hata hivyo mwanamke mwenye akili, hawezi kuwa na mazoea na wanaume.

Maadui wa mapenzi yenu, hutumia ukaribu wao na mke wako kujifanya/ pretending kuwa wanamjali na wanampenda, lengo ni kuvuta tamaa ya moyo wa mkeo wako kwa ni uhakika kuuvuta upendo hawawezi. Tamaa ya mkeo ikifanikiwa kuvutwa kwa ukaribu na mazoea basi penzi linaweza kuwa mashakani kwani anaweza kuliwa kisha mkatengana kimwili lakini mioyo yenu ingali ipo pamoja.
Mbinu ya kukufanya mwanamke usichepuke ni kutokuwa na ukaribu au mazoea na wanaume. Ni hatari kwani kuna vuta tamaa yako iliyolala, usisahau kuwa mchepuko wako hauna uwezo wa kuvuta upendo wako kwenda kwake, haiwezekani na haitawezekana kamwe. Laba u-pretend yaani tamaa. Ila sio Real

Wanawake wengi sometimes hushindwa kutofautisha tamaa na upendo, hivyo hujikuta wakiwaacha waume zao waliopenda kisha kushikamana na michepuko lakini kwa vile tamaa haidumu, ikishaisha wanakuja kugundua kuwa walikuwa tuu na tamaa. Hii pia hutokea kwa wanaume baadhi. Kurudi haiwezekani kila mmoja alianza maisha yake. Wote wataishi maisha ya taabu kwani walitengana kimwili lakini mioyo yao ingali pamoja.

Nikupongeze kufika mpaka hapa, makala inaweza kuwa ilikuwa ndefu lengo sio kukuchosha bali kukupa kitu kizuri chenye maelezo toshelevu. Wavivu wa kusoma huwaga nawaambia wasome mpaka watakapoishia.

Ulikuwa nami

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa Sasa Sumbawanga
Shukrani sana ,Mpare wa Makanya
 
Mfalme Daudi alimtambua Mungu vizuri lakini alichepuka sembuse Mimi.....kuchepuka hakuzuiliki mkuu

Huyo Mfalme Daudi unaweza usimkute peponi kama vile Musa alivyotoswa na Mungu kufika Kanaani. Usimuasi Mungu kwa sababu fulani alimuasi, atakayehukumiwa ni wewe na mimi, huyo hatakuwepo
 
Back
Top Bottom